Header Ads

LightBlog

KUTEKWA NA KUTESWA KWA KIBANDA




Wateswe au wauawe wangapi ndipo tustuke?


 Picha: Absalom Kibanda


Na Ndimara Tegambwage

MWANDISHI wa habari Absalom Kibanda, amevamiwa. Akapigwa. Akachokonolewa jicho. Akachomolewa kucha. Akakatwa kidole. Akang’olewa meno. Akaachwa kufa nje ya lango la nyumba yake iliyoko mtaa wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.

Ni usiku wa kuamkia jana, Jumatano. Hivi sasa Kibanda, mhariri mkuu mtendaji wa New Habari Media Group – kampuni inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai na The African, yuko taabani kitandani.

Aliyofanyiwa Kibanda ni yaleyale aliyofanyiwa Dk. Steven Ulimboka, kiongozi wa madaktari katika mgomo mkuu wa mwaka jana wa kushinikiza serikali kuweka mazingira bora ya kazi katika hospitali zake kwa kununua vifaa, dawa na kutoa mishahara inayostahili.

Dk. Ulimboka aliburutwa kwenye lami. Akakunjwakunjwa kama godoro na kuingizwa kwenye gari dogo. Akapigwa mara kwa mara kwa fimbo, makofi na mateke. Akang’olewa meno na kucha; akatupwa kwenye msitu wa Mabwepande, kilometa 45 nje ya jiji la Dar es Salaam. Aliponea chupuchupu.

Kwahiyo, mbinu zilizotumika kumtesa Kibanda siyo mpya. Zimewahi kutumiwa. Unaweza kusema haraka kuwa waliomtesa mwandishi, ama wamesomea chuo kimoja au ni walewale waliomtesa Dk. Ulimboka.

Je, baada ya Kibanda, nani? Lakini kabla ya Kibanda, nani? Mwaka 2008, watu watatu wakiwa na panga, chupa yenye tindikali na gongo la mti, walivamia chumba cha habari cha gazeti la MwanaHALISI tulimokuwa tumebaki wawili.

Walifanikiwa kummwagia tindikali machoni, mwandishi na mkurugenzi mtendaji wa kampuni inayochapisha gazeti hilo, Saed Kubenea. Hakupofuka kabisa lakini lazima aende India kila baada ya miezi minne kwa matibabu ya macho.

Nakumbuka kunyukana na vijana wawili – mmoja mwenye panga na mwingine mwenye gongo – hadi panga lililolenga katikati ya kichwa change lilipokoseshwa shabaha, kutua kwenye kisogo kulia na kudondokea nyuma yangu. Nilishonwa nyuzi 15. Nani alikuwa amewatuma?

Desemba 2009, mwandishi Frederick  Katulanda wa Mwanza, alivamiwa nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza sauti na kudai kuwa ana nyaraka za akaunti za benki za halmashauri ya jiji la Mwanza.

Walikuwa na mapanga. Walikuwa wakichagizana kwa kusema, “Kata kichwa! Kata kichwa!” Waliondoka na mafaili. Walimwachia kilema mguuni na makovu mikononi.

Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi wa jiji la Mwanza, walikusanywa na wenye uwezo kufanya maandamano makubwa kwa walichoita “kupinga mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo” na kudai kwamba alikuwa Mkenya na “siyo raia wa Tanzania.”  

Hii ilikuwa baada ya filamu iitwayo “Darwin’s Nightmare” kuonyesha jinsi wananchi wakazi wa jiji wanavyokula mapanki badala ya samaki.

Mgamba alidaiwa kuwabeba watengeneza filamu na kuwaonyesha maeneo ambako kweli kunguru na binadamu walikuwa wanagombea mabaki (mifupa) ya samaki baada ya viwanda kunyofoa minofu ya kuuza Ulaya. Mgamba alilazimika kuwa “mkimbizi” jijini Dar es Salaam.

Sept 2010 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, katika eneo la Nyambiti, jimbo la Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, mwandishi Frederick Katulanda alivamiwa na kupigwa na watu wapatao 15 waliojiita “Green Guard” – wa “chama cha kijani.”

Katika “kumshughulikia,” Katulanda anasema, walikuwa wakionyesha kuwa na ujuzi mkubwa wa judo na karate huku wakidai kuwa anawaandika “vibaya” Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwaka 2011 mwandishi Richard Massatu alikutwa amekufa katika eneo la Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari viliripoti kuwa macho yake yalikuwa yametobolewa na kuwekwa gundi aina ya super glue; mguu wa kushoto na mbavu vilikuwa vimevunjika.

Vyombo vya habari viliripoti kuwa Massatu aliyekuwa mmiliki na mhariri mkuu wa gazeti la Kasi Mpya (sauti ya umma), alionekana mara ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa na maofisa wa polisi na usalama katika baa iitwayo Cross Park katika eneo la Igoma.

Daudi Mwangosi, mwandishi wa kituo cha televisheni cha Channel Ten aliuawa kwa kupigwa risasi katikati na mikononi mwa polisi na hasa mbele ya mkuu wa polisi wa mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.

Hii ilikuwa tarehe 2 Septemba mwaka jana. Kesi bado iko mahakamani. Picha zinazoonyesha Mwangosi alivyolipuliwa, zinatia simanzi kwa kila anayethamini utu.

Mwaka huu, tarehe 3 Januari, maiti ya mwandishi Issa Ngumba iliokotwa katika pori la mlima Kajuruheta, kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko katika mkoa wa Kigoma.

Ngumba alikuwa mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Alikutwa amekufa baada ya kutoweka nyumbani kwa siku tatu.

Tangu mwezi uliopita, mwandishi wa habari Erick Kabendera anayeishi Dar es Salaam, anaishi kwa wasiwasi. Wazazi wake waishio Bukoba, wamehojiwa na “ofisa usalama” kwa kile kilichoitwa “uhalali wa uraia wao.”

Kabendera, ambaye ncha ya kalamu yake haipindwi kwa woga wala upendeleo, amekuwa akiripoti kupigiwa simu na kutishiwa kwamba “atarudishwa kwao.” Naye hajui kwao kwingine isipokuwa Tanzania.

Juzi, Jumanne, mwandishi Charles Misango wa TanzaniaDaima, alishindwa kurudi nyumbani kwake, Kimara nje kidogo ya Dar es Salaam.

Kwa siku nzima familia yake ilishinda ikiripoti watu tofauti waliokuwa wakifika nyumbani kwake wakimuulizia na wengine kuzengea nyumba tu.

“Nilipomwambia mhariri wangu juu ya hali hiyo, aliniambia ‘usiwe mjinga; nenda ukalale hotelini.’ Nilikwenda kwa rafiki yangu mwenye ua mkubwa, nikaegesha gari na kulala katika gari langu kwa kuwa alikuwa na wageni wengi,” anasimulia Misango.

Misango ni mmoja wa wahariri wanaokabiliwa na tuhuma za “kuandika uongo.” Kesi yao iko mahakamani jijini Dar es Salaam.

Kuna orodha ndefu ya waandishi wa habari waliotishwa na wanaoendelea kutishwa; waliopigwa na polisi na askari magereza (Ukonga, Dar es Salaama) kwa tuhuma mbalimbali; waliotishiwa maisha kwa simu na hata kwa kufuatiliwa na watu wasiowafahamu.

Mnamo 27 Januari mwaka huu, Ansbert Ngurumo, mhariri mtendaji wa sasa wa TanzaniaDaima alivumishwa kwamba amefariki dunia. Taarifa hii ilipelekwa pia kwenye mtandao mpana na unaoheshimika wa Jamii Forum (JF).

Hakuna ajuaye kama hakukuwa na nia ya kuua au kudhuru Ngurumo. Livumalo lipo na Ngurumo alipewa ushauri wa “…kuwa makini” kwani kila uvumi una shina lake.

Ngurumo amekuwa muwazi siku zote kuelezea jinsi baadhi ya walioko madarakani walivyoshindwa kumshawishi kuwapenda, kuwanyenyekea na hata kufanyakazi nao. 

Tatizo lililopo ni kwamba kila janga lilipotokea, baadhi ya waandishi walijitenga na kusema, “Shauri yao, nao wamezidi.” Nani amezidi wapi? Kumekuwa na tabia ya kujitenga na kubaguana.

Huko tuendako, baada ya kujikata kutoka shina kuu la wanataaluma, tunakuwa kama vifaranga vya kuku visivyo na ulinzi wa mbawa wala kelele za mama. Tunajianika mmojammoja kwa mwewe kututafuna mmoja baada ya mwingine. Tutaisha!

Nani atalinda maisha ya waandishi wa habari Tanzania? Tayari mmoja yuko kariku kufa kwa woga. Aliwaambia wenzake jana kwenye viwanja vya hospitali ya Muhimbili (MOI), “Labda tutafute makazi nje hadi mwisho wa utawala wa awamu hii nne…”

Huu ni woga, labda ni upumbavu pia. Kwamba kumekuwa na taarifa za madai ya kuua waandishi wawili maarufu wa habari na wanasiasa wawili mashuhuri; siyo sababu ya kukimbia nchi.

Kuwa na umoja katika taaluma, kuandika zaidi na hasa kuandika ukweli; kuchunguza, kuchambua na kufafanua zaidi – kuweka jamii wazi juu ya kinachoendelea – hivi vinaweza kuwa ngao kuu kwetu sasa na huko tuendako.

Bali tujenge mashaka juu ya mfanano wa mbinu za kutesa na kuua. Watesaji na wauaji waweza kuwa watu walewale. Wako wapi? Tuwasake na kuwaanika. Tunaweza katika umoja wetu.

Picha 2: Kibanda za Salva Rweyemamu, mkuu wa mawasiliano ikulu

https://www.facebook.com/ndimara.tegambwage

No comments

Powered by Blogger.