Header Ads

LightBlog

SERIKALI YATENDA UHALIFU KWA WANANCHI

Kufungia magazeti ni uhalifu dhidi ya wananchi na haki yao

SERIKALI inaendelea kufungia vyombo vya habari. Orodha inaongezeka. Mara hii ni zamu ya Mwananchi na Mtanzania.

MwanaHALISI lilifungiwa miezi 15 iliyopita (mwaka mmoja na robo). Hakuna dalili za kulifungulia. "Redio mbao" zinasema hata wamiliki wake wasiruhusiwe kuanzisha gazeti jingine. Limekuwa suala la binafsi.

Hatua ya serikali ya kufungia gazeti hilo imeathiri na inaendelea kuathiri waandishi, wake/waume zao na watoto wao; wazazi wao, ndugu waliowategemea, wauza magazeti, wenye maduka karibu na ofisi za gazeti hili, wauza matunda, mihogo, karanga, kahawa na kashata waliokuwa wakitua MwanaHALISI.

Wengi wameathirika hivyo kiuchumi. Sasa waandishi wamekuwa wabangaizaji kwa kuomba vibarua katika magazeti ya wengine. Wananchi wengi wameathirika kwa njia ya kukosa taarifa.

Mtu mmoja serikalini au kundi la watu; wanatumia nafasi zao kutaka kuua kwa njaa waandishi na familia zao; na kunyima wananchi taarifa muhimu zinazowawezesha kupata uelewa juu ya wanavyotawaliwa na jinsi ya kujinasua kutoka mkenge wa ghiliba, wizi na ufisadi.

Jana serikali iliongeza machungu kwa waandishi na wananchi na orodha yote niliyotaja hapo juu kwa amri ya kufungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania. Na serikali inajua. Hiyo siyo njia sahihi ya kutenda kazi. Serikali inaingilia kazi na majukumu ya mahakama.

Kwa ufupi, serikali inapuuza na kudharau mahakama. Kuna sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, katili kama ilivyo lakini bado inatumika na watawala ndio wameiweka mbelekoni. Kwanini serikali haiitumii kwa njia ya kwenda mahakamani? Inaogopa nini? Woga wake ni upi?

Kuna Baraza la Habari Tanzania (MCT). Limejaa na linashirikisha wataalamu wa nyanja muhimu katika tasnia hii - waandishi wa habari na wanasheria. Lina uwezo mkubwa wa kusikiliza na kutolea uamuzi malalamiko ya mtu au taasisi yoyote. Serikali hailitumiii.

Wahusika ndani ya serikali wanatumia ubabe wa amri kwa nia ya "kuua sisimizi kwa kutumia nyundo," lakini nje ya mkondo wa sheria au ushauri wa kitaaluma ambao unaheshimika zaidi kuliko amri au mitulinga.

Kesho serikali itazima gazeti au chombo kingine cha habari. Itaondosha ajira za waandishi. Itafinyaza fursa za kujiendeleza katika taaluma hii. Itanyakua haki ya uhuru wa kupata taarifa na habari. Itafanya kazi zake gizani na kwa hiyo bila mrejesho kutoka kwa jamii pana iliyokuwa inapata taarifa kupitia vyombo vya habari vinavyofungiwa.

Kufungia au hata kufuta chombo cha habari, licha ya kwamba ni kuvunja haki za binadamu; vilevile ni kuziba mifereji ya fikra ya jamii; kuongeza umasikini, kuasisi woga miongoni mwa watu, kujenga visima vya chuki na hasira dhidi ya serikali; kutaka watu waishi kwa umbeya na kurudisha jamii katika ujima.

Hatupendi kuamini kuwa haya yanatendwa na serikali inayojiita ya "kidemokrasia" na inayojigamba kuwa na uwazi na utawala bora. Hapana! Kuna serikali ngapi - moja itende demokrasia na nyingine itende uhalifu dhidi ya haki ya uhuru wa habari? Ghiliba!

Tumependekeza tangu 1985. Kwamba serikali iache wananchi na waandishi wa habari waiseme wanavyoiona. Kama sivyo ilivyo, basi ipuuze. Kama ndivyo ilivyo, basi ijisahihishe. Serikali ina maguvu mengi ya kutumia kuleta mabadiliko kwa maslahi ya watu; na siyo kwa kuangamiza uhuru wa kufikiri na kutoa mawazo.

Inakokwenda serikali, siko!

ndimara.

No comments

Powered by Blogger.