Header Ads

LightBlog

CCM YABANWA MBAVU, YABAKIA KUJITETEA

SITAKI

Waliozoea kubana upinzani nao wabanwa

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kuwa mtovu wa shukrani kwa waliosoma makala yangu ya wiki iliyopita juu ya ahadi za mgombea urais Jakaya Kikwete alizotoa mkoani Kagera na ambao wamenipelekea maoni; hasa wakazi wa Bukoba, Ukerewe na Kigoma.

Ni kilio kitupu. Tuanze na aliyesahihisha tukio la kihistoria. Huyu alisema meli ya mv Viktoria iliingia ziwani Viktoria mwaka 1963 (siyo 1965) baada ya kukata maji kwa “kipindi kirefu” katika mto Thames nchini Uingereza. Namshukuru.

Mwingine akasema nilionekana kuonyesha kuwa mv Viktoria bado inafanya kazi. Ameniuliza, “Watu wangapi wanapanda meli yako hiyo? Siku hizi watu hawana imani nalo. Wanapanda mabasi. Kutoka Bukoba saa 12 asubuhi unakuwa Mwanza kabla ya saa sita mchana siku hiyohiyo. Nani atapanda mzoga. Limebaki kubeba mikungu ya ndizi.”

Huyo naye amejitambulisha kuwa anatoka Bukoba. Sasa huyu mwingine anatoka Ukerewe. Anasema mv Serengeti iliyokuwa ikienda kisiwani humo imeegeshwa gatini. Hawana huduma.

Amesema “ka-meli kengine kanakoitwa Butiana, miezi mine au mitano iliyopita, kalizimikia ziwani” ambako walikwama na hatimaye kukokotwa saa sita baadaye. Hakuna usafiri.

Nacho kivuko cha Clarias, ambacho kina umri mkubwa kuliko mbao zilizokiunda, kimeanza kuwa na mwendo usioweza kukifanya kishinde iwapo kitashindanishwa na kinyonga. Ukerewe wanalia. Si leo. Si jana. Si juzi. Kilio cha miaka mingi kama kile cha Bukoba.

Mwingine huyu hapa. Anatoka Bunazi. Anajadili mambo mawili; tena kwa ufupi. Kwanza, anasema mkuu wa wilaya amesema hawezi kushiriki kugawa eneo la ranchi ya Kakunyu ambalo mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (rais) aliagiza likatwe na kugawiwa wananchi wenye uhaba wa ardhi, badala ya kuwafukuza.

Anasema mkuu wa wilaya amesema kauli ya mgombea haitoshi. Kwamba kilichopatikana kwa karatasi (hati ya kisheria), sharti kuondolewe katika hadhi hiyo kwa karatasi pia. Shaka imejengeka hasa.

Pili, anasema mgombea aliahidi uwanja wa ndege wa kimataifa lakini wananchi wana shaka kubwa. Anasema, makao makuu ya nchi, Dodoma hayana uwanja wa ndege wa kimataifa; Mwanza mji wa pili kwa ukubwa nchini hauna uwanja wa kimataifa.

Anasema uwanja wa Songwe, Mbeya ambao “wanatwambia utakuwa wa kimataifa, haujakamilika. Tunajiuliza kuna kitu gani kikubwa Misenyi (Bunazi) ambacho kinaweza kufanya serikali ijenge haraka uwanja wa ndege wa kimataifa, kilometa 40 au 50 kutoka mjini Bukoba.”

Lakini mkazi wa Kigoma/Ujiji ndiye ametoa mpya. Anaandika, “…acha haya ya kununuliwa meli mpya Bk; sisi Kigoma amesema anataka iwe kama Dubai, wakati umeme tu ni mtihani huku tuna maporomoko ya mto Maragalasi.”

Ahadi hizi zote Bukoba na mkoani Kagera kwa jumla, ni kama ahadi nyingine zilizotolewa na zinazoendelea kutolewa na mgombea wa CCM na baadhi ya wagombea wengine wa urais na ubunge wa chama hicho na vyama vingine nchi nzima.

Kinacholeta tofauti kati ya mgombea wa CCM na wagombea wa avyama vingine, ni kwamba Kikwete hawezi kujitofautisha na urais. Mara nyingi pia, anaongea kwa mamlaka ya rais.

Kwa mfano, anapoagiza wananchi wakatiwe vipande vya ardhi kutoka kwenye ranchi, anaongea kwa kofia ya mwenye mamlaka juu ya ardhi, kwa mujibu wa sheria – rais – hata kama kauli yake itapingwa na kupinduliwa na wateule wake.

Lakini wingi wa ahadi, hasa zinazohusisha hata ujenzi wa viwanja vya ndege, Dubai ya Kigoma, meli, vivuko, bajaji kwa wajawazito (ahadi ya zamani); ahadi za kulipa mishahara ya wafanyakazi wa mgodi wa mkaa wa mawe Kiwira na kufufua mgodi huo, zinaonekana wazi kuwa zinatoka kwa kiwewe.

Ndiyo maana mmoja wa wasomaji ameandika, “Kikwete si anajua kuwa ni awamu ya mwisho. Hata akiahidi yasiyotekelezeka, alimradi anamalizia muda wake ikulu; atakayemrithi aweza kusema ‘siyo mimi niliyeahidi.’”

Kauli hii ya msomaji inaleta mazingira ambamo anayetoa ahadi na amri, atakuwa ameshinda. Haingalii upande mwingine. Bali hiyo siyo hoja ya msingi.

Hoja kuu ni kinachomsukuma Jakaya Kikwete kutoa ahadi nyingi na kwa wingi mara hii. Hiki kinaweza kupatikana katika kuchunguza mazingira ya kisiasa ya wakati tuliomo.

Kwa mara ya kwanza, tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, serikali imewambwa msalabani katika kampeni za uchaguzi mkuu wa rais na wabunge. Nayo imekiri.

Hoja za vyama vya upinzani zimelenga kuonyesha udhaifu katika sera na mipango ya serikali ya CCM. Zimeibua vitendo vya wizi na ufisadi chini ya serikali ya chama cha umri mkubwa. Zimeweka wazi uongo, uzemba na usanii wa viongozi.

Mara hii hoja siyo za maneno matupu. Zimesheheni takwimu na vielelezo juu ya kilichotendeka; alitenda nani, lini, wapi na katika mazingira yapi. Ni hivi: Hoja zimepangwa na kila hoja ina ushahidi mwanana ambao haupingiki. Ambao hauwezi kupuuzwa.

Rais mtaafu Benjamin William Mkapa, waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye na Rais Amani Abeid Karume, wamenukuliwa wakijadili mazingira ya sasa katika kampeni kuelekea uchaguzi mkuu.

Kwenye sherehe ya harusi ya mtoto wa Karume, mjini Zanzibar, kama miezi miwili iliyopita, viongozi hao walinukuliwa wakijadili “uimara” wa hoja za upinzani na umakini wa Dk. Willibrod Slaa.

Yalikuwa mazingira ya sherehe lakini mmoja wa viongozi hao alinukuliwa akisema kuwa chama chao kimezoea kutoa takwimu bila ufafanuzi; lakini safari hii kuna mahiri (Dk. Slaa) wa kutafsiri na kutoa takwimu nyingine zenye fafanuzi ambazo zitakuwa kisiki kwa mgombea wa CCM.

Kwa kauli hizo, alikuwa amepatikana wa kuvunja pingu za takwimu ambazo watawala walizoea kumwagwa mbele ya wananchi bila fafanuzi au walizitumia kujikweza.

Kwa mfano, kutaja wingi wa vyumba vya madarasa kama maendeleo wakati havina madawati, walimu, vitabu, chaki, maabara, maktaba na vifaa vingine.

Hizi ni takwimu zilizopeperushwa na watawala – ghiliba ya wazi kabisa – na kujikinga nyuma yake wakisubiri kupigiwa makofi na kupewa kura. Mifano ya takwimu hizi ni mingi.

Ni takwimu zinazokidhi mahitaji ya mitaji mikuu mitatu ya watawala walioko madarakani kwa miaka 50 sasa. Mitaji hiyo imekuwa ujinga, umasikini na woga.

Ujio wa mageuzi uliondoa woga mkubwa uliokuwa umetanda na kwa kiwango kikubwa kupandikiza ujasiri wa kuuliza maswali na kudai majibu.

Ujinga na umasikini viliendelea kushamirishwa na takwimu malaya zilizopewa tafsiri yoyote ile kukidhi mahitaji ya wakati uliopo.

Kuibuka kwa tafsiri ya takwimu basi, na kutolewa takwimu zinazokinzana na zile zilizokuwa zikighubika akili za wengi, kumekuwa njia muwafaka ya kuongea na umma na kuuondoa katika kiza nene.

Aidha, kuibuka kwa uchanganuzi mwanana kunafuatia pia kudhihirika kwa vitendo vya wizi mkubwa na ufisadi wa mabilioni ya shilingi unaodaiwa kufanywa na, au kwa baraka za watawala.

Mazingira haya ndiyo yanasaidia kujenga hoja nzito kuhusu mustakbali wa taifa – lakini siyo chini ya uongozi na utawala wa sasa unaotuhumniwa kutenda au kushiriki au kunyamazia yale ambayo yamekuza ujinga na kuongeza umasikini.

Hakika hoja za aina hiyo ni ngumu sana kukabili. Watawala wa sasa, wakiongozwa na anayegombea urais kwa chama kilichoko ikulu, hawana majibu. Hawana!

Wanachoweza kufanya ni kuambaa nchi nzima; wakitoa kila ahadi kwa kubakiza moja tu wasiloweza kuahidi – ufalme wa mbiguni. Basi.

Hilo ndilo chimbuko la ahadi nyingi za Kikwete. Zitakuwa zaidi ya tulizosikia. Hata hivyo, ahadi hazijibu hoja. Zitabaki ahadi na maelezo yake na wakati mwingine amri na maelekezo.

CCM itakiri, leo au kesho – na siyo suala la ushabiki bali uchambuzi sahihi – kuwa hoja za sasa za upinzani hazijibiki. Kama kuchaguliwa itakuwa ni kwa mazoea tu yaliyodumishwa na mitaji yake miwili iliyobakia: ujinga na umasikini.

Kwani kinachofanyika hivi sasa na ambacho hakijawahi kufanywa, ni kwamba CCM na serikali vimechukua upande ule ambako vimekuwa vikisukumiza wapinzani na wananchi – ule wa kujitetea; wa kujihami.

Kwa chama kilichoko ikulu kuwa katika nafasi ya kujikinga, kujihami na kujitetea wakati wote; kuna maana kuwa “yamewafika.” Kuwa mabadiliko yaja.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

1 comment

Innocent Kasyate said...

Mzee hongera kwa wananchi wengi hawakupiga kura 58%. Upinzani wafanye nini ili kuhakikisha watu wengi wanapiga kura?
Jk amepata kura za 42% waliojitokeza na akapata 61%. CCM ina wanachama 3000 tu, JK kapata kura takriban 5000, swali tujiulize je ile 58% iliyobaki kwa vyovyote vile wengi wao si ccm. Je ni kwanini hawakutokea? Mimi nimekosa majibu kabisa.

Powered by Blogger.