Header Ads

LightBlog

JE, KIPO CHA KUSIKILIZA?


 Dhana na Umuhimu wa Utangazaji
kupitia Vyombo vya Habari vya Umma

Maadhimisho ya Siku ya Utangazaji Duniani yaliyoandaliwa na Baraza la Habari tanzania (MCT) kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam, 13 Februari 2013

UCHOKOZI: Na Ndimara Tegambwage

Utangulizi
Utangazaji kwa njia ya “vyombo vya habari vya umma” ni moja ya mijadala muhimu katika tasnia ya habari duniani. Kwa mfano, ni chombo cha umma au ni chombo kinachotangazia umma? Je, chombo chochote kinachotangazia umma siyo chombo cha umma?

Je, mmiliki wa vyombo vya habari – redio na televisheni – ambavyo vipindi vyake vinatangazia wasikilizaji wengi, hana vyombo vya umma? Utamkataza kuviita vya umma au utashawishi wasikilizaji wasiviite vya umma?

Je, haiwezekani serikali kuwa na vyombo vya utangazaji “vya umma visivyo vya umma?” Au, basi tukubali kuwa vyombo, hata kama vitatangazia umma mpana, viitwe tu vyombo vya habari vya utangazaji KWA umma; lakini siyo vya umma?

Mijadala juu ya yote haya haiwezi kuitwa “manenomaneno tu.” Hapana. Ni hoja nzito. Bali leo, kwanini tusijikite katika “miliki” – vyombo vya habari vya utangazaji vinavyomilikiwa na umma. Na hapa, kwa nchi, umma uwe ujumla wa wananchi wote.

Kwa mkondo huo, tunaweza kuwa na vyombo vya habari vya watu binafsi vinavyofikia umma mpana, bali havimilikiwi na umma huo – hata kama vipindi vyake vitakuwa vinatoa maarifa, vinachochea hisia za kitaifa na kitamaduni, vinafikirisha, vinaliwaza, vinajenga ujasiri katika maisha; au tuseme tu kwamba vinapendwa na kushabikiwa.

Ni katika mazingira haya pia tunaweza kuwa na vyombo vya habari vya utangazaji vinavyomilikiwa na umma; lakini havifanyi kazi bora kuliko vile ambavyo vinamilikiwa na watu binafsi.

Mwelekeo wa mijadala
Hebu tujikite katika mkondo wa mantik][ ya vyombo vya utangazaji vya umma iliyozoeleka. Hivi haviwi vya umma mpaka viwe vinaendeshwa kwa kodi za wananchi.

Hivi ni vyombo vinavyopaswa kuwa na mipango ya kujiendesha iliyo wazi na inayoeleweka; vyenye bajeti zinazotosheleza mahitaji ili visiyumbe na hatimaye kutafuta ufadhili ambao unaweza kuangamiza maadili na uhuru wake.

Ni vyombo huru ambavyo havistahili kukwazwa na yeyote – awe mkurugenzi mkuu wake, katibu mkuu wa wizara, waziri, rais au serikali. Havistahili kubanwa kwa shinikizo za kisiasa au za kibiashara; au kutegemea serikali imeamkaje au uchumi wa nchi umelalia upande gani.

Ni vyombo vinavyopaswa kusikika karibu na mbali; na kufikia idadi kubwa ya wananchi, kama siyo walipakodi wote – wazima na wagonjwa, masikini na tajiri, mijini na vijijini, nyumbani na makondeni.

Yote haya ni kutaka kuhakikisha kuwa ile kodi ya wananchi inatumika kujenga na kukuza fursa zao za kupata taarifa za ndani na nje ya nchi; fursa za kupokea mawazo mbalimbali; fursa za kutoa maoni bila woga na kuwezesha wasikilizaji kuanzisha na kushiriki mijadala inayohusu maisha na mazingira yao; na mijadala mingine iliyo mbali na uso wao.

Hivi vitakuwa vyombo vya habari vya utangazaji ambavyo vipindi vyake vitalenga kugusa makundi yote – kijamii, kichumi, kielimu, kisaikolojia, kiutamaduni na kukuza uelewa hata katika elimu ya uraia na elimu kwa wapigakura.

Vyombo vya umma vinavyogharimiwa na umma kwa njia ya kodi vinatarajiwa, moja kwa moja au ndani kwa ndani katika vipindi vyake kuonyesha, pamoja na mambo mengine, wajibu wa watawala na watawaliwa, umuhimu wa umoja wa taifa na haki kwa kila mmoja ili amani iweze kutawala.

Tunajadili vyombo vya habari vya umma ambavyo tungepende kuona vinawajibika kwa Bunge na siyo kwa serikali; vile ambavyo uhusiano wake na serikali sharti uwe wazi kwa kila mmoja kuona na kutathimini.

Tukumbushane basi hapa, kwamba tunajadili vyombo vya umma na siyo vya serikali. Hivi ni vyombo vilivyo chini ya shirika/taasisi moja iliyo huru na iliyoundwa rasmi kisheria ili kuvisimamia na kuhakikisha kuwa vinabaki katika uhuru uliotarajiwa ili viweze kutoa taarifa na habari za kweli, uwazi na bila kuingiliwa na serikali.

Serikali haina fedha. Serikali inakusanya kodi za wananchi. Hivyo miliki ya serikali siyo lazima iwe miliki ya umma, hata kama ilitakiwa kuwa hivyo. Mara nyingi, kutokana na upungufu mkubwa kiutendaji na maslahi binafsi ya viongozi ndani ya serikali, hutokea serikali ikaogopa vyombo vya habari, hata vile inavyomiliki; hivyo kuhamisha au kufukuza watendaji wake wakuu, kukemea waandishi na kutishia kuwafukuza kazi au kuwafukuza moja kwa moja.

Leo hii, wakati tunaadhimisha siku ya redio; siku ya utangazaji duniani, tunahitaji kuangalia mbele na kuona tunahitaji vyombo vya aina gani ambavyo wananchi wataridhia vitumie jasho lao na kwa manufaa yao.

Vyombo visivyofungwa wala kufungiwa na polisi au rais. Visivyozuiwa na jua wala mvua. Visivyosita kutamka shibe wala njaa. Visivyoona aibu wala woga kutaja mwizi, fisadi wala muuaji; awe kabwela au mkurugenzi wa kampuni kubwa au waziri au hata rais. Vyombo visivyoita usiku mchana na mchana usiku.

Najisikia kupendekeza hapa pia kuwa hivi ni vyombo vya habari vya umma vitakavyosheheni waandishi wa habari wenye weledi wa hali ya juu; wanaojitahidi kupata maarifa zaidi kila siku na wasiohongeka. Vyombo vyenye viongozi ambao kwao, woga na upendeleo ni misamiati, tabia na vitendo vilivyofutwa zamani katika kufikiri na kutenda kwao.

Changamoto za “kuunganisha mafundo”
Tumeona awali kwamba hata wenye vyombo ambavyo haviendeshwi kwa kodi za wananchi moja kwa moja, wanaweza kusema wana vyombo vya umma kwa kuwa wanafikia idadi kubwa ya watu.

Wapo, ingawa ni wachache, wanaokuja na hoja kuwa mali zao hazikudondoka kutoka mbinguni; ni makusanyo ya humuhumu kwa jasho la watu wa humuhumu na ulinzi wa jamii ya humuhumu. Kwahiyo fedha zao za kuendeshea vyombo hivyo, ni kama kodi za wananchi zilizolipwa kwa njia nyingine nyingi “zisizoonekana waziwazi.”

Hebu tukubaliane nao. Baada ya hapo tujenge misingi mingine ambayo inapaswa kuonyesha tofauti kati ya chombo cha mtagazaji mfanyabiashara na mtangazaji wa umma.

Lengo kuu la chombo kinachoendeshwa kwa kodi za wananchi linapaswa, au hakina ni kumfikia kila mwananchi bila kujali hadhi yake kijamii au kimapato. Msingi huu unazingatia usawa katika matumizi ya chombo cha umma na unashawishi kuwemo basi, vipindi mbalimbali vinavyogusa wamiliki kwa ngazi zote.

Msingi mwingine ni kuwa chombo huru ambamo waandishi watakuwa huru na ambamo sauti za wananchi –   mawazo yao, hata yanayogongana na kukosoana, yatapata nafasi ya kusikika na kujadiliwa. Hili ni moja ya mambo ambayo yatahalalisha uendeshaji wa vyombo hivi kwa kodi za wananchi.

Ni uhuru huu pia na kuonekana kwa walipa kodi kutumia vyema vyombo vyao, ambako kutadhihirisha uhuru wa vyombo vyenyewe. Lakini kama hayo hayakusikika wala kuonekana; na badala yake wakaona na kusikia viongozi tu wa serikali na wanasiasa, basi watapoteza imani katika vyombo husika. Vinaweza kufa.

Kuna upekee. Vyombo vinavyoendeshwa kwa kodi za wananchi vinapaswa kuonyesha upekee wa aina yake na ikibidi viwe mfano kwa vyombo vya wengine vya kibiashara. Vyombo vya wananchi vinapaswa kutekenya makundi yote katika jamii; kufika kunakosuswa, kuongea na waliodharauliwa na kuwapa sauti, kustua waliobweteka; kuleta vipindi vinavyowagusa na kuwashirikisha na kukutana na serikali kwa shabaha ya kupata hoja na majibu yake kwa yale ambayo vyombo vimekusanya.

Ni upekee huu ambao hata vyombo vya kibiashara vinaweza kuiga na hata kudandia kufikia umati ambao tayari umefikiwa na vyombo vya utangazaji vya wananchi.

Vyombo vya wananchi vina fursa ya kuwa na ujasiri wa  kueleza madai na matakwa ya wamiliki, kutetea maslahi yao; na siyo uzandiki na mbambikizano wa matangazo ya kila aina ya biashara – mkondo ambao unaweza kuzamisha dhamira ya vyombo na kufinyaza hamu ya kutumikia wamiliki – umma wa walipakodi.

Hitimisho
Mwalimu wangu alikuwa akipenda kusema na kurudia mara kwa mara darasani kuwa, uhalali wa vyombo vya utangazaji vya wananchi ni kutoa huduma kwa wananchi. Kwani vipindi vyake hukuza maarifa, hupanua upeo na kuwezesha wananchi kujielewa vema na kuelewa vema wengine duniani kote. Nilikubaliana naye. Nakubaliana naye leo.

Kumekuwa na tatizo la wananchi wengi kutofikika hata pale ambako kuna vyombo vinavyoendeshwa kwa kodi zao. Hawana televisheni. Hawana redio, hata zile ndogo za mikononi. Hawana wa kuwahimiza kununua redio hizo haswa pale ambako televisheni haishikiki au haionekani.

Ili ujumbe ufike, kutangaza tu hakutoshi. Kusikiliza na kusikilizwa ni muhimu ili kuwe na taifa linaloongea. Linalojadiliana. Linalotoa mawazo. Linalofanya maamuzi. Taifa linalofanya siku ya utangazaji duniani iwe ya maana.

Je, tuwe na kampeni nchi nzima za kuhimiza wananchi kununua redio? Nani atafanya kazi hii? Kuwepo msukumo wa kuunda vyama vya wasikilizaji? Kuwepo vituo vya kusikilizia redio na kutazama televisheni? Je, kuna cha  kusikiliza ambacho kinagusa matakwa ya wasikilizaji moja kwa moja na kinaweza kuwa motisha wa kununua redio?

Tanzania inasimama wapi? Tunavyo vyombo vya habari vya utangazaji vya umma? Viko wapi? Vinafanya nini? Ni vile vinavyotangaza habari za viongozi mpaka waishe kwa mpangilio wa rais, makamu wa rais, waziri, katibu mkuu, mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, mtendaji kata au shehia na mwenyekiti wa mtaa au kitongoji?

Tunayeshawishi kununua redio atasikiliza nini kama sauti yake haijawahi kusikika akisema ana kiu, ana njaa, anataka msaada? Atagharimia vipi na kwanini agharimie chombo ambamo hawezi, hata siku moja, kusikika akisema nimeshiba au nimefurahi au nimesikitika.

Asanteni!





https://www.facebook.com/ndimara.tegambwage

No comments

Powered by Blogger.