Header Ads

LightBlog

VURUGU CHADEMA KUUA HARAKA IMANI YA WANANCHI WENGI

Mbowe: Jenga chama ndani ya umma, acha mahakama

Na Ndimara Tegambwage

JE, kuna haja ya mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kumburuza Zitto Kabwe mahakamani kwa madai ya kumtuhumu kupokea fedha kutoka kokote kule?

Ushauri: Hakuna haja wala sababu.

Vyombo vya habari vimeripoti wiki hii kuwa Mbowe “anasadikiwa” kuwa na nia ya kumshitaki Zitto Kabwe mahakamani.

Kisa? Eti Zitto, ambaye tayari amenyang’anywa unaibu katibu mkuu wa chama na unaibu msemaji mkuu wa upinzani bungeni, “amemdhalilisha” Mbowe kwa kumtuhumu kuchukua fedha kutoka kwa Nimrod Mkono na Rostam Aziz.

Katika mazingira ya kawaida, kila mwanasiasa anapaswa kujibu tuhuma alizotwishwa. Kujibu na siyo kushitaki.

Kama anayetoa tuhuma amekwenda mahakamani, ni vema kwenda kujibu mahakamani. Kama ametoa tuhuma kupitia redio, ni vema kujibu kupitia redio. Kama ni kupitia televisheni au magazeti, ni muhimu kujibu kupitia hukohuko.

Siku hizi kuna mitandao ya kijamii. Kama tuhuma zimepitia huko, ni vema mtoa tuhuma akajibiwa hukohuko au kupitia chombo ambacho kimenukuu tuhuma za mtandao na kuzichapisha au kuzitangaza. Siyo kushitaki na siyo mahakamani.

Muhimu hapa ni kujibu tuhuma. Ukiwa mwanasiasa na ukatuhumiwa kuwa gari lako limewahi “kukamatwa na nyara za serikali;” fanya hima ujibu. Usipojibu, basi tuhuma inaganda na kudumu.

Ukituhumiwa wizi wa kuvunja benki au kuibia wananchi kupitia miradi yao midogo au mikubwa, jibu haraka na ikiwezekana papohapo au siku hiyohiyo.

Usipojibu, tuhuma inaganda au inatapakaa; utaendelea kutoa mwanya kwa muhusika kusambaza tuhuma kwa shabaha anayojua mwenyewe.

Ukituhumiwa ujangili, hakikisha unajibu haraka na inakuwa kwenye rekodi kuwa ulitoa majibu na majibu thabiti yanayoendana na tabia na mwenendo wako kama unavyoonekana katika jamii.

Usipojibu, tuhuma itaenea na wote waliopata kuisikia watakuwa wakikutazama na kukuona katika sura hiyo ulimochorwa.

Kama jamii haijaelewa na kukubali mienendo ya ushoga, na wewe siyo shoga au ni shoga, ni vema kujibu haraka tuhuma kwamba wewe ni shoga.

Ni vema kuweka msimamo wako katika hilo na kwa wafuasi wako kujua na labda hata kuheshimu au kudharau. Usipojibu, siyo tu utaendelea kudhoofisha wafuasi wako, bali utakosa pia fursa ya kujenga mantiki ya kile ufanyacho au unachosimamia.

Hoja hapa ni kujibu na siyo kushitaki. Hakika hakuna sheria inayozuia mtu kwenda mahakamani na kujibu kwa njia ya kushitaki. Hapana! Bali jambo linalohitaji jibu kupitia njia lilimotokea, halina sababu ya kugeuzwa kuwa shitaka.

Usipojibu uko matatani. Wanaoweka rekodi zako kisiasa ni wengi. Wanaodondosha unyayo wao kila unapotoa wako ni wengi.  Wanaofuatilia kauli zako tangu alfajiri hadi uendapo kitandani ni wengi. Wanaotaka kuchukua nafasi yako ya kisiasa ni wengi pia.

Usipojibu, siku ya siku, ukiwa unatafuta nafasi ya kisiasa, utatwangwa kombora la kile ambacho hukujibu na wakati huo hutaweza kupata majibu ya kuwaridhisha waliokulenga tangu zamani.

Ni kwa msingi huu sharti ujibu tuhuma. Katika hili, Mbowe anaweza kushauriwa na wenzake kuwa hana haja wala sababu ya kwenda mahakamani kumshitaki Zitto. Iko wapi? Kama anayemtuhumu hakwenda mahakamani, yeye anakwenda huko kufanya nini?

Chukua mfano wa Nimrod Mkono, wakili wa mahakama kuu na mbunge wa Musoma Vijijini. Akijibu tuhuma za kutoa mamilioni ya shilingi kwa Mbowe, alisema hajawahi kufanya hivyo. Basi. Rekodi inabaki hiyohiyo hadi zitakapopatikana taarifa tofauti.

Naye Rostam Aziz amejibu kwa kejeli kwamba tangu alipoona kuna “siasa uchwara” katika chama chake (CCM), amekaa kimya na hataki kurejea katikati ya minyukano kupitia madai ya yeye kumpa Mbowe mamilioni ya shilingi.

Hilo nalo linabaki hivyo hadi yatakapopatikana maelezo ambayo yanakinzana na kauli hiyo – na majibu hayo. Kujibu tuhuma na hata malalamiko, ni muhimu katika siasa.

Bali tuhuma za sasa, kutoka kwa mmoja wa waliokuwa viongozi wakuu wa Chadema, zinaweza kuzua mtafaruku mkubwa ndani ya chama tawala: Kwamba viongozi wake wanatoa fedha za kuneemesha chama cha upinzani ili mgombea urais wake ashinde!

Kwamba akishinda iweje? Kwamba wanataka kuhamia upinzani? Kwamba wao ni popo – wamesimama kuwili? Kwamba wanasaliti chama chao, ili iweje? Kwamba wameona mgombea wao anapwaya? Tuhuma hizi zinaweza kuwa zinalenga nini?

Hii ndio maana hata anayejibu tuhuma sharti awe makini. Kwa mfano, tuhuma hizi zinalenga nini: Kuchongea viongozi wa CCM? Ili iweje? Wafukuzwe? Wakifukuzwa itakuwaje nafuu kwa Chadema au faida kwa CCM? Lakini hata bila kufika huko, na hata kama walitoa, ni kweli walitoa kama viongozi wa CCM?

Hapa kuna kitu gani cha kupeleka mahakamani? Hakipo. Ikitokea akawepo wa kusema “twende mahakamani,” anakwenda kusema nini na kwa manufaa ya nani?

Haiwezi kuwa “potelea mbali, acha chombo kizame?” Kama ni hivyo, hoja ya kupeleka mahakamani iko wapi? Na nani hajui mahakama – kwamba hata kama huna hoja na hutaki kushinda; unaweza kutumia uwanja huo kumwaga mchele kwa ajili ya kuku na njiwa na kunguru na tai?

Nani asiyejua kuwa mahakama zinachukua muda mrefu kukata mashauri? Nani hajui kuwa katika mambo ya siasa, na katika chama kilekile; mkondo wa mahakama unaanika uongo ambao wahusika wameapa kutosema?

Yuko wapi asiyejua kuwa katika mazingira ya kihasama –  ndani ya chama kimoja – na hasa katika mwonekano wa wazi wa upande mmoja kupoteza, lazima upande huo uwe na tabia ya “potelea mbali?”

Turejee katika mazingira ya sasa ya Chadema: Nani anaweza kuthibitisha kuwa hivi sasa na kati ya upande wa Zitto na upande wa chama kuna ambaye bado anashikilia kupatikana kwa MWAFAKA, kushikana mikono na kusema “yamekwisha?” Nani?

Tunapofikia hatua ya kutokuwa na matumaini ya kushikana mikono, kukumbatiana na kusema yamekwisha, basi hapo ndipo kila tuhuma inahitajika kujibiwa na hatua ya kwenda mahakamani kupuuzwa; labda kuwe na uhalifu na siyo madai ya jumlajumla tu yanayotokana na minyukano ya kisiasa.

Kuna ukweli kwamba kuandikwa na kutangazwa kila siku katika vyombo vya habari; na hasa kutangazwa kwa ugomvi, malumbano na minyukano mbalimbali kunaweza kuleta kile kinachoitwa “sura mbaya” kwa chama.

Lakini kuandikwa ni bora kuliko kutoandikwa; ambako ni kuwa mfu. Minyukano yenye mwelekeo wa kusafisha safu, yaweza kuanika yaliyofichika ambayo sharti yawe wazi na kuondolewa kwa afya njema ya chama cha siasa.

Kwa kuzingatia haya, hakuna sababu ya Mbowe kwenda mahakamani kutokana na tuhuma zilizotajwa. Azijibu. Zijibike. Wasonge mbele ndani ya CHAMA na ndani ya UMMA; na siyo ndani ya mahakama.

Mwisho
 (imechapishwa katika MAWIO la 16 Januari 2014)
Powered by Blogger.