Header Ads

LightBlog

WALIMU WANAPOFANYWA NDONDOCHA

Amri 10 za CCM kwa walimu?

Na Ndimara Tegambwage
WIKI iliyopita nilikuwa darasani, katika ukumbi wa Taasisi ya Benki Kuu (BoT) jijini Mwanza. HakiElimu walikuwa wakifafanua maana ya “Elimu Bora” na mimi nikielekeza jinsi ya kuandika habari za uchunguzi katika eneo hili.

Ghafla simu yangu ikalia. Ni ujumbe. Wanaita sms. Naichukua na kusoma ujumbe. Sina sababu ya kukalia kilichokuwemo kwenye ujumbe huu.

Zilikuwa “amri 10” za Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa walimu nchini. Niziandike au nisiziandike…? Basi, kwa kuwa sikusikia jibu lako naziandika:

1. Mara zote mfanye mwalimu kuwa mwoga kwa chama (CCM) na serikali
2. Mlaghai kwa wito na si kipato
3. Mfundishe kuwa mpole ili asidai haki zake
4. Mfanye asiajiriwe sekta nyingine ili umtumie
5. Mlipe kidogo atumike milele
6. Mtumie kwenye chaguzi na sensa ili ajione bora.
7. Msifie kila siku avimbe kichwa
8. Weka viongozi wa CCM kwenye CWT asifurukute
9. Mtumie kama ubao wa matangazo kwa Tshirts za CCM
10. Mara zote wagawe na kuwatawala.

Nilianza kucheka peke yangu. Kicheko kikaenea kwa wengine. Kila mmoja darasani akaanza kucheka hata kabla ya kuwaambia kipi kilikuwa kinanichekesha. Ukawa kama ule ugonjwa wa kucheka ukumboa shule mara kwa mara.

Ndipo nikaanza kuwasomea ujumbe wa simu. Wengi walicheka. Wachache walinuna. Huwezi kujua haraka kwa nini hao wachache walinuna. Labda waliwasikitikia walimu au labda walikuwa makada wa chama kinachodaiwa kuwatotoza walimu.

Je, waliocheka? Niliuliza mmoja wa washiriki wa mafunzo. Alijibu kuwa amefurahishwa na ujumbe mkali, wa maana tena wakati walimu wakiwa wanajiandaa kuandamana kudai haki zao, ukiwa umeandikwa kwa njia ya kejeli.

Mwingine akasema amefurahishwa na hali ya juu mno ya usanii ya kuwasilisha jambo kubwa na lenye ujumbe mkali lakini kwa njia inayoonekana ya utani.

Mwingine akasema ni ujumbe uliokomaa; usioweza kupuuzwa na unaoeleweka zaidi. Huyo aliongeza, “Huo ndio ukweli wenyewe kuhusu walimu.” Huyu ni mwandishi wa habari aliyewahi kuwa mwalimu.

Ujumbe wa simu ulikuja wakati mwezeshaji Gervas Zombwe wa HakiElimu amemaliza kufafanulia washiriki “Nini maana ya elimu bora.” Alikuwa pia amewauliza iwapo waliishawahi kuona taarifa yoyote ya serikali juu ya elimu bora.

Kwa mfano, wanafunzi wanajua kusoma na kuandika? Wanaelewa kinachofundishwa? Wameshika walichosoma na kusomeshwa? Wana uwezo wa kuuliza maswali kuonyesha sasa wameelewa?

Labda hayo ni madogo. Angalia haya hapa. Je, kwa elimu inayotolewa, serikali inajua jinsi ya kupima iwapo elimu imewasaidia wanafunzi? Imewapa uwezo kufikiri? Kuzalisha mawazo? Kudadisi? Kukataa mambo kadhaa katika jamii kutokana na uelewa utokanao na elimu?

Je, serikali ina njia za kupima yote haya na mengine? Kama njia ipo, mbona hakuna ripoti juu ya vipimo hivi? Inawezekana kuna vipimo lakini matokeo yake hayawekwi wazi? Au serikali haifanyi vipimo hivyo na ina sababu ya kutofanya hivyo?

HakiElimu wana usemi kwamba elimu siyo cheti. Kuna walioanzisha ugomvi tayari na shirika hili kwa kauli hiyo tu. Lakini ukikaa na hao walioanzisha ugomvi utasikia wakilalamika, “Yule bwana ana digrii lakini hakuna anachoweza.”

Kwa nini amefikia kupata cheti cha Kidato cha IV, cha VI au digrii bila kufahamu kuwa hajui chochote? Si kwa kuwa hakuna vipimo vya uelewa? Si kwa kuwa hakuna vipimo vya elimu bora vinavyozingatia uwezo wa kufikiri, kudadisi na kuzalisha mawazo ang’avu yanayojitegemea?

Si kwa kuwa vipimo vilivyopo vinalenga kupima uwezo wa kukumbuka tu lakini siyo uwezo wa kufikiri? Si kwa kuwa mitihani ni ya kuvizia na iliyolenga kujenga misingi ya kubahatisha tu na siyo ujenzi wa akili inayojitegemea?

Hoja ya HakiElimu kuwa elimu siyo vyeti haipingi kuwa na vyeti au digrii. Digrii ni muhimu. Siyo moja. Nyingi tu. Lakini utukufu wa digrii uwe kichwani na siyo kwenye karatasi. Kwamba, cheti kiwe kitambulisho tu cha muhusika aliyepata uwezo wa kufikiri na ung’amuzi.

Ndiyo maana lazima watoto wapelekwe shule. Lakini watoto hawaendi shuleni kutafuta digrii. Wanakwenda kutafuta elimu. Wakiishaipata, wapewe cheti kama ithibati.

Ukimaliza shule ya msingi, sekondari au chuo kikuu bila kuwa na uwezo wa kufikiri, kudadisi, kuzalisha mawazo na kupembua masuala kadha wa kadhaa, unapewa cheti kwa misingi ipi? Umesoma lakini hujapata elimu na hustahili kupewa cheti.

Hapa, cheti au digrii itakuwa liwazo tu kwa ujinga uliotukuka kwa kupitia madarasa mengi na kupata marafiki wengi kwa miaka mingi darasani. Basi.

Lakini mwalimu anayepaswa kutoa elimu tangu ngazi ya chini ya elimu ya awali, yuko katika mazingira yapi? Ana elimu gani, achilia mbali karatasi ziitwazo vyeti na digrii? Ana vifaa gani?

Mbali na yote hayo, je, ni mwalimu yuleyule ambaye ujumbe wa simu unaelezea kwamba amefungwa mikono na miguu na kwamba sharti aimbe utukufu wa chama tawala, alemae, asilete uasi, awe ndondocha ndipo atathaminiwa?

Kuna mambo matatu hapa: Ujumbe wa simu. Mgomo wa walimu. Darasa la HakiElimu. Yote yalikuja kwa wakati mmoja. Kuna kila sababu ya kuyatafakari kwa pamoja.

Je, watawala wanahitaji elimu bora kwa nchi hii? Kama hawahitaji, wajue wananchi wanahitaji. Mahali pa kuanzia ni kuwa na lugha moja ya kufundishia – Kiswahili – ambayo kwa kiwango kikubwa inaeleweka kwa mwanafunzi na mwalimu.

Jambo jingine ni kuwa na mtaala mmoja wa kufundishia. Leo hii kuna mtaala wa Aga Khan, mtaala wa Cambridge na mtaala wa “taifa” (?!) Mitaala mitatu katika nchi moja. Hii ni kwa manufaa ya nani?

Kingine ni kuweka utaratibu wa kupima elimu bora – kujua kusoma na kuandika, kufikiri na kudadisi. Lakini upatikanaji wa elimu hii utatokana, pamoja na mambo mengine, mapinzuzi makubwa katika kuimarisha uwezo wa walimu wenyewe na mazingira waliyomo.

Kama mwalimu atakabwa koo ili aabudu siasa, kama ujumbe wa simu unavyotaka niamini; hata kile kidogo, ambacho kingepatikana katika mazingira magumu, hakitapatikana.

Itakuwa kama serikali imefunga shule na kuamua nchi itawaliwe na watu wawili: Mzee siasa za chama tawala na ujinga. Lakini bado serikali inaweza na ina fursa kubwa ya kubadili mkondo huu.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili 19/10/2008. Mwandishi anapatikana kwa simu 0713 614872 na imeili:ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.