Kufungia gazeti: Ni woga, ubabe au ulimbukeni?
MwanaHALISI: Nusu mwaka kifungoni
'Kwa kufunga gazeti wamewaweka pia wasomaji gerezani popote walipo'
LEO ni siku 172 tangu serikali ifungie gazeti la
MwanaHALISI “kwa muda usiojulikana.” Siku hizo ni sawa na miezi mitano na siku
22 au miezi sita kasoro siku nane. Ni nusu mwaka.
Kwa muda usiojulikana maana yake ni mpaka serikali
itakapotaka (yenyewe). Itakapojisikia. Itakapofurahi. Itakapopigiwa magoti na wamiliki
wa gazeti. Itakapoombwa na marafiki wa gazeti. Itakaposhinikizwa vya kutosha na
wapigania uhuru wa habari.
Kwa muda usiojulikana yaweza kuwa pale viongozi wa
serikali waliofungia gazeti watakapotembelewa na akili na uelewa kuwa
hawapaswi/hawakupaswa kuingilia uhuru wa kupata, kutafuta na kukusanya habari;
au pale serikali itakapoamuliwa na mahakama; au wenye gazeti watakapoamua kulichapisha
kwa mapenzi ya wananchi bila kujali serikali inasema nini. Hilo nalo
linawezekana.
Nusu mwaka. Serikali inayojidai kutenda na kulinda
haki za raia wake imeamua kuwa wafanyakazi wa gazeti la MwanaHALISI wawe
ombaomba mitaani; au wasambaratike kwa kuhama kampuni au wafe kwa njaa – potelea
mbali! Kama hii ndiyo haki, basi ni haki ya mashetani.
Imekuwa safari ndefu – nusu mwaka – lakini
iliyojaa karaha na kinyaa. Hapa kuna serikali inayojigamba kutawala kwa
“misingi ya demokrasia;” lakini ni serikali hiyohiyo inayotaka kutawala gizani
– kishirikina; na inayonyakua uhuru wa wananchi wake wa kutoa, kupata na
kusambaza taarifa na habari.
Hapa kuna watawala wanaojigamba kuwa wakweli na wawazi
lakini wanaficha hata kilichowazi kwa kila mmoja. Wanafungia gazeti kwa nia ya
kuua jicho la nyongeza la jamii; kuziba sikio la nyongeza la jamii na kusiliba
mdomo wa nyongeza ya jamii. Wanataka jamii mfu – isiyoona uoza, isiyosikia
mipango ya “uhaini” dhidi ya jamii na isiyotoa kilio cha wengi.
Kufungiwa kwa MwanaHALISI kulisononesha nyoyo; kukazika
shauku, kukanyakua maarifa, kukapora uhuru na kukaondoa mategemeo. Watawala wanajua
lakini hawajali.
Hili ni gazeti lililofungiwa wakati habari kuu
katika vyombo vyote vya habari nchini ilikuwa “Utekaji na utesaji wa Dk. Steven
Ulimboka.” Kufungiwa kwa gazeti, katika mazingira haya, tena kwa muda
usiojulikana, kulionekana kwa wasomaji wake, wafuatiliaji na wachunguzi kuwa
njia ya kuzima mifereji ya ukweli iliyokuwa ikielekea kumwaga ushahidi mwanana
katika macho na masikio ya wasomaji wake.
Funga! Ili lisiandike habari nyeti juu ya unyama
aliofanyiwa kiongozi wa madaktari katika kudai vitendeakazi na mazingira bora
ya kazi. Funga! Lisifumue taarifa za nyongeza na mkondo wa mawasiliano. Funga!
Ili lisiendelee kuumbua wahusika – kuanzia waliobuni “mradi” hadi
waliotekeleza. Funga! Ili dunia nje ya Tanzania isije kujua unyama unaohusishwa
na serikali.
Leo, kama ilivyokuwa siku ya kwanza ya siku 172 za
kifungo cha MwanaHALISI, ninaendelea kukubaliana na wasomaji, wafuatiliaji na
wachunguzi juu ya sababu za kufungiwa kwa gazeti: Kuingiza taifa gizani ili
lisiweze kuona masuala muhimu ambayo gazeti hili limekuwa likiibua.
Kinachosikitisha ni kwamba watawala, kwa upofu
wao, katika suala la Ulimboka, hawakuona kuwa gazeti lilikuwa linatoa taarifa
za ndani na za kweli ambazo zingesaidia serikali kujiondoa katika tope la
“kutaka kumuua Ulimboka.”
Watawala walishindwa, labda kwa kiwewe tu,
kueleawa kuwa taarifa za ndani na za kina zingeonyesha muhusika mmoja na siyo
serikali yote wala ikulu yote. Hawakuona kwamba taarifa za kina zingesafisha
hata Usalama wa Taifa na Polisi – ambao ndio walikuwa wanatungwa kidole.
Kwa vipi? Ikulu siyo pango la wauaji. Ni makao
makuu ya mtawala wa nchi. Haitarajiwi kuwa makazi ya watekaji, watesaji au
wauaji. Kwahiyo, kama ikulu kuna mtuhumiwa mmoja, watawala wana haki na sababu
ya kuachia wanaojua kazi kuwasaidia kufichua nani anachafua heshima na uhalali
wa ikulu.
Vivyo hivyo kwa usalama wa taifa. Hawanabudi kukaa
kitako na hata kuomba msaada wa nyongeza kutoka kwa wanaojua kazi yao, ili
kufichua wanaotaka “kuharibu sifa” zao. Kwani, kazi ya usalama wa taifa siyo kuteka, kutesa na kuua.
Anayefanya hayo sharti awekwe wazi ili chombo hicho kibaki kikiaminiwa. Vivyo
hivyo kwa jeshi la polisi.
Mvumo wa taarifa za gazeti ambao ungetunga wahusika
mmojammoja kama shanga katika “sakata la Ulimboka,” ungenusuru ikulu, usalama
wa taifa na polisi. Hapo ndipo ukweli na uwazi ambavyo vinaimbwa, vingesaidia
serikali kuondokana na uchafu unaoweza kuiondolea imani ya wananchi na uhalali
wake.
Tumekuwa tukiiambia serikali, tena mara nyingi
tangu 1985 – kwamba iwapo chombo cha habari kitakosea, basi kipelekewe
mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Watawala hawataki hilo, bali wanataka
kuonyesha kuwa wako juu ya sheria za nchi. Wanatumia ubabe.
Amini usiamini. Hata madikiteta wanahitaji taarifa
na habari sahihi na za kina; hata zile zinazoonyesha wanavyonyukana ndani kwa
ndani. Wameachana na ubazazi wa kufikiri kuwa, kama gazeti halikuandika au
limezuiwa kuandika, basi jambo husika
halitafahamika na hivyo watatulia. Hawafanyi hivyo leo. Wanakataa kuishi
kwa umbeya au vitaarifa vya kuwapongeza, kuwasifu na kuwapakata, wakati
halihalisi ni tofauti.
Serikali ambayo haina taarifa juu yake na haijui
wananchi wanasema au wanajua nini juu yake na wao wenyewe; haiwezi kuchukua
hatua. Sasa serikali inayoua vyombo vya habari hadi itakapopakatwa,
kubembelezwa na kupigwa busu, siyo serikali ya wananchi. Hata kama watawala
wake watadai kuwa walichaguliwa na wananchi, sharti tukubaliane kuwa ilikuwa
kiinimacho. Huwezi kuchaguliwa kutawala halafu ukapora waliokuchagua uhuru wao
wa kufikiri na uhuru wa kauli.
Ni siku 172 leo tangu serikali izuie wasomaji kuona
kipenzi chao MwanaHALISI. Kwamba vyombo vingine vya habari havijaguswa, haina
maana kwamba serikali ina ushoga wa kudumu na vyombo hivyo. Vikitaka haki
vitazimwa. Vikitaka uhuru vitaning’inizwa. Vikitaka ukweli vitafungiwa “kwa
muda usiojulikana.”
Kisichoeleweka vema na haraka kwa wengi ni kwamba,
kufungia MwanaHALISI au gazeti kama hilo au lolote lile
lililokwishajitambulisha kuwa mdomo wa umma, ni kuweka kifungoni mamilioni ya
watu na kuwaondolea kichocheo cha kufikiri.
Wangapi watakubali kubaki kifungoni bila
kuhukumiwa na mahakama; bali kwa utashi dhaifu na “hukumu” ya waliobeba mamlaka
ya kisiasa? Binafsi, sikubali!
fuatia pia: ndimara facebook
1 comment
nafikiri ni woga kwa serikali kufichuliwa maovu wanayo yatenda."likini tukumbuke kua itafika mahali unaye kandandamzwa naye atachoka tu"
Post a Comment