Header Ads

LightBlog

KAMA SERA YA ELIMU HAIPO TUWASAIDIE KUIANDIKA

Mwendelezo kwa andishi la Richard Mabala juu ya usiri wa serikali kuhusu mitaala ya elimu (mtandao wa MABADILIKO Tanzania) lenye kichwa 'siri ya sera.'

siri ya sera au sera ya siri?

makengeza acha utani!
unachezea intelijensia?
makengenza acha mizaha;
hutaki wanaona mbali
yao nchi kulinda?
huoni wenye uchungu
walindao siri za nchi;
wale wenye uchungu
kuliko uchungu wenyewe
kwa yao nchi tamutamu?

mwalimu umesahau?
ukiandika unarithisha
ukiandika unafikirisha
ukiandika unagawana
ukiandika unazidisha
ukiandika unaongeza
lakini pia unatoa;
nani atakukubalia?

kwa intelijensia yao
andiko linatishia
heri amri mdomoni
kuliko neno karatasini
heri kauli yeyuki
kuliko andiko shahidi
kila ajaye, kila aondokaye
mtaalawe kichwani kufungia.

makengenza kumbuka:
waziri: futa michezo shuleni
muda wa kusoma waibwa
waziri: achana na historia
inakumbusha maasi
waziri: achana na kiswahili
hakitaleta ajira
waziri: asilimia 30
zatosha kuwa mshindi.

kesho waziri mwingine:
waziri: historia muhimu
watoto wetu wajue
waziri: kiswahili lazima
hii lugha ya taifa
waziri: michezo ya jenga mwili
na akili kukuza;
kila shule na viwanja
waziri: somo moja kitabu kimoja
wanafunzi tusikanganye.

kila anayekuja
ana chake mfukoni;
kilichoduni ndu!
kilichobora ndu!
mawaziri ndio sera
mawaziri ndio mitaala;
nyuma yao "kidumu"
katika ujinga ndindindi!

walimu wakinge sikio
waambiwacho ndicho;
wanafunzi wakariri
kile wanachomegewa
cha kuvuna kiduchu
shule vinyamkera.

anayepita kapita
hata kwa mtihani wa sokoni;
anayekwama kakwama
hata awenazo za kufikiri
tunasubiri takwimu
waloshinda walofeli
uoza kutamalaki
si la kwanza, si la kuminanne
si chuo kikuu peke yake:
hata katika ajira
maofisini, viwandani, biasharani.

tumleeje huyu kinda
tumpe yapi mazingira
aweze kukua na mwanga?
tumpe vipi vianzio
kujenga nguzo za kufikiri.
kuta za ujinga kubomoa
na maarifa kukusanya?
kama mitaala ni siri
kila mmoja afanya vyake;
ni ngoma ya gizani
haina mtazamaji.

makengenza endeleza hapo
tunapojenga msingi:
tuendapo sekondari
ya kwanza na ya pili,
tufikapo kwenye vyuo
tudaiko utaalamu,
bila mwongozo ni nini
kama siyo gombesugu?

intelijensia ya watawala
yaona kujua ni siri
walojua zamani
haohao wanatosha;
kujua zaidi ya hao
ni kutafuta "vurugu;"
vuta hivyo walivyo
mradi kuimba wajua!

tukinyamaza twafa
sisi leo na wengine kesho
uzao wote twazika
kama woga utatukumba;
tukisimama twaweza
kauli kutoa, vitendo kuonyesha
na msingi kujenga!

mitaala siyo siri
tuidai, tuipate!
kama haipo
basi tuchangie kuitunga.

ndi.


Angalia pia:: facebook: ndimara.tegambwage

No comments

Powered by Blogger.