Header Ads

LightBlog

OMBAOMBA YA KIKWETE INANUFAISHA NANI?










Safari za nje na ombaomba ya JK


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kusikia Jakaya Kikwete akisema kuwa asigefanya safari zake nyingi nje ya nchi, basi wananchi wangekufa njaa.

Huyu rais aliyemaliza muda wake anataka kusema kuwa alikuwa anakwenda kuhemea; kuomba kishika-roho ili Watanzania wasife njaa.

Ndivyo alivyonukuliwa akisema kwenye mikutano ya hadhara ya kuomba kura katika majimbo mawili ya uchaguzi ya Urambo – Mashariki na Magharibi mkoani Tabora.

Wakati mgombea urais akisema hayo, Bolozi wa Ujerumani nchini, Guido Herz anawaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa nchi yake inashangazwa na umasikini ulioko nchini, tena katikati ya “raslimali nyingi.”

Balozi anarudia yale ambayo yamesemwa kwa miaka nendarudi kuwa nchi hii, pamoja na raslimali nyingine, ina mito, maziwa, bahari, ardhi nzuri kwa kilimo na vivutio vya utalii.

Balozi anasema, “Kwa hakika siwezi kutaja sababu ya kuifanya Tanzania isipige hatua ya maendeleo,” bila shaka na kuondokana na umasikini wa kipato (ajira), chakula, elimu, mavazi, usafiri, maji, umeme na mahitaji mengine ya jamii.

Ni njaa ipi ya Watanzania anayosema Jakaya Kikwete ambayo imekuwa ikimpeleka nje ya nchi?

Hapa ndipo tunaweza kushona alichowahi kusema Mwalimu Julius Nyerere kuwa, ni upumbavu kufa kwa njaa wakati unaishi katika bonde lenye rutuba.

Katika mazingira haya, ni vigumu kumruhusu mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutumia kampeni za uchaguzi mkuu kujidhalilisha, yeye na watawala waliomtangulia.

Hakika hapa Jakaya Kikwete anajianika, kwamba ameshindwa kazi; na kwa njia ya ushauri wa bure, asijaribu kurudia kauli ile mbele ya wakulima masikini anaowaomba kura. Watamnyima.

Wakulima wamejilisha kwa ndizi, muhogo, mahindi, viazi, mtama, uwele, ulezi, karanga, maharage na mazao mengine.

Wamejipatia matumizi kwa kuuza mazao yaliyotajwa hapo juu, pamoja na pamba, miwa, korosho, nazi, alizeti, karafuu na kahawa. Wafugaji wamelinda maisha yao kwa mifugo – mbuzi, kondoo na hasa ng’ombe.

Wananchi masikini wamevua samaki kutoka mito na maziwa ambayo husema kila siku kuwa wamejaliwa na Mwenyezi Mungu; wamekula na kuendelea na maisha.

Wengine wamefukua dhahabu, almasi, tanzanite na madini mengine “tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu” kwa kutumia vijiti, majembe na koleo – alimradi wamepata vipande vya kuuza, kupata fedha na kusogeza miaka mbele.

Pamoja na kilimo, ufugaji, uvuvi na uchokonoaji madini kwa njia za kale, wananchi wengi wamebaki masikini. Wanatumia nyenzo duni.

Wengi wana mashamba madogo. Maeneo madoyo ya kulima na kuchungia. Wanapata mazao kidogo. Wanakula kidogo. Wanauza kidogo. Wanabakia na kidogo. Wanajiviringisha katika udogo-udogo ambao ni umasikini usioisha.

Hili ni somo pana lisoloweza kuenea kwenye kipande hiki cha ukurasa. Bali ni somo linaloeleweka vema kwa wakulima, wafugaji, warinaasali na wakusanya matunda porini; wafanyakazi na wasio na kazi, kwa kuwa ndio wanaishi maisha hayo.

Ukichunguza utaona udogo unaojadiliwa unatokana na “ubongo mdogo wa watawala,” kwa maana tatu.

Kwanza, kukosa uwezo wa kufikiri. Pili, kukosa utashi katika kutumikia wananchi. Tatu, uroho wa kijuha – wizi, matumizi ya kutanua na ushirika na watu wa nje katika kuibia nchi.

Huwezi kusema unakwenda kuhemea nje ya nchi kwa ajili ya mtu ambaye umemnyang’anya ziwa ambalo limekuwa chanzo cha mapato yake (samaki na fedha) na kiungo cha uhai wake.

Wananchi wanalia – nyavu zao na mitumbwi vimechomwa moto; wamekamatwa, kupigwa viboko na kuchomewa nyumba ili mwekezaji ziwani apate usalama wa kukomba “samaki wa mungu.”

Hilo bakuli la ombaomba wa kitaifa, limemletea nini huyu aliyeachwa utupu na ambaye watawala hawataki kusikiliza kilio chake?

Haiingii akilini kudai unakwenda kuhemea nje ya nchi kwa ajili ya mfugaji wa Kilosa ambaye watawala wamenyang’anya ng’ombe 600 au 1,000 na hata 2,000. Kuna nini lake ndani ya pochi ya mhemeaji aliyeacha amemfukarisha?

Hakuna mtawala awezaye kwenda kuhemea kwa ajili ya wafugaji ambao ng’ombe wao wameswagwa na kupotea porini, nyumba zao kuchomwa moto na wao kuamriwa, kwa mtutu wa bunduki, kuhamia wasikojua – kwa kauli za “rudi kwenu.”

Anayekwenda kuhemea atawakuta wapi watu hawa ili awape alichopata? Kama siyo mzaha basi ni ukatili usiomithilika.

Chukua wachimbaji wadogo – wale wa vijiti, majembe na koleo. Wameswagwa kutoka walikoishi uhai wao wote. Wametengwa na chanzo cha “uchumi” na maisha yao. Sasa ni jinai kukutwa na madini “waliyopewa na Mwenyezi Mungu.”

Nani ataamini kuwa hata makombo kutoka kapu la mhemeaji Jakaya Kikwete, yataweza kuwafikia watu hawa, licha ya madai kuwa anakwenda nje kuhemea ili wasife njaa? Yatawakuta wapi?

Nenda Rukwa, Ruvuma, Mbeya na Iringa – mikoa inayozalisha mahindi kwa wingi mpaka ikaitwa “Wababe Wanne.” Mazao wanayo. Hayana soko la ndani. Wanazuiwa kuuza kokote wanakotaka.

Ndivyo ilivyo kwa wakulima wa kahawa Kagera na wakulima wa karafuu Unguja na Pemba. Bado kuna ukiritimba ambao hauendani na siasa za watawala za soko huria.

Hakuna mwenye haki wala wajibu wa kuhemea kwa niaba ya wakulima hawa. Wana uwezo wa kijilisha; bali serikali imekuwa ikiwanyang’anya uwezo huo ili iweze kuwatawala kwa urahisi.

Serikali imekataa kufanya hata jambo dogo na kununua nafaka kutoka kwa wakulima, kwa bei nzuri kwa ajili ya kutunisha mfuko wa akiba (GSR). Kwa njia hii yaweza kuchochea mashindano katika kilimo na hivyo wananchi kulima zaidi na chakula kuwa kingi.

Serikali ikishindwa kujenga mazingira ya kutumia mabonde, ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, bahari, madini, misitu na mbuga za wanyama; badala yake ikadai rais wake anakwenda kuomba chakula nje ya nchi, ijue imeshindwa kazi.

Hakuna awezaye kuelewa mantiki ya kuwa ombaomba katikati ya utajiri wa aina hii wa raslimali; wala hakuna atakayehusudu ombaomba katika mazingira ambamo watawala wenyewe ndio, ama chanzo au kichocheo cha njaa na umasikini.

Kwa nini basi tusikubaliane kuwa, watawala wetu wanakwenda nje ya nchi kutafuta utumwa; kwani hawataki kuishi kwa uhuru unaotokana na rasliamli lukuki zinazopaswa kuendelezwa kwa manufaa ya watu, ndani na nje ya nchi yao.

0713 614872
ndimara@yahoo.com

2 comments

Unknown said...

watanzania ni wajinga ndo maana wanashabikia kauli mbovu kama hizo mbona hakuzitoa musoma,mbeya,kagera,shinyanga, au moshi anawaahutubia rimbukeni wasiojua lolote ambao wamkumbatia ufisadi kwa bwana mtanashati rostam kusema kweli kama angeyasema hayo kenya, zambia, malawi, afrika kusini au ulaya hapo hapo wangetawanyika na kupiga mayowe uuuuuuuuwi!mara tatu na ungekuwa mwisho wake lakini kwetu hapa ufanye hivyo huku umevaa kanga na t.shirt akikuvua utabaki mtupu, kusema kweli watanzania sisi ni wajinga acha tufanywe mazoba maana tunasikiliza sana ya shehe yahaya,kilaini,kuwa jk ni mteule.we have to die for our own cause. tunaendekeza sh 2000 za ccm

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mzee Ndimara, sikujua kuwa una blogu kali hivi! Ni mara yangu ya kwanza kutembelea uga wako na nakujua si kuanzia hapa bali kwenye utunzi wa vitabu. Nitakuwa nikikutembelea nawe nitembelee kwenye freethinking yangu nadhani unaipata.
Nimefurahishwa na kutotafuna maneno kwako. Waandishi wengi wanaogopa au tuseme ni wanafiki. Wanaogopa kuita kulego kulego na mlevi mlevi mwizi mwizi fisadi fisadi na mengine kama hayo.

Powered by Blogger.