FURSA ILIYOPOTEA?
DK.
SHEIN HAJUI JINSI YA KUKUMBUKWA
DAIMA?
Dk. Ali Mohamed Shein hajui jinsi ya
kuandika historia isiyofutika. Hajui. Angekuwa anajua asingekuwa ameng’ang’ania
kiti cha urais aliopoteza miezi mitatu iliyopita.
Katika mazingira tuliyomo, Dk. Shein
aweza kusema na kutenda – kwamba:
1.
Asilazimishwe kuwa rais Zanzibar wakati anajua kuwa hakushinda. Aachie.
2.
Asichonganishwe na umma wa Zanzibar kwa kitu kinachopita; tena haraka.
Aachie.
3.
Asifanywe kondoo wa kafara kwa madai ya kulinda umoja wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM). Aachie.
4.
Asifanywe chanzo cha mfarakano mkuu na hata umwagaji damu; eti kwa kuwa
analinda uhai wa CCM Visiwani. Aachie.
5.
Asifanywe kinga ya wachochezi wa ubaguzi wa rangi na asili ya watokako.
Aachie.
6.
Asifanywe mjinga, mpuuzi na mroho wa madaraka; kumbe wanaomsukuma ndio
wenye maslahi mapana; hata ya kifisadi. Aachie.
7. Asipoteze hadhi yake ya kisomo na utendaji
katika kipindi chake chote cha uongozi; vyote vikaonekana kuwa si kitu. Aachie.
8.
Asifanywe kuwa mtu asiye na uwezo wa kufikiri – kuona, kusikia na
kutenda inavyopasa – kwa mtu mstaarabu na mweledi. Aachie.
9.
Asifanane na walafi wa kale na kale wasemao hawawezi kuachia madaraka
kwa madai kuwa hawajaona “mwingine anayefaa.” Upuunzi mtupu. Nani amewatafuta
na kuwakosa. Aachie.
10. Asishindwe kuona mikono
lukuki ya historia ikiwa imekunjuliwa, tayari kumpokea Dk. Shein na kumweka
kwenye nafasi yake anayostahili na hata kuenziwa. Aachie.
11. Asikatae kushiriki kazi kuu
ya kuepusha migogoro na hata vita; na papohapo kuwa balozi wa amani kutoka
Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika. Aachie.
12. Asipoteze nafasi hii adimu
ya kuwa kiongozi mwingine katika Afrika asiyeenda kwa nguvu za ulafi na tamaa
isiyoelezeka ya ufalme wa kisiasa – angalia: Uganda, Kongo, Burundi, Rwanda,
Zimbabwe – wengi tu. Wanataka na wanajigamba kuwa watafia kwenye kidonda kama
inzi. Aachie.
13. Afahamu kuwa siyo kila
wakati mihula ya utawala wa kisiasa huenda kwa hesabu za miaka. Anaweza
akaingia leo akatoka kesho – kwa sababu mbalimbali nje ya uwezo wake, uwezo
wangu; na bado nchi ikaendelea kuwapo. Aachie.
14. Afahamu kuwa maisha ya watu wa Zanzibar
na Tanganyika, ndio muhimu zaidi kuliko maslahi ya CCM, viongozi wake maslahi
yake binafsi. Aachie.
15. Ajue kuwa atakuwa mtu huru;
anayetembea kifua mbele, anayeheshimika na anayepigiwa mfano; kuliko kutumiwa
kama chambo au kichocheo cha vurugu, mifarakano na hata ukimbizi na umwagaji
damu (kama ilivyowahi kuwa). Aachie.
Tutamwona wa hekima, heshima; na jasiri
atendaye kwa manufaa ya wananchi wake na taifa lake; hata dunia yake. Akatae kuwa
mkuki wa kuchomea wanaotafuta mwafaka kwa njia iliyokubaliwa kikatiba na
kisheria – Uchaguzi. Aitikie sauti ya wapigakura wa Zanzibar. Ndio waamuzi wa
kweli na pekee. Aachie ngazi .
Tanzania ya wapenda amani na utulivu
itambeba. Afrika itamuenzi. Historia itamwandalia makao ya furaha kwa uhai wake
wote uliosalia.
Hata baada ya kifo chake – na kwa imani
yake – roho yake itawekwa mahali panapostahili – bila shaka karibu na watu wake
ambao atakuwa amekataza kusaliti.
Inawezekana. Huu ndio ufalme kuliko wa
kinyang’au wa “sinzia nikumalize!” Dk. Shein upo?
ndi.
No comments
Post a Comment