Header Ads

LightBlog

Nani watalinda bomba la gesi?Gesi ya Mtwara na 
ubabe wa serikali

Gesi ikipatikana Mtwara, isombwe hadi Dar es Salaam ili izalishwe nishati ya umeme. Ikipatikana Tanga, ipelekwe Dar es Salaam. Ikipatikana Kigoma sharti pia ipelekwe Dar es Salaam. Huu ni ukame wa akili. Lakini ukame huu siyo wa leo. Kuna wakati watawala na watendaji wao nchini waliwahi kuishiwa akili kama ilivyo sasa. Ni nyakati zile nilipoandika kitabu kiitwacho “Duka la Kaya” – unyafuzi wa akili usiomithilika!

Sukari itazalishwa Kagera. Itasombwa na kupelekwa Dar es Salaam. Ile ya Mtibwa, Morogoro itapelekwa Dar es Salaam. Ile ya Moshi itapelekwa Dar es Salaam. Kutoka Dar es Salaam wataandaa kile walichoita “mgao” au “mgawo.” Sukari itasombwa kutoka Dar es Salaam kurudishwa kijiji jirani na kiwanda cha sukari Kagera, Mtibwa na Moshi. Ni ukame wa akili na wizi usiovumilika, vilivyodhihirika miongoni mwa wanasiasa na watendaji.  Yalikuwa matusi ya aina yake kwa wasomi na usomi wao.

Nenda Morogoro. Angalia viwanda vilivyolundikwa mjini Morogoro wakati waziri wa viwanda alikuwa pia mbunge wa Morogoro – Amir Jamal. Pale waliweka hata kiwanda cha ngozi huku wakijua vema kuwa kiwanda kama hicho kingewekwa maeneo ya wafugaji – kwenye ngozi nyingi – Mwanza, Shinyanga na Umasaini; wakaweka kiwanda cha tumbaku huku wakijua kiwanda kingekwenda Tabora ambako wanalima asilimia 60 ya zao hilo. Angalia na vingine. Ni makengeza ya makusudi alimradi muhusika amepindishia kwake au kwao.   

Ujuha huu wa kiuchumi ni ghali sana. Siyo ghali kwa wanaoupanga na kuutekeleza – kwani wao ndio wanufaikaji wakuu wa mipango, mbinu na mikakati – bali kwa wananchi ambao wangenufaika angalao na hicho kidogo kinachosalia. Lakini ni mipango ya “potelea mbali;” mipango ya “watakaokuja baadaye watatafuta vyao;” mipango ya “chukua chako mapema.”

Kwani umeme ukizalishwa Mtwara, penye gesi, hauwezi kusambazwa nchi nzima? Ukizalishwa popote pale nchini hauwezi kufikishwa unapohitajika; ni mpaka gesi italii ndani ya mabomba, ifike Dar es Salaam ndipo umeme upatikane?

Kwa wenye nia safi na waliodhamiria kuleta mabadiliko kila sehemu ya nchi hii, kugundulika kwa utajiri (maliasili/raslimali) pale wanapoishi, sharti kuchochee akili mpya; siyo ya kuhamisha utajiri huo, bali kuutumia hapo ulipo ili kubadili maisha ya wenyeji na kuondoa hadithi za kisiasa za “tutawaletea” wakati hakika “tunawanyang’anya” utajiri, maendeleo, mabadiliko.

Tunaweza kujiuliza: Kuna nini katika usafirishaji gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam badala ya kuzalisha umeme palepale Mtwara na kuusambaza kwingine? Jibu la haraka ni swali hili: Kulikuwa na nini katika kuchukua sukari kutoka viwanda vya sukari (Kagera, Mtibwa na Moshi) hadi Dar es Salaam na baadaye kuirejesha huko ndipo iuzwe kwa wananchi katika vijiji jirani na viwanda; tena mara hii kwa bei ya juu zaidi! Ni njia nyingine ya kuongeza gharama ambayo hailipwi na watunga “dili” bali wananchi; ni njia nyingine ya ukwapuaji. Ni wizi.

Kama nilivyowahi kuandika kwa njia hii, wananchi wa Mtwara hawataki kupewa gesi katika makopo, vikapu, madumu na chupa; bali wanataka angalao, kufanana na wanaoishi karibu au katikati ya utajiri wao na nchi yao. Njia pekee ya kufanana au hata kuwa hivyo; na inayowezekana mara moja, ni kuzalisha umeme kutoka gesi ya Mtwara, hapohapo Mtwara.

Historia imetuonyesha, siyo tu Tanzania na Afrika, bali hata nje ya bara hili, kwamba pale ulipopatikana utajiri wa maliasili, wananchi wakazi wamekumbwa na adha ainaaina. Badala ya neema imekuja balaa. Nchini hapa, kuhamishwa kwa nguvu, kutopewa fidia, kuuawa, kulemazwa kwa risasi za moto, kunywa maji yaliyoingia sumu kutoka migodini na umasikini usiomithilika hatua 10 tu kutoka kwenye uzio wa mgodi, yote haya yamekuwa balaa la aina yake.

Kama kwamba haitoshi, serikali haionekani kufanya lolote kulinda na kuhifadhi watu wake. Inachofanya ni kuendelea kugawa kwa kampuni za nje, maeneo zaidi ya kuchimba madini na hivyo kuhamisha wananchi zaidi na kufukarisha maelfu kwa maelfu. Sasa kampuni za kuchimba madini zimeanza kuingia ubia na polisi mikoani ili ziweze kulindwa “dhidi ya wananchi” ndani ya nchi yao. Hao ndio polisi wanaodaiwa kuwa walinzi wa raia na mali zao! Kama mali ya raia imeishachukuliwa au kuharibiwa na polisi yuko upande wa tajiri kutoka nje ya nchi; uko wapi usalama wa raia na iko wapi mali yake? Tumebakiza nini kama siyo kuuza mioyo yetu!

Mtwara wana ujumbe mfupi na unaoeleweka. Wanasema zalishia umeme hapa. Toa umeme hapa na peleka kwingine. Elekeza wawekezaji kwenda Mtwara au chochea wakazi wake kuzalishia bidhaa Mtwara kwenye gesi na umeme. Hili lina maana pana kwa wakazi wa Mtwara.

Sikilizeni mkazi wa Mtwara. Albert Msosa, fundi bomba anayeishi mjini Mtwara anasema, pamoja na mengine mengi, kuzalishwa kwa umeme kutokana na gesi hapo Mtwara kutachochea fikra juu ya matumizi ya umeme maishani mwao; kutakuwa moja ya vichocheo vya wananchi na hata watu kutoka nje kwenda na kuwekeza kwa njia ya viwanda; kutachochea kuibuka kwa viwanda vidogo na vya kati; kutaondosha uwezekano wa kufanya wakazi wa Mtwara kuwa kolokoloni wa kulinda bomba la gesi; kutazalisha ajira kwa watu wengi zaidi.

Huyo ni fundi bomba. Wengine wa viwango tofauti vya elimu, maarifa na uelewa wanasemaje? Serikali ya Rais Jakaya Kikwete iwasikilize. Aliyeumwa na nyoka hukimbia mjusi au hata kamba gizani. Yaliyowakumba North Mara, Bulyanhulu, Geita, Nzega, Buzwagi na kwingineko ambako utajiri ulitengwa haraka na wamiliki wao wa asili, yanatishia pia uhai wa wakazi wa Mtwara. Hicho ndicho chimbuko la  kilio chao!

Picha: Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini

Soma: www.facebook.com/ndimara.tegambwage

No comments

Powered by Blogger.