Header Ads

LightBlog

BAADA YA KUONA WAMEZIDIWA KETE NA UMAARUFU WA DK. WILLIBROD SLAA

Wachovu wa CCM na umbeya wao: MWANZO WA UCHAKACHUAJI

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI wananchi waingizwe kwenye ubishi wa kipuuzi unaopaliliwa na kunawirishwa na wachovu wa siasa.

Wiki hii tumesikia baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakidai kuwa watashitaki Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wamesema watapeleka malalamiko kwa Tume na Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba Chadema imefanya kampeni kabla ya Tume kuruhusu.

Kinachotia kichefuchefu ni baadhi ya wanasiasa upande wa upinzani kuitikia kibwagizo cha CCM na wao kuimba kuwa Chadema na CCM wanaweza “kuchukuliwa hatua.”

Hali iko hivi: Dk. Willibrod Slaa anateuliwa na chama chake kugombea urais. Chama kinaanua kufanya mikutano katika miji mikuu ya mikoa kadhaa. Kinambeba mteule wake. Hii ni kwa sababu kuu mbili:

Kwanza, kumtambulisha kwa wanachama wake na wananchi. Pili, kuendeleza kazi yake ya kisiasa kama chama chochote kile kilichohai.

Chama kilichohai, kikipata fursa, sharti kiitumie kuwafikia majaji wakuu katika taratibu za kidemokrasia; ambao ni wananchi wapigakura.

Chadema haikufanya hivyo juzi tu. Imekuwa ikifanya hivyo kila inapotaka kuwa karibu na wananchi; na wapigakura.

Hivyo ndivyo CCM imefanya. Imetangaza wagombea wake, halafu ikawapeleka kwenye mikutano ya hadhara – kwa wapigakura – ili wanachama wenzao na wananchi wawafahamu.

Chama kingine chenye ushindani ni Chama cha Wananchi CUF. Hiki hakikuwa na kiongozi wa kutambulisha kwani mgombea urais wake mwaka huu, ni Profesa Ibrahim Lipumba ambaye tayari amepigiwa kura za urais mara tatu.

Hata hivyo, CUF muda mfupi baada ya kutangaza mgombea wake, iliweka wazi kwa mgombea, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho kitaifa, atatembelea mkoa wa Dar es Salaam kwa madhumuni ya “kuangalia uhai wa chama.”

Hiyo nayo ni fursa nyingine kwa chama makini kuwa karibu na wananchi na wanachama wake wakati muhimu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Ukiangalia kwa makini, utaona kuwa kila chama kina njia zake za kufanya kazi za kisiasa – iwe asubuhi, adhuhuri, alasiri, mangharibi au usiku.

Muda huu wa maandalizi ya kuingia kipindi maalum cha kampeni na uchaguzi mkuu, hautawaliwi na pingu za NEC. Ni muda na eneo huru la kuzidisha kazi za kisiasa.

Hasa ni kipindi maalum kwa vyama upande wa upinzani, kutekenya jamii, kuizindua, kuielimisha, kuishawishi na kuiandaa kuachana na ukale ulioizonga na kuipa kilema – kudumaa.

Kwa mfano, kwa upande wa Chadema, ni wakati wa kuendeleza na kuhitimisha kwa nguvu, kazi ya kisiasa inayoitwa “Operesheni Sangara” – iliyovuma na kuvuna nyoyo za wengi – kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu.

Kwa upande wa CUF, ni wakati mzuri wa kuendeleza na kuhitimisha kazi ya kisiasa iliyoitwa “Zinduka” – iliyozindua wengi – kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu.

Kwa hiyo, kinachoipa kiwewe CCM, siyo Chadema “kufanya kampeni” kabla ya muda uliopangwa na Tume, bali umaarufu wa mgombea wa Chadema anapolinganishwa na yule wa chama chao.

Kiwewe kinatokana na mgombea mpya anayefahamu vema serikali na nyendo zake. Anayejua serikali ilivyokwama kwenye tope la ufisadi, ukosefu wa ubunifu; ukame wa mbinu mpya na ahadi tuputupu.

Kelele za CCM zinalenga kufanya mwendelezo wa ghiliba kwa wananchi. Chama hiki, kama ilivyo serikali yake, kina midomo mingi na uwezo wa kupakazia.

Kina vyombo vya habari vya serikali (wanadai ni vya umma), ambavyo vinatawaliwa na makada wake. Humu hupitishwa kampeni na propaganda angamizi.

CCM ina “marafiki” wenye vyombo vya habari ambao huipendelea kwa kila hali kuliko hata gazeti lake la UHURU.

Kwa kutumia midomo yake mingi; laghai wake wengi; ujuzi na uzoefu wa kutunga ghiliba na kupakazia, chama hiki kinaweza kuanzisha mjadala finyu, kikaupa mvumo, ukapandikiza mitafaruku na kupotosha wananchi wengi.

Chama hikihiki kinaweza kutumia kauli za nguvu kuyumbisha watendaji serikalini; kutishia walioko madarakani katika sehemu muhimu kama Tume ya uchaguzi na kuogofya wananchi.

Haitakuwa mara kwanza kwangu kujenga hoja kwamba watawala wetu wamekuwa wakitegemea sana ujinga, woga na umasikini wa wananchi (vilivyosimikwa na chama kinachopanga ikulu), kama mitaji yake mikuu katika juhudi za kubaki madarakani kwa nusu karne sasa.

Chama hiki kina watu wenye ujasiri wa kukataa ukweli; wakaidi wa kutaka kila mmoja aone, kwa mfano, kuwa hili ni chungwa wakati ni kiazi kikuu.

CCM isingekuwa hivyo, kama ilivyofafanuliwa hapo juu, viongozi wake wasingejitokeza kupandikiza uzushi kwamba Chadema imefanya kampeni kabla ya NEC kutangaza.

Kwani kampeni za kuwaelimisha wananchi kujua kuwa diwani, mbunge au rais huyu hafai; anayefaa ni fulani kutoka chama kingine, hazisubiri uchaguzi mkuu.

Hii ni kazi ya Oktoba hadi Oktoba, kwa kipindi chote cha miaka mitano ya wanaokuwa madarakani na wanaokuwa wakisubiri kuingia.

Katika kipindi chote hiki NEC inajiandaa kusimamia uchaguzi lakini wanasiasa wanakata mbuga kuandaa wananchi kwa “mavuno.”

Hapa hakuna udhibiti hadi unapoingia rasmi kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu. Kazi za kisiasa za chama chochote, haziruhusiwi wala hazipaswi kuzuiwa na Tume. Na pasito zuio kuna uhuru kamili.

Chukua mfano huu: Katika mazingira ambako hakuna sheria inayolazimisha kila mmoja kuvaa tai shingoni, hakuna anayeweza kukamatwa na kushitakiwa kwa kutovaa tai. Hakuna sheria inayombana.

Hiyo ndiyo hali iliyopo katika kipindi ambapo wachezaji watarajiwa wa mchezo wa siasa hawajajifunga kushiriki; na mchezo wenyewe haujaanza.

Huwezi kuwabana. Huwezi kusema aliye nje ya uwanja ameharibu kanuni na taratibu za mchezo. Kudai hivyo ni kupanda mbegu ya uhasama ambao CCM na serikali yake, havina uwezo wa kuzima ndimi zake pale zitakapokuwa zimechomoza.

Hivi sasa, CCM ni chama kinachokwenda kwa mazoea tu. Hakina jipya ingawa kinataka kubaki ikulu, kwa “gharama yoyote ile.”

Na hili la kubaki madarakani kwa gharama yoyote ile, ndilo liwezalo kuleta maafa kwa nchi na watu wake.

Kwani wanajua kuwa kuondoka kwao kutaweka wazi mengi machafu ambayo yamekuwa yakitendeka. Hili, viongozi wake hawataki kuliona wala kulisikia.

Wako tayari kuua mbegu mpya na bora kwa kupitia madai yasiyo kichwa wala miguu, alimradi wamebaki ikulu.

Lakini katika hili la kupakazia kufanya kampeni mapema, tundu limezibwa. Hata kwa mgongo wa “tu-vyama twingine” kwenye upande wa upinzani, kama vile Tanzania Labour Party (TLP) ka Augustine Mrema, CCM itaendelea kukaliwa kooni.

Tayari kuibuka kwa Dk. Slaa kumebadili mwelekeo wa siasa nchini na kuleta uwezekano wa kuifinyaza CCM na mikonga yake.

Bali wananchi wanataka umoja wa vyama; kwa maana ya ushirikiano katika uchaguzi huu ili mradi wa kuadabisha CCM uweze kufanikiwa.

Umbeya na ghiliba ya CCM vyaweza kuzimwa. Je, hili la ushirikiano laweza kufikiwa? Tusubiri.

0713 614872
ndimara@yahoo.com

(Makala hii ilichapishwa katika Tanzania Daima, Novemba 2010 katikati ya vuguvugu la uchaguzi na CCM ilipoanza kuhaha)
Powered by Blogger.