Header Ads

LightBlog

SERIKALI INAPOKATAA KUTUMIA KANUNI ZAKE

SITAKI

Na Ndimara Tegambwage

Serikali inayokataa kujifunza

SITAKI awepo wa kubeza hatua ya Profesa Benno Ndulu, yule Gavana wa Benki Kuu (BoT), ya kusimamisha watendaji katika benki hiyo ambao wanatuhumiwa kushiriki ufisadi.

Tangu taarifa za wizi na ufisadi nchini zianze kufumuka kwa wingi, ni mara ya kwanza juzi, Ijumaa, taifa limesikia mtu mmoja tu anayefahamu sheria, kanuni na taratibu za utumishi.

Huyo ni Profesa Benno Ndulu. Amesema hivi: Wale wote wanaotuhumiwa na hata kushukiwa kushiriki katika ufisadi kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya benki hiyo, wamesimamishwa kazi na benki inaanza kuwachunguza.

Hiyo ndiyo sheria. Huo ndio utaratibu. Hiyo ndiyo kanuni ya utendaji. Haiwezekani mtu mmoja aliyeko juu madarakani akawa pekee wa kutuhumiwa katika utendaji mbovu au hata wizi na ufisadi kana kwamba alikuwa anafanya kazi peke yake.

Kutuhumiwa kwa Daudi Ballali kutenda au kuidhinisha au kufumbia macho ufisadi ndani ya BoT na mambo yakaishia kwake tu, ni kukataa kufikiri.

Ballali asingeweza kufanya kazi peke yake. Kama alibuni njia ya kutenda, basi kulikuwa na watendaji. Kama alibariki mchoro, basi kuna waliochora na waliotekeleza. Kama alizembea, kuna walionufaika na uzembe wake. Ni mshololo wa wahusika.

Kile ambacho Profesa Ndulu amefanya; kusimamisha kazi watuhumiwa wote kwenye mstari wa utekelezaji, ndicho kilihitajika kufanywa tangu mwanzo wa mfumuko wa taarifa za ufisadi katika benki.

Hicho ndicho kilistahili kufanywa katika wizara za serikali ambako watuhumiwa ni mawaziri na tayari mawaziri wameng’olewa. Hebu tuangalie Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma.

Tusome Kifungu F. 34 cha Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma, Toleo la 1994. Kifungu kinatoa madaraka ya kumsimamisha ofisa kutumia madaraka yake na kumfungulia mashitaka.

Kanuni inasema mashataka sharti yafanywe mara moja au katika siku 30 na endapo hayawezi kufanywa katika kipindi hicho, basi ofisa msimamizi ataomba kibali kwa Katibu Mkuu (Utumishi) cha kuongezewa muda, kueleza kwa nini muda wa awali haukutosha na ni katika muda gani sasa muhusika atatamkiwa mashitaka rasmi.

Aidha, Kifungu F. 38 cha Kanuni za Kudumu kinaelekeza jinsi mtuhumiwa anavyoweza kuchukuliwa hatua ya kiutawala.

Katika hili, mtuhumiwa anasimamishwa kutumia madaraka yake, katika eneo moja au maeneo yote anakohusika. Hii inafanywa pale inapobainika kuwa kuendelea kuwa na madaraka hayo kunaweza kuwa ni kuendelea kutenda kosa.

Hatua hii inaendelea hadi hapo uchunguzi wa polisi utakapokuwa umekamilika. Bali hatua hii haimwondolei muhusika haki yake ya kupata mshahara.

Msingi wa hatua hizi ni kukakikisha kwamba muhusika haendelei kuwa ofisini, akitumia madaraka yaleyale wakati kuna kasoro, shutuma na tuhuma juu ya matendo yake mwenendo wake kwa ujumla.

Tatizo ni kwamba hatua hizi hazijaonekana kutumiwa katika siku za karibuni, hasa tangu mfumuko wa tuhuma za wizi na ufisadi.

Wizara za serikali ambazo zimekumbwa na tuhuma na mashitaka ya waziwazi, zinajua kanuni hizi. Viongozi wizarani wameziweka kanuni katika mafaili au kwenye kuta kama urembo tu.

Mahali pengine viongozi wizarani wanazitumia kanuni hizi kutishia waajiriwa wapya kwamba wanaweza kuchukuliwa hatua hizi au zile lakini wao hawataki kabisa kuzitumia.

Kutokana na udhaifu huu, watuhumiwa wa wizi na ufisadi wameendelea kubaki madarakani; kuficha au kuharibu nyaraka muhimu ambazo zingesaidia kuleta ufumbuzi wa tatizo, au wameendeleza wizi na ufisadi, tena bila kikwazo chochote kiutawala au kisheria.

Hivi sasa kuna taarifa kwamba katika Wizara ya Nishati na Madini peke yake, kuna orodha ya watumishi wapatao 50 ambao wamepangwa kuhamishwa. Vivyo hivyo katika wizara nyingine.


Wizara ya Nishati na Madini imekumbwa na tuhuma nyingi za ufisadi. Taarifa za uhamisho zimeshonwa pia kwenye tuhuma za ufisadi. Kama mawaziri wake tayari wameng’olewa, pale kuna waliokuwa wakifanya kazi chini yao.

Kuna washirika wa kweli wa kile kilichong’oa mawaziri. Kuna waasisi wa mipango iliyozaa kasheshe. Kuna maofisa wa kuagiza na kuagizwa waliokamilisha ufisadi. Kuna waliodharau au waliokataa kuripoti ufisadi.

Katika wote hawa, nani anamhamisha nani? Nani anamsogeza mwenzake mbali na jiko? Nani anajua nini ili abaki pale au aondolewe; ili kuhifadhi au kuficha ukweli au uwongo?

Serikali imenyamazia kanuni zake. Imekataa kuzitumia. Haya ni makosa ya kukusudia. Ndani ya ofisi wamebaki walioshiriki ufisadi badala ya kuwaondoa, angalau kwa muda, kuruhusu uchunguzi na hatua muwafaka.

Serikali irudi kwenye misingi yake. Profesa Ndulu ameonyesha njia. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, tafadhali chukua somo. Serikali isikatae kujifunza; au hata kuiga hili la Profesa Ndulu.

(Makala ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili tarehe 16 Machi 2008. Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872, imeili: ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.