Header Ads

LightBlog

UNYANYASAJI WANAWAKE WAENDELEA

SITAKI
Makongoro anavyonyanyasa shemeji yake

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Makongoro Nyerere aanzishe mgogoro kati yake na Leticia Nyerere, mke wa zamani wa ndugu yake, Madaraka Nyerere.
Vyombo vya habari vimemnukuu Makongoro akisema, kwenye mkutano wa hadhara jimboni Kwimba, kwamba Leticia asijaribu kujihusisha na ukoo wa Nyerere kwa kuwa tayari aliishachika.

Siyo rahisi kujua iwapo Makongoro ameagizwa na Madaraka kusema aliyoyasema; kwani hakusema hivyo. Haijafahamika iwapo kulikuwa na kikao cha ukoo kuamua juu ya matumizi ya jina la Nyerere.

Lakini muhimu zaidi ni kwamba, haijafahamika kuwa kila anayejitambulisha kuwa wa ukoo wa Nyerere anapendwa zaidi, anaaminika na kupewa kura.
Hapa kuna upogo katika jamii ambao umefanya wanawake watupilie mbali majina ya wazazi wao na badala yake kujibandika majina ya waume zao.

Ni upogo uliogeuka mtindo, hasa mume anapokuwa mtu wa kujiweza na mke anapenda kuitwa Mrs. Fulani – mwenye mali, nyumba nzuri, magari na fedha zisizokauka mfukoni.
Bali ni kupoteza utambulisho. Kipi bora, kujitambulisha kama mtoto wa Fulani au mke wa Fulani? Tukiwa sekondari kulikuwa na mwanafunzi mmoja aliyeitwa Festo Kokugonza. Mwendelezo mwingine huo.

Kwamba siyo lazima kuwa na ubini wa baba. Waweza pia kuwa na ubini wa mama na maisha yakasonga mbele bila kelele wala mikwaruzo.

Lakini hebu turudi kwa Leticia Nyerere. Je, haijulikani kweli kwamba alikuwa ameolewa katika ukoo wa Nyerere? Si taarifa hizi ziko wazi kwa kila mmoja kujua, hasa wakati huu wa kutafuta ufalme wa kisiasa?

Je, ni lazima kufuta jina la mume pale mwanamke anapomwacha mume au anapoachika? Je, kuendelea kulitumia kuna maana kwamba unataka kurudi au hutaki kuharibu utambulisho uliokuwa tayari umejengeka?

Je, kuendelea kulitumia jina hilo kwa utambulisho tu kuna maana kuwa unalithamini sana au sasa ni lebo maalum ambayo kuibadili kunaweza kukugharimu?

Je, kujigamba tu kwamba mtu anatoka katika ukoo fulani kunaweza kuleta manufaa yoyote wakati anaowaambia wanajua kuwa sivyo ilivyo?

Je, hata kama mtu atajidai na kujinadi kuwa ni wa ukoo fulani, ukoo huo una kitu gani cha ajabu na cha manufaa kwa jamii kiasi kwamba kujitambulisha nao tu wewe utakuwa umenufaika?

Nyerere alionyesha mfano mmoja mkubwa ambao mabwege wengi huutumia kumlaumu. Alijua watoto wake ni watoto kama watoto wa watu wengine.

Hakuwapendelea kwa kuwapeleka shule zenye majina makuu au kuwapeleka Ulaya na kuwaficha huko na ujinga wao, ili warejee hapa kwa mbwembwe wakati hawana akili; kama viongozi wengine wanavyofanya.

Kama kuna lolote katika ukoo wa Nyerere ni kwamba ulimzaa Julius Kambarage Nyerere; aliyetokea kuwa jasiri, mwenye uwezo wa kiakili na aliyeongoza harakati za kuleta uhuru wa Tanganyika.

Kama kuna lolote katika ukoo huu ni kwamba, hatuhitaji kutafuta zaidi, bali kwa ufupi tu, ulitoa Nyerere kama tulivyomwona, tulivyomfahamu na tulivyomwelewa. Basi.
Waliobaki – mke wake, watoto wake na wengine katika ukoo – sharti wajisimamie na hawawezi kwenda kwa sifa ya ukoo wa Nyerere.

Jamii itawaona na kuwaelewa kama mtu mmojammoja, mwenye sifa yake binafsi, udhaifu wake binafsi, ubora wake binafsi; kwani hakuna kitu maalum kinachoweza kuitwa alama ya ukoo wa Nyerere.

Hii ndio maana, pale Butiama na katika ukoo, hakuna kinachomwakilisha Nyerere kama Nyerere – akili yake, uwezo wake, siasa zake, visheni yake, utashi wake na mengine mengi.

Alichokumbuka Makongoro – ng’ombe 30 – ambao baba yake alitoa ili Madaraka amwoe Leticia, ni historia isiyofutika na ambayo inamwingiza mama huyo katika familia mpya, ukoo mpya hata usingekuwa wa Nyerere.

Isipokuwa siyo siri, kwamba akili na uwezo wa Nyerere havikuwa mali ya ukoo; vilikuwa mali yake binafsi, lakini kwa uchambuzi mpana – hazina ya taifa.
Bahati mbaya hakuvirithisha kwa yeyote – awe mke wake, watoto au ukoo wake. Ukitaka waweza kusema hivi; kwamba wanaovitambua, kuviheshimu na kuvienzi, ni watu wengine, wakiwemo wa mataifa na wala siyo hata chama chake alichoanzisha – CCM.

Kuna mamia kwa maelfu ya watu ambao wanaweza kumtetea Nyerere; kutaka asichafuliwe kwa hoja kubwa na nzito kwa kuangalia aliyoyafanya kuliko kung’ang’ania ukoo.

Vyovyote itakavyokuwa, kwa kuwa Leticia ameingia ulingoni, ataulizwa anatoka wapi; hilo jina la Nyerere alilipataje; huyo Nyerere ni yupi na yuko wapi? Atajieleza.

Watakaopenda kumshangilia kuwa aliishaonja maisha katika moja ya nyumba ya watoto wa Julius Nyerere, acha waseme. Watakaosema “unyerere” wake hauna uzito, acha wapuuze.
Bali kwa Makongoro kufunga safari kutoka Musoma hadi Kwimba kumwambia shemeji yake asijitambulishe na ukoo wa Nyerere, hakika ni njia nyingine ya udhalilishaji.

Julius Kambarage Nyerere hakuwahi kuwa, na siyo mali ya ukoo. Inawezekana Leticia anamtaja leo baada ya kuingia katika siasa, kama wengine wanavyomtaja.

Huwezi kukaa na Nyerere, kwa mfano, akichimba mtaro wa mabomba ya maji wa Ntomoko; akijenga nyumba za wanakijiji Kibondo kwa wiki mbili; halafu ukamsahau, wakati una rais anayewekewa mkeka na kuvalishwa glovu mikononi ndipo apande mti.

Huwezi kusoma vitabu na maandishi mengine ya Nyerere; ukaelewa fikra zake halafu ukashindwa kumuunga mkono au kumpinga na hata kumsema mara kwa mara kufuatana na jinsi ulivyomwelewa; hasa unapokuwa na rais asiye na hoja za kutoa changamoto kwa ubongo.

Huwezi kuwa na Nyerere anayeanzisha chama cha siasa na baadaye kusema kinanuka rushwa na kutishia kukikimbia akisema “siyo baba, siyo mama;” wakati una utawala ambao unachefua kwa rushwa, wizi na ufisadi usiomithilika.

Ushauri wangu kwa rafiki yangu Makongoro Nyerere ni kwamba, siyo tu amwache shemeji yake Leticia achanje mbuga na kutafuta ubunge kwa uhusiano wowote ule; bali awaache wote wanaomtaja Nyerere, kwa wema au ubaya na kwa sababu yoyote iwayo.

Nyerere siyo mali ya mtu mmoja, familia au ukoo. Na Nyerere hahitaji utetezi; bado anajiweza, hata baada ya kuaga dunia.

Aidha, tusisahau kuwa upogo uliogeuka mtindo, utaendelea kutumiwa na wanaume wengi kudhalilisha wanawake, wakidhani kuwa hata wanapokuwa hawawagharamii tena, bado wananufaika kwa majina yao.

Huu siyo tu uongo, bali ujinga ulioambatana na ubabe wa miaka mingi na unaoendelezwa na ulimbukeni miongoni mwa wanaume, wakifikiri au kudhani tu kwamba majina yao yana ulimbo wa maisha bora.


Mwisho

No comments

Powered by Blogger.