UJINGA ULIOPATA DIGRII, UPROFESA
SITAKI
Prof. Maghembe anavyokana siasa
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI Profesa Jumanne Maghembe awe mfano wa jinsi usomi unavyoweza kuota kutu, kuwa butu na hata kuwa sumu.
Profesa huyu ndiye waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi; mbunge anayejaribu kutetea kiti chake, lakini kiongozi ambaye wizara yake ina ndimi mbili juu ya haki ya wanafunzi kupiga kura mwaka huu.
Maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya serikali walijiandikisha kupiga kura pale vyuoni kwao. Wizara ilijua hilo. Tume ya Uchaguzi ilijua na kupanga hivyo. Wanafunzi walijua watakuwa vyuoni. Serikali kwa jumla ilijua hilo.
Ghafla serikali ikasema muhula mpya wa masomo katika vyuo vyake utaanza mapema Novemba na siyo mwishoni mwa Oktoba – tofauti ya siku kumi tu.
Maana ya maamuzi hayo ni kwamba wanafunzi hawatakuwa kwenye maeneo walikojiandikisha kupiga kura. Hawatapiga kura. Hapa ndipo zimetokea kauli mbili za serikali zinazoleta utata.
Kauli ya kwanza ni kwamba maandalizi ya malipo kwa wanafunzi wanaoomba mikopo hayatakuwa yamekamilika mwishoni mwa Oktoba.
Kauli ya pili na iliyotolewa na waziri wiki iliyopita ni kwamba, vyuo vitafunguliwa mapema Novemba kwa sababu kumekuwa na mabadiliko katika mfumo wa udahili.
Waziri anataka kila mmoja amwamini, yeye na serikali yake, kuwa katika siku 10 (kumi tu), ambazo ni tofauti kati ya tarehe ya awali ya kufungua vyuo na tarehe mpya, maandalizi ya malipo yatakuwa tayari na tofauti ya muda wa udahili itakuwa imetoweka.
Hivi ni visingizio. Ni njia ya kuwapora wanafunzi fursa na haki yao ya kupiga kura, hasa wale ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwawezesha kwenda vyuoni mapema; au kuwa karibu na vyuo ili wapige kura na siku 10 baadaye waingie vyuoni.
Katika baadhi ya nchi duniani, kuna mifumo ya kuhakikisha raia wake waishio ughaibuni, wanashiriki zoezi la uchaguzi huko watokako. Serikali huhakikisha kila kura inakusanywa.
Walioko katika ofisi za kibalozi nje ya nchi, wafanyabiashara, wanafunzi na hata walioko katika majeshi, huwezeshwa kupiga kura makwao kutoka pale walipo.
Tanzania, hapahapa, humuhumu, maelfu ya kura yanaachwa hivihivi, njenje. Kuna tatizo. Siyo rahisi kufikiri kuwa siyo njama za kuzika utashi wa maelfu ya wanafunzi. Kwa kadri hali ilivyo, kuna uwezekano mdogo sana kwa serikali kubadili mwelekeo.
Hapa ndipo kuna mtihani wa nyongeza kwa wanafunzi vyuoni: Kufanya vyovyote iwavyo, kuwa maeneo walikojiandikisha – bila kusikiliza waziri wala tume – ili waweze kupiga kura.
Hatua hiyo, inayoweza kufanywa na wanafunzi wachache, wengi au wote, yaweza kuwa ushahidi wa kudumu wa kupigania haki na kichocheo kwa vijana wengi katika kuthamini na kupigania haki zao.
Ni hatua hii pia itakayoweza kumrudisha darasani Prof. Maghembe, mara hii akifundishwa na wanafunzi wa umri mdogo, juu ya haki ya raia ya kupiga kura kuchagua yule anayeona anafaa kumwongoza.
Kwani ni Maghembe aliyekaririwa wiki iliyopita akisema kuwa anawashangaa wanafunzi kuweka shinikizo la kuwa vyuoni mapema ili waweze kupiga kura.
Amenukuliwa pia akisema vyuo vya elimu ya juu siyo taasisi za kuendesha siasa bali ni “…maeneo yanayotumika kufundishia wataalamu wa kada mbalimbali.”
Tayari wanafunzi wamemjibu profesa. Wamemuuliza: Kama vyuo ni mahali pa kazi pekee ambayo waziri ametaja, kwa nini chuo kiliruhusu uandikishaji wanafunzi, tena hapo vyuoni?
Prof. Maghembe hawezi kupata jibu kwa swali hili kama ambavyo hawezi kupata majibu kwa maswali mengine kuhusiana nalo.
Kwa mfano, profesa anasema nini kuhusu siasa kuwa moja ya masomo muhimu na kwamba chuo kikuu ni eneo la kuoka wataalamu katika sayansi ya siasa? Na hilo linafanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kama hajui hilo, basi kuna kila sababu ya kutilia mashaka nia, shabaha, uwezo wake wa uelewa na elimu yake, kwani kupiga kura siyo zoezi la ndimu mchangani.
Pamoja na kuoka na kuipua wataalamu katika sayansi ya siasa, elimu ya kiwango cha chuo kikuu inapaswa kuwa ufunguo wa akili katika nyanja mbalimbali za maisha, ikiwemo siasa.
Aidha, siyo lazima uwe katika idara au kitivo kinachohusiana na siasa ndipo ujue mazingira yako ya kisiasa na jinsi zinavyokuathiri – wewe na jamii yako.
Hii ni kwa kuwa kila eneo la jamii linahusika na kuathiriwa – vizuri au vibaya – na siasa za wakati uliopo. Ndivyo ilivyo pia katika vyuo vikuu.
Maamuzi yanayotumiwa na watendaji na kufanya nchi hii iendelee kuwa makazi ya watu wengi, woga, masikini na wajinga, ni ya kisiasa.
Taratibu na mazingira yanayosababisha watoto wamalize madarasa saba bila kujua kusoma na kuandika; yanayolea wizi mkuu na ufisadi usiomithilika; ama zimetokana au zimeathiriwa na maamuzi ya kisiasa ya wakati huu.
Mfumo wa maisha unaofanya waliohitimu chuo kikuu, hata maprofesa, wapauke haraka na wengine hatimaye kupoteza uwezo wa kufanya maamuzi na hata kusoma na kuandika; umeathiriwa kwa kiwango kikubwa na siasa za nyakati tulizomo.
Wahitimu vyuo vikuu, wanaokwenda kuwa walimu, wanasheria – mawakili na mahakimu – madaktari, mainjinia, mabwana na mabibi shamba na mifugo, wana-mipango na wengine, hawanabudi kujua mwelekezaji ni siasa.
Mfumo wa utawala wa wanafunzi vyuoni, unaoamuliwa kwa njia ya uchaguzi wa viongozi wao na kushirikisha kila mmoja bila kujali anasomea nini, ndilo rejeo la haraka kwamba wasomi vyuoni wanapaswa kuwa hai juu ya kinachotendeka katika jamii na hasa kinachogusa haki zao.
Kama Profesa Maghembe anafikia hatua ya kusema siasa haziwahusu walioko vyuo vikuu, ama amesahau, amepotoka au amepauka.
Siyo rahisi kuzungumzia elimu ya juu bila kugusa mustakbali wake kwa jamii, kupitia mipango iliyowekwa au kuathiriwa na siasa zilizopo.
Kwa hiyo, kudai kuwa vyuo siyo mahali pa siasa na kuweka vikwazo kwa wanafunzi ili wasifurahie haki yao ya kuchagua viongozi wanaotaka, ni kuendeleza ujuha ambao uliishafukuliwa na kutupwa nje ya vyuo na hata shule nyingi nchini.
Maghembe hasononeki kwa wanafunzi kushindwa kupiga kura. Serikali yake pia haisoneneki. Labda walishajua kuwa wanafunzi hawatapigia kura chama chao.
Lakini walijuaje? Hiyo si kama kufyatua risasi gizani ambako waweza kukuta unaumiza au unaua mkeo, baba au mwanao?
Zimebaki siku 21 kupiga kura katika uchaguzi mkuu. Wanafunzi wa vyuo vikuu bado wanasubiri serikali itende maajabu.
Hayapo. Hayaji aua hayaji haraka.
Kuna kazi moja ambayo wanafunzi wanaweza kufanya iwapo serikali haitabadili msimamo. Wabaki walipo. Wahimize wananchi kuamka mapema na kupiga kura. Wafanye uwakala kwa vyama vyao.
Kufanya hivi siyo kudhalilika. Njia hii ina faida mbili kuu. Kwanza, kuanzia hapo, wataelewa hila na husuda walizonazo watawala na kwamba haziondoki kamwe kwa sala kanisani wala msikitini.
Pili, watajifunza kuchukia na kuchukua hatua – mwanzo na mwisho wa lelemama – kwa njia ya kujiunga na wanaharakati kupigania haki zao na wote, ambao wakati wowote, waweza kunyang’anywa haki zao.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
(Imechapishwa katika Tanzania Daima Jumapili ya 10/10/2010)
No comments
Post a Comment