MSUKUMO WA KATIBA MPYA WAONGEZEKA
Katiba mpya siyo kwa hisani
Na Ndimara Tegambwage
KATIBA mpya ya nchi ambayo wananchi wanataka, si mali ya rais. Si mali ya waziri mkuu. Wala katiba hii haipatikani kwa hisani ya mtawala yeyote. Hapana.
Wananchi wanataka kuandaa makubaliano juu ya mamlaka ya usimamizi na utawala; na misingi inayoweka udhibiti wa mamlaka katika mahusiano ya watawala na watawaliwa na miongoni mwa vyombo vingine vya dola.
Kwa ufupi, wananchi wanataka kushiriki kuandaa taratibu, kanuni na misingi itakayokuwa mwongozo mwafaka wa jinsi wanavyotaka kujitawala; na siyo katiba ya kuviziana ya mfumo wa chama kimoja.
Hapa unaweza kusema wananchi wanataka kuandika mkataba kati yao na watawala, wa sasa na wa baadaye, jinsi nchi yao inavyopaswa kuendeshwa katika nyanja zote za maisha.
Itakuwa historia. Sharti iwe. Wananchi wote – kwa kuulizwa au kwa utaratibu wowote ule wa kushirikisha maoni yao, akiwemo mtawala mkuu – watakuwa wamepata fursa ya aina yake ya kukubaliana jinsi wanavyotaka kujitawala.
Wiki iliyopita, kwenye ukurasa huu, tulieleza jinsi watawala wanavyojua vema jinsi katiba iliyopo ilivyo na kasoro nyingi.
Kwa ufupi tulisema wanajua kuwa rais anaweza kupata kura zisizo halali; lakini hawezi kulalamikiwa mahakamani. Katiba inaziba fursa hiyo.
Tulionyesha pia kuwa katiba ya sasa inazuia mtu kugombea nafasi yoyote ya kisiasa iwapo si mwanachama wa chama cha siasa. Ni ubaguzi mchafu.
Rafiki yangu anasema huo ni “ukabila wa kichama;” wa kuziba haki ya mtu kwa sababu dhalili lakini za uchu wa kunyanganya haki ya mwingine.
Watawala wanaelewa vema kuwa kuna raia wenye akili nzuri, elimu ya kutosha na uwezo wa kufikiri na kutenda kuliko baadhi ya wanachama wa chama chao waliopachikwa madaraka; lakini kwa “ubaguzi wa kichama,” wanaziba fursa zao za kutumikia taifa.
Haya yote Rais Kikwete anayajua. Pinda anayajua. Wanajua kuwa siyo sahihi. Siyo haki. Lakini wanayaendeleza. Wanayapakata kwa kuwa yanawawezesha, wao na chama chao, kukaa kileleni. Yanawachafua.
Chukua mfano mwingine. Watawala wanajua kuwa kazi kama zile za mkuu wa wilaya (DC) na mkuu wa mkoa (RC), zingekuwa zinachukuliwa na watu waliopatikana kwa kupanda ngazi kikazi katika maeneo ya utawala.
Sasa wafanyakazi wenye elimu na uzoefu wanaachwa; badala yake wanachukuliwa “wowote wale,” wakiwemo maaskari wastaafu ambao hawana ujuzi wala uzoefu katika kazi hizo.
Inagharimu serikali muda na mabilioni ya shilingi ya kodi za wananchi, kufundisha, bila mafanikio, watu wazima ambao hata siku moja maishani mwao hawakuota kuwa kwenye utawala.
Mkono wa kuteua unafika hata kwa wakurugenzi wa halmashauri na manispaa kwa sababu moja kuu: Kuongeza idadi ya wafuasi na watendaji kisiasa kwa niaba ya chama kilichoko ikulu.
Mteule wa rais anakuwaje kiranja katika utawala wa wananchi katika halmashauri, badala ya madiwani kutafuta na kuajiri mtendaji ambaye wanaona ana sifa za kuwatumikia?
Ni baadhi ya wateule hawa ngazi ya wilaya (wanaokuwa wasimamizi wa uchaguzi), ambao wamekuwa chanzo cha migogoro wakati wa uchaguzi kwa vile wamekuwa wakitishiwa kuwa, kama chama tawala hakikushinda watapoteza kazi.
Haya yanaweza kupatikana katika mazingira ya katiba ya sasa na safu hii itaendelea kufafanua.
Sasa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anasema serikali iko tayari “kufanya marekebisho” ya katiba ya nchi.
Alikuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Ijumaa iliyopita na kunukuliwa akisema atamshauri rais ili marekebisho hayo yafanyike katika kipindi cha “miaka mitatu.”
Hauhitajiki uchunguzi wowote kujua kuwa Pinda tayari aliishakutana na Kikwete na kujadili hoja hii kabla hajatangaza kuwa atakwenda kumwona.
Waziri mkuu hatangazi kila anapotaka kumshauri rais. Aidha, siyo lazima rais akubaliane na uamuzi wa waziri mkuu. Kwa hiyo, hatua ya kutangaza kuwa anakwenda kumshauri rais inaweza kutafsiriwa kuwa ameagizwa na rais kutoa kauli hiyo.
Hata hivyo, hiyo siyo hatua mbaya wala ndogo. Ni hatua inayoonyesha kuwa, angalau mara hii, masikio ya watawala yamefunguka.
Tatizo lipo kwenye hatua ya Pinda kumshauri Kikwete. Kama ilivyoelezwa hapo awali, katiba haiji kwa hisani ya rais. Rais anahitaji katiba mpya. Itakuwa yake kama ilivyo kwa raia yeyote wa nchi hii.
Rais anahitaji katiba itakayomwondolea uwezekano wa kushutumiwa na kutuhumiwa kutenda visivyo; kuwa anaminya, ananyang’anya au anavunja haki za raia na haki za binadamu.
Rais anataka katiba nzuri, kuliko hii iliyopo, ili huko tuendako, watawala wapya wasije kumgeuzia kibao na kuitumia kumminya kama Frederick Chiluba alivyomtendea rais mstaafu Kenneth Kaunda huko Zambia.
Rais aliyeko madarakani anahitaji katiba inayotabasamu kwa wote; isiyojenga kinyongo wala kuminya haki ya mwingine. Hii italeta mazingira bora ya utawala ambapo kila aliyeko madarakani atajisikia kuwa huru hata pale anapokuwa amestaafu.
Katiba mpya itamfanya rais na watawala wenzake, kutembea bila kujishuku; na wasipotenda haki, ama watasahihishwa waziwazi, bila woga wala aibu; au watatemwa kabla muda wao wa utawala kumalizika kwani kutakuwepo utaratibu mwafaka na mwepesi wa kufanya hivyo.
Katiba isiyo na nia mbaya, inamhakikishia rais anayemaliza muda wake, utulivu kwa maisha yake yote, akila chake, akifurahia shahada zake za heshima alizopewa na vyuo vikuu ambazo zitakuwa zikipamba kuta za nyumba zake maridadi.
Rais Kikwete hana cha kupoteza kwa kuanzisha sasa mchakato wa katiba mpya. Kama kipo cha kupoteza ni woga usio na msingi. Bali kwa hili, aweza kunyakua sifa ambazo zimewashinda marais wote waliomtangulia.
Hata hivyo, nimekuwa nikipata ujumbe wa simu (sms) kutoka kwa baadhi ya wasomaji kuwa wananchi wengi hawajui katiba ya sasa inasema nini na kwamba wanahitaji kuelimishwa kwa “muda mrefu” kabla katiba mpya haijapatikana.
Nimewajibu kuwa wananchi wanajua kuwa utawala bora ni ule unaotambua, kuheshimu na kulinda haki zao binafsi za kuzaliwa.
Ni utawala unaopaswa kusimamia na kuhakikisha kuwa haki zao za kiuchumi, kisiasa, kiimani na nyingine zote zinafurahiwa na wote.
Lakini wanapoona kuwa haki zao hizo zinakanyangwa, unakuwa ujumbe wa kutosha kuwa hakuna katiba; kama ipo basi si “katiba nzuri” au hakika sio yao. Wanataka katiba tofauti; mpya.
Wanajua hakuna makubaliano kati ya watawala na watawaliwa; kama yalikuwepo basi yamefutwa au watawala wameasi; na hivyo kuna umuhimu wa kuwa na “kitu kipya.”
Ni muhimu kweli kusoma katiba, lakini haina maana kuwa ambao hawajaisoma hawajui kuwa, ama katiba haipo au iliyopo ni katili. Wanataka katiba mpya.
(Wiki ijayo: Mifano ya uhusiano kati ya katiba na maisha ya kawaida ya wananchi)
0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 22-29 Desemba 2010)
No comments
Post a Comment