Header Ads

LightBlog

Kiatu cha John Tendwa kinapwaya


Polisi, mauaji, polisi, mauaji

Na Ndimara Tegambwage
SITAKI John Tendwa. Amenukuliwa akisema kuwa polisi kuua raia ni jambo la kawaida. Swali linakuja: Kwa hiyo?

Wengi tunajiuliza: Kwa hiyo nini? Kwa hiyo polisi wa Tanzania waue tu? Kwa hiyo waige au waendelee kuua? Kwa hiyo liwe taifa la polisi kuua raia tu badala ya polisi kulinda raia na mali zao? 

Tendwa alinukuliwa akisema hayo Ijumaa usiku katika kipindi cha “Kiti Moto” kupitia kituo cha televisheni cha ITV. 

Kauli ya Tendwa inatokana na utetezi wake wa kile kinachofanyika nchini: Mauaji ya wananchi yanayofanywa na polisi. Wanamjadala wenzake walimpa mifano mingi ambako polisi wameua raia.

Katika mjadala huo, Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi nne zenye idadi kubwa ya wananchi waliouawa na polisi.

Ikatajwa kuwa polisi wa Tanzania hawana hata chombo cha kuwaangalia au kuchunga mwenendo wao. 

Ikaelezwa kuwa polisi wa Tanzania wakiua wanaunda tume yao kuchunguza mauaji waliyofanya na kumalizia kwa kunyamaza au kuhalalisha mauaji.

Ni hapo Tendwa alipopakua kilichokuwa rohoni mwake kwa kusema mbona hata katika nchi nyingine polisi wanaua wananchi.

Haihitaji akili ya nyongeza kuona kuwa Tendwa anatetea mauaji. Anatetea udhalimu. Anahalalisha mateso na vifo. Anafurahia tendo la polisi kuua.

Tusema tu hapa kuwa kuna baadhi ya askari polisi wanaochukia mauaji. Wapo! Nimeongea nao. Sasa Tendwa anatetea nani?

Jana niliongea na baadhi ya maofisa wa ngazi ya juu katika jeshi la polisi kuwauliza iwapo Tendwa alikuwa anaongea kwa niaba ya jeshi la polisi au alitumwa kufanya hivyo. Wote wanne wakasema hawezi kutumwa kitu kama hicho.

Siyo kweli basi kwamba msajili wa vyama aliishiwa msamiati ndipo akasema aliyosema. Siyo kweli kwamba alipitiwa. Siyo kweli kwamba alikuwa amechoka. Hapana! 

Kauli ya Tendwa ndiyo “mlo” aliokuwa ameandalia wasikilizaji wake katika kipindi cha Kiti Moto. Ndiyo mvinyo aliyotaka isindikize kauli zake nyingine. Kama sivyo, aliingizaje hili la hata katika nchi nyingine polisi huua wananchi?

Mfano wa mauaji wa hivi karibuni ni ule wa Mufindi, Iringa ambako mwandishi wa televisheni Daudi Mwangosi alilipuliwa kwa bomu akiwa mikononi mwa polisi.

Niliwahi kuandika kuwa sitaki John Tendwa, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa sababu nyingi nilizotaja moja wapo ikiwa vitisho kwa vyama vya upinzani na kubeba, katika mbeleko, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Leo simtaki Tendwa kwa kuwa anatetea umwagaji damu. Amevaa kiatu kisicholingana na mguu wake. 

Ni hivi: Tendwa alipewa kiatu. Aliyempa kiatu ni rais. Huyu rais hakumpima. Wala hakumpa kwanza ajaribu. Alimwabia “Vaa hiki hapa!” 

Angalia kiatu chenyewe. Kwa mwonekano ni kizuri. Ni cha gharama kubwa pia. Ni cha heshima. Ni cha kwendea mahali pa wenye hekima. Lakini bahati mbaya saizi ya kiatu hiki ni kubwa mno. 

Tendwa alionekana akivaa kiatu kile, lakini hakika alikuwa anachomeka tu miguu.  Alichomeka. Akavuta. Akavuta, mithili ya mtoto anayeanza kusimama na kutembea huku wazazi wakiimba “…kasimama dede.” Huyooo!

Sasa Tendwa hata kuvuta kiatu kile havuti. Amegundua hakikuwa chake. Matambara na karatasi za kupachika mbele, nyuma na upandeni ili kuimarisha mguu, ama yamekuwa ghali au tendo lenyewe limeleta usumbufu. 

Tendwa sasa anavaa ndala. Hizo ndizo saizi yake. Tatizo ni kwamba pale alipowekwa si mahali pa ndala bali kiatu; tena kiatu kutoka kwa rais.

Sitiari hii inafaa kuelezea jinsi Tendwa alivyoshindwa kufanya kazi yake. Jinsi anavyopwaya katika nafasi hii na jinsi anavyoacha kilichochake na kufanya kisichochake.

Kwa nafasi aliyonayo Tendwa, akionekana anashabikia na hata kufikia hatua ya kutetea walioua; na kuonyesha kuwa hata raia katika nchi nyingine huwa wanauawa na polisi, basi anakuwa ameonyesha mchoko wa aina yake.

Mara chache wateule wa aina yake hujiingiza katika mijadala ya aina hii ambayo inaweza kuchukuliwa kuwa ndio msimamo wa waliowateua. 

Tendwa anafanya yote haya kuhalalisha ubabe wa chama chake. Kila mahali ambapo polisi wanaua, na kama kulikuwa na shughuli ya kisiasa, basi Tendwa atasikika akisema “Nitafuta chama.”

Mara zote ametishia kufuta chama cha siasa. Chama anachotishia kufuta siku zote ni chama cha upinzani. Hawezi kusema lolote kwa CCM. Hawezi kuuma kidole kinachomlisha! Tendwa huyo! 

Haina maana kupendekeza Tendwa afukuzwe kazi. Hatafukuzwa. Haina maana kumwambia ajiuzulu. Hatajiuzulu.

Haina maana kumwambia Tendwa aombe radhi kwa wananchi. Hataomba maana huenda asielewe vilevile kile alichofanya anachostahili kuombea radhi. 

Kitu kimoja ni wazi. Marais wetu watakumbukwa, pamoja na mambo mengine, kwa kuweka watu wasio na uwezo madarakani na wakadumu humo kwa kupakatwa hata walipothibitika kupwaya, kunyauka na kupauka.

Kwani kwa kauli ya Tendwa, na kwa serikali inayojali na kuthamini haki na utu wa watu wake, jamaa huyu angevalia ndala zake nje ya ofisi ya umma.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la TanzaniaDaima Jumapili tarehe 9 Septemba 2012)

No comments

Powered by Blogger.