Header Ads

LightBlog

WANAGAPI WATAPIMWA AKILI TANZANIA?

Vimbwanga vya Ikulu, BoT na walinzi

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kupuuza vimbwaga. Vina maana yake katika mazingira maalum ya utawala uliopo. Ilitokea katika historia ya nchi hii, moto ukaunguza Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Wengi walistuka. Wengine walishangaa. Wengi walihisi kulikuwa na njama za kuficha wizi au kuharibu ushahidi kwa kuchoma nyaraka. Ndani ya benki maofisa walikanuliana macho na kauli za “sihusiki” zikawa salaam za kila siku.

Kilichostua wengi wakati huo na hadi sasa ni aliyeshitakiwa. Alikuwa mlinzi – korokoroni. Kesi ilinguruma. Ulijengwa ushahidi wa kushindilia na kuokoa. Hukumu hii hapa. Ni mbele ya jaji.

Jaji anachukua hukumu iliyoandikwa. Anageuzageuza kurasa. Anateremsha miwani yake ambayo inagota kwenye pua. Anawaangalia waliofurika mahakama kwa kupitia juu ya miwani yake. Anawaangalia washitakiwa. Anaanza kusoma hukumu.

Ni maneno mengi. Ni sentensi nyingi. Ni aya nyingi kwenye karatasi nyingi. Mahakama imetulia, tuli! Anasoma. Anahoji na kujijibu. Anatulia kwa sekunde kadhaa na kuvuta pumzi huku waliojaa mahakama wakisubiri “hukumu.”

Kwa kauli zisizo na usumbufu wa maneno marefu, magumu na ya mchanganyiko wa Kiingereza na Kilatini, ambayo hutumiwa na wanasheria wengi, jaji anasema kuwa, kila anapoangalia pale mahakamani, haoni waliotenda jinai ya kuchoma benki.

Alikuwa na maana kwamba wahusika hawakuwa mahakamani. Hawakushitakiwa. Aliyekuwa kizimbani, kwa maoni yake, uelewa na kwa mujibu wa sheria, hakuwa na hatia. Alimwachia. Mlinzi hakuelewa. Wasikilizaji walipigwa na mshangao.

Waliochoma benki hawajawahi kufikishwa mahakamani hadi leo. Hata hivyo, mabenki hayaungui kwa moto wa sigara za wapita njia na hakuna joto la kukamata watuhumiwa wengine. Labda moto huo ulikuwa mwanzo wa kindumbwendumbwe kilichoko BoT leo.

Sikiliza ya Ikulu, Dar es Salaam. Ni alfajiri au asubuhi. Ikulu kunawaka moto. Nani kaunguza makao ya rais (mara hii yumo Benjamin Mkapa)? Wengi wanastuka. Wengine wanashangaa. Wengi wanahisi kuna kilichounguzwa ili kuharibu ushahidi.

Magari ya kuzima moto ikulu hayapo. Wanaowahi kufika ikulu ni kampuni binafsi ya ulinzi na zimamoto. Lazima walinzi wa langoni wajiulize iwapo zimamoto ya “moto wa binafsi” inaweza kuzima moto wa “ofisi ya umma.”

Subiri kidogo. Wakawasubirisha. Moto haukusubiri. Hadi uamuzi unafanywa, kwamba kampuni binafsi yaweza kuzima “moto wa umma,” moto uliishatafuna vipande vya ikulu.

Hapa hakuna kesi. Wataalam wanaeleza chanzo na hakuna wa kukamata. Lakini ikulu imeungua na ikulu haziungui kwa moto wa sigara za mpitanjia. Ni vimbwanga vya Tanzania.

Wiki iliyopita mwanaume mmoja aliingia ikulu bila kubisha hodi. Akaenda hadi maeneo ya ofisi. Bila shaka akakagua au akashangaa mandhari ya ofisi kuu ya taifa. Kwani wale ndege kishingo – tausi, wanaoranda bustanini humo kila siku hulipa kiingilio?



Baada ya utalii huu wa muda mfupi, mwanaume huyo alichuma ua bustanini ikulu; labda kwa shabaha ya kutaka kuwaonyesha wenzake kuwa alikuwa ndani ya ikulu bila kukaribishwa na rais wala ofisa yeyote. Akaanza kutoka kupitia lango kuu.

Tofauti na vimbwanga vya BoT na moto wa ikulu, hiki kina manjonjo ya aina yake: Kabwela asiye na kitanda kaingia ikulu bila kikwazo. Walinzi walikuwa wapi? Mtoto wa watu kajiingilia ikulu na analo la kusimulia, nyumbani au kijiweni.

Bahati – yoyote ile – mbaya au nzuri, mwanaume huyo akadakwa langoni akiwa anatoka. “Unatoka wapi wewe? Kwanza uliingiaje mpaka kule?” Ni maswali lakini hayana uzito bali mwanaume huyo hafanyi mikwara. Anajieleza. Huko ndiko wanaita kumatwa. Sasa kuna taarifa kuwa mtu huyo apelekwe hospitali kupimwa akili.

Katika hali yakawaida, nani anastahili kupimwa? Hapa kuna kijana aliyeingia ikulu bila kelele wala mikwaruzo na alikuwa anatoka bila kubughudhi yeyote isipokuwa akiwa amebeba ua alilochuma. Huyu apimwe nini?

Pale ikulu anakaa rais wake. Wanakaa watumishi wa umma. Wapo askari wa kulinda amani na amani ni amani yake na wakaao ikulu na wengine wanaoingia. Apimwe nini?

Si angepimwa asiyejua kuwa ikulu inapaswa kuwa eneo la utalii wa watu wa nje na ndani ya nchi na kwamba ni moja ya vivutio na sehemu ya elimu kwa jamii?

Kati ya walinzi na mwanaume aliyeingia ikulu bila hodi, nani apimwe akili? Wale ambao hawakuona mtu anaingia na aliyeingia na kutoka bila kufanya baya lolote, nani hasa apimwe akili?

Kwanza ikulu imekuwa moja ya “vijiwe” maarufu. Imezungukwa na watafuta kivuli wakati wa jua kali; wauza maji, karanga na kahawa. Hivi karibuni, baada ya wakazi wakuu wa ikulu kufoka ndipo askari wakazizunguka na kufanya kamatakamata ya zimamoto.

Lakini Makamu wa Rais Mohammed Shein amestuka zaidi hivi karibuni. Anasema ofisi zimegeuzwa soko. Ni biashara “mtindo mmoja.” Wauzaji wanaingia na kutoka, utadhani kazi za serikali zimehamishiwa kwingine; kilichochukua nafasi hiyo ni uuzaji na ununuzi wa sidiria, suruali, chupi, t-sheti, blausi, mashati, vipodozi na nywele za watu wa kale!

Wangapi watapimwa akili? Yule tu aliyeingia ikulu au na walinzi wa ikulu, watumishi wote wa ikulu, wakuu wa ikulu, wafanyabiashara – wa kuuza na kununua – wa ikulu? Nani atasalia katika kupimwa akili? Wauza karanga getini?

Ukimaliza vituko vya ikulu na BoT, njoo kwenye vituko vya kupotea kwa vilaputopu. Kwa maana ya sasa, “laptop” ni kompyuta ndogo ya mkononi au mezani. Inatumika kama kompyuta yoyote ile bali ni rahisi kubeba.

Sasa sikiliza vimbwanga vya laputopu. Leo laputopu ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) imepotea. Wanasema imeibwa “kiaina.” Huyu ndiye amekabidhiwa mamlaka ya kuamua nani ashitakiwe nani asishitakiwe. Kalaputopu kage kanaweza kuwa na nini?

Leo hiihii laputopu ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeibwa. Wanasema imeibwa “kiaina.” Huyu ndiye mkuu wa idara ya vipimo nyeti anayekimbiliwa wa mwisho kutoa uthibitisho wa lolote linalohitajika kupimwa kikemia. Kalaputopu kake kanaweza kuwa na nini?

Kaa chini utunge matukio haya kama shanga: Moto wa BoT, moto wa ikulu, mwanaume anayetokea lango kuu la ikulu akiwa na ua mkononi na kupotea kwa laputopu za watumishi wa ngazi ya juu serikalini. Kizaazaa! Nani apimwe akili? Watapimwa wangapi?

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 17 Mei 2009)

No comments

Powered by Blogger.