Kukurukakara za CUF
Chama cha
Wananchi (CUF) kinapita katika tanuri la moto. Ulioanza kama mnyukano wa
kawaida, sasa umekuwa janga linaloweza kutokomeza chama. Upande wa chama hicho unaoongozwa
na Prof. Ibrahim Lipumba, umefukuza uanachama wabunge wanane (8). Tayari wamevuliwa
pia ubunge. Upande mwingine chini ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad unapinga.
Tayari umeitisha unachoita vikao halali vya chama.
Ifuatayo ni taarifa ya
“Baraza Kuu la Uongozi la Taifa” kama ilivyotolewa 28 Julai 2017 (inawekwa hapa kusaidia ufuatiliaji wa
kinachoendelea na kujenga hazina ya uchunguzi na uchambuzi kwa siku zijazo).
THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF - CHAMA CHA WANANCHI)
MAAZIMIO YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA
UTANGULIZI:
Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) leo hii
Ijumaa, tarehe 28 Julai, 2017 limefanya kikao cha dharura kilichoitishwa na
Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa kufuata masharti ya Katiba ya Chama ya mwaka
1992 (Toleo la 2014), kifungu cha 80 (1). Wajumbe 45 kati ya wajumbe 52 halali
wa Baraza Kuu wamehudhuria ambao ni sawa na asilimia 86 ya wajumbe wote.
Katika kikao hiki, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipokea, kujadili
na kufanya maamuzi kuhusu ajenda moja tu iliyowasilishwa kwake na Kamati ya
Utendaji ya Taifa ambayo ilikuwa ni:
Taarifa kuhusu kile kinachoitwa kuwavua uanachama Wabunge wanane (8)
na Madiwani wawili (2) wa Viti Maalum kupitia CUF kilichotangazwa kufanywa na
Ibrahim Lipumba na kikundi chake ikiwa ni mwendelezo wa hujuma za Dola dhidi ya
Chama cha CUF.
Baada ya mjadala wa kina, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linapenda
kutoa maazimio yafuatayo kuhusiana na tukio hilo na mwendelezo wa vitendo na
matukio mengi ya hujuma yanayofanywa na Dola dhidi ya CUF:-
1. KUHUSU UHALALI WA BARAZA
KUU LA UONGOZI LA TAIFA:
Kutokana na mkanganyiko unaosababishwa na upotoshaji wa makusudi
unaofanywa na Ibrahim Lipumba na kikundi chake wa kuitisha watu wa kuokota
barabarani na kuwakusanya Buguruni huku akiwaita kuwa ndiyo Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa la CUF, tumeona kuna haja ya kuweka kumbukumbu sahihi ili
kuepusha upotoshaji huo usiendelee.
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama huwa linaundwa kila baada ya
miaka mitano kupitia Uchaguzi Mkuu wa Chama ndani ya Chama na hupata wajumbe
wake kupitia uchaguzi unaofanywa na Mkutano Mkuu wa Taifa (wajumbe 25 kutoka
Tanzania Bara na wajumbe 20 kutoka Zanzibar), wajumbe 14 wanaoteuliwa na
Mwenyekiti kwa kushauriana na Makamu Mwenyekiti na kisha kuthibitishwa na
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, wajumbe wanaoingia kwa nafasi zao wakiwemo
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chama, Wenyeviti na Makatibu wa Jumuiya za
Chama na Viongozi wa Kambi za Wabunge na Wawakilishi wa Chama. Viongozi Wakuu
wa kitaifa wa Chama pia ni wajumbe.
Wafuatao ndiyo Wajumbe halali waliochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa
uliomalizika Juni 27, 2014 hapo Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuwa wajumbe wa
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) watakaokaa madarakani kwa kipindi cha
miaka mitano (2014 – 2019) hadi watakapochaguliwa wengine na Mkutano Mkuu wa
Taifa kwa mujibu wa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 (Toleo la 2014):-
VIONGOZI WAKUU:
1. Mwenyekiti (alijiuzulu tarehe 5 Agosti,
2015 na kujiuzulu kwake kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa dharura
tarehe 21 Agosti, 2016).
2. Makamu Mwenyekiti
(alitekeleza agizo la BKUT kuhama Chama kuwa mgombea mwenza wa Urais kupitia
UKAWA).
3. Katibu Mkuu – Maalim Seif
Sharif Hamad (ambaye bado yupo).
KUTOKA KUNDI LA WAJUMBE 25 WA TANZANIA BARA AMBAO BADO WAPO:
1. Mhe. Nuru Awadh Bafadhil
2. Mhe. Moza Abeid
3. Mhe. Athumani Henku
4. Mhe. Fatuma Omar Kalembo
5. Mhe. Sophia M. Khaify
6. Mhe. Katani A. Katani
7. Mhe. Salum Kh. Barwani
8. Mhe. Bonifasia Mapunda
9. Mhe. Fatuma A. Chitepete
10. Mhe. Juma S. Nkumbi
11. Mhe. Nassir A. China
12. Mhe. Kulthum Mchuchuli
13. Mhe. Karume J. Mgunda
14. Mhe. Twaha I. Taslima
15. Mhe. Julius N. Samamba
KUTOKA KUNDI HILI WALIOFARIKI:
16. Mhe. Ashura Mustapha
KUTOKA KUNDI HILI WALIOHAMA CHAMA:
17. Mhe. Lwebora P. Ndarpoi
18. Mhe. Mohamed A. Khalifa
19. Mhe. Mkiwa A. Kimwanga
KUTOKA KUNDI HILI WALIOFUKUZWA
UANACHAMA:
20. Mhe. Chief L. Yemba
KUTOKA KUNDI HILI WALIOSIMAMISHWA UANACHAMA:
21. Mhe. Magdalena H. Sakaya
22. Mhe. Kapasha H. Kapasha
23. Mhe. Thomas D.C. Malima
24. Mhe. Abdul J. Kambaya
25. Mhe. Omar M. Masoud
KUTOKA KUNDI LA WAJUMBE 20 WA ZANZIBAR AMBAO BADO WAPO:
1. Mhe. Hamad Masoud Hamad
2. Mhe. Abubakar Khamis
Bakari
3. Mhe. Said Ali Mbarouk
4. Mhe. Khalifa Mohamed Issa
5. Mhe. Omar Ali Shehe
6. Mhe. Riziki Omar Juma
7. Mhe. Masoud Abdalla Salim
8. Mhe. Hija Hassan Hija
9. Mhe. Najma Khalfan Juma
10. Mhe. Salim Bimani
11. Mhe. Nassor Ahmed Mazrui
12. Zahra Ali Hamad
13. Fatma Abdulhabib Ferej
14. Mhe. Shaaban Iddi Ame
15. Mhe. Pavu Juma Abdallah
16. Mhe. Abdilahi Jihad Hassan
17. Mhe. Hassan Jani Masoud
18. Mhe. Mohamed Kombo Ali
19. Mhe. Hemed Said Nassor
KUTOKA KUNDI HILI ALIYEFUKUZWA UANACHAMA NA TAWI LAKE NA
KUTHIBITISHWA NA BKUT:
20. Mhe. Rukia Kassim Ahmed
WAJUMBE WALIOTEULIWA NA MWENYEKITI KWA KUSHAURIANA NA MAKAMU
MWENYEKITI NA KISHA KUTHIBITISHWA NA BKUT:
1. Mhe. Zainab A. Msafiri
2. Mhe. Hashim B. Mzirai
3. Mhe. Shaweji M. Mketo
4. Mhe. Abdalla Mtolea
5. Mhe. Joran Bashange
6. Mhe. Elina Kimei
7. Mhe. Mustapha Wandwi
8. Mhe. Ahmed Marshed Khamis
9. Mhe. Ismail Jussa Ladhu
10. Mhe. Nunuu S. Rashid
11. Mhe. Shambuli A. Makame
12. Mhe. Abdalla Bakari Hassan
13. Mhe. Yussuf Salim Hussein
KUTOKA KUNDI HILI WALIOSIMAMISHWA UANACHAMA:
14. Mhe. Shaaban Kaswaka
VIONGOZI WAKUU WA JUMUIYA ZA CHAMA:
1. Mhe. Hamidu Bobali –
Mwenyekiti Jumuiya ya Vijana
2. Mhe. Mahmoud A. Mahinda –
Katibu Mtendaji Jumuiya ya Vijana
N.B.
- Viongozi wa Jumuiya
ya Wanawake ambao ni Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej (Mwenyekiti) na Mhe. Fatma
Omar Kalembo (Katibu) walikuwa wameshaingia kwa nafasi za wajumbe wa
kuchaguliwa.
- Jumuiya ya Wazee
bado haijafanya uchaguzi na viongozi wake wa Sekretarieti ya Wazee hualikwa tu
kuhudhuria vikao vya BKUT.
KIONGOZI WA WABUNGE WA CUF BUNGENI:
1. Mhe. Riziki Shahari Mngwali
MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI YA CHAMA:
1. Mhe. Abdalla S. Khatau
JUMLA YA WAJUMBE HALALI WALIOPO SASA:
Kutokana na mchanganuo huu, idadi ya sasa ya Wajumbe halali tuliopo
tunaounda Baraza Kuu la Uongozi halali la Chama ni 52 ambapo wajumbe 25
wanatoka Tanzania Bara na wajumbe 27 wanatoka Zanzibar.
Mkutano Mkuu wa Taifa haujalivunja wala haujachagua Baraza Kuu
jengine. Kama lipo jengine la pili hilo litakuwa ni Baraza Kuu feki, na chombo
chochote kitakachoundwa na Baraza Kuu lisilokuwa hili lililotokana na Mkutano
Mkuu wa Taifa katika kipindi hiki cha miaka mitano (2014 – 2019), chombo hicho
nacho kitakuwa ni feki kama ilivyo kwa Kamati feki inayojiita ya Nidhamu na
Maadili.
Kwa msingi huo huo, maamuzi halali ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa
ni yale yanayofanywa na Baraza Kuu linaloundwa na wajumbe walioorodheshwa hapo
juu. Wajumbe wengine feki watakaojiita Baraza Kuu wakifanya maamuzi kuhusu
jambo lolote lile, maamuzi yao hayo yatakuwa feki pia.
2. KUHUSU KINACHOITWA
KUFUKUZWA UANACHAMA WABUNGE WANANE (8) NA MADIWANI (2) WA CUF:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa halijakutana popote siku ya Jumapili,
tarehe 23 Julai, 2017 kufanya maamuzi yoyote ya kuwafukuza uanachama Wabunge
wanane (8) na Madiwani wawili (2) wa CUF kama ilivyodaiwa na mtu anayeitwa
Ibrahim Lipumba na kikundi chake. Kwa msingi huo, Baraza Kuu linawataka
Watanzania kufahamu kwamba:-
(a) Linaendelea kuwatambua
Wabunge na Madiwani hao kuwa wanachama halali wa CUF tena ni wanachama wa
kupigiwa mfano wenye nidhamu na maadili ya hali ya juu. Baraza Kuu
linawapongeza kwa mapenzi yao kwa Chama chao na msimamo wao thabiti usioyumba
katika kukitetea Chama waliouonesha pale walipokataa kuitikia wito wa Kamati
feki ya Maadili na Nidhamu.
(b) Pamoja na matangazo ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kutangaza kwamba Wabunge hao wanane wamepoteza sifa za Ubunge kwa
hicho kinachoitwa “kufukuzwa uanachama” na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza
majina ya wateule wengine wa kujaza nafasi hizo, Baraza Kuu ambalo ndilo
lililowateua hapo awali bado linaendelea kuwatambua wafuatao kuwa Wabunge wake
halali:
1. Mhe. Severina Silvanus
Mwijage, (MB);
2. Mhe. Saumu Heri Sakala,
(MB);
3. Mhe. Salma Mohamed
Mwassa, (MB);
4. Mhe. Riziki Shahari
Mngwali, (MB);
5. Mhe. Raisa Abdallah
Mussa, (MB);
6. Mhe. Miza Bakari Haji,
(MB);
7. Mhe. Khadija Salum Ally
Al-Qassmy, (MB); na
8. Mhe. Halima Ali Mohamed,
(MB).
(c) Baraza Kuu pia linaendelea
kuwatambua Madiwani wa Viti Maalum, Mhe. Leila Hussein Madibi (Ubungo) na Mhe.
Elisabeth Magwaja (Temeke) kuwa madiwani halali wa CUF katika Wilaya zao.
(d) Baraza Kuu limeridhika kwamba hicho kinachoitwa “kuwafukuza
uanachama” na kuwatangaza kuwa wamepoteza sifa za Ubunge na papo hapo kutangaza
majina mengine eti kujaza nafasi zao, ni mpango kabambe uliosukwa na Dola kwa
kushirikiana na kibaraka Ibrahim Lipumba na kikundi chake na ndiyo maana
Watanzania wameshuhudia KASI YA AJABU (supersonic speed) katika utekelezaji
wake, kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa katika utekelezaji wa maamuzi kama hayo
huko nyuma. Bunge hili hili liliendelea kuwatambua Wabunge kadhaa katika
vipindi tofauti miaka iliopita ambao walishafukuzwa uanachama tena na vikao
halali vya vyama husika.
(e) Baraza Kuu limeshangazwa
na hatua ya Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai kujifedhehesha na kujiaibisha kwa
kusema uongo kwa Watanzania kwamba eti alijiridhisha kuwa Wabunge wanane wa
Chama Cha Wananchi (CUF) ‘wamefukuzwa Uanachama kulingana na taratibu za Chama
hicho na hivyo wamekosa sifa za kuendelea na Ubunge”.
(f) Baraza Kuu limejiridhisha
kwamba Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye kwa mujibu wa
Katiba ya CUF ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Chama na pia kwa nafasi hiyo
ndiye Katibu wa vikao vya Mkutano Mkuu wa Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa la Chama alimuandikia Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai barua rasmi,
Jumanne, tarehe 25 Julai, 2017 akimueleza kwamba hilo lililoitwa Baraza Kuu la
Uongozi la CUF halikuundwa na wajumbe halali wa Baraza Kuu. Hiyo ni mbali na
ukweli kwamba hakuna Mtanzania asiyejua kuwa uhalali wa kibaraka Lipumba na
genge lake unapingwa na Chama cha CUF kwa kesi ambazo ziko Mahakamani. Kwa
hakika Spika Ndugai amepoteza sifa na haiba ya kuongozo Bunge ambalo ni mhimili
mmojawapo wa Dola na ambao ulipaswa kuwa alama ya uadilifu katika nchi na
anapaswa kujiuzulu kwa kuidhalilisha na kuichafua heshima na haiba ya nafasi ya
Spika.
(g) Baraza Kuu linapongeza na kuunga mkono hatua waliyoichukua
Wabunge hao ya kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga uhalali wa hatua
iliyotangazwa ya kwamba ati wamefukuzwa uanachama na ambapo katika kesi hiyo
wanaiomba Mahakama Kuu itamke kwamba wao bado ni wanachama halali wa CUF na
hivyo bado ni Wabunge halali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia CUF katika nafasi za Viti Maalum na kutupilia mbali tangazo la Spika la
kuwatangaza kuwa si Wabunge na lile la Tume ya Taifa ya Uchaguzi la kutangaza
majina mengine ya kujaza nafasi hizo.
(h) Baraza Kuu linamuagiza Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif
Hamad, kuwaandikia Rais wa Bunge la Afrika (PAP), na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani
(IPU) kuhusu fedheha na aibu hii iliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuonesha jinsi demokrasia isivyoheshimiwa Tanzania.
(i) Baraza Kuu linawataka
Watanzania hususan wanawake kuona ni jinsi gani CCM kupitia taasisi za kidola
isivyowajali, isivyowaheshimu na isivyowathamini wanawake ambao ni zaidi ya
asilimia 50 ya Watanzania wote kwa kuwatendea kitendo cha kuwadhalilisha kwa
kuwaondoshea uwakilishi wao halali kupitia Wabunge wazoefu waliokuwa watetezi
madhubuti wa haki za wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.
(j) Baraza Kuu linawataka
Wabunge na Madiwani wote wa CUF nchi nzima kukipuuza kikundi cha wahuni
kinachojiita “Baraza Kuu” na kwamba Baraza Kuu halali la Chama linaendelea
kuwatambua wote kama Wabunge na Madiwani halali wa CUF.
3. KUHUSU KUJIDHALILISHA KWA
TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI NA KUKIUKA KANUNI ZAO WENYEWE KATIKA UTEUZI WA
WABUNGE WA VITI MAALUM:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limesikitishwa na hatua ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi kujidhalilisha na kujishushia hadhi kwa kushiriki katika
hujuma hizi za Dola dhidi ya CUF. Mbali na yale yaliyoyaelezwa hapo juu, hata
kama ingekuwa kufukuzwa Wabunge hao wa CUF kulikuwa na halali na kumefanywa na
chombo halali cha Chama, basi Kanuni walizojiwekea wenyewe Tume katika uteuzi
wa watu wa kujaza nafasi hizo huo unafuata mpangilio wa majina kama ulivyokuwa
umewasilishwa na Chama husika wakati wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa viti
maalum wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. CUF ilipeleka orodha yake ambayo
haihusishi majina yaliyotangazwa. Hivyo ndiyo kusema hata kama hicho
kinachoitwa kufukuzwa uanachama Wabunge hao kingekuwa halali (jambo ambalo si
halali kama ilivyokwisha elezwa hapo juu), basi kwa Kanuni za Tume yenyewe,
watu wa kujaza nafasi hizo wasingekuwa hao waliotangazwa. Kwa maelezo haya,
Baraza Kuu linaweka bayana yafuatayo:-
(a) Kitendo kilichofanywa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kimezidi kuidhalilisha na kuishushia hadhi Tume hiyo
na kwamba kwa kushiriki kwake katika hujuma hizi chafu ni ushahidi mwengine
kwamba Tanzania hatuna Tume huru ya Uchaguzi; bali Tume iliopo inafuata
maelekezo ya Dola tu kuhujumu vyama vya upinzani.
(b) Baraza Kuu linaitaka (linai-challenge) Tume ya Taifa ya Uchaguzi
kutoa hadharani barua ya Katibu Mkuu wa CUF iliyoandikwa kwao mwaka 2015 ikiwa
na majina ya wanachama wake walioteuliwa kuwa wagombea wa viti maalum vya
wanawake na kuonesha iwapo hao iliowatangaza walikuwa katika mpangilio wa
majina yaliyoteuliwa na Chama. Iwapo haitofanya hivyo, iwaeleze Watanzania na
jumuiya ya kimataifa kwa nini waendelee kuiamini Tume hiyo.
(c) Baraza Kuu linatoa wito
kwa jumuiya ya kimataifa na hususan Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika lake
la Mpango wa Maendeleo (UNDP) ambalo limekuwa likifanya kazi na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi kutafakari upya iwapo Tume hiyo bado ina hadhi na heshima ya
kuendelea kuungwa mkono na Shirika hilo, Umoja wa Mataifa, na washirika wa
maendeleo kwa ujumla wakati imejianika waziwazi kuwa inafanya kazi ya kuhujumu
demokrasia Tanzania badala ya kuimarisha.
4. KUHUSU HUJUMA ZA DOLA
DHIDI YA CUF, VYAMA VYENGINE VYA SIASA NA TAASISI NYENGINE ZA KIDEMOKRASIA NA
HAKI ZA BINADAMU HAPA NCHINI:
Baada ya kujadili kwa kina mwendelezo wa mipango ya hujuma dhidi ya
CUF iliyoanza mwaka jana na ambayo inaendelezwa kwa nguvu na kwa kasi, na kwa
kutafakari matukio mengine ya hujuma dhidi ya vyama vyengine vya siasa na
taasisi nyengine zinazosimamia demokrasia, haki za binadamu na utawala wa
sheria hapa nchini, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeazimia yafuatayo:
(a) Limeridhika kwamba Wakuu
wa Dola nchini Tanzania wana mpango mkubwa wa kuua demokrasia hapa nchini kwa
kuviangamiza vyama makini vya siasa vilivyoonekana tishio kwa chama
kinachotawala cha CCM katika uchaguzi mkuu uliopita na pia kupambana na taasisi
zinazoheshimika na zinazojiamini katika kusimamia masuala ya demokrasia, haki
za binadamu na utawala wa sheria.
(b) Baraza Kuu liamini kuwepo mpango huo baada ya sasa kuonekana wazi
kwamba mipango ya hujuma dhidi ya CUF hadi sasa imeshahusisha Ofisi ya Msajili
wa Vyama vya Siasa, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Polisi,
baadhi ya Wakuu wa Wilaya, Ofisi ya Spika wa Bunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi
(NEC), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na bila shaka yoyote Idara ya
Usalama wa Taifa (TISS). Vipi Idara ya Usalama wa Taifa iwe haioni hujuma hizi
za wazi na athari zake kwa usalama wa Taifa?
(c) Baraza Kuu linaona kuwa
hujuma dhidi ya CUF zinatokana na ushindi mkubwa wa chama hiki katika uchaguzi
mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015 ambapo kilimbwaga mgombea Urais wa Zanzibar
kwa tiketi ya CCM kwa tofauti ya kura 25,836 pale mgombea wa CUF, Maalim Seif
Sharif Hamad alipopata jumla ya kura 207,847 dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. Ali
Mohamed Shein, aliyeambulia kura 182,011. CUF pia ilifanikiwa kuongeza majimbo
yake kisiwani Unguja kutoka manne (4) hadi tisa (9) mbali ya kuendelea
kubakisha majimbo yake yote 18 kisiwani Pemba. Mafanikio haya na ushindi huu
mkubwa umekuwa mwiba kwa watawala na ndiyo hujuma zote hizi zinatelekezwa ili
kuisambaratisha CUF, jambo ambalo Baraza Kuu linawahakikishia Watanzania kuwa
halitofanikiwa.
(d) Kwa upande mwengine, mafanikio ya UKAWA katika Uchaguzi Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uthubutu uliooneshwa na Watanzania wanaotaka
mabadiliko ndiyo yanayopelekea pia kuandamwa kwa:
- CHADEMA;
- NCCR;
- Wabunge wa Upinzani
wanaoongoza katika ukosoaji wa Watawala;
- Wanaharakati
wanaotetea uhuru wa kujieleza kama Jamii Forums;
- Wasanii ambao wametumia vipaji vyao
kuwakosoa Watawala;
- Watumiaji wa
mitandao ya kijamii hasa vijana;
- Vyombo vya habari
yakiwemo magazeti, vituo vya radio na TV;
- Taasisi za fani na
stadi zinazohoji kama ilivyotokea kwa TLS; na
- Wana-CCM wenye
mawazo yanayokinzana na yale ya Watawala.
(e) Baraza Kuu linasikitishwa
na mtindo unaoonekana kutaka kujengwa wa kutojali Katiba na Sheria katika
kuongoza na kuendesha nchi na badala yake kutegemea matamko ya Rais. Mengi ya
matamko hayo na matendo yanayofuatana nayo hayaendani na Katiba na Sheria za
nchi ambazo aliapa kuzilinda wakati anashika madaraka ya nchi.
(f) Baraza Kuu linaona
mwenendo huu unaoelekea kukandamiza demokrasia na hatimaye kuiua kabisa hauleti
taswira njema kwa mustakbali wa Taifa letu. Taifa ambalo halitoi nafasi kwa
watu wake kutoa mawazo yao hadharani huwa linakaribisha manung’uniko ya chini
kwa chini ambayo ni hatari kwani yanapelekea watawala kutojua hisia halisi za
wananchi. Baraza Kuu linaitaka Serikali na vyombo na taasisi zake kujitathmini
upya juu ya wapi wanalipeleka Taifa.
Mwisho
No comments
Post a Comment