Header Ads

LightBlog

SHERIA YA MABWEGE HII HAPA
SITAKI

Na Ndimara Tegambwage

Lugha ya Tume ya Uchaguzi Haieleweki

SITAKI uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wa kulazimisha matumizi ya Kiswahili peke yake katika kampeni za uchaguzi mkuu.

Nakumbuka ilikuwa hivyo mwaka 1995 wakati nagombea ubunge jimbo la Muleba Kaskazini. Bado ni hivyo hata leo. Safari hii matumizi ya lugha yamekuwa moja ya masharti ambayo vyama vimelazimishwa kusaini.

Kiswahili ni lugha ya taifa. Ni lugha kuu inayotumiwa na wengi ndani ya soko la ajira – serikali na makampuni yake, shuleni na baadhi ya vyuo; katika biashara za kati, ndogo na katika mawasiliano ya kawaida.

Kiswahili kimeenea mijini – miji mikubwa na midogo na katika baadhi ya vijiji ambako kimetumiwa kwa muda mrefu au wakazi wake wamekuwa na mwingiliano mkubwa na wale wanaozungumza lugha hii.

Kwingineko Kiswahili kimeenezwa na shule za msingi na sekondari ambako walimu na wanafunzi wameathiri matumizi ya lugha za asili, bila kusahau juhudi za makusudi za kupambana na ujinga kwa njia ya Elimu ya Watu Wazima (Kisomo Chenye Manufaa).

Kampeni za kisiasa nazo zimekuwa na mchango mkubwa kwa uenezi wa lugha hii, zikiongezea kwa mipango ya awali, mara baada ya uhuru, ya kusambaza vipeperushi na filamu juu ya matakwa na mbinu za “maendeleo” katika Kiswahili.

Pamoja na yote hayo, bado nchini Tanzania kuna maeneo ambako kuta za lugha za asili zingali imara; na hasa imara sana.

Ni lugha hizi za asili ambazo zimeendelea kuwa chimbuko la misamiati na istilahi mbalimbali kwa matumizi ya sasa ya kukuza Kiswahili na hata kueleza maana halisi ya kile wanachosema wale wanaotumia lugha yao.

Siyo bahati mbaya basi kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuna idara inayoshughulikia lugha za asili. Watafiti katika eneo hili hawafanyi kazi ya “kuzienzi” lugha hizi za asili – iwapo tutaazima vineno vya kisiasa – bali wanavuna maarifa ndani ya lugha hizo na kupitia lugha hizo.

Kuwepo kwa lugha hizo kunakoweza kusaidia kuelewa jamii na utamaduni wake – kwa kudhamiria au kwa utuki tu – kumekuza na kunawirisha Kiswahili na hata lugha nyingine za asili.

Hii ndiyo maana kumekuwa na wanaharakati wa ngeli na ngeli wakitetea kuendelea kuwepo lugha za asili zilizohifadhi hekima na falsafa za jamii ambako zinatumika.

Aidha, ni lugha hizi ambazo watafiti wanaoumba kamusi za Kiswahili na hata lugha nyingine zinazotumika katika maeneo haya, wanakimbilia kupata maneno halisi – hasa istilahi katika ufundi na teknolojia ya kale na sasa.

Hizi basi siyo lugha za kuua hivihivi tu kisiasa. Bado zina nafasi muhimu katika jamii kama vile walivyo watu wanaozitumia; na wanaendelea kuwa Watanzania hata kama hawawezi kuongea Kiswahili.

Sasa Tume ya Uchaguzi inasema wanasiasa wanaotafuta kura katika uchaguzi mkuu wasitumie lugha nyingine yoyote ile isipokuwa Kiswahili.

Maagizo ya tume yanafanana na kanuni za Wizara ya Habari zinazolazimisha kila chombo cha habari kilichosajiliwa nchini, kutumia ama Kiswahili au Kiingereza – lugha mbili peke yake.

Ukichanganya haya ya maeneo mawili, utaona kuwa wasiojua Kiswahili hawapaswi kujua kinachotangazwa redioni au kinachoandikwa kwenye magazeti.

Ni hivi: Kama hawajui lugha hizo – Kiingereza na, au Kiswahili – basi potelea mbali. Ndiyo tafsiri ya kile ambacho Tume inasema na ambacho serikali inasisitiza. Ndivyo wenye vyama walivyoweka saini kutetea.

Anayeomba kura, aingie Usukumani. Maeneo ambako Kiswahili hakitumiki kwa kiwango kikubwa. Pale ambako maneno ya Kiswahili yanatumika kwa ushabiki tu – ama kueleza kuwa anayeyajua ni “mkora” au “mwerevu” kutoka mjini.

Hapa, Tume inataka anayeomba kura atumie Kiswahili. Atatumia. Baada ya hotuba kuna kipindi cha maswali. Hakuna anayeuliza kwa kuwa hakuna aliyeelewa. Kuna haja gani basi ya kufanya kampeni katika “lugha ya kigeni?”

Nendeni Loliondo vijijini, katika mkoa wa Arusha. Kuna shule za msingi. Wanafunzi na walimu wana akili nzuri. Wanajua kuwa Kiswahili na Kiingereza, zote ni lugha za ngeni.

Baadhi ya walimu wanafundisha kwanza kwa Kimasai na baadaye kuweka katika Kiswahili. Njia bora kabisa. Ni kwa misingi sahihi kwamba lugha ya kufundishia iwe ile ambayo mwalimu na mwanafunzi wanaelewa. Mara hii ni Kimasai.

Wazazi katika eneo hili ambao ndio wapigakura, wanajua vema lugha yao moja – Kimasai. Wanaokwenda magulioni mara kwa mara ndio wameokoteza istitahi za kibiashara katika Kiswahili.

Sasa aende mwanasiasa anayetafuta kura. Amwage hapa kampeni yake kwa Kiswahili. Ataondoka kama alivyokwenda. Mtupu. Bila kura hata moja. Kwa nini? Kwa kuwa hawakumwelewa; lakini pia kwa kuwa naye ni mpumbavu – anatumia lugha ambayo anajua vema kuwa anaowaambia hawaijui.

Hili lina tafsiri moja kuu. Kwamba kwa miaka 50 ya utawala wa chama kimoja, watawala wamekuwa wakiimba na kijipiga vifua kuwa wana “lugha ya taifa – Kiswahili.”

Kumbe yamekuwa majigambo yasiyo na mashiko. Wameshindwa kueneza lugha hiyo hapa nchini kama walivyoshindwa kutumia wataalam wake kuigeuza kuwa “bidhaa” ya kuingiza fedha za kigeni.

Wameshindwa kukuza Kiswahili; wameshindwa kukuza lugha za asili; wameshindwa kutoa ajira kwa wanaojua lugha hizo ili wawe wakalimani kwa wasiojua lugha za kigeni; wamebakia na amri – “Tumia Kiswahili!”

Kwa amri na mantiki ya Tume, wasiojua Kiswahili “shauri yao.” Hii siyo haki.

Wananchi wanaojua lugha zao wanastahili kupelekewa kampeni katika lugha zao; na kama njia ya kueneza lugha kuu, wapiga kampeni waombwe kudondosha maneno ya Kiswahili hapa na pale kama kupanda mbegu.

Vinginevyo itafikiriwa kuwa serikali, na vyombo vyake, imeamua kuwatenga, kuwatelekeza, kuwasahau na kuwanyima haki ya kushiriki siasa za nchi yao, wale wote ambao hawajui Kiswahili au Kiingereza.

Sheria, kanuni na taratibu zinazoondoa haki ya mtu; kupoteza utashi wake, tena ndani ya nchi yake, hazistahili kuheshimiwa na haitakuwa mara ya kwanza kukataa kuzishemu.

Njia bora ya kuzipinga ni kuongea na wananchi katika lugha yao. Wananchi ndio watakuwa watetezi.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

No comments

Powered by Blogger.