SERIKALI IKITENDA JINAI, WANANCHI WAFANYEJE?
WAZIRI MKUCHIKA (pichani juu) ATAKA KUNYAMAZISHA WANANCHI
Na Ndimara Tegambwage
SERIKALI imeficha ukweli. Katika hatua hii, serikali inaweza kutuhumiwa kusema uwongo; na kusema uwongo ni kutenda jinai. Je, serikali ikitenda jinai itakuwaje?
Katika taarifa yake, serikali imepiga marufuku kile ilichoita “malumbano” kati ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kwa maelezo kuwa “yanaweza kutumbukiza taifa katika uvunjaji amani.”
Taarifa ya Waziri wa Habari, George Mkuchika kwa vyombo vya habari juzi Jumatatu imesema serikali “haitakubali kusikia malumbano” hayo na “haitavumilia kuona vyombo vya habari vikichangia kuligawa taifa katika makundi na kudumaza maendeleo.”
Hapa ndipo penye mgogoro. Wasomaji wa magazeti, wasikilizaji redio na watazamaji wa televisheni hawajawahi kuona kile serikali inachokiita “malumbano.”
Mengi ametuhumu watu kuwa “mafisadi.” Mmoja wao ni Rostam. Naye Rostam amejibu, tena kwa kutumia chombo cha umma – Televisheni ya Taifa (TBC1).
Kwa akili ya kawaida, kilichotendeka ni kuibua hoja zilizokuwa zikienda chinichini. Kilichoanikwa ni matendo ya watu binafsi yanayohusu uchumi na maisha ya wananchi.
Kile ambacho serikali inaita “malumbano” ni eneo la “soko huria” la mawazo ambamo, kwa miaka miwili sasa, wananchi wamekuwa wakichangia kwa njia ya kulalama kwamba keki ya taifa inaliwa na wachache.
Sasa serikali inasema “haitakubali kusikia” na wala “haitavumilia” kuona vyombo vya habari na waandishi wakichangia kugawa taifa.
Huu ndio udikiteta mchafu. Kwanza, serikali inatafuta nini katika “malumbano?” Kama ni malumbano kweli, si iwaache walumbanao wafanye wafanyavyo? Malumbano si huisha hoja zikiisha?
Pili, serikali inajikoroga. Upande mmoja inasema kuna malumbano kati ya watu wawili; na upande mwingine inasema wananchi wameanza kugawanyika; hawa wakiunga mkono Mengi na wale wakiunga mkono Rostam.
Basi haya siyo malumbano. Huu ni mjadala wa hoja za kina. Ni mdahalo wa gonga nikugonge wa kuibua mazito na machungu yanayohusu jamii. Ni uwanja wa kumwaga taarifa kwa wenye macho kuona na wenye masikio kusikia. Ni kitanzi pia cha wasema uwongo.
Lakini serikali inasema sasa basi! Nyamaza! Huu ni ukatili. Ni udikiteta. Kuna hasara gani kwa wananchi kuwa upande wanaotaka, wanaoelewa, wanaothamini na waliotayari kutetea?
Tatu, serikali haisemi ukweli pale inapodai kuwa nchi itaingia katika “uvunjaji” amani. Watu huru wanapojadili yanayowahusu wao na jamii yao, haitazamiwi serikali ijenge visingizio vya kupotea kwa amani.
Watu wakiona mabaya yanatendeka; wakakaa kimya au wakanyamazishwa, wakajenga chuki kimyakimya, wakafura kwa hasira; basi linalofuata ni mlipuko mkubwa kuliko mabomu ya Mbagala.
Mlipuko huu ni hatari zaidi, hata na hasa kwa watawala, kuliko mdahalo juu ya nani “anakula nini.” Bali sasa ni wazi kwamba kwa hatua ya serikali ya kuzima mjadala, lazima “kuna jambo.”
Nne, serikali makini ingefurahia mdahalo. Ingepata vyanzo vizuri na sahihi vya taarifa mwanana za kufanyia kazi iwapo ina nia kweli ya kufanya kazi. Lakini inaonekana imechoka haraka na mapema.
Sasa siyo tu serikali haitaki kusikia, bali pia haitaki wananchi wasikie na washiriki mjadala. Huu ni udikteta mchafu.
Mtu angetarajia “mapapa” watajwe na “fisadi nyangumi” watajwe ili wananchi waone tofauti kati ya papa na nyangumi. Waone nani anaamsha hisia zao ili waone na kupigania haki na maisha yao.
Hakika, mmoja wa samaki hawa wakubwa aweza kuwa mwandani wa wananchi. Panahitajika uibuaji taarifa. Upembuzi. Uchokonozi wa kina na ushiriki wa wananchi katika mjadala. Kuzima hili ni ukatili wa kidikteta.
Tano, serikali inatumia vitisho kuzima mjadala. Inanukuu na kujivunia sheria katili zenye harufu ya kifashisti kama hii Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na nyingine yenye chembechembe za kibedui – Sheria ya Utangazaji ya mwaka 2003.
Katikati ya majigambo ya utawala bora, ukiona bado kuna watawala wanaojivunia sheria zinazopingana hata na katiba zao, na uhuru na haki za wananchi, basi ujue udikteta umeota mvi. Wanaua uhuru na haki ili watawale misukule na siyo watu wanaofikiri na wenye utashi.
Sita, kwa serikali “kutahadharisha” wahariri na waandishi, ina maana ya kuwafunga midomo na mikono. Wasifikiri. Wasitende. Wasubiri serikali iamue andika hili, andika lile.
Saba, kuna upandikizaji woga. Waziri anasema sheria “zinakataza mtu, watu kuzungumzia au kujadili suala ambalo tayari liko mahakamani.” Hakuna sheria ya aina hiyo.
Chukua maneno ya waziri kama yalivyonukuliwa hapo juu. Ama waziri hakuelewa sheria inasemaje au ameinukuu nje kabisa ya muktadha. Sheria aina hiyo itakuwa za kishetani.
Magwiji wa sheria waliishafundisha kuwa waamuzi wa kesi mahakamani siyo hakimu au jaji peke yake. Kuna wakili wa pande mbili na kuna wananchi wanaofuatilia kesi.
Kila fungu litatoa hukumu yake; na hilo ndilo hufanya hakimu au jaji awe makini akijua siyo mwamuzi pekee, hata kama waamuzi wengine hawakuketi mbele ya mahakama.
Kwa hiyo suala la kutojadili kilichoko mahakamani ni uzushi unaolenga kutisha na kunyamazisha wananchi. Hata kuibuliwa kwa madai ya nyongeza, nje ya yale ambayo mtuhumiwa tayari amesomewa mahakamani, siyo kosa.
Ni kweli kabisa maoni nje ya mahakama yaweza kusaidia kuweka wazi zaidi kinachoendelea mahakamani. Hiyo ni kama mawakili watakuwa wamepata taarifa zaidi za kunoa stadi kuchokonolea kile ambacho walikuwa hawakukiona na kukiwasilisha kwa ustadi zaidi.
Lakini mjadala nje ya mahakama hauwezi, hata kidogo, kuharibu kinachoendelea mahakamani. Vitisho kama vile vya Mkuchika ndivyo vinaweza kuharibu mbongo za watu na kuwapokonya uhuru wa maoni. Naomba kuwasilisha.
Kwa hiyo, serikali imetumia mabavu kujaribu kuzima mjadala ambao ungeisadia. Sasa kuna madai kuwa imefanya hivyo kwa kuogopa itaguswa pale – kati ya papa na nyangumi.
Kuna kila sababu ya kupinga udhalimu huu katika nyakati tulizomo. Tukinyamaza watawala watashindilia watu kwenye magunia kama dagaa na kututupa mwaloni.
Kuvunjika kwa amani ni visingizio. Kutumia visingizio kukwepa ukweli ni kuficha ukweli hadi kufikia viwango vya kusema uwongo.
Kusema uwongo kuwa mjadala utaleta maangamizi kitaifa ni kutenda jinai.
Serikali ikitenda jinai wananchi wafanyeje?
0713 614871
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 13 Mei 2009)
No comments
Post a Comment