Header Ads

LightBlog

USHINDI 'CHAKUPEWA' WA CHAMA CHA MAPINDUZIMADAI YA WIZI WA KURA YATAWALA MIJADALA
MAJUMBANI, SHULENI, VYUONI, SOKONI, MAOFISINI


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kuwaudhi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwaambia kuwa aliyeshinda katika uchaguzi mkuu siyo Jakaya Kikwete bali Dk. Willibrod Slaa na kambi ya upinzani.

Pamoja na kutotaka kuwaudhi, sitaki pia kuandika kwa urefu kwa kuwa matukio ya hivi karibuni, yanayohusu uchaguzi, yangali mabichi na wananchi wanahitaji kuyajadili, kuyatafakari na kuyafanyia kazi.

Niseme tu kwamba waliokuwa bado na shaka juu ya uwezekano wa CCM kuwekwa kando, kufungiwa virago na kuondoshwa ikulu, sasa waanze kufikiri upya. Inawezekana!

Kile ambacho kinatangazwa kuwa ushindi wa CCM wa asilimia 61 katika uchaguzi mkuu ndicho hasa kinaonyesha mporomoko wa chama hicho na uwezekano wa kuenguka.

Lini Tanu na CCM viliwahi kufikia asilimia 60 za kinachoitwa “ushindi” hata katika mazingira ya “ushindani wa mwendawazimu” anayekimbia peke yake na hatimaye kudai ameshinda?

Lini, tangu kurejeshwa kwa maneno ndani ya katiba “mfumo wa vyama vingi vya siasa,” lakini kubakia chama kimoja kifikra na kiutendaji, CCM imewahi kupewa asilimia 60?

Nani, miongoni mwa viongzi wa CCM, akiwemo mwenyekiti Jakaya Kikwete, aliwahi kuota Tume inawapa asilimia 60 au kupata kiwango hicho kwa njia zao za abrakadabra?

Hata Kikwete alipokuwa anaanza na kufunga kampeni, alitangaza kuwa atashinda kwa “kishindo kuliko hata ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita” – 2005. Yako wapi?

Je, ni mtindo wa watawala wa Uingereza wakati wa Vita Vikuu vya Pili? Walikuwa wakitangaza kuwa tayari vita vimeisha; Wajerumani wamesambaratika na wengine wamejisalimisha.

Nia ilikuwa kuamsha na kujenga morali ya wapiganaji wao na kuzamisha na kufisha morali ya Wajerumani na waliowaunga mkono.

Yawezekana CCM imefikia viwango hivyo? Propaganda za “kyakutinisa kitakulye” – kinachoogopesha lakini kina madhara kidogo au hakina madhara kabisa?

Chukua mfano mmoja. Kwa maamuzi ya haraka na ya dakika ya mwisho, kwamba Dk. Slaa ndiye awe mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama cha zamani CCM kimetikisika hadi mizizi.

Kwa miezi mitatu tu ya kuwafikia wananchi, hata mahali ambapo chama cha Dk. Slaa hakikuwahi kusikika, elimu ya uraia kwa njia ya mikutano ya hadhara imepenya kwa kasi.

Kwa miezi mitatu tu ya kuwafumbua macho wananchi na kuwasaidia kuchambua matatizo yao, wameelewa kuwa kumbe watawala wao wamekuwa sehemu ya matatizo yao. Hivyo hawana msaada kwao.

Yote hii ni kwa vile kwa miaka mingi wameishi kama wafungwa; wana utulivu ya magereza lakini bila amani. Sasa wameona anayewasaidia kutafakari maisha yao na kwa kiasi fulani kukata baadhi ya minyororo kwa kauli chambuzi.

Kwa mzunguko wa miezi mitatu, ulioongozwa na Dk. Slaa, kwa hoja nzito na kauli za matumaini mapya, CCM imeporomoka kutoka “ushindi wa kishindo” hadi asilimia 61 ilizopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Katika baadhi ya maeneo, na hasa kule ambako CCM iliishakuwa serikali, polisi, mahakama na bwana jela, ujumbe wa Chadema na Dk. Slaa umefanya baadhi ya wananchi waone kuwa “kumbe CCM ni chui wa karatasi.”

Miezi mitatu ya kutafuta kuwaamsha wananchi kuchukua serikali yao kutoka kwa waliochoka na walioshindwa kuleta, siyo tu mabadiliko bali hata matumaini, imezaa uelewa mpana.

Ukichukua asilimia 61 za wanaotamba kubakia ikulu na kulinganisha na maarifa – uelewa, ung’amuzi, mwamko, matumaini mapya na utayari wa wananchi kushiriki katika kuleta mabadiliko katika maisha yao, ndipo utagundua kuwa CCM “wameliwa” au “wamejila wenye.”

Chukua mfano mwingine. Profesa Kulikoyela Kahigi alishinda katika kura za maoni ndani ya CCM; jimbo la Bukombe. Akafanyiziwa. Rufaa yake ikazimwa. Vijana na wazee wakasema, “…nenda kule tutakupigia kura hukohuko.” Leo ni Mbunge.

Juhudi za Yusuf Makamba, katibu mkuu wa CCM, kujaribu kugeuza mkondo, zilikwama. Alifikia hatua ya kutukana wanachama na viongozi wake kuwa wamrejeshee mashati yake ya kijani, kama wanakuwa wanachama mchana tu na usiku wanakwenda upinzani. Kyakutinisa kitakulye!

Mfano huohuo unahusika Maswa Magharibi ambako ghiliba na husuda vilikuwa sehemu ya sala ya viongozi wa CCM kwa shabaha ya kumzima John Shibuda.

Shibuda alihama CCM baada ya kuenguliwa. Naye akasema hakuna chama pale na kwamba kilikuwa kinaishi kwa pumzi ya rushwa. Wananchi wamemlinda. Wamemchagua.

Miezi mitatu ya kazi ya Dk. Slaa na chama chake; juu ya kazi ya awali ya sauti ya mageuzi; vimejenga ujasiri usiomithilika nyoyoni mwa umma.

Kila mahali ambako uelewa na maarifa vimesambazwa na kuzama vichwani na nyoyoni mwa wananchi, CCM imedaiwa kuvuna sifuri au kujichukulia “kwa mbinu.”

Wala Dk. Slaa hana sababu ya kusononeka na kulia. Hapana! Ameshinda. Mara hii ushindi wa kishindo; tena ulio halali na tofauti na vungavunga ya CCM.

Kiwewe kilichotembelea CCM kutokana na wimbi kubwa la upinzani na nguvu ya mgombea wa Chadema, vimefanya chama hicho kilichopanga ikulu kiweweseke, kiishiwe nguvu na hata kuwa butu.

Ni kiwewe kilichofanya viongozi wa CCM wajiingize katika kujadili uchumba, ushenga na ndoa ya Dk. Slaa. Ni hichohicho kilichofanya waanzishe mtandao wa vineno vya kashfa na kuvisambaza nchi nzima.

Kiwewe hichohicho ndicho kilifanya CCM wabuni uwongo juu ya Dk. Slaa kuwa ni mbishi, kaidi na anayegombana na vyombo vya ulinzi na usalama na anayetaka kuleta vita.

Walilenga kuwa wananchi wakisikia Dk. Slaa “anagombana na askari,” basi watamkimbia na CCM itakuwa imepona upele ulioletwa na upupu wa ufisadi.

Eti wananchi waogope vita vya kujikomboa lakini wasijali mafisadi wanaowaibia na kufanya maisha yao yatoweke haraka kuliko kama kungekuwa na vita! Kyakutinisa kitakulye.

Ni CCM waliopenyeza katika hotuba zao, madai ya vita na kumbukumbu za vita vya Burundi na Rwanda ili wananchi wakatae mpiganaji wa Chadema.

Ni chama hicho chenye kupanga ikulu, ambacho kilianzisha na kuvumisha kuwa kuna “udini” kikilenga kuzamisha sauti za wapenda mabadiliko.

Wakati askofu wa katoliki anasema, mwaka 2005 kuwa Kikwete, ambaye ni mwislam, ni “Changuo la Mungu,” CCM walikaa kimya. Leo, Kikwete anachuana na mkristo mwenye rekodi nzuri na ambaye hashikiki kwa hoja, CCM inaibua madai ya udini.

Chadema imetumia uchaguzi mkuu huu kuandaa mtaji kwa ajili ya uchaguzi ujao. Kile ilichobakiziwa kwa njia ya idadi ya kura na asilimia, ni ushahidi tu.

Wekezo kuu la Chadema katika uchaguzi ni elimu iliyowaacha wananchi na maarifa mapana; ujasiri wa kusema “hapana” na utashi wa kuchagua chenye thamani na endelevu.

Kwa kutumia mizani hiyo, mbegu ya mabadiliko imepandwa nyoyoni mwa wananchi wengi; haiharibiki kwa ukame wala mafuriko ya kisiasa.

Ndiyo maana ni halali kusema Chadema imevuna; ukitaka – imeshinda. Si kwa asilimia peke yake ambazo zaweza kutiliwa shaka, bali hasa kwa wekezo la maarifa na ujasiri ambavyo ni muhimu kesho, kuanzia ngazi ya kaya.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima mara baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu, Novemba 2010)
Powered by Blogger.