Header Ads

LightBlog

SERIKALI NA MCHOKO WA HABARI

SITAKI Na Ndimara Tegambwage


Mradi wa serikali wa kujisifia

SITAKI wananchi washangae kwa nini utaratibu wa serikali wa kujiremba kwa vitenge, kujipaka mafuta na kujipulizia pafyumu umekwama.

Huu ni ule mpango wa mawaziri wa serikali kujitokeza, kila mmoja kwa siku yake, kuwaambia waandishi wa habari, amefanya nini, wapi, ana matarajio gani na zipi ni changamoto zake na wizara yake.

Mpango huu ulitangazwa rasmi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, tawi la Utawala Bora, Philip Marmo, alipoongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Desemba 3 mwaka jana.

Tangu hapo, siku baada ya siku, vyombo vya habari vimeripoti kuwa baadhi ya mawaziri wameshindwa kutenda kama walivyotarajiwa. Ama hawakutokea siku walipotarajiwa au wametoa taarifa kuwa wataongea siku wanayotaka.

Mpango huu wa mawaziri kuongea na waandishi wa habari kila siku, ni zoezi la kusambaza taarifa za serikali. Unatokana na mstuko ulioipata serikali kwamba haiandikwi ipasavyo; hivyo kuwatoa uwani mawaziri ili waseme kile ambacho wanataka wananchi wasikie.

Ni mpango unaotokana na serikali kustuka kwamba inaandikwa “vibaya;” au haitangazwi vizuri na kikamilifu; kwa hiyo mawaziri wake wajitokeze na kueleza wanachofanya.

Zoezi hili la serikali lilifuatia ziara ya mawaziri mikoani ambako inadaiwa serikali iliwatuma kufafanua bajeti ya mwaka 2007/2008. Huko, wengi walizomewa, kuchekwa na kupuuzwa na wananchi.

Wananchi wengi waliuliza, “Kulikuwa na kitu gani kigumu katika bajeti ya mwaka huo, na siyo miaka mingine, kilichostahili maelezo ya mawaziri na siyo mtendaji wa kata, mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa?”

Na maelezo ya mawaziri hayakuhusu matanuzi ya serikali katika ununuzi wa mashangingi; ilivyobinafsisha mabenki kwa gharama ya “bure;” ilivyoingia mikataba ya kishetani na makampuni ya umeme; ilivyogawa madini na vito vya thamani kwa watu wa nje huku ikibaki kuchukua mrabaha tu.

Mawaziri hawakuwaeleza wananchi jinsi serikali inavyohimiza ujenzi wa matundu yanayoitwa madarasa na kujimiminia sifa; wakati hakuna walimu, madawati, vitabu, maabara na vifaa vingine muhimu kwa elimu.

Mawaziri hawakuwaeleza wananchi kwamba serikali imeanzisha mtindo wa kuoka walimu kama chapati – wiki sita tu – pa!pa! Hawakueleza kwamba walimu hao, wasio na elimu, ujuzi, kanuni wala taratibu za kutoa elimu, ndio wanasaidiana na serikali kudidimiza nchi.

Wananchi hawakuelezwa jinsi viongozi wa serikali walivyojiingiza katika wizi na uporaji wa fedha katika Hazina ya nchi na Benki Kuu (BoT) kwa kupitisha fedha hizo katika kampuni feki za ndani na nje ya nchi.

Kwa hiyo, mambo kama hayo, na mengine mengi, yamekuwa yakijadiliwa kwenye vyombo vya habari; yakionyesha sura nyingine ya serikali ambako baadhi ya viongozi wanashiriki katika ufisadi usiomithilika.

Ni katika mazingira haya serikali ilibuni utaratibu wa kuziba mapengo. Kuhakikisha kwamba waziri mmoja anawamwagia waandishi wa habari, takwimu na masimulizi marefu, manene na mapana ambayo wanaweza kuandika kwa wiki nzima.

Kwa hiyo, kwa mujibu wa mkakati wa serikali wa kujitangaza kupitia mikutano ya mawaziri na waandishi wa habari; serikali hadi Januari 16 mwaka huu, ambapo Marmo alisema ndipo utaanza utaratibu tofauti, ingekuwa imejipangusa vumbi la kashfa.

Hakika ni kupangusa vumbi na siyo kuondoa kashfa. Angalau kwa kipindi cha wiki sita, serikali inakuwa imepata muda wa kupumua. Lakini sasa, siyo kila waziri anafaulu kuibeba serikali. Wengine hawajajiweka tayari na wengine hawana cha kusema.

Hili nalo linaonyesha kuwa lilikuwa suala la kukurupuka; ambalo halikuandaliwa vizuri na halikukubaliwa na wahusika wote. Vinginevyo kusingekuwa na mushikeli wa huyu kasafiri au yule ni mgonjwa.

Kwani wizara siyo waziri. Kama waziri hayupo kuna naibu. Kama naibu hayupo kuna Katibu Mkuu au hata Ofisa wa Habari wa wizara. Lakini pia mazingira yamebadilika.

Inaonekana serikali bado iko nyuma sana katika kutambua mazingira ya sasa ya vyombo vya habari na uandishi wa habari kwa ujumla.

Uandishi wa habari za “kupewa mkononi” umebakia kwa vyombo vichache vinavyomilikiwa na serikali, na katika nchi chache duniani, hasa za kidikiteta. Vyombo vya habari vyenye hadhi vimechukua sura ya “kuku wa kienyeji;” anayeparura ardhi na kujitafutia.

Habari ya kuletewa mezani, katika ofisi kuu ya habari ya Idara ya Habari (MAELEZO), siyo habari tena. Hiyo ama imechoka, imechakaa au inalazimishwa kwenye soko. Waandishi wa habari waliofunzwa na walimu wazuri, wanajua hivyo.

Hii haina maana kwamba “habari chakupewa” haifai kabisa. Hapana. Inafaa. Inakupa mahali pa kuanzia kuchokonolea habari yenyewe, kwani kile unachopewa kimerembwa na soko linahitaji habari ambayo haijanakishiwa.

Kwa hiyo, kwa kusoma ndani ya “habari chakupewa,” mwandishi mzuri huweza kuanza kufuatilia habari yenyewe, isiyovalishwa vilemba au vitenge; isiyopakwa mafuta na kupuliziwa pafyumu. Isiyolenga kusifia na kutukuza watawala, bali yenye nguvu ya kutoa ujumbe sahihi kwa watawala na wataliwa.

Si muhali kwa serikali kutoa maelezo juu ya mipango yake, kazi zake, mafanikio, mapungufu, mikakati na changamoto zake. Lakini kutegemea kuwa hiyo ndiyo njia ya kujisafisha, hasa katika mazingira ya sasa ya utoaji habari, ni kushika gugumaji wakati unazama.

Kinachohitajika ni kuwa wazi; kuruhusu mwananchi kuhoji mipango, utendaji na taratibu; na kuacha waandishi wa habari kuandika wanachoona na hata wanachotaka kwa wakati huo.

Hakuna shaka kuwa mradi huu wa mawaziri ulilenga kuziba akili za waandishi kwa tarakimu na vitaarifa lukuki. Vinginevyo, ulilenga kutahini mawaziri juu ya utendaji wao. Vyovyote itakavyokuwa, umeshindwa.

(Makala za SITAKI huchapishwa katika Tanzania Daima Jumapili)
simu:0713 614872
imeili:ndimara@yahoo.com

1 comment

Yusa Imori said...

Serikali Ya Kikwete haina Viongozi Makini, sidhani kama hii ni habari kwa sasa!! Wasiwasi wangu ni kwamba hata huyo (KIKWETE) aliewachagua hajui watu makini kwanza ameweka wizara kama utitiri halafu haoni makosa Yao (hao mawaziri) ndo maana hajawahi kuthubutu kuwatimua. Historia ya Nchi hii itamkumbuka kwa kuwa na dhamana ya kusaidi wanyonge wengi wa Tanzania na kushindwa kufanya hivyo, sisi ambao ni vijana bado tunamuachia Mungu kwa sababu hatujui tutarithi nini kutoka kwa wazee wetu zaidi ya Majangwa, Mbuga Zilizabinafsishwa, mahandaki yaliyowahi kuwa na madini, na utumwa katika nchi yetu.

Powered by Blogger.