MARUHANI WALINDA IKULU DAR
SITAKI
Kikwete anayelindwa na mashetani
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI kusikia na kuamini kuwa vyombo vya ulinzi nchini vimeshindwa kazi – Polisi, Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Usalama wa Taifa.
Sitaki kuamini kuwa tayari walinzi wanakaa tu; lakini wanalipwa mishahara na marupurupu mengine – wanatumbukiza mifukoni na matumboni – bila kufanya kazi yoyote ya kumlinda “Rais wa Jamhuri ya Muungano.”
Sitaki kuamini kuwa nadharia za kisasa za ulinzi, silaha za kisasa na uvumbuzi unaoendelea katika medani ya ulinzi, vinaweza kutupwa chini na badala yake akatafutwa mtu, watu au vikundi vya kumlinda rais.
Sitaki kukubali wawepo watu binafsi, vikundi na makampuni ya ulinzi; tena ya kumlinda rais – na huenda na wananchi na mali zao – ambavyo havitambuliki kikatiba.
Sitaki kuamini kuwa walinzi – waliosomea kazi hiyo na hata waliopendelewa kuwa katika nafasi hiyo muhimu – wanaweza kukubali “kuwekeana mikataba” na watu binafsi, makampuni na mataifa ili kulinda nchi yao.
Sitaki kuamini pia kuwa walinzi – wataalam wa zana na wenye maarifa makuu – wanaweza kujisalimisha kwa Sheikh Yahya Hussein ambaye anaona ulinzi wa rais na ikulu sharti uwe mikononi mwake.
Sitaki kuamini kuwa rais wa Jamhuri ana taarifa kuwa walinzi wake hawatoshi kumlinda; hawawezi kumlinda na kwamba zana zao na maarifa yao vimeshindwa kumwekea usalama unaostahili.
Sitaki kuamini kuwa rais anaamini kuwa hana ulinzi wa kutosha; kwamba majeshi yake yamechoka na kuchakaa na sasa sharti atake, apewe au atafutiwe ulinzi wa nyongeza nje ya silaha na maarifa yanayotambuliwa kitaifa na kikatiba.
Sitaki kuambiwa kuwa rais anaweza kukubali kulindwa na vyombo vingine nje ya vile tunavyofahamu kitaifa na kikatiba. Atakuwa amedharau nchi yake, watu wake, majeshi yake na katiba ya nchi yake.
Lakini mnajimu Sheikh Yahya Hussein anasema, bila woga wala aibu kuwa “sasa atamlinda Rais Jakaya Mrisho Kikwete” kwa ulinzi maalum ambao hauonekani.
Mnajimu huyo wa Magomeni, Dar es Salaam, alisambaza waraka katikati ya wiki hii akielezea jinsi Rais Kikwete alivyoandamwa na wabaya na kwamba kuishiwa nguvu uwanjani Jangwani tarehe 21 mwezi uliopita, kulitokana na uchawi.
Haijafahamika iwapo Sheikh Yahya ndiye alitangua uchawi uliomwangusha Kikwete; ulikuwa uchawi wa kiwango gani; uliolenga nini na uliotoka kwa nani.
Kwa kauli ya mnajimu, haikufahamika “amemwokoa” mara ngapi, amemkinga mara ngapi na anaaminika kwa kiwango gani kwa mkuu wa nchi.
Mwaka jana alipotabiri kuwa atakayejitokeza kushindana na Kikwete, ndani ya chama chake, atakufa kifo cha ghafla, ndipo wengi walianza kumhusisha Yahya na wapangaji wa ofisi kuu ya nchi.
Kwa nia njema na labda kwa kutambua kazi yake nzuri, msemaji wa ikulu alipoulizwa juu ya kauli ya Yahya, alisema kuna haja ya “kuheshimu kauli” ya kila mmoja. Lakini Jakaya Kikwete hakusikika akisema lolote.
Haikufahamika iwapo kwa “kuheshimu kauli” msemaji wa ikulu alikuwa na maana ya kila mmoja kuwa na haki ya kutoa kauli au alikuwa anasisitiza umuhimu wa kutambua na kuzingatia utabiri wa Sheikh Yahya.
Wakati huo, Sheikh Yahya hakusema iwapo amemwekea kinga Rais Kikwete. Hakusema kifo cha ghafla kitaletwa na nani na nini – nyota, mwezi, mizimu katika mzunguko wa kinga-nikukinge au ua-nikuue.
Bali vyovyote iwavyo, kuibuka tena kwa mnajimu zikiwa zimebakia siku 51 kufanya uchaguzi mkuu, kumechukuliwa na wengi kuwa njia ya kuimarisha utabiri wake; kuongeza nguvu za “kinga” yake na hata kuonyesha “mteja wake” kuwa hajamtupa mkono; pamoja na yote yanayojitokeza.
Hii ni mara ya kwanza kwa Sheikh Yahya kusema analinda rais aliye ikulu. Uhusiano huu kati ya mtu binafsi na ofisi kuu hauwezi kuwa umejitokeza ghafla.
Yawezekana pia uhusiano huu umekuwepo kati ya mganga huyu mwenye “ulinzi” (unaozidi ule wa maaskari na mashushushu) na marais waliotangulia; bali hapa hatuna uwezo wa kuwasemea.
Swali la haraka ambalo kila mmoja anaweza kujiuliza ni: Mlinzi huyu wa majeshi yasiyoonekana, analipwa posho au mshahara? Analipwa kiasi gani?
Nani anamlipa mlinzi huyu? Fedha hizo zinatoka kwenye kodi za wananchi au yule ambaye anajisikia amelindwa na kufanikisha matakwa na malengo yake?
Nikiwa bungeni pale Dodoma, mwaka 1997, mbunge mmoja wa CCM aliyekuwa akifurahia hoja zangu, alinitambulisha kwa wageni kutoka jimboni mwake ambao ambao pia walitambulishwa kwa wawakilishi bungeni.
Alitambulisha wageni saba; wakiwa wanawake watatu na wanaume wanne. Alinieleza kuwa aliyemtambulisha mwishoni “ndiye mtu wangu muhimu” – mganga/mlinzi.
Uganga na kinga ndani ya nyumba za watu binafsi. Uganga ndani ya ofisi za serikali. Uganga ndani ya bunge. Uganga ndani ya ikulu – kwa kuombwa au kwa kujipendekeza. Uganga!
Nimekumbuka ikulu ya Banjul, Gambia ambako tuliambiwa mapema mwaka jana kuwa Rais Sheikh Profesa Alhaj Dk. Yahya Abdul-Aziz Jemus Junkung Jammeh, naye ni mganga wa aina yake; pamoja na “kutibu ukimwi.”
Katikati ya ulofa huu unaoitwa kinga, watoto wa kike wa hata umri wa miaka 12, wanabakwa na wazungu – katika mahoteli na mabaa yaliyotapakaa mjini Banjul; kufanywa wajawazito na kutupwa mitaani wakilia na kusaga meno. Umasikini wa kutaga mayai!
Imani za “kukinga” zimedumaza akili; zimekwamisha uwezo wa kufikiri; zimezamisha matumaini ya wengi huku zikifanya watawala washughulikie kitu kimoja tu: kujikinga.
Bila shaka hapa Sheikh Yahya alikuwa anajitangaza ili wagombea nafasi mbalimbali wapate kumkumbuka na kumwendea, hasa wakizingatia kuwa ndiye mtoa kinga kwa rais badala ya vyombo vya dola.
Wale askari wasioonekana; zile silaha zisizoonekana; ule utaalam usiosomewa vyuoni wala kufundishwa majumbani; ni mashetani ambao mnajimu anataka yamlinde Kikwete.
Tunasubiri mgombea urais wa CCM kukubali kwa faragha au hadharani kupata ulinzi huo; jambo ambalo litakuwa na maana moja tu: kwamba amefukuza kazi majeshi yote nchini na kuajiri mashetani.
Haitakuwa ajabu kuona hata walinzi wake kwenye msafara wake wa sasa wakiondolewa na yeye kubaki na wapiga debe wa umoja wa vijana wa chama chake. Tunasubiri.
0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
No comments
Post a Comment