KLABU HAI YA WAANDISHI DAR
Klabu ya waandishi wa habari ya Dar es Salaam (DCPC) jana Jumatano (28 Agosti 2013) ilifanya warsha ya siku moja jijini katika Hoteli ya Peacock. Ilihusu utekelezaji shughuli zake chini ya kaulimbiu ya klabu nchini mwaka huu isemayo: Klabu ya waandishi wa habari ni nguzo ya maendeleo ya mkoa. Lifuatalo ni wasilisho la Ndimara Tegambwage aliyealikwa kutoa uchokozi.
SASA TUTENDE TUNACHOTAMANI
NINATAMANI kuwa na klabu ya waandishi
wa habari. Iwe ya kujenga umoja na ushirikiano wa waandishi katika eneo letu.
Iwe ya kutukutanisha wakati wowote, kwa jambo lolote linalohusu mwanachama,
klabu na taaluma.
Ninatamani kuwa na klabu ya waandishi
inayosimamia misingi ya taaluma kwa njia ya kuzingatia maadili. Inayohimiza
wanachama wake kusoma na kujisomea ili
kuongeza elimu, maarifa na stadi. Inayotafuta fursa za ndani na nje za
wanachama wake kupanua upeo wa fikra na utendajikazi.
Ninatamani kuwa na klabu ya waandishi
inayojifunza na kufunza wanachama wake mbinu za utendaji kazi na katika
mazingira anuai. Inayotafuta jinsi wanachama wake wanavyoweza kujiendeleza –
ndani na hata nje ya nchi. Inayotafuta fursa za kukuza na kuimarisha
ushirikiano miongoni mwa waandishi wa habari, klabu yao na wadau wa
habari.
Sina uhakika kama hii ndiyo klabu mliyonayo – Klabu ya Waandishi wa
Habari Dar es Salaam (KWAHADA).
Fursa za elimu na maarifa
Ninatamani klabu ya jiji kubwa la Dar
es Salaam, yenye fursa kedekede za elimu na maarifa. Penye wanataaluma wengi.
Penye sifa za kazi za viwango vya juu. Penye utajiri wa uzoefu. Penye wepesi wa
mawasiliano ya ndani na nje ya nchi.
Ninatamani klabu yenye mahusiano ya
kitaaluma na asasi kama vile Tanzania Media Fund (TMF). Ili ikuze uwezo wa
wanachama wake katika nyanja ya habari za uchunguzi. Ikuze stadi na hata kuibua
vipaji.
Natamani klabu inayoshirikiana moja
kwa moja na asasi kama vile Baraza la Habari Tanzania (MCT). Ili kuwa
mtekelezaji na msimamizi wa maadili ya kazi. Ili kulinda na kutetea haki ya
uhuru wa kuandika na uhuru wa habari.
Klabu yenye mahusiano na asasi za
ndani na nje zinazopigania umuhimu wa waandishi kujisimamia katika utekelezaji
wa kazi zao badala ya kushikiwa kiboko na watawala.
Sina uhakika kama hii ndiyo klabu mliyonayo.
Maktaba na Press Centre
Ninatamani klabu ya waandishi yenye makazi
maalum – Press Centre. Makazi yenye zana za kazi, maktaba na kituo cha vyanzo
maridhawa vya taarifa na habari, kwa matumizi ya waandishi wa ndani na nje ya
nchi.
Ninatamani klabu yenye utaratibu wa
kila wiki au kila mwezi wa kuwa na mgeni; kutoka ndani au nje ya nchi, kuhojiwa
na waandishi juu ya jambo muhimu la wiki au lolote muhimu walilochagua kwa
wakati uliopo.
Hii, licha ya kuwa chemchemi mpya ya
taarifa, itakuwa kiungo kati ya klabu na wadau wa habari – serikali,
waserikali, mashirika, kampuni, asasi, vyombo vingine vya habari na watu binafsi.
Hiki ni chanzo cha taarifa, lakini pia ni darasa.
Ninatamani kuwa na klabu yenye uwezo
wa kuandaa ajenda muhimu za kitaifa na kwa kushirikiana na klabu na wadau
wengine, kuzifafanua, kuzifuatilia, kuzipigania na kuzing’ang’ania “hadi
kieleweke.” Huu utakuwa mbadala wa kudonoa hoja na hata kuzika nyingine zingali
hai.
Ninatamani kuwa na klabu itakayokuwa
nguvu ya pamoja ya kufuatilia, kuhoji, kukemea na kukabiliana, kwa njia yoyote
ile, na lolote linalotishia uhai wa mwandishi mmojammoja; umoja wa waandishi
katika klabu, uhai wa klabu na uhai wa jamii tunayotumikia.
Sina uhakika kama hii ndiyo klabu mliyonayo. Niruhusu basi niseme kuwa hivyo
ndivyo vipengele vya malengo ambavyo tunahitaji kuwekea mikakati ya utekelezaji.
Klabu na maendeleo
Nimealikwa hapa kujadili mada isemayo,
“Klabu ya Waandishi wa Habari ni Nguzo
ya Maendeleo ya Mkoa.”
Binafsi sioni mkoa haraka. Ninaona mtu
katika kaya, mtaa, kitongoji, kijiji, kata na wilaya. Mtu. Huyu ndiye anapaswa
kutumikiwa ili kuleta mabadiliko katika maisha yake. Na mabadiliko ndiyo
maendeleo.
Kwahiyo, tunapojielekeza kwenye mkoa,
tunalenga kushawishi wasimamizi wa “muungano wa tawala za wilaya” na wataalamu
wao – kuona umuhimu na uhalali wa kuwa karibu na klabu ya wanahabari ili
kufikia na kuhudumia yule ambaye ni tofali la kwanza kwenye mwili wa jamii: Mtu
mmoja.
Ni wazi kwamba bila taarifa na
habari, kunakuwa na utupu usionawirisha ubongo. Kile kitekenyi cha mabadiliko
kwa njia ya kufikiri kinachotokana na mlisho wa taarifa sahihi, kinakosekana au
kinatoweka.
Jukumu la wadau
Kwahiyo, wadau wa habari – watawala
(serikali mkoani), watendaji wake, wafanyabiashara wakubwa, mabalozi wa nchi
mbalimbali, wananchi kwa ujumla wao – wana nafasi ya kushiriki ujenzi na
uimarishaji wa klabu. Baadhi ya serikali duniani (ikiwemo ya Sweden) hutoa
ruzuku kwa vyombo vya habari makini, siyo kwa kuvihonga, bali kuviwezesha kuwa
chokonozi zaidi, makini zaidi na kufikia jamii pana.
Kuna njia nyingi za wadau kushiriki
kujenga klabu ya waandishi wa habari Dar es Salaam. Hapo awali nimejadili kazi
za klabu kuwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wanachama wake ili kuongeza elimu,
maarifa na stadi. Utendaji bora unaundwa na kunawirishwa kitaaluma.
Kwahiyo, njia za wadau kushiriki kujenga
na kuimarisha klabu ya kudumu ya Dar
es Salaam, kwa manufaa ya mkoa na taifa, ni pamoja na kuiwezesha kuwa na makazi
ya kudumu, ya hadhi ya jiji (vikiwemo vifaa); kuwa na mfuko kwa ajili ya
mafunzo ya nyongeza kwa waandishi; na kuhiari kutoa taarifa kwa waandishi pindi
wanapowaendea.
Mwandishi ni mtafutaji. Ni
mfuatiliaji. Ni mwanikaji wa alichovuna kwa ajili yako na jamii kuona, kujua na
kunufaika. Anatafuta taarifa. Wewe unazo. Mpe. Ameona utekelezaji wa mipango yenu
una walakini. Anakuomba maelezo. Mpe. Amenusa wizi/ufisadi ofisini mwako. Anakuomba
maelezo. Mwambie.
Mwandishi ameona mafanikio au kukwama
katika ofisi, kampuni au shirika lako na anataka kujua siri ya hilo. Mweleze.
Una jambo la kuwasilisha kwa umma. Mpe. Kwa njia hii, wewe na yeye mtakuwa mmeshiriki
kuleta au kufanikisha maendeleo.
Hitimisho
Tukiwa na klabu ya waandishi wanaothaminika
kwa kazi, watendaji watajihisi kuwa na “mchungaji” begani mwao. Maadili
hukamilishwa na uchungaji unaoanika matendo ya wenye madaraka. Baya ambalo
wangefanya wataliacha. Wataamka saa nane usiku kutoa taarifa za umma.
Watendaji watafungua mafaili kwa
mwandishi kupata usahihi. Watakemea ofisa anayeficha taarifa. Watatonya
waandishi kipi kinakwenda ovyo. Wataumbua waandishi wanoomba rushwa. Lakini wakificha
taarifa hawatasikitika pale watakapozikuta ukutani.
Je, kwa haya na yote tuliyoorodhesha hapo awali, tuanzie
wapi? Tuanze lini? Tuanze na lipi? Kazi kwenu.
Mwisho
*Ndimara
Tegambwage ni mwelekezaji (mentor) katika habari na mawasiliano. Simu: +255
713614872
imeili: ndimara@yahoo.com; blogu: ndimara.blogspot.com (uhuru hauna
kikomo…) Inapatikana pia kwenye: www.facebook.com/ndimara.tegambwage/
No comments
Post a Comment