SERIKALI YAHAHA KUNYAMAZISHA HakiElimu
SITAKI
Waziri anayekemea HakiElimu
Na Ndimara Tegambwage
SITAKI waziri anayeabudu woga na utii bandia. Sitaki waziri anayeabudu ukasuku na kubeza kazi nzuri ya elimu. Taifa litaangamia.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Lucy Nkya aliripotiwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, akisema matangazo ya asasi ya HakiElimu yanaamsha “chuki katika jamii.”
Kwa kujiamini, Nkya anaripotiwa kuambia Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuwa HakiElimu inakosoa tu; inajenga vijana na watoto kuona serikali ni ya kifisadi; na kuahidi, “Iko siku serikali itaonyesha makucha yake.”
Sasa twende kwa mfano wa waziri wa tangazo “baya:” Kwamba HakiElimu inatoa tangazo linalohusu wizi wa mabilioni ya shilingi kutoka akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika benki Kuu (BoT).
Katika tangazo hili wanafunzi wanaulizwa thamani ya fedha; nao wanajibu kwa kuthamanisha fedha hizo zilizoibwa (Sh. 133 bilioni) na vitu halisi.
Huyu analinganisha fedha hizo zilizoibwa na idadi ya zahanati ambazo zingejengwa nchi nzima. Yule analinganisha fedha hizo na shule ambazo zingejengwa nchi nzima. Mwingine analinganisha kiasi hicho na mishahara ya walimu nchi nzima na kwa kipindi gani.
Iko wapi njia bora ya kufundishia thamani ya fedha au vitu kuliko hii? Uko wapi “uhalifu” wa HakiElimu?
Angalia msanii maarufu nchini, Masoud Kipanya. Anaonyesha kuwa ukitaka kujua thamani na wingi wa Sh. 133 bilioni, tandika chini noti za Sh. 10,000 – moja baada ya nyingine – kutoka katikati ya jiji la Dar es Slaam.
Katuni inaonyesha noti ya mwisho ya Sh. 10,000 (kwenye Sh. 133 bilioni), itatandikwa stendi ya mabasi ya Arusha mjini. Hiyo ni baada ya kubandika njia nzima, zaidi ya kilometa 500 kwa barabara kutoka Dar es Salaam kupitia Ubungo, Kibaha, Mlandizi, Chalinze, Segera, Moshi hadi Arusha mjini.
Chukua mfano wa ukubwa na thamani ya majengo ya hospitali ya Bugando, jijini Mwanza. Hayo ndiyo majengo ya kwanza kwa urefu na eneo jijini humo (maghorofa).
Sasa sikiliza mkazi wa Mwanza anayeelezea ukubwa wa nyumba nyingine alizoona katika miji mingine, “Eee, ni kubwa kweli. Yanaingia mabugando mawili!” Umuhimu wa kulinganisha na kuthamanisha.
Zingatia ubunifu katika njia mbili za mwisho hapo juu. Lakini na njia ya HakiElimu inayolalamikiwa, ndiyo muwafaka katika kuwezesha mwanafunzi, hata mtu mzima, kufikiri, kubaini na kuelewa. Tarakimu kavu hazina maana kama hazikupewa thamani.
Mwanafunzi anahitaji nyenzo za kumsaidia kufikiri. Hasa baada ya kujua kusoma na kuandika, mwanafunzi hawi tena “kapu la mama” la kujaza kila ushikacho; bali ubongo unaokuzwa kwa uchambuzi na upembuzi.
Kwa hiyo, mwanafunzi aliyewezeshwa mapema, kuangalia kwa makini, kutafakari, kuhoji na kudadisi, kuchambua, kuthamanisha na kumiliki stadi za maisha, ndio mwakilishi wa elimu bora ambayo ni msingi imara wa taifa linalotaka maendeleo.
Ni nyenzo hizi ambazo hukwangua ukurutu wa kasumba vichwani mwa watoto na wazazi wao; huua upupu katika mbongo zilizokengeuka na huweka mazingira ya kupokea kwa kuchambua na hatimaye kuangamiza ukasuku.
Waziri Nkya analalamikia wanafunzi kupewa nyenzo za kufikiri, kuthamanisha na kutenda. Anasema kauli za kutaja thamani ya fedha za EPA kwa kutumia vielelezo, zinasababisha kuzomewa kwa watoto wa baadhi ya viongozi wanaodaiwa kuiba, hadi wanahamishwa shule.
Kuna haja ya kuzingatia haya: Kazi ya elimu, na hii ni daima, ni kuondoa ujinga; kufukuza ukungu na giza; kuondoa utata na mashaka; kuhakiki uhalisia wa hali na kushikisha stadi ili mtu aweze kuvuka mazingira aliyomo na kuingia maisha bora zaidi.
Wanafunzi wanaooanza kushika haya mapema wanabadilika haraka. Wanaelimika kwa maana halisi ya neno hilo; bila unafiki wala upendeleo. Hawahitaji tena huruma ya mwalimu, sifa za mwanasiasa, wala wazazi wa kuwaibia mitihani. Wanafikiri.
Sasa kama wanafunzi wameanza kubaini kuwa miongoni mwao kuna wenye wazazi walioiba; kwamba watoto wa walioiba hubebwa kwa magari ya wizi hadi shuleni, sokoni na harusini; kwamba watoto hao wana fedha za kuchezea, hupata chakula cha mchana, hawadaiwi karo wala michango, basi tayari wameanza kupata elimu.
Kwa wanafunzi kutambua mahusiano miongoni mwao; kuelewa nani anafanya nini linalosaidia au linaloanganiza taifa; kutambua matabaka miongoni mwao na jamii kwa ujumla; na kujua ni tabaka lipi limeapa kuangamiza mengine na kwa nini; hakika hiyo ni elimu.
Elimu hii haiwezi kuwa imetokana na HakiElimu peke yake. Kuna vyanzo vingi: magazeti, redio, televisheni, mikutano, asasi nyingi, simu za mkononi, maongezi mitaani, katika vyombo vya usafiri na katika uchambuzi wa maisha ambao wanafunzi wamewezeshwa kufanya.
Elimu yote hii, kwa njia mbalimbali, ndiyo Waziri Nkya anaita kuamsha “chuki katika jamii?” Lakini waziri ana ujumbe: Kwamba kuna chuki ndani ya jamii, lakini “isiamshwe.” Wanyonge wanyongwe, mapapa wadunde. Basi.
Bali suala la kuzomea watoto wa “mafisadi” linahitaji msisitizo wa aina yake. Wanafunzi, kwa kupitia wanafunzi wenzao, wanazomea kupe aliyejipachika kwenye mgongo wa mwananchi. Hawajali kama ni baba wa huyu au yule. Na hii haikuanza jana na haikuletwa na HakiElimu.
Hata hivyo, kuzomea ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Pale ambapo walioko madarakani wanaweza kunyamazia ukupe na uozo, zomeazomea huwakurupusha mafisadi na kuwanyima raha.
Ni zomeazomea hiyo ambayo pia hufanya watawala, kwa aibu, wakae wameziba nyuso zao kwa viganja kama nyani (Asante Shaaban Robert). Hapo ndipo wanaigia wanafunzi walioanza kupata nyenzo za maisha na kuhamasisha kuwa mafisadi wasizomewe tu bali watengwe na jamii staarabu.
Waziri Nkya na labda hata wenzake, anaonekana kutaka taifa lenye watoto “wanaojazwa” kauli, nyimbo, ngonjera na mashairi ya wasifu ili wawe na “utii na heshima kwa serikali na viongozi” na hatimaye waondoke na “elimu ya karatasi.”
Anataka taifa ambalo wanafunzi wake watalazimishwa au kulaghaiwa kuabudu, kusifia na kushangilia ufisadi, eti kwa kufanya hivyo ndiyo kudumisha “utii.” Hakika hilo ni taifa linalojinyonga kimyakimya na taratibu. Litaangamia.
Hata kama wezi wa fedha za EPA wanachefuka na hawataki kutajwa tena; hata kama wenzi wao – wake, waume, watoto, ndugu na marafiki – watakuwa wamechoka kuitwa wanavyoitwa; huu hauwezi kuwa msingi wa Waziri Nkya kukemea HakiElimu.
Kwanza, ujumbe wa HakiElimu katika matangazo anayolalamikia waziri siyo wa kubuni. Ni takwimu za serikali na wadau wengine wengi ambazo zinapewa maana.
Pili, njia hii inayotumiwa na HakiElimu ni njia sahihi na bora zaidi kwa kuwa inafikirisha na kumwachia nyenzo muhusika ili aweze kuangalia maeneo mengine katika maisha binafsi na taifa.
Tatu, ujumbe katika tangazo haukulenga wanafunzi peke yao. Jamii iliyojaa wengi wenye fikra za aina ya waziri, inahitaji ujumbe wa aina hii, kwa mtindo huu wa uwasilishaji, kwa ajili ya ukombozi wa mtu mmojammoja na jamii yote.
Nne, waziri bado anaamini katika “mabavu ya serikali,” hivyo anajisikia kuwa kileleni ambako, kama wengi walioko huko, anapumzisha akili na kuanza kutumia vitisho, kejeli na mabavu.
Tano, inaonekana bado waziri ana mawazo kuwa huwa kuna serikali moja katika maisha ya watu na hii aliyomo haitaondoka “milele.” Hapana. Serikali huzaliwa na kufa. Huenda ijayo haitakuwa na mafisadi au itakithiri kwa ufisadi.
Sita, kauli na hatua ambazo waziri anafikiria ni za vitisho; zinaashiria uporaji na uingiliaji uhuru wa kufikiri na kuwasiliana; na zinajenga msingi wa kuvunja haki za binadamu.
Saba, waziri analalamika kuwa HakiElimu ina mwendo wa kukosoa tu. Hapa waziri anataka serikali isifiwe. Kama serikali inatenda wajibu wake kwa nini isifiwe?
Kama serikali imesahau, imedharau, imeshindwa kutenda wajibu wake, kwa nini isikumbushwe kwa njia ya kutaja dosari? Asasi za kiraia hazikuundwa kuisifia serikali bali kuwa wadau muhimu katika kuhudumia wananchi.
Nane, kuna kila sababu ya kujenga mashaka juu ya waziri kutumwa au kujituma kujaribu kutishia kuua mkondo sahihi wa kupata elimu bora. Nkya anashauriwa kujifunza na kuvumilia. Lakini muhimu, aache HakiElimu ifanye kazi yake.
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili(26/10/2008). Mwandishi anapatikana kwa simu: 0713 614872 na imeili ndimara@yahoo.com).

2 comments
Hii ni wazi kwamba kidogo kidogo mafisadi na mawakala wao, wameanza kupata shida kutokana na uwezo wa asasi mbalimbali na vyombo vya habari kuamsha moyo wa kizalendo miongoni mwa watanzania, katika kupigania uadilifu na uzalendo katika utendaji serikalini.
Kama kuna kundi ambalo linalostahili kuelimishwa ili liwe na udadisi wa mambo, basi ni WATOTO. Kila mtanzania ana wajibu wa kujenga akili ya mtoto yenye uwezo wa kutambua kwamba taifa hili ni letu sote, na rasilimali zilizopo zinastahili kuboresha maisha ya watu wote na si wachache kama ilivyo sasa. Huu ni wajibu wetu sote, HAKI ELIMU na wengineo wanaonyesha mfano tu. Kizazi kijacho(watoto) kipewe uwezo wa kutambua kwamba ufisadi ni aibu na ni dhuluma.
Mzee endelea tu na kuwabana hawa viongozi wetu wasiokuwa na elimu ya kutosha.
Kuna tatizo la kielimu hapa mzee, hivi kweli waziri anayeittwa Dokta fulani anaweza kutoa kauli ambayo haijaka sawa? ni nini kama si upunguani?
Nawakilisha
Post a Comment