Header Ads

LightBlog

SERIKALI ITABEBA TRL MPAKA LINI?

Mbeleko ya serikali TRL

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI wananchi washindwe kujenga mashaka juu ya uhusiano wa serikali na waendeshaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Machi mwaka huu waendeshaji, wawekezaji, wabia au “marafiki” wa serikali walishindwa kulipa kima cha chini cha mshahara kama walivyokuwa wamekubaliana na wafanyakazi – kutoka Sh. 80,000 hadi Sh. 160,000 kwa mwezi.

Ilikuwa baada ya vuta nikuvute, mgomo wa wafanyakazi uliokuwa umepangwa kufanyika mwezi huo ukasitishwa. Serikali iliingilia kati, kuwakingia kifua waendeshaji, wawekezaji, wabia au marafiki zao katika kampuni ya RITES kutoka India.

Kwa serikali kukingia kifua mtu wa nje dhidi ya wananchi wapatao 3,200 siyo kazi ndogo. Ni gharama kubwa iliyosababisha serikali kupokonya kodi ya wananchi kiasi cha Sh. 3.6 bilioni ili kulipa wafanyakazi. Ili kuzuia wasigome. Ili kuokoa menejimenti ya TRL.

Tangu Machi serikali imelipa kima cha chini TRL cha Sh. 160,000 kwa mwezi kwa ahadi kuwa ifikapo Agosti, menejimenti ya TRL itaanza kulipa Sh. 200,000 kwa mwezi kama ilivyoahidi. Imeshindwa. Kwa mara nyingine serikali imeingilia kulipa malimbikizo na mishahara kwa wafanyakazi wa TRL.

Kuna nini kati ya serikali na TRL? Kuna udugu gani kati ya serikali na kampuni inayoendesha menejimenti ya kampuni ya reli? Kuna uhusiano gani kati ya maofisa serikalini na maofisa wa kampuni ya RITES kutoka India?

Je, serikali iliyoibeba menejimenti ya TRL mapema mwaka huu kwa kodi za wananchi, inajua kinachoendelea ndani ya TRL? Inajua udhaifu wa menejimenti hiyo au inaendelea kuifungia dripu ya mabilioni ya shilingi huku kirusi kikiendelea kuitafuna mfupa?

Kama serikali ilitaka kujivua biashara ya usafirishaji kwa njia ya reli, inatafuta nini katika kubeba menejimenti dhaifu isiyoweza hata kulipa mishahara ya wafanyakazi?

Serikali inalipa mishahara TRL ili baadaye ipate nini? Au inalinda maslahi ya nani au inataka kumlinda nani asiumbuke kutokana na uamuzi iliochukua au mahusiano kati ya serikali, maofisa serikalini na kampuni ya RITES?

Maswali haya yanaulizwa kwa kuwa haiwezekani kuwa “bure tu.” Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwahi kusema Machi mwaka huu kuwa pande zote mbili – serikali na RITES hawakuwa wawazi wakati wa kutoa taarifa za kuandaa mkataba.

Ilinong’onwa kuwa kila upande haukueleza uwezo wake halisi, jambo ambalo linasababisha hata kushindwa kulipa mishahara. Kama hivyo ndivyo, kwa nini mkataba usivunjwe kwa vile umejengwa kwenye ulaghai?

Je, kutoweka wazi taarifa sahihi wakati wa kuandaa mkataba kulifanywa kwa makusudi? Ili iweje? Ili nani anufaike? Ilikuwa kwa makusudi au kupitiwa? Kama kupitiwa, kwanini serikali haijachukua hatua inayostahili?

Je, maofisa wa serikali waliosema uwongo au waliotoa taarifa zisizo za kweli, wamechukuliwa hatua gani? Kama kuna kasoro ya kutokuwepo taarifa sahihi, kwa nini serikali inaendelea kuneemesha mkataba wenye malengo tofauti?

Hapa kuna madai kwamba serikali inawakopesha na kwamba watarudisha fedha hizo. Kama ni kukopesha, kwa nini serikali haikukopesha wananchi ili waendeshe kampuni yao?

Kuna suala la kulipa wafanyakazi – wananchi – wasipate adha wakati serikali yao ipo. Lakini serikali inalipa mishahara ili mapato ya RITES yafanyiwe kazi gani?

Nani anajua RITES wanapata kiasi gani kwa saa, kwa mwezi na kipindi chote hicho tangu waingie mkataba na waanze kazi? Wao wanamlipa nani kama siyo mfanyakazi?

Inaonekana RITES walikuja na baadhi ya wafanyakazi wao, hata madereva wa treni. Kuna ushahidi wa kutosha kuwa wako wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

Je, hata hawa wanalipwa kutoka kodi ya wananchi wakati wa kuepusha migomo? Serikali inafanya hayo ili iweje na kwa manufaa ya nani? Tulizo hilo linalofanywa na serikali kuipa afueni menejimenti na TRL, linalenga kumkinga nani hasa?

Hivi haiwezi kuwa kweli kwamba menejimenti ya TRL inafanya jeuri kwa makusudi kwa kuwa ina siri na baadhi ya viongozi serikalini? Kwamba wako pamoja na serikali haiwezi kufanya lolote? Kwamba serikali ikiwa kaidi basi watalipua bomu?

Kuna mambo mengi TRL ambayo yanastahili kujengewa mashaka. Mkataba wa menejimenti ya kampuni hiyo na uhusiano wa menejimenti na uongozi serikalini, ni moja ya mambo makuu ya kuchunguzwa (hili tutalijadili katika makala ifuatayo).

Kuna jinsi wafanyakazi wanavyoendeshwa, kama wao wanavyodai, “kama gari bovu.” Mfanyanyazi – fundi wa TRL wa miaka nendarudi, anawekwa benchi kwa miezi kadhaa kwa kuambiwa hajui kazi. Lini aliacha kujua kazi yake na kipi kilimsibu?

Kuna dereva wa treni anayechengwa na menejimenti kuwa hajui kazi yake wakati vichwa vyote vimezeekea mikononi mwake. Ujuzi wake umefyonzwa na nini?

Kwa ujumla kuna malalamiko kuwa menejimenti ya TRL inawaweka kando wafanyakazi wake wa siku nyingi na wenye ujuzi; badala yake inaingiza wafanyakazi kutoka nje ya nchi.

Kuna madai ya usafirishaji wa vichwa vya treni kwenda India. Kuna yanayohusu kuwepo vichwa visivyofanya kazi lakini vinalipiwa mamilioni ya shilingi kila mwezi.

Kuna mengine yanayohusu ugeuzaji vichwa vya zamani vya nchini kuwa spea kwa vichwa vinavyotoka India ambavyo inadaiwa ni vibovu.

Katikati ya madai haya, serikali inaendelea kulipa mishahara, kuipakata na kuibeba kwenye mbeleko menejimenti ya TRL. Serikali ina nini TRL na RITES? Hapa ndipo tunaanzia kujenga mashaka.

Bali kwa wafanyakazi, wembe uleule – kudai ujira unaolingana na kazi inayofanywa na kugoma kufanya kazi pindi nguvu na akili zao vinapodhalilishwa kwa ujira duni na nje ya mapatano na mwajiri.

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili 21 Septemba 2008. Mwandishi wake anapatikana kwa simu: 0713-614872 na ndimara@yahoo.com)

No comments

Powered by Blogger.