Header Ads

LightBlog

UDANGANYIFU KARIBU NA KRISMASI

SITAKI
Usafiri mbaya wa ‘Air Buffalo’



Na Ndimara Tegambwage


SITAKI wasafiri wanaokwenda kazini, matembezini au makwao kwa kutumia usafiri wa mabasi, watapeliwe, wasumbuliwe na waghadhabishwe na wamiliki wa mabasi.

Mfano mbaya ambao haustahili kufanywa na kampuni yeyote inayotoa huduma ya usafiri wa mabasi, na ambao haustahili kurudiwa ni ule wa kampuni inayomiliki mabasi ya Air Buffalo.

Nifuateni. Kuna wasafiri. Hawa wanakwenda Bukoba. Wengine wanakwenda miji mingine ya njiani. Wana tiketi kwa ajili ya safari. Siku ya safari ni Ijumaa. Tarehe 19 Desemba 2008. Saa 12.30 asubuhi.

Ninamsindikiza ndugu yangu. Niko kituo kikuu cha mabasi ya mikoani, Ubungo, jijini Dar es Salaam. Nimefika hapa saa 11 alfajiri. Saa 12 kasoro robo wamiliki wa basi la Air Buffalo wanatangaza, “Basi la Air Boffalo la njia ya kati halitaondoka saa 12.30. Litaondoka saa moja kamili. Tunasikitika kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.”

Kwa tangazo hilo nilihisi aina ya utapeli. Tangazo lilisema “njia ya kati” na siyo kituo/mji wa mwisho - Bukoba. Nadadisi. Naambiwa katika basi hilo kutakuwa na abiria wanne wanaokwenda Kigoma. Kwa hiyo tangazo limechukua mtindo wa “Reli ya Kati.”

Ni saa moja kamili asubuhi. Hakuna basi. Hakuna ofisa wa kampuni kueleza kilichotokea. Hakuna tangazo jingine. Napiga simu ofisi za Air Buffalo – Simu:0755555575. Naambiwa gari litakuwa kituoni katika muda wa dakika 30.

Ni saa 2.30. Hakuna gari. Napiga tena simu ofisini. Namba zipo kwenye tiketi za abiria. Najibiwa gari litakuwa kituoni “wakati wowote.” Saa tatu. Saa nne. Kila abiria anasema, “Tumetapeliwa.” Nikaita Buffalo. Simu inalia. Hakuna anayepokea.

Kila mmoja alianza kukumbuka”Bijampola” – wale vijana waliokuwa na kampuni hewa na basi hewa lakini wakaandikisha majina mengi ya wasafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba na kuyeyukia mitaani siku na tarehe ya kusafiri.

Ndipo nikaamua kushirikisha polisi. Yule polisi niliyeita akanambia siku hizi ni wakili. Akanipa mamba ya polisi mwingine. Polisi huyo akasema hahusiki sana lakini pale ofisini kwake kulikuwa na kamanda wa usalama barabarani kanda ya Dar es Salaam aliyetaja jina lake kuwa ni Sanga.

Nikamweleza Sanga kisanga kilichoko Ubungo. Akasikiliza kwa hamu. Akanambia, “Nipe dakika 30 niandae vijana wangu.”

Katika dakika 30 hadi 40 hivi, polisi, wakiandamana na maofisa wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA), walikuwa ndani ya kituo cha mabasi Ubungo wakiongea na wasafiri waliokuwa wakionekana kuchoka na kuwa na karaha.

“Tumekwishawaona wenye basi. Endelea kusubiri hapa,” alieleza ofisa wa Sumatra. “Gari linaletwa. Wale ambao hawataki tena kuendelea na safari watarudishiwa fedha zao; wanaotaka kuendelea wataondoka na basi,”

Kwa mujibu wa Sumatra, nauli ya basi kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba ni Sh. 55,000. Wasafiri wa Ijumaa kwenye basi la Buffalo walikata tiketi kwa Sh. 65,000 au zaidi.

Muda si muda basi liliingizwa kituoni. Lilionekana la zamani sana, ukilinganisha na mabasi mapya na ya kisasa yanayokwenda Bukoba na sehemu nyingine ndani na nje ya nchi. Abiria waliingia kwa msongamano. Sumatra wakaamuru abiria warudishiwe fedha zinazozidi kiwango cha Sh. 55,000 na basi likaondoka. Ilikuwa kama saa tano na nusu na siyo saa 12.30 asubuhi kama abiria walivyokuwa wameahidiwa.

Kama dakika 50 hivi tangu basi litoke Ubungo, nikapata simu ya ndugu yangu niliyekuwa nasindikiza. Alisema hivi, “ Bado tuko Kiluvya. Dereva na kondakta wametuacha hapa; wakapanda basi na kurudi Dar es Salam.”

Wale ambao hawakuanza safari saa 12.30 asubuhi. Wale ambao wamekuwa juani kituoni kwa zaidi ya saa nne na nusu. Wametelekezwa nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

Nilianza upya mawasiliano. Ni kama nilivyofanya asubuhi. Polisi. Sumatra. Abiria. Polisi. Sumatra. Abiria. Polisi…Saa 12 jioni, ofisa wa Sumatra akanieleza kwamba wamewalazimisha wakodishe gari kutoka kampuni yoyote na “kusafirisha abiria wao.”

Huku abiria wakiwa wanajiandaa kurejea Dar es Salaam, kwani pale walipoachwa kulikuwa ni vichaka vitupu, ofisa wa Sumatra akanambia kuwa yuko kituo cha mafuta Ubungo akisimamia waweke mafuta kwenye basi linalokwenda kuwachukua abiria waliotelekezwa Kiluvya.

Saa moja na nusu usiku, abiria walikuwa wanaanza kuingia katika basi. Lakini waliambiwa pia kuwa basi hilo lingewafikisha tu Kahama. Kutoka hapo wangepata “usafiri mwingine.”

Nikarudi kwa ofisa wa Sumatra. Akanithibitishia kuwa ni kweli Buffalo wamekodisha gari la kupeleka abiria hadi Kahama na kwamba Buffalo wamethibitishia mamlaka kuwa wameandaa usafiri kutoka hapo hadi Bukoba. Nami nikawa nimechoka kama abiria.

Kama wamiliki wa Buffalo wasingefuatwa na kung’ang’anizwa, hakika wasingekwenda hata kwenye kituo cha mabasi cha Ubungo. Walikuwa waoga wa kusema iwapo gari ni bovu au wafanyakazi walikuwa hawajalipwa posho au kulikuwa na kitu kingine kilichokuwa kinawakwaza.

Hiyo ndiyo Air Buffalo. Nauli juu ya kiwango. Kukimbia abiria na kutotaka kuwaambia kinachoendelea. Kuwatelekeza porini kwa zaidi ya saa tano. Kuweka maisha yao hatarini, kwani wangeweza kuvamiwa na kuporwa kila walichokuwa nacho.

Hilo ni Air Buffalo lenya namba ya usajili T 155 ADU iliyoandikwa kwenye tiketi za wasafiri lakini lenyewe likionekana kuzeeka sana; kuchoka sana na hatimaye kuishia Kiluvya, nje kidogo ya Dar es Salaam.

Sumatra walifanya kazi yao. Polisi walifanya kazi yao pia. Nami nilitenda wajibu wangu wa kuwakutanisha; kuwakumbusha na labda kuwasumbua kwa kuwapa ripoti za abiria mara kwa mara.

Lakini kwa upande wa Air Buffalo, hakika hivi sivyo jinsi ya kuwa kampuni ya usafirishaji abiria. Usafirishaji wa abiria unapaswa kuwa mwepesi, wa kicheko na furaha wakati wote – tangu kukata tiketi, kupanda basi, kusafiri hadi kuteremka.

Lakini nani anaweza kujitokeza na kutetea Air Buffalo pale atakapokuta abiria waliokuwa wasafari kwa gari T 155 ADU wakisema “hawa bwana ni matapeli?” Yupooo?

0713 614875
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapaili, 21 Oktoba 2008)

No comments

Powered by Blogger.