Header Ads

LightBlog

YA DAUDI MWANGOSI YAENDELEA


 Daudi Mwangosi

Nimeweka makala hii hapa kwa kuwa nimeona mwandishi wa TanzaniaDaima amedonoa vitu vingi kutoka blogu yangu lakini hakukiri kufanya hivyo. Nitaongea na mhariri juu ya hili.Wanataka tufe kama kuku wa kisasa
TanzaniaDaima, 4 Septemba 2012


Na Mwandishi Wetu

MWANDISHI Daudi Mwangosi ameuawa. Alikuwa kazini katika kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi katika mkoa wa Iringa. Ameuawa akiwa mikononi mwa polisi.

Alikuwa akirekodi moja ya matukio muhimu katika maendeleo na mabadiliko ya nchi hii kisiasa na kiuchumi.

Mwangosi amelipuliwa kwa bomu; angalau mpaka sasa ndivyo waandishi walioshuhudia kwa macho na kamera, walivyomudu kutuelezea. Ndivyo pia hali hali ya mwili wake inavyoonyesha.

Amekatikakatika mwili. Amevurugwa mwili mzima. Ni nyama tupu – nyekundu kwa damu – mithili ya mnyama aliyeraruriwa na wenzake katikati ya pori la mawindo.

Kinachoonekana katika picha muhimu ni matumbo nje, vipande vya nyama na vidole vitatu vya mkono wa kushoto alikosukumizwa na kulalia mara ya mwisho.

Picha nyingine inaonyesha akiwa bado anazongwa na askari; akinyang’anywa kamera zake, akisukumwa chini huku mmoja wa askari akilenga kwa makini na karibu sana na mwili wake, “bunduki yenye mdomo mpana.”

Kilichobakia kwa Daudi Mwangosi ni miguu kuanzia chini ya magoti – masalia ya mwandishi wa televisheni na aliyewahi kuwa mwandishi wa muda wa baadhi ya magazeti nchini.

Mwandishi alikuwa akisaka habari. Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilikuwa kinafanya kazi ya kisiasa ya kufungua matawi yake na ofisi yake.

Kuna umuhimu wa waandishi wa habari kuwa katika maeneo haya. Kuona. Kusikia. Kunusa. Kushuhudia kwa makini. Kuandika na kutangaza. Kuweka rekodi ya kilichosemwa na kilichotendeka kwa manufaa ya waliombali na karibu, kwa manufaa ya watafiti, lakini pia kwa kumbukumbu za vizazi vijavyo.

Aliuawa katika mazingira hayo kijijini Nyololo. Maneno yake ya mwisho yaliyonukuliwa na mmoja wa waandishi wa habari ni “…msiniue…msiniue…mimi niko kazini.” Hakika alikuwa kazini. Aliuawa.

Kinachotia moyo ni kwamba baadhi ya waandishi waliokuwa pamoja naye waliendelea kupiga picha. Ndiyo hizi hapa. Waliendelea kuandika. Taarifa ziko magazetini, redioni na katika televisheni.

Mashujaa waandishi walibuni haraka jinsi ya kufanya kazi katika mazingira mapya yaliyoibuliwa na polisi. Mazingira ya vita. Mazingira hatarishi.

Baadhi wamerekodi tukio kwa kutumia kamera zao na wengine kutumia simu za mkononi. Mbona teknolojia itaumbua wengi! (?)

Wamerekodi tukio. Wanatunza tukio. Wanasambaza tukio dunia nzima. Ni kazi takatifu: Tuone. Tuzingatie. Tufikiri. Tutende.

Hivi vita dhidi ya waandishi wa habari vimeanza. Vitaendelea mpaka wapi na mpaka lini? Nani atavikomesha? Nani ana nia ya kuvikomesha kama siyo waandishi wenyewe?

Mazingira yaliyotoa roho ya Mwangosi yamepoteza pia viungo vya miili ya waandishi na wananchi waliokuwa kwenye ofisi za Chadema kushuhudia ufunguzi. Siyo mkutano wa hadhara.

Woga waweza kuua waandishi wote. Ujasiri waweza kusalimisha wengi na kuunda wengi wengine katika taaluma inayokua kwa kasi.

Tuandike. Tuandike. Hata mengine mengi ya Mwangosi ambayo hayajafahamika yatahitajika kuwekwa wazi kwa dunia kuona na kuchukia unyama huu usiomithilika.

Hii ni muhimu hasa tukizingatia ripoti ya mwandishi wetu kutoka Iringa akimnukuu Mkuu wa Polisi Mkoani (RPC), Michael Kamuhanda.

RPC amenukuliwa akisema kuwa …Chadema hawana jeshi wala vifaa vya kupambana na polisi, hivyo wakijaribu kutotii sheria lazima washurutishwe.

Maana ya kauli hiyo ni kwamba mwandishi aliuawa wakati polisi wakipambana na Chadema ambayo wanaelewa fika kuwa haina silaha wala vifaa vyovyote vya kuwawezesha kupambana na jeshi lake.

Mwaka juzi polisi waliua watu watatu Arusha kwenye maandamano ya Chadema. Wote hawakuwa wanachama wa chama hicho.

Juzi mjini Morogoro silaha zao zimerekodiwa kuua mtu mmoja akiwa barazani kwake. Hakuwa mwanachama wa Chadema.

Jumapili hii Daudi Mwangosi ameuawa mikononi mwa polisi wakati akifanya kazi za kampuni yake ya televisheni na wala siyo kutafuta nafasi ya uongozi kisiasa katika Chadema.

Watakufa wangapi ndipo polisi wakemewe? Wafe wangapi ndipo umma ustuke na kusema: Hapana? Nani mwandishi mwingine au wengine wafie mikononi mwa polisi ndipo waandishi wapate maarifa?

1 comment

mchonde said...

salaam mzee Ndimara,nakupongeza kwa jinsi ulivyobarikiwa na Muumba na jins ulivyo na upeo wa kuweza kuchambua mambo na mijadala mbalimbali na kuweza kutufikia sisi. Nakupongeza sana.ninaitwa mchonde, dar es salaam

Powered by Blogger.