KATIKA JINA LA HAKI
Miswada ikienda kimyakimya
watapitisha kanyaboya, tutalia
Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, waandishi wa habari nchini
Tanzania wamekuwa wakitaka serikali kuwasilisha bungeni miswada miwili ya
habari. Hii ni miswada iliyotokana na juhudi kubwa ya waandishi wa habari,
marafiki wa habari, wanaharakati ainaina wanaopigania uhuru wa habari na
wananchi – makundi na mmojmmoja – kwa shabaha ya kujenga mazingira bora ya haki
na uhuru wa kukusanya, kupewa na kutawanya habari. Ni kazi nzuri ambayo
serikali imekalia kwa kipindi chote hicho.
Sasa kuna kinachoonekana kuwa juhudi za kuwataka wabunge kujadili
kwa kina “miswada hiyo” ya habari na kuipitisha. Lakini kuna haja ya kujiuliza
kwanza: Ni miswada ipi wanataka wabunge wajadili na kupitisha?
Kilichopelekwa serikalini kutoka kwa wadau wa habari, ni
mapendekezo. Serikali imeyakalia kwa miaka yote hiyo chini ya mawaziri watatu –
anatoka huyu anaingia huyu – bila kuyafanyia kazi. Hatimaye tumeanza kusikia
serikali ikisema, kupitia wasemaje wake wanaojikanganya kwa tarehe za
kuwasilisha bungeni, kuwa itapeleka miswada hiyo bungeni.
Utaratibu ni kwamba serikali inasoma mapendekezo. Inafanya
maamuzi. Inapeleka mapendekezo kwa mwandishi mkuu wa sheria ambaye anaumba
maoni na hoja za serikali katika sura ya muswada wenye mwelekeo wa mapendekezo
ya wadau wa habari. Tuko pamoja?
Hapa ndipo kuna kazi. Serikali inaweza kuazima na kutumia maneno
yaleyale yanayotumiwa katika mapendekezo ya wadau lakini ikaja na “moyo tofauti
wa sheria” katika maumbile mapya yanayopelekwa bungeni.
Ninajua kuna wanaoamini serikali kwa asilimia 100/100. Lakini
naomba kuwakumbusha mapendekezo ya muswada wa mashirika yasiyo ya serikali.
Tuliumba kitu chetu. Tukaipa serikali. Ikachukua. Ikapongeza. Ikampa mwandishi
wa sheria. Kilichotoka humo ni kibaya zaidi – katili, nyakuzi, ning’inizi na
hatarishi kuliko hali ilivyokuwa kabla ya sheria.
Ikitokea hivyo katika miswada ya sheria, serikali itasema: “Walitaka
sheria, tukawapa sheria; sana wanalalamikia kitu gani?” Tutagota upya.
Hoja:
Kama serikali inasema ipo tayari kupeleka miswada ya habari bungeni; basi kwa
nia njema ifanye hivi: Iweke wazi miswada hiyo kwa waandishi wa habari, wadau
wa habari na wananchi; waisome, waijadili, wailinganishe na mapendekezo ya
wadau wa habari, waijazie (kama itahitaji kujaziwa), wapendekeze mengine –
mapya au ya awali yaliyonyofolewa, kabla ya kuiwasilisha bungeni.
Hili ni muhimu sana. Lisipofanyika, serikali itawaambia
wabunge, “Hiki ndicho wadau wamekuwa wakidai. Tunaomba muwapitishie.” Ni
wabunge wachache watagundua tofauti au ghiliba; na hao wachache hawatazuia
miswada kupitishwa. Tutarudi palepale – kubishana na kuzozana na serikali na wa
serikali.
Katika jina la haki, miswada ya serikali iwekwe wazi kwanza;
tuione, tuisome, tuijadili na kuijazia. Na kama serikali ingekuwa ya uwazi, kwa
kipindi chote tangu ikabidhiwe mapendekezo, ingekuwa imeumba miswada yake,
kuiweka mbele ya umma kwa mjadala na kupata miswada muwafaka. Haikufanya hivyo.
Sasa yaweza kuleta bomu litakaloua hata chembechembe za kilichokuwepo na
kilichotupa fursa ya kudai haki ya habari.
see also ndimara's facebook
No comments
Post a Comment