Wasioona walipoigaragaza Everton mchana kweupe
Kuna mambo mawili ambayo nilitarajia kuona na kusikia katika vyombo
vya habari jana. Sikuyasikia. Sikuyaona.
Kwanza, nilitarajia kuona vichwa vya habari magazetini vikilipuka,
kwa njia ya kutabiri, kuwa: Everton yagaragazwa 6 – 0. Sikuona.
Nilitarajia kusoma magazetini, kusikia redioni na kuona kwenye
televisheni msisitizo wa kauli ya mmoja wa wanafunzi wasioona.
Baada ya kumgusa kichwani “mzungu” wa Everton – mmoja wa wachezaji –
mwanafunzi huyo asiyeona alitamka kitu kinachofanana na maneno haya: Tumekuwa
tukiwasikia. Sasa tumefurahi kuwaona laivu.
Maneno hayo yana ujumbe. Sijayaona. Sijayasikia. Hakuna ambapo
waandishi walithubutu hata kuandika, Wasioona wanaona, waulize Everton; kikiwa
kichwa cha habari fafanuzi lakini pia kinachochochea kufikiri.
Wachezaji wa Everton walitua Dar es Salaam juzi, Jumatano jioni. Jana
walipambana na washindi wa Kombe la Sport-Pesa ambao ni timu ya Gor Mahia ya
Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa.
Hoja yangu inatokana na ratiba ya Everton; timu kutoka Uingereza
(England) ilioyoongozana na nyota wake wa sasa ambaye ni mchezaji wa zamani wa
Manchester United, Wayne Rooney.
Ratiba ilionyesha kuwa baadhi ya wachezaji watatembelea Shule ya
Msingi Uhuru Mchanganyiko ya jijini Dar es Salaam ambako kuna wanafunzi
wasioona. Walikwenda pale.
Kwa mujibu wa gazeti hili toleo la jana, wachezaji wa Everton
waliokwenda Uhuru Mchanganyiko, walicheza “soka katika uwanja mdogo na watoto
hao huku wakiwa wamefunika macho yao kwa vitambaa maalum.”
Matokeo ya “pambano” hilo yalikuwa: Everton 0 – 6 Uhuru Mchanganyiko.
Isomeke hivi: Wasioona waibuka washindi. Isomeke hivi: Wasioona wa “kweli”
wawashinda wasioona wa “kujaribu.”
Kuna mambo ya kujifunza hapa. Ndugu zake Rooney walitaka kuonja
kutoona. Walionja. Walipata matokeo palepale. Lakini kuna kitu ndani ya kutaka
kuonja.
Unatamani haraka awepo wa kusema, “…tulikuwa kama wao kwa muda.
Tulijua machungu ya kuwa walivyo. Tulithibitisha madhara ya upungufu. Tuliona
maisha wanayoishi na jinsi fursa zao zilivyofungwa; na katika hali hiyo, tukashindwa
kufunga hata goli moja.”
Sina uhakika kama nia ya walioandaa ugeni huo imetekelezwa; bali ni
katika mazingira hayo mmoja wa wanafunzi amesema wamekuwa wakiwasikia; lakini
sasa wanawaona laivu.
Tumezoea kusema kuwa kuona laivu ni kuona kwa macho – hiki hapa. Leo,
asiyeona ndiye anasema ameona laivu. Huhitaji juhudi kubwa kutambua kuwa
wasioona wanaona.
Bali waweza kusema wanaoona hawaoni kuwa wasioona wanaona na wana
vionjo vyao ambavyo wanaoona ambao wako katika nafasi za kuwawezesha wasioona
kufurahia fursa muhimu ndio hawaoni au wanakataa kuona njia za kusaidia
wasioona kwa macho.
Wasomaji wawili wamenipelekea ujumbe kuhusu mechi kati ya Everton na
Uhuru Mchanganyiko. Mmoja amesema hilo suala la kuigiza kutoona halikuwa zuri.
“Hiyo siyo kudhalilisha?” ameuliza mmoja wao.
Mwingine akasema, “Wameonyesha uaminifu; vinginevyo wangebakiza
upenyo ili washinde. Waliziba macho kabisa na kukubali kuwa wameshindwa.”
Ukweli ni kwamba hii ilikuwa fursa pekee na ya aina yake kwa
waandishi wa habari kuripoti “mechi” tofauti kabisa na walivyozoea. Hawajazoea?
Ni kweli kwamba wasomaji, wasilikizaji na watazamaji mchezo wa mpira
wa miguu, hawajazoea kuonyeshwa au kusoma ripoti za aina ya kandanda kama
ilivyokuwa kati ya kundi la Everton na Uhuru Mchanganyiko.
Watoto wasioona hawajawahi kucheza au kuwa na mashindano au kufanya
mazoezi kati yao na timu ya nje ya nchi. Kucheza na kushindana siyo muhimu
zaidi. Hawajawahi kufanya pamoja mazoezi ya kawaida.
Hii ina maana kwamba hata waandishi wa habari hawana uzoefu wa
kuripoti kandanda la wasioona. Ndio maana hatuoni kitu katika vyombo vya habari
juu ya kandanda la juzi. Bado wanaona ni mizaha na hawashangai kuwa Everton
ilibwagwa 6-0.
Ni hapo nilikumbuka rafiki yetu “Sauti ya Kiza” Andanenga – asiyeona
lakini mwanafasihi wa viwango vyake na gwiji wa tungo komavu.
Tukiwa kwenye kikao kimoja, katika maongezi ya kwaida, Andanenga
aliniambia, “Unajua Ndimara, wasioona wanaona sana. Ukitaka kujua hilo subiri
umeme ukatike usiku…”
Alisimulia jinsi wanaoona wanavyohangaika usiku pindi taa za umeme
zinapozimika; lakini akasema utaona yeye akitoka taratibu na kwenda anakojua na
kuchukua anachohitaji.
Tayari ujumbe ulikuwa umefika. Akili yake inaona. Ni macho tu ambayo
hayaoni; lakini yeye siyo kipofu. Uthibitisho mwingine ni kazi zake za fasihi.
Bado kuna kazi kubwa ya kuthamini hisia za wasioona, wasiosikia na
wasiotembea na kujifunza jinsi ya kuwaripoti.
- Makala hii imechapishwa ukurasa wa 11 katika gazeti la Mwananchi toleo la 14 Julai 2017 chini ya safu ya Kutoka Meza ya Mhariri wa Jamii.
No comments
Post a Comment