Header Ads

LightBlog

UFISADI BENKI KUU TANZANIA

SITAKI Na Ndimara Tegambwage

BALALI AKIRUDI ITAKUWAJE?

SITAKI kumchokonoa Daudi Ballali, yule gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT); bali sitaki pia akae kimya kuhusu tuhuma zinazomkabili. Akae kimya kumlinda nani?

Akikaa kimya itakuwa na maana kwamba ama amedhoofika kimwili na kiroho au amehongwa; na amehongwa “kichafu” fedha ambazo hakika hazihitaji kwa sasa na katika maisha yake yote.

Ballali ni mtu. Akifinywa anaumwa. Akitukanwa ananuna. Akisutwa anastuka. Akisingiziwa anatafuta utetezi. Akifikia kufanywa kondoo wa kafara, anaguna, ananguruma, anakataa kwa kishindo. Na hivyo ndivyo Watanzania wanataka awe.

Hebu fikiria Ballali aliyeamua na kutamka, “Acha lije na lijalo.” Huyu atakuwa Ballali mbogo. Anayekataa kufa peke yake. Au mlokole wa dakika ya mwisho. Muumini wa haraka katika madhehebu ya umma, anayetaka kuorodhesha washirika wake.

Jaribu kufikiria Ballali mpya anayevuta pumzi ndefu, kisha kukohoa kwa nia ya kunyoosha sauti yake na kutamka, “Kampuni hii ni ya rais. Niliambiwa niwape fedha kiasi hicho.” Kichaa au mlokole?

Fikiria Ballali, anayepumua kawaida, bila kutweta na asiyeoyesha wasiwasi wowote; akikuangalia machoni na kwa tabasamu ya mbali anasema, “Kampuni hizi mbili ni za rafiki yake rais. Nilipigiwa simu na mkuu akikiangiza nisiwacheleweshe.”

Uuuwi! Hata kabla hujapata nguvu za kuhimili kishindo hicho, unamwona na kumsikia Ballali akisema, “Hii kampuni ya Kijani Kuliko Kijani ni ya makada wa chama kizee cha siasa; nilishinikizwa kuwamegea.”

Utasema nini? Utajisikiaje? Utamfikiriaje Ballali ambaye miaka yote amekuwa akijigamba kuwa anafanya kazi nzuri na kwamba uchumi unapaa mithili ya nyimbo za wanasiasa waliovamia ikulu?

Usione aibu kutoa maoni yako. Ikishindikana sema unataka au hutaki. Lakini hili ni suala linalotekenya na asiyetekenyeka kwa hili, basi amepoteza fahamu au amesinyaa au ameganda kwa woga, aibu au ufisadi.

Fikiria Ballali aliyevaa gamba la ujasiri. Anasema hataki kuwashitaki wanaodai katenda ufisadi, bali anataka kusema mabilioni ya shilingi kutoka BoT yalikwenda kwa nani.

Uko wapi moyo ambao haustastuka? Wangapi watazimia kwa kishido hicho? Wangapi watauza mali zao haraka au hata kuzigawa na kukimbia nchi kabla hawajafungwa matambara yanayowaka moto na kuimbiwa kidumbwendumbwe?

Fikiria Ballali mpya anayeweza kueleza kwa nini alilipa mabilioni ya shilingi kwa kampui ya kuchimba dhahabu ya Meremeta, iliyokuwa Buhemba, Musoma ambako iliharibu mfumo wa maisha wa wananchi wa kuwafukarisha kiuchumi na kijamii.

Jaribu kufikiria Ballali wa leo, siyo jana, anayeeleza kwa ufasaha, nani alimlazimisha kulipa mabilioni ya shilingi kwa kampuni ya Tangold na kampuni nyingine ambazo zimegudulika kuwa za kitapeli.

Hapana. Jaribu kufikiria Ballali “mwenyewe” anajitokeza na kusema kwamba hizi shilingi bilioni 133 wanazodai kumfukuzia kazi, ni “hela ndogo sana,” na anaongeza kuwa yeye amelipa mara 50 zaidi ya hizo.

Utasema nini iwapo Ballali atajitokeza na kusema kwamba kiasi kikubwa cha fedha alizochotea kampuni zilikwenda katika biashara binafsi, siasa, wanasiasa na viongozi wakuu wa nchi? Sema!
Wakati ukigwaya kwa kishindo hicho, Ballali aweza kuongeza kuwa, watawala wakuu katika kipindi cha 1995 hadi 2005 na wale waliopo sasa, ndio walikuwa wakimwomba, kumwagiza na kumshinikiza atoe fedha kwa kampuni zao, ndugu zao, rafiki zao, watoto wao na chama chao.

Utasemaje wewe? Ni watawala haohao ambao wamekataa kusema Ballali yuko wapi kipindi chote cha madai ya kuugua na kufanyiwa operesheni. Ni hivi, Gavana wa Benki Kuu ya nchi anaugulia katika hospitali ambayo watawala wa nchi yake hawajui ilipo?

Inawezekana usiwe na la kusema. Usiwe na kutaka au kutotaka, kwa kuwa serikali haiwezi kukiri ujinga kuhusu alipo gavana wakati ina mkono mrefu na mahusiano na serikali na mashirika makubwa duniani.

Ndio maana wenye jicho la nyongeza wanaona kuwa sakatala BoT ndiyo sasa linaanza; linafumuka. Achana na kauli awali za baadhi ya wabunge kuwa hoja ya ufisadi ilikuwa siasa tupu.

Achana na kauli za Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba za kubeza hoja ya ufisadi ndani ya BoT akidai ni “kelele za wapinzani zisizo na msingi.”

Leo hii, Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano anapomfukuza kazi Gavana Billali, huyu Bwana Makamba anachonga njia ipi ili asigongane na Kikwete?

Kujitokeza kwa Ballali kusema kilichotokea, alichobuni, alichoagiza, alichoshurutishwa kufanya, alichodanganywa na, au alichotenda kwa manufaa yake mweyewe, kunaweza kuwa ufunuo mkubwa katika siasa za nchi hii.

Tatizo ni kwamba Ballali ama amefichwa, au amejificha, au anaogopa kujitokeza, au amehongwa kifisadi ili apotee na tubaki kupiga mihayo na mayowe.

Lakini kwa serikali iliyo makini; inayojitangaza kupambana na rushwa na ufisadi; inayotaka kujua yaliyotokea, tena kwa kina, inaweza kumhakikishia Billali ulinzi na usalama ili ajitokeze na kusema kilichotokea.

Serikali ya Kikwete inaweza kukubali hilo? Ikubali na iseme, “Acha huyu bwana atuache uchi, tutavaa vizuri baadaye?” Kama iko makini itafanya hivyo. Kama haiko makini, siyo tu itachekwa, bali italaaniwa pia kwa kukataa chanzo muwafaka cha taarifa mahususi juu ya janga la taifa hili.

Sitaki serikali ya Kikwete ikatae ofa hii.

(Mwandishi anapatikana pia kwa simu: 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com)

4 comments

chemshabongo said...

kwanza naomba nikupe pole kwa yaliyo kukuta kufikia hatua ya kumwaga damu ukiwa kazini, pili nakupa pongezi kwa kazi nzuri unayofanya katika kutuweka watanzania katika hali ya kutambua ni nini kinachoendelea nchini. nakupongeza sana na usirudi nyuma baba! tupo pamoja

N N said...

Kumbuka kaka wataalamu wa dunia hii ni hatari. Utadhani kuwa ubadhilifu na ufisadi wote uko hapo tza tu, lakini ukweli ni kwamba umeenea kote. Waenezao haya ni wachache tu duniani. Na haya yalianza zamani.
Ingia website hizi uone.
http://judicial-inc.biz/slave_traders_.htm,
http://judicial-inc.biz/b.lood_diamonds.htm,
http://judicial-inc.biz/J_oran_va_der_sloot_supplement.htm,
http://judicial-inc.biz/thersea_heinz_kerry_bio.htm,
http://judicial-inc.biz/1.osephardim_of_curacao.htm,
http://judicial-inc.biz/j_history_caribbean_jews.htm,
http://www.blacksandjews.com/Jews.of.Black.Holocaust.ag.html,
http://sunray22b.net/slavery.htm,
www.jewwatch.com, www.erichufschmid.net, www.iamthewitness.com, www.prothink.org.

Christian Bwaya said...

Uhuru hauna kikomo. Kikomo Kinawekwa na maadui wa uhuru. Umesema kweli.

Kazi zako zinamfunza kila mwenye haja ya kujifunza. Nimechagua kuwa mmoja wao.

Innocent Kasyate said...

Mzee Ndimara pole sana kwa matatizo katika harakati zako. Nimekufahamu miaka mingi hasa enzi za uanzilishi wa mageuzi hapa Tanzania wakati huo nikisoma sekondari.
Sina shaka unajua athari za kazi yako kwako na kwa taifa ni chanya.Ila wanaotaka ziwe hasi ni wengi bali jua tuko wachache nyuma yako.
Mafisadi tutapambana nao tu milele.

Powered by Blogger.