MASHAMBULIZI KWA MWANAHALISI/SHUKRANI ZA MWANDISHI
SITAKI Na Ndimara Tegambwage
SITAKI kuwa mtovu wa shukrani. Nasema asante kwa wote waliofika hospitalini na nyumbani kunijulia hali kutokana na kuvamiwa na kujeruhiwa kwa panga nikiwa kazini.
Nasema nastahili hiyo pole ninayopewa kwa kuwa nilikuwa kazini, katika ofisi za gazeti la MwanaHALISI, Mtaa wa Kaseba, Mwananyamala jijini Dar es Salaam, ambako ninatoa ushauri katika kutafuta, kupokea na kuandika habari.
Ilikuwa Jumamosi, yapata saa mbili na nusu usiku wa 5 Januari 2008. Ofisi ilivamia. Wavamizi hawakutaka chochote isipokuwa waliamuru tulale chini ili waweze kutukatakata kwa panga. Tulikataa.
Katika vita hivyo, nilipigwa panga la mgongoni na kichwani lakini ningali naandika. Bila shaka kuna mzozo mkubwa kati ya waliotuvamia na waliowatuma. Wameshindwa kukamilisha walichotumwa; nami nawasishi wasikubali kutumwa tena kazi ya aina hii.
Bali kwa siku nane mfululizo sasa, nyumba yangu, jijini Dar es Salaam, imekuwa ukumbi wa wageni; wale wanaoniongezea matumaini ya kupata nafuu haraka na wanaopunguza maumivu kwa kauli za kufariji.
Tangu asubuhi hadi usiku ninapokwenda kulala, ninabubujikwa na machozi ya furaha kwa kuona nyumba inavyojaa watu waliobeba salaam za kunitakia heri; watoto vijana na watu wa makamo. Wakati wote ni pole na “waihuka!”
Angalia huyu hapa. Ananikabidhi shilingi elfu mbili. Anasema ninunue jwisi. Mwingine huyu hapa; ananishikisha shilingi elfu tano; anasema ninunue matunda. Yule pale alinipa elfu ishirini; anasema ninunulie dawa. Machozi yananibubujika.
Binti huyu amebeba kasha lenye vikasha sita vidogo vya jwisi; anasema, “Unahitaji kunywa jwisi kwa kiwango kikubwa. Humu kuna Vitamin C ambayo ni muhimu katika hali uliyomo.” Ni mapenzi “yanayotonesha.”
Rafiki yangu, akiandamana na mke wake na watoto wao, ameleta mkungu wa ndizi na kilo tatu za nyama; harakaharaka anasema, “Unahitaji kula vizuri. Ulipoteza damu nyingi na sharti uirejeshe haraka.” Watoto wananikumbatia na machozi yanaasi vizingiti.
Binti yangu anaingia na familia yake. Anafanya kama wengine waliomtangulia. Ananikabidhi shilingi laki moja na kusema, “Baba, hii utanunulia dawa kama zitahitajika.”
Nyuma yake kuna jirani yetu anayeleta kilo mbili za unga akisema, “Nguvu zangu zinakomea hapa. Pole sana.” Kila mtu na alichonacho. Ni pole, ni waihuka. Hakuna kidogo wala kikubwa; zote ni ishara za upendo kwa mwanao, ndugu yao, rafiki yao na jirani yao.
Napokea simu kila baada ya dakika mbili au tatu na hii inaendelea hadi usiku wa manane; na asubuhi ninaamshwa na ujumbe au mkoromo wa simu. Najisikia kutoumia. Kutoumwa. Najisikia kupona katikati ya mbubujiko huu wa mapenzi ya jamii.
Nasikia kwa mbali, waandishi wa habari na wenye vyombo vya habari wakipaza sauti za kulaani uvamizi wa chumba cha habari. Natamani kuamka na kujiunga nao. Najawa na nguvu isiyomithilika; inayozidi ile niliyotumia kukabiliana na wavamizi.
Narejewa na fikra kwamba hata waliotumwa kuvamia watakuwa wameacha kutweta. Wamepoa. Wanajiuliza kwa nini walijaribu kuua mwalimu wa waandishi wa habari; kwa nini walitaka kuondoa uhai wa yule ambaye kalamu yake haijawahi kuwasaliti.
Najiridhisha kuwa sura zile; maumbile yale; umri ule ni vya watu wa kutumwa, kwani kigazeti kidogo ninachofundisha jinsi ya kuwa makini na kukipa miguu ili kisimame, hakijawahi kuwasakama wala kuwasaliti watu wa tabaka lile.
Najisikia kuwa na nguvu zaidi; na kwa nini isiwe hivyo wakati nimesimama katikati ya wanaonipa moyo kwamba nilichokuwa ninafanya, kabla ya uvamizi, ni kazi ya wananchi; na kwamba nastahili kuendelea nayo.
Gazeti la MwanaHALISI ambako nikuwa nikisaidia kufundisha na kuelekeza waandishi wa habari kwa miezi sita sasa, limeanza kujijengea hadhi na umaarufu kutokana na jinsi wanavyoandika na wanachoandika.
Waandishi wanadiriki kumwambia mfalme kuwa amekaa uchi, badala ya kumung’unya maneno na mfalme akabaki uchi mbele ya watawaliwa.
Hiki ni kigazeti kinachoendeshwa kwa misingi ya “umachinga” na mara nyingine, baada ya kutoa ushauri na vijana wakaingia kazini, namuuliza mchapishaji, “Nasikia leo hamna uwezekano wa kutoka?” Mara nyingi atanijibu haraka, “Inshallah.”
Kwa maana hiyo, hili ni gazeti dogo linalohitaji kukua; linalohitaji mtaji wa uhakika; linalostahili kusaidiwa kujenga misingi – ile ya menejimenti na ya uandishi; na linalostahili kutetewa kwa kuwa limejitambulisha na umma na hakika, angalau mpaka sasa, linaongozwa na matakwa ya sasa ya umma.
Ningependa kuendelea kushauri MwanaHALISI, kama ninavyofanya kwa magazeti mengine madogo na waandishi binafsi, hadi hatua ya kutembea. Kwa msingi huo, kuvamiwa na kukatwa mapanga nikiwa katika ushauri kwa gazeti la aina hii, ni heshima.
Gharama pekee kwa damu yangu iliyomwagika nikiwa kwenye ushauri katika gazeti la MwanaHALISI ni kuona gazeti hilo linakuwa na wahariri mahiri, waandishi wa viwango vya juu na menejimenti iliyosheheni taaluma.
Sitaki kuona MwanaHALISI linakufa. Ujumbe kwa waliotuma wavamizi ni kwamba “Hakuna kurudi nyuma.” Gazeti likishakuwa la umma, ambako ningependa MwanaHALISI lielekezwe, basi jamii italilinda pamoja na watendaji wake wote.
(Ndimara anapatikana: Simu 0713 614872; imeili: ndimara@yahoo.com. Makala hii imechapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, 13 Januari 2008)

3 comments
Pole sana mwalimu wangu. Inatia moyo kuona kuwa bado unatumia uhuru wako wa kujieleza pamoja na vitisho. Kama ulivyosema, Uhuru Hauna Kikomo.
Kumbukeni balaa hii yaanzia mbali. Ilianza wakati kikundi fulani cha watu duniani kiliona uwezekano wam kutengeza feza kwa kuuza watu.
Toka zama hizo paka leo utumwa waendelea.
Utumwa wa leo ni kuwa na kontrolli ya mabenki kuu, ukopaji wa hela-na kutoza interst kubwa, media, majeshi, mahakama, marais wote duniani au watu muhimi serikalini. Wanaivest pesa zote na nguvu zote kuendeleza utumwa huu. Wanatumia freemasons na secret socoeties nyinginezo nyingi.
Kwanza vita vya baridi, sasa vita against terrorists.
Nani ni terrorist?? NI yeyote yule anaeleza ukweli, anayewaexpose.
Kumbukeni kazi ya mwafrika ni kueleza ukweli na kuleta justice kwa wenzetu.
Pole sana Mzee.Mungu atakubariki upone haraka.Kwa hao waliotumwa kuwadhuru,Mungu awasamehe kwani hawajui watendalo.
Post a Comment