NANI RAIS ZANZIBAR?
Dk. Magufuli anapomtaka Maalim Seif ‘apige kazi’ Zanzibar
(Mwananchi, Januari 1, 2016)
Kutoka Meza ya Mhariri wa Jamii
Wiki iliyopita ilikuwa “Wiki ya
Zanzibar.” Kwanini? Kwa sababu wapinzani wakuu wawili kisiasa Visiwani walikuwa
Dar es Salaam.
Hao ni Ali Mohamed Shein na Maalim Seif
Shariff. Walikuwa Dar es Salaam kumweleza Rais
Dk. John Magufuli jinsi mazungumzo ya kumaliza mgogoro wa Zanzibar
yanavyoendelea na hatua iliyofikiwa.
Tarehe 28 Oktoba mwaka huu, Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha alitangaza kufutwa kwa
uchaguzi mkuu na matokeo yake Zanzibar.
Wakati Jecha anatangaza kufutwa kwa
uchaguzi na matokeo yote, tayari matokeo ya majimbo 33 yalikuwa yametangazwa.
Hadi tangazo la kufuta uchaguzi, kila
chama kilikuwa na viti 27 vya uwakilishi. CCM haikuwa imepata hata kiti kimoja
kisiwani Pemba. CUF ilikuwa imenyakua viti tisa Unguja. Ngome kuu ya CUF ni
Pemba.
Sasa kwanini mwenyekiti wa ZEC alifuta
uchaguzi? Alidai kwamba kulikuwa na vurugu katika maeneo mbalimbali; kwamba
yalijitokeza mazingira yaliyofanya uchaguzi usiwe huru na wa haki; kwamba
Maalim Seif Shariff Hamad alijitangazia ushindi.
Sheria ya uchaguzi inatoa adhabu kwa
mtu anayetangaza matokeo badala ya Tume. Je, Maalim Seif ameshitakiwa?
Hakushitakiwa. Hajashitakiwa.
Sheria ya uchaguzi inatoa mamlaka kwa
Tume kusimamisha au kuahirisha uchaguzi katika eneo ambako kuna tatizo. Je,
kuna hatua yoyote iliyochukuliwa kule ambako inadaiwa kutokea vurugu? Hapana.
Jecha alifuta uchaguzi wote – ambako
inadaiwa kuwa na vurugu na kule ambako kulikuwa na utulivu; na usalama.
Sasa hili lina uhusiano gani na kwenda
Dar es Salaam kwa wagombea wa vyama hasimu – CCM na CUF? Kuna mambo mawili
makubwa:
Kwanza, mgombea wa CUF ambaye ni katibu
mkuu wa chama chake na makamu wa kwanza wa rais katika serikali ya umoja wa
kitaifa (SUK), Maalim Seif anashikilia kuwa uchaguzi ulifutwa baada ya yeye
kuonekana ameshinda.
Maalim anabeba “makabrasha muhimu”
yenye taarifa mbalimbali kuthitbitisha ushindi wake na chama chake. Anadai
kufuta uchaguzi ni njama za kutaka kupora ushindi wa chama chake na wapigakura
wa Zanzibar.
Pili, CCM inadai kuwa ufutaji matokeo
ilikuwa hatua sahihi. Inataka sasa uchaguzi urudiwe.
CUF inakataa kurudia uchaguzi. Inadai
siyo haki wala sahihi. Inataka ujumuishaji matokeo uendelee kutoka pale zoezi
lilipositishwa.
Maalim Serif na CUF wanadai kuwa
na matokeo sahihi.
King’ang’anizi chao
kinatokana na kile wanachoita “zana za ukweli” – fomu za matokeo na
zilizosainiwa kutoka vituoni.
Kuna madai kuwa CCM imekwisha
jiimarisha kwa kuongeza idadi kubwa ya wapigakura Visiwani na ndio maana
inataka uchaguzi urudiwe.
Inadaiwa walioongezeka ni watendaji
katika chama hicho na serikalini; na askari polisi na JWTZ.
Katika mazingira haya, CCM imebanwa.
Ina kitu mdomoni. Ikikitema itakuwa imetema utamu. Ikikimeza itakuwa imemeza
moto. Kote kuna madhara.
Lakini ni kweli kwamba uchaguzi na
matokeo yake yote vilifutwa? Hapana. Siyo kweli. Baadhi ya matokeo, ingawa
yalitamkwa kufutwa, hayakufutika. Kuna walioyakingia kifua.
Baadhi ya waliochaguliwa kuwa wabunge
wa bunge la Muungano, walikwenda Dodoma haraka na kuapishwa. Ni hao waliombeba
mgombea urais wa Muungano kutoka upande wa pili wa Muungano.
Je, katika mazingira haya, uchaguzi
ukirudiwa Zanzibar ina maana na hao walioko bungeni Dodoma watarudi kwenye
kinyang’anyiro?
Kurudi katika uchaguzi ni kubatilisha
ubunge wa Wazanzibari waliokwishaapa. Ni
kumwacha rais katika mgogoro mkubwa kisiasa na kikatiba – ambamo yumo
tayari.
Kuendelea kuwa wabunge katika bunge la
Muungano; huku Zanzibar wakirudia uchaguzi, ni kujinyima uhalali na hivyo
kuonekana mamluki waliochukuliwa rasmi kuhalalisha matakwa ya CCM.
Rais Magufuli hawezi, kama ambavyo
hastahili, kukubaliana na hili na bado akabaki kuonekana mwadilifu mbele ya
Watanzania na jumuia ya kimataifa.
Kwanini? Kwa sababu uchaguzi
uliobatilishwa hauwezi kuzaa wachache ambao sio batili. Na ili “waliobatili”
wawe halali – ingawa awali walifanywa halali kwa shabaha maalumu – sharti
ujumuishaji kura za uchaguzi wa Oktoba uendelee kutoka pale ulipositishwa.
Hii maana yake ni kwamba huwezi kurudia
uchaguzi Zanzibar. Ama uchaguzi unaendelea kwa kujumuisha matokeo; au
majumuisho yaliyopo (hadi kusitishwa kwa uchaguzi) yanachukuliwa kuwa ndio
matokeo sahihi na halali ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Je, Rais Magufuli anaona “ukora” huu wa
kisiasa Zanzibar? Je, anaweza kutema wabunge waliompa “uhalali” kwa kuwarejesha
katika kukurukakara za kuomba kura?
Sikiliza kauli za marais Magufuli na
Shein baada ya kikao cha Dar es Salaam.
Vyombo vya habari vilimnukuu Rais
Magufuli akisema amehakikishiwa na Maalim Seif kuwaa wanaendelea vizuri katika
mazungumzo; na kwamba amemtaka “…wakamalize majadiliano yao na apige kazi.”
Ikulu haijakanusha.
Naye Dk. Shein alinukuliwa akiwaambia
waandishi wa habari, “…mazungumzo yanaendelea vizuri na yatakapomalizika
tutatoa taarifa kwa umma kuwaeleza maafikiano yaliyofikiwa.”
Kauli hizi mbili hazitofautiani. Kama
Magufuli ana maana ya anachosema, na kwa misingi iliyoelezwa hapo juu; basi
siyo tu hakuna sababu wala haja ya kurudia uchaguzi; bali hakuna uchaguzi.
ndi.
No comments
Post a Comment