Saturday, August 12, 2017

DC amchapa viboko baba kisa gari kupigwa mawe

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga


Na Renatha Msungu, 
Nipashe, Jumamosi, 12 Agosti 2017


MKUU wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amemcharaza viboko mzazi wa mmoja wa watoto walioshambulia gari lake kwa mawe na kuvunja kioo cha nyuma jana.

Gari hilo lenye namba za usajili STL 669, lilishambuliwa na watoto watatu katika barabara kuu ya Kondoa-Dodoma, kwenye kijiji cha Paranga wilayani Chemba.

Kufuatia kupasuliwa kwa kioo hicho, DC alisimamisha gari hilo na kuwakimbiza watoto waliolipiga mawe, hali iliyozua purupushani kwa muda.

DC huyo aliwakimbiza watoto hao kwa lengo la kuwakamata na kuwaadhibu lakini hakuweza kuwakamata baada ya kumzidi mbio.

Hata hivyo, wananchi walioshuhudia tukio hilo walimtajia DC majina na sehemu wanakoishi watoto hao ili awafuate majumbani kwao.

Ndipo mmoja wa wazazi wa watoto waliohusika na shambulio hilo alikutwa nyumbani akiendelea na shughuli zake na alipohojiwa na DC kuhusu malezi ya mtoto wake, aliingia katika majibizano yaliyomkera DC Odunga.

"Malezi? Malezi gani unataka kwangu? Mtoto ametoka shule, mimi nitajuaje anayoyafanya mtaani?" Aliuliza mzazi huyo wa kiume na kufafanua kuwa "mimi najua (mtoto) yuko shule, sijui kama amevunja kioo chako."

Ndipo DC alipoonekana kukerwa na majibu hayo hivyo kuchukua fimbo na kuanza kumcharaza mzazi huyo huku akimshutumu kwa malezi mabaya.

DC alimcharaza viboko mzazi huyo wa kiume kabla ya kumuingiza kwenye gari la polisi akiwa amefungwa pingu, kwa madai ya kuendelea kujibu kwa jeuri wakati akiulizwa maswali kuhusu  malezi ya mtoto wake.

Mzazi huyo aliendelea kujibu kuwa hastahili kupigwa kwa kuwa kosa si lake na kusema kuwa apelekwe popote pale, lakini haki yake itajulikana kwa sababu wakati watoto hao wanapiga mawe kioo cha gari yeye hakuwepo.

Watoto watatu hao waliofanya tukio hilo wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka saba hadi 10.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia Odunga na mzazi huyo wakivutana huku mzazi akisikika akisema "aliyevunja kioo ni mtoto... chukueni tu hatua vyovyote haki yangu nitaipata".

Mwenyekiti wa kitongoji anakoishi mzazi huyo aliingilia kati na kudai kuwa matukio hayo ya kurushia mawe magari katika eneo hilo yapo na walishayakemea katika mkutano wa kitongoji yakapungua.

Alisema wahusika huwa ni watoto na vijana wa eneo hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Odunga alisema kijiji hicho kimekuwa na tabia ya kuweka mawe barabarani pamoja na kupiga magari mawe jambo ambalo siyo sahihi.

Alisema wanajipanga kwa ajili ya kuanza operesheni ya kuhakikisha tabia hiyo inakomeshwa kabisa "kwa sababu ni hatari kwa wasafiri na jamii kwa ujumla".

Alisema wataendelea na msako wa polisi ili kubaini familia ambazo zina vijana wenye tabia hiyo kupitia jamii inayowazunguka.

Kufuatia purukushani hiyo gari la polisi wilaya lilitinga katika eneo hilo na kuwachukua watu sita wakiwahusisha na upigaji mawe magari, akiwemo mtoto mmoja aliyetajwa kuhusika jana.

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema ameagiza watu hao waliokamatwa watolewe rumande.

Alisema Jeshi la Polisi litaendelea na upelelezi kwa ajili ya kukusanya ushahidi wa tukio hilo na baadaye hatua zaidi zitachukuliwa kwa wahusika

Kamanda Mambosasa alisema amechukizwa na kitendo cha Mkuu huyo wa Wilaya kujichukulia sheria mkononi na kumjeruhi mzazi huyo.

"Amemjeruhi maeneo ya kichwani kwa rungu na mkono wake umevimba kutokana na kipigo alichokipata." alisema Kamanda Mambosasa. "Hii si haki kiongozi kujichukulia sheria mkononi…"


Friday, August 11, 2017

Magufuli avunja Mayai ya Maafa


Siyo kila chenye watatu au vitatu ni cha “Utatu.” Ndiyo maana kuna “matatu” ambayo hayana uhusiano na waumini katika Utatu wa Maandiko.

Jina la Matatu la Kenya linatokana na magari madogo ya abiria yaliyokuwa yakitoza “mapeni matatu” – senti 10 tatu – zilizokuwa nauli katika miaka ya 1950 katika miji mingi ya nchi hiyo.

Matatu au utatu wa sasa umetoswa kabla haujachipuka. Ni Rais John Pombe Magufuli aliyetosa utatu wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Mbunge Juma Mkamia na muumini wa CCM, Lawrence Mabawa.

Mwinyi: Kama siyo kwa Katiba ya nchi, ningependekeza Magufuli awe rais wa kudumu/milele.

Mkamia: Nitawasilisha hoja bungeni ya kuondoa ukomo wa urais wa vipindi viwili.

Mabawa: Nitazunguka nchi nzima nikifanya kampeni kushawishi kuungwa mkono kwamba Rais Magufuli aendelee kuwepo kwa zaidi ya vipindi viwili.

Pote yalipoanza maasi ya aina hii dhidi ya Katiba, yalianza namna hii: Watu wachache. Nje ya Ikulu. Nje ya nyumba ya rais. Mbali na rais. Wakitamani. Wakinong’ona. Wakisema. Wakiimba. Wakifyatuka: Rais aendelee. Na rais alisikia. Alishawishika. Alikubali. Alijiandaa. Alibaki.

Huo ni ushawishi unaotaga mayai ya maafa! Mayai hayo yakiachwa hadi kuanguliwa, huleta vifaranga ambavyo hujenga woga miongoni mwa watawala ambao huanza kushuku kila mmoja kuwa siyo mwenzao, anawapinga; kuwa anawasema vibaya, kuwa anataka kuwang’oa, kuwa ana njama za “kuwamaliza!”

Kadri vifaranga vinavyokua, huchochea uadui usio wa kisiasa dhidi ya wapinzani wa kisiasa; huongeza woga miongoni mwa walio karibu na mtawala wanayetaka aishi madarakani; huanza kutafunana wenyewe kwa wenyewe kama senene – kila mmoja akimshuku mwenzake katika kupigania kupendwa na kuaminiwa; huwaingiza katika ndumba na ushirikina.

Rais Magufuli amenukuliwa wakati wa ziara ya mkoa wa Tanga wiki iliyopita akisema, katika hili atasimamia kulinda Katiba; atatumikia kwa kipindi chake na kipindi hicho kikiisha, atakabidhi “kijiti kwa mwingine.”

Kwa kauli hiyo, amevunja mayai ya husuda kabla hayajaanguliwa na kutawanya sumu ya kutawala milele au kwa muda zaidi ambayo tayari kwingine imeleta kutoaminiana, kusutana, kugombana, kupigana na kuuana.

Lakini nani anasema washawishi wamekoma baada ya kushushuliwa? Wanaweza kuendelea. Wanaweza kuongezeka. Wanaweza kukusanyana na kupeleka ujumbe badala ya kutoa kauli zilizotawanyika. Wanaweza!

Kisingizio chao kitakuwa kwamba wana uhuru wa kufikiri na kutoa maoni. Kweli wanao. Lakini waletacho ni maoni binafsi yenye sumu; yanayolenga kuangamiza misingi mikuu iliyowekwa na Katiba; lakini pia yanayolenga kuua utashi, uhuru na haki za wengi wengine kwa kutumia sheria au marekebisho ya Katiba.

Afrika ina somo moja kuu. Kule wenye fikra hizo walipojaribu na kufanikiwa; hata wanaotawala hawana raha. Hawana furaha ya kuwa madarakani. Hawana amani. Hata kinachoitwa ushindi wa mia kwa mia, hakileti tabasamu kwenye nyuso zilizokunjamana kwa woga; na nyoyo zilizofura kwa mihuri ya suto.


Je, Magufuli anahitaji kukumbushwa mara zote juu ya hili, ili ajenge uthabiti na asitetereke? Au, akumbushwe pia maeneo mengine mengi ambako Katiba imesema na kuzingatia lakini hajapatamka kwa uthabiti huohuo?

Wednesday, August 9, 2017

Barabara ya Dar es Salaam iliyoleta ugomvi



Jana tarehe 8/8/217 niliokoa vijana wawili wasitoane macho na kung’oana meno. Nilikuta wamekabana koo. Nikaamuru dereva wangu asimame.

Wakati ninatoka katika gari, wakawa ndio wanaangushana chini na kuanza kuviringishana kwenye vumbi huku wakipigana ngumi kichwani.

Ilichukua kama dakika tano hivi kuwaachanisha. Nikauliza kilichowasibu.

Mmoja akasema: “…huyu ni mpumbavu. Anasema kuwa barabara hii ilikuwa ya lami lakini sasa ni udongo mtupu. Mimi nikamwambia haiwezekani lami itoke kiasi cha kubaki vumbi namna hii; lakini yeye anabisha. Ndipo tukashikana…”

Mwingine akasema: “…hili jinga tu. Mimi nimekuwa nikipita barabara hii kwa miaka mitano sasa nikienda shule. Ilikuwa ya udongo; baadaye wakaweka lami. Sasa lami imekwisha yote katika kipindi cha miaka mitatu hivi na imerudia hali ileile ya vumbi.

“Huyu (aliyekuwa akipigana naye) hakuwepo hapa lakini anabisha na kuanza kunitukana na kusema kuwa lami haiwezi kuisha katika kipindi hicho. Ndio umekuta tumekamatana lakini ni kutokana na huyu kunitukana.”

“Barabara ya Ugomvi” ni ile inayochomoka kwenye Barabara ya Shekilango, Sinza Afrika Sana kupitia Kituo cha Polisi cha Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Ni kweli, barabara hii ilikuwa vumbi wakati wa jua na matope wakati wa mvua. Wakaweka kifusi (sijui nani!). Baadaye wakaweka lami (sijui nani) ikateleza na karibu dunia yote ikahamia huko. Leo ni vumbi tupu.


Je, unaweza kusaidia kuoroshesha visababishi vya ugomvi huu wa kung’oana meno na macho? Barabara yenyewe ni hii katika picha.

Saturday, July 29, 2017

Ndimara na CUF



Ijumaa, 28 Julai 2017
Kilichofanyika na kinachoendelea kufanyika CUF; na kwa CUF, ni kuasisi mfumo wa kuua uhuru na haki za watu; ni kujenga woga usiomithilika na ambao utafanya wengi waishi mithili ya msukule; ni kupanda mbegu za "uharamia wa kisiasa..."

Ijumaa, 28 Julai 2017

NANI awezaye kusema kwa uhakika au hata kutabiri, kwamba Prof. Lipumba hatapeleka kwa Spika, orodha nyingine ya wabunge wa chama chake - CUF ili watimuliwe bungeni? Nani awezaye kusema kwa uhakika kwamba, katika orodha hiyo, hakutakuwa na wabunge wa kuchaguliwa ambao watakuwa wanakabiliwa na tuhuma zilezile zilizowakumba wabunge wa viti maalum? Ikifika hapo, nani atazuia Tume ya Uchaguzi (NEC) - baada ya kuarifiwa na Spika kuwa wabunge wamefukuzwa na chama chao - kutangaza kuwa majimbo yako wazi, na hapo kuitisha uchaguzi mpya? Nani?

Kukurukakara za CUF


Chama cha Wananchi (CUF) kinapita katika tanuri la moto. Ulioanza kama mnyukano wa kawaida, sasa umekuwa janga linaloweza kutokomeza chama. Upande wa chama hicho unaoongozwa na Prof. Ibrahim Lipumba, umefukuza uanachama wabunge wanane (8). Tayari wamevuliwa pia ubunge. Upande mwingine chini ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad unapinga. Tayari umeitisha unachoita vikao halali vya chama. 

Ifuatayo ni taarifa ya “Baraza Kuu la Uongozi la Taifa” kama ilivyotolewa 28 Julai 2017 (inawekwa hapa kusaidia ufuatiliaji wa kinachoendelea na kujenga hazina ya uchunguzi na uchambuzi kwa siku zijazo).


THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF - CHAMA CHA WANANCHI)

 MAAZIMIO YA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA LA

UTANGULIZI:
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) leo hii Ijumaa, tarehe 28 Julai, 2017 limefanya kikao cha dharura kilichoitishwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa kwa kufuata masharti ya Katiba ya Chama ya mwaka 1992 (Toleo la 2014), kifungu cha 80 (1). Wajumbe 45 kati ya wajumbe 52 halali wa Baraza Kuu wamehudhuria ambao ni sawa na asilimia 86 ya wajumbe wote.

Katika kikao hiki, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa lilipokea, kujadili na kufanya maamuzi kuhusu ajenda moja tu iliyowasilishwa kwake na Kamati ya Utendaji ya Taifa ambayo ilikuwa ni:

Taarifa kuhusu kile kinachoitwa kuwavua uanachama Wabunge wanane (8) na Madiwani wawili (2) wa Viti Maalum kupitia CUF kilichotangazwa kufanywa na Ibrahim Lipumba na kikundi chake ikiwa ni mwendelezo wa hujuma za Dola dhidi ya Chama cha CUF.

Baada ya mjadala wa kina, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa linapenda kutoa maazimio yafuatayo kuhusiana na tukio hilo na mwendelezo wa vitendo na matukio mengi ya hujuma yanayofanywa na Dola dhidi ya CUF:-

1.   KUHUSU UHALALI WA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA:
Kutokana na mkanganyiko unaosababishwa na upotoshaji wa makusudi unaofanywa na Ibrahim Lipumba na kikundi chake wa kuitisha watu wa kuokota barabarani na kuwakusanya Buguruni huku akiwaita kuwa ndiyo Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF, tumeona kuna haja ya kuweka kumbukumbu sahihi ili kuepusha upotoshaji huo usiendelee.

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama huwa linaundwa kila baada ya miaka mitano kupitia Uchaguzi Mkuu wa Chama ndani ya Chama na hupata wajumbe wake kupitia uchaguzi unaofanywa na Mkutano Mkuu wa Taifa (wajumbe 25 kutoka Tanzania Bara na wajumbe 20 kutoka Zanzibar), wajumbe 14 wanaoteuliwa na Mwenyekiti kwa kushauriana na Makamu Mwenyekiti na kisha kuthibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, wajumbe wanaoingia kwa nafasi zao wakiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Chama, Wenyeviti na Makatibu wa Jumuiya za Chama na Viongozi wa Kambi za Wabunge na Wawakilishi wa Chama. Viongozi Wakuu wa kitaifa wa Chama pia ni wajumbe.

Wafuatao ndiyo Wajumbe halali waliochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa uliomalizika Juni 27, 2014 hapo Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuwa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) watakaokaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano (2014 – 2019) hadi watakapochaguliwa wengine na Mkutano Mkuu wa Taifa kwa mujibu wa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 (Toleo la 2014):-

VIONGOZI WAKUU:
1.    Mwenyekiti (alijiuzulu tarehe 5 Agosti, 2015 na kujiuzulu kwake kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa dharura tarehe 21 Agosti, 2016).
2.    Makamu Mwenyekiti (alitekeleza agizo la BKUT kuhama Chama kuwa mgombea mwenza wa Urais kupitia UKAWA).
3.    Katibu Mkuu – Maalim Seif Sharif Hamad (ambaye bado yupo).

KUTOKA KUNDI LA WAJUMBE 25 WA TANZANIA BARA AMBAO BADO WAPO:
1.    Mhe. Nuru Awadh Bafadhil
2.    Mhe. Moza Abeid
3.    Mhe. Athumani Henku
4.    Mhe. Fatuma Omar Kalembo
5.    Mhe. Sophia M. Khaify
6.    Mhe. Katani A. Katani
7.    Mhe. Salum Kh. Barwani
8.    Mhe. Bonifasia Mapunda
9.    Mhe. Fatuma A. Chitepete
10. Mhe. Juma S. Nkumbi
11. Mhe. Nassir A. China
12. Mhe. Kulthum Mchuchuli
13. Mhe. Karume J. Mgunda
14. Mhe. Twaha I. Taslima
15. Mhe. Julius N. Samamba
KUTOKA KUNDI HILI WALIOFARIKI:
16. Mhe. Ashura Mustapha
KUTOKA KUNDI HILI WALIOHAMA CHAMA:
17. Mhe. Lwebora P. Ndarpoi
18. Mhe. Mohamed A. Khalifa
19. Mhe. Mkiwa A. Kimwanga
 KUTOKA KUNDI HILI WALIOFUKUZWA UANACHAMA:
20. Mhe. Chief L. Yemba
KUTOKA KUNDI HILI WALIOSIMAMISHWA UANACHAMA:
21. Mhe. Magdalena H. Sakaya
22. Mhe. Kapasha H. Kapasha
23. Mhe. Thomas D.C. Malima
24. Mhe. Abdul J. Kambaya
25. Mhe. Omar M. Masoud
KUTOKA KUNDI LA WAJUMBE 20 WA ZANZIBAR AMBAO BADO WAPO:
1.    Mhe. Hamad Masoud Hamad
2.    Mhe. Abubakar Khamis Bakari
3.    Mhe. Said Ali Mbarouk
4.    Mhe. Khalifa Mohamed Issa
5.    Mhe. Omar Ali Shehe
6.    Mhe. Riziki Omar Juma
7.    Mhe. Masoud Abdalla Salim
8.    Mhe. Hija Hassan Hija
9.    Mhe. Najma Khalfan Juma
10. Mhe. Salim Bimani
11. Mhe. Nassor Ahmed Mazrui
12.  Zahra Ali Hamad
13. Fatma Abdulhabib Ferej
14. Mhe. Shaaban Iddi Ame
15. Mhe. Pavu Juma Abdallah
16. Mhe. Abdilahi Jihad Hassan
17. Mhe. Hassan Jani Masoud
18. Mhe. Mohamed Kombo Ali
19. Mhe. Hemed Said Nassor
KUTOKA KUNDI HILI ALIYEFUKUZWA UANACHAMA NA TAWI LAKE NA KUTHIBITISHWA NA BKUT:
20. Mhe. Rukia Kassim Ahmed
WAJUMBE WALIOTEULIWA NA MWENYEKITI KWA KUSHAURIANA NA MAKAMU MWENYEKITI NA KISHA KUTHIBITISHWA NA BKUT:
 1.    Mhe. Zainab A. Msafiri
2.    Mhe. Hashim B. Mzirai
3.    Mhe. Shaweji M. Mketo
4.    Mhe. Abdalla Mtolea
5.    Mhe. Joran Bashange
6.    Mhe. Elina Kimei
7.    Mhe. Mustapha Wandwi
8.    Mhe. Ahmed Marshed Khamis
9.    Mhe. Ismail Jussa Ladhu
10. Mhe. Nunuu S. Rashid
11. Mhe. Shambuli A. Makame
12. Mhe. Abdalla Bakari Hassan
13. Mhe. Yussuf Salim Hussein
KUTOKA KUNDI HILI WALIOSIMAMISHWA UANACHAMA:
14. Mhe. Shaaban Kaswaka
VIONGOZI WAKUU WA JUMUIYA ZA CHAMA:
1.    Mhe. Hamidu Bobali – Mwenyekiti Jumuiya ya Vijana
2.    Mhe. Mahmoud A. Mahinda – Katibu Mtendaji Jumuiya ya Vijana
N.B.
-          Viongozi wa Jumuiya ya Wanawake ambao ni Mhe. Fatma Abdulhabib Ferej (Mwenyekiti) na Mhe. Fatma Omar Kalembo (Katibu) walikuwa wameshaingia kwa nafasi za wajumbe wa kuchaguliwa.
-          Jumuiya ya Wazee bado haijafanya uchaguzi na viongozi wake wa Sekretarieti ya Wazee hualikwa tu kuhudhuria vikao vya BKUT.
KIONGOZI WA WABUNGE WA CUF BUNGENI:
 1.    Mhe. Riziki Shahari Mngwali
MWENYEKITI WA BODI YA WADHAMINI YA CHAMA:
1.    Mhe. Abdalla S. Khatau
JUMLA YA WAJUMBE HALALI WALIOPO SASA:
Kutokana na mchanganuo huu, idadi ya sasa ya Wajumbe halali tuliopo tunaounda Baraza Kuu la Uongozi halali la Chama ni 52 ambapo wajumbe 25 wanatoka Tanzania Bara na wajumbe 27 wanatoka Zanzibar.

Mkutano Mkuu wa Taifa haujalivunja wala haujachagua Baraza Kuu jengine. Kama lipo jengine la pili hilo litakuwa ni Baraza Kuu feki, na chombo chochote kitakachoundwa na Baraza Kuu lisilokuwa hili lililotokana na Mkutano Mkuu wa Taifa katika kipindi hiki cha miaka mitano (2014 – 2019), chombo hicho nacho kitakuwa ni feki kama ilivyo kwa Kamati feki inayojiita ya Nidhamu na Maadili.
       
Kwa msingi huo huo, maamuzi halali ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ni yale yanayofanywa na Baraza Kuu linaloundwa na wajumbe walioorodheshwa hapo juu. Wajumbe wengine feki watakaojiita Baraza Kuu wakifanya maamuzi kuhusu jambo lolote lile, maamuzi yao hayo yatakuwa feki pia.

2.   KUHUSU KINACHOITWA KUFUKUZWA UANACHAMA WABUNGE WANANE (8) NA MADIWANI (2) WA CUF:

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa halijakutana popote siku ya Jumapili, tarehe 23 Julai, 2017 kufanya maamuzi yoyote ya kuwafukuza uanachama Wabunge wanane (8) na Madiwani wawili (2) wa CUF kama ilivyodaiwa na mtu anayeitwa Ibrahim Lipumba na kikundi chake. Kwa msingi huo, Baraza Kuu linawataka Watanzania kufahamu kwamba:-

(a)  Linaendelea kuwatambua Wabunge na Madiwani hao kuwa wanachama halali wa CUF tena ni wanachama wa kupigiwa mfano wenye nidhamu na maadili ya hali ya juu. Baraza Kuu linawapongeza kwa mapenzi yao kwa Chama chao na msimamo wao thabiti usioyumba katika kukitetea Chama waliouonesha pale walipokataa kuitikia wito wa Kamati feki ya Maadili na Nidhamu.

(b) Pamoja na matangazo ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza kwamba Wabunge hao wanane wamepoteza sifa za Ubunge kwa hicho kinachoitwa “kufukuzwa uanachama” na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza majina ya wateule wengine wa kujaza nafasi hizo, Baraza Kuu ambalo ndilo lililowateua hapo awali bado linaendelea kuwatambua wafuatao kuwa Wabunge wake halali:
1.    Mhe. Severina Silvanus Mwijage, (MB);
2.    Mhe. Saumu Heri Sakala, (MB);
3.    Mhe. Salma Mohamed Mwassa, (MB);
4.    Mhe. Riziki Shahari Mngwali, (MB);
5.    Mhe. Raisa Abdallah Mussa, (MB);
6.    Mhe. Miza Bakari Haji, (MB);
7.    Mhe. Khadija Salum Ally Al-Qassmy, (MB); na
8.    Mhe. Halima Ali Mohamed, (MB).

(c)  Baraza Kuu pia linaendelea kuwatambua Madiwani wa Viti Maalum, Mhe. Leila Hussein Madibi (Ubungo) na Mhe. Elisabeth Magwaja (Temeke) kuwa madiwani halali wa CUF katika Wilaya zao.

(d) Baraza Kuu limeridhika kwamba hicho kinachoitwa “kuwafukuza uanachama” na kuwatangaza kuwa wamepoteza sifa za Ubunge na papo hapo kutangaza majina mengine eti kujaza nafasi zao, ni mpango kabambe uliosukwa na Dola kwa kushirikiana na kibaraka Ibrahim Lipumba na kikundi chake na ndiyo maana Watanzania wameshuhudia KASI YA AJABU (supersonic speed) katika utekelezaji wake, kasi ambayo haijawahi kushuhudiwa katika utekelezaji wa maamuzi kama hayo huko nyuma. Bunge hili hili liliendelea kuwatambua Wabunge kadhaa katika vipindi tofauti miaka iliopita ambao walishafukuzwa uanachama tena na vikao halali vya vyama husika.

(e)  Baraza Kuu limeshangazwa na hatua ya Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai kujifedhehesha na kujiaibisha kwa kusema uongo kwa Watanzania kwamba eti alijiridhisha kuwa Wabunge wanane wa Chama Cha Wananchi (CUF) ‘wamefukuzwa Uanachama kulingana na taratibu za Chama hicho na hivyo wamekosa sifa za kuendelea na Ubunge”.

(f)   Baraza Kuu limejiridhisha kwamba Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye kwa mujibu wa Katiba ya CUF ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Chama na pia kwa nafasi hiyo ndiye Katibu wa vikao vya Mkutano Mkuu wa Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama alimuandikia Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai barua rasmi, Jumanne, tarehe 25 Julai, 2017 akimueleza kwamba hilo lililoitwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF halikuundwa na wajumbe halali wa Baraza Kuu. Hiyo ni mbali na ukweli kwamba hakuna Mtanzania asiyejua kuwa uhalali wa kibaraka Lipumba na genge lake unapingwa na Chama cha CUF kwa kesi ambazo ziko Mahakamani. Kwa hakika Spika Ndugai amepoteza sifa na haiba ya kuongozo Bunge ambalo ni mhimili mmojawapo wa Dola na ambao ulipaswa kuwa alama ya uadilifu katika nchi na anapaswa kujiuzulu kwa kuidhalilisha na kuichafua heshima na haiba ya nafasi ya Spika.

(g) Baraza Kuu linapongeza na kuunga mkono hatua waliyoichukua Wabunge hao ya kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga uhalali wa hatua iliyotangazwa ya kwamba ati wamefukuzwa uanachama na ambapo katika kesi hiyo wanaiomba Mahakama Kuu itamke kwamba wao bado ni wanachama halali wa CUF na hivyo bado ni Wabunge halali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CUF katika nafasi za Viti Maalum na kutupilia mbali tangazo la Spika la kuwatangaza kuwa si Wabunge na lile la Tume ya Taifa ya Uchaguzi la kutangaza majina mengine ya kujaza nafasi hizo.

(h) Baraza Kuu linamuagiza Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, kuwaandikia Rais wa Bunge la Afrika (PAP), na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kuhusu fedheha na aibu hii iliyofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuonesha jinsi demokrasia isivyoheshimiwa Tanzania.

(i)   Baraza Kuu linawataka Watanzania hususan wanawake kuona ni jinsi gani CCM kupitia taasisi za kidola isivyowajali, isivyowaheshimu na isivyowathamini wanawake ambao ni zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote kwa kuwatendea kitendo cha kuwadhalilisha kwa kuwaondoshea uwakilishi wao halali kupitia Wabunge wazoefu waliokuwa watetezi madhubuti wa haki za wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

(j)   Baraza Kuu linawataka Wabunge na Madiwani wote wa CUF nchi nzima kukipuuza kikundi cha wahuni kinachojiita “Baraza Kuu” na kwamba Baraza Kuu halali la Chama linaendelea kuwatambua wote kama Wabunge na Madiwani halali wa CUF.

3.   KUHUSU KUJIDHALILISHA KWA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI NA KUKIUKA KANUNI ZAO WENYEWE KATIKA UTEUZI WA WABUNGE WA VITI MAALUM:

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limesikitishwa na hatua ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujidhalilisha na kujishushia hadhi kwa kushiriki katika hujuma hizi za Dola dhidi ya CUF. Mbali na yale yaliyoyaelezwa hapo juu, hata kama ingekuwa kufukuzwa Wabunge hao wa CUF kulikuwa na halali na kumefanywa na chombo halali cha Chama, basi Kanuni walizojiwekea wenyewe Tume katika uteuzi wa watu wa kujaza nafasi hizo huo unafuata mpangilio wa majina kama ulivyokuwa umewasilishwa na Chama husika wakati wa uteuzi wa wagombea wa ubunge wa viti maalum wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. CUF ilipeleka orodha yake ambayo haihusishi majina yaliyotangazwa. Hivyo ndiyo kusema hata kama hicho kinachoitwa kufukuzwa uanachama Wabunge hao kingekuwa halali (jambo ambalo si halali kama ilivyokwisha elezwa hapo juu), basi kwa Kanuni za Tume yenyewe, watu wa kujaza nafasi hizo wasingekuwa hao waliotangazwa. Kwa maelezo haya, Baraza Kuu linaweka bayana yafuatayo:-

(a)  Kitendo kilichofanywa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kimezidi kuidhalilisha na kuishushia hadhi Tume hiyo na kwamba kwa kushiriki kwake katika hujuma hizi chafu ni ushahidi mwengine kwamba Tanzania hatuna Tume huru ya Uchaguzi; bali Tume iliopo inafuata maelekezo ya Dola tu kuhujumu vyama vya upinzani.

(b) Baraza Kuu linaitaka (linai-challenge) Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoa hadharani barua ya Katibu Mkuu wa CUF iliyoandikwa kwao mwaka 2015 ikiwa na majina ya wanachama wake walioteuliwa kuwa wagombea wa viti maalum vya wanawake na kuonesha iwapo hao iliowatangaza walikuwa katika mpangilio wa majina yaliyoteuliwa na Chama. Iwapo haitofanya hivyo, iwaeleze Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwa nini waendelee kuiamini Tume hiyo.

(c)  Baraza Kuu linatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na hususan Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Shirika lake la Mpango wa Maendeleo (UNDP) ambalo limekuwa likifanya kazi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutafakari upya iwapo Tume hiyo bado ina hadhi na heshima ya kuendelea kuungwa mkono na Shirika hilo, Umoja wa Mataifa, na washirika wa maendeleo kwa ujumla wakati imejianika waziwazi kuwa inafanya kazi ya kuhujumu demokrasia Tanzania badala ya kuimarisha.

4.   KUHUSU HUJUMA ZA DOLA DHIDI YA CUF, VYAMA VYENGINE VYA SIASA NA TAASISI NYENGINE ZA KIDEMOKRASIA NA HAKI ZA BINADAMU HAPA NCHINI:
Baada ya kujadili kwa kina mwendelezo wa mipango ya hujuma dhidi ya CUF iliyoanza mwaka jana na ambayo inaendelezwa kwa nguvu na kwa kasi, na kwa kutafakari matukio mengine ya hujuma dhidi ya vyama vyengine vya siasa na taasisi nyengine zinazosimamia demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria hapa nchini, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeazimia yafuatayo:

(a)  Limeridhika kwamba Wakuu wa Dola nchini Tanzania wana mpango mkubwa wa kuua demokrasia hapa nchini kwa kuviangamiza vyama makini vya siasa vilivyoonekana tishio kwa chama kinachotawala cha CCM katika uchaguzi mkuu uliopita na pia kupambana na taasisi zinazoheshimika na zinazojiamini katika kusimamia masuala ya demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria.

(b) Baraza Kuu liamini kuwepo mpango huo baada ya sasa kuonekana wazi kwamba mipango ya hujuma dhidi ya CUF hadi sasa imeshahusisha Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Polisi, baadhi ya Wakuu wa Wilaya, Ofisi ya Spika wa Bunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na bila shaka yoyote Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Vipi Idara ya Usalama wa Taifa iwe haioni hujuma hizi za wazi na athari zake kwa usalama wa Taifa?

(c)  Baraza Kuu linaona kuwa hujuma dhidi ya CUF zinatokana na ushindi mkubwa wa chama hiki katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015 ambapo kilimbwaga mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM kwa tofauti ya kura 25,836 pale mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alipopata jumla ya kura 207,847 dhidi ya mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, aliyeambulia kura 182,011. CUF pia ilifanikiwa kuongeza majimbo yake kisiwani Unguja kutoka manne (4) hadi tisa (9) mbali ya kuendelea kubakisha majimbo yake yote 18 kisiwani Pemba. Mafanikio haya na ushindi huu mkubwa umekuwa mwiba kwa watawala na ndiyo hujuma zote hizi zinatelekezwa ili kuisambaratisha CUF, jambo ambalo Baraza Kuu linawahakikishia Watanzania kuwa halitofanikiwa.

(d) Kwa upande mwengine, mafanikio ya UKAWA katika Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na uthubutu uliooneshwa na Watanzania wanaotaka mabadiliko ndiyo yanayopelekea pia kuandamwa kwa:

-          CHADEMA;
-          NCCR;
-          Wabunge wa Upinzani wanaoongoza katika ukosoaji wa Watawala;
-          Wanaharakati wanaotetea uhuru wa kujieleza kama Jamii Forums;
-          Wasanii ambao wametumia vipaji vyao kuwakosoa Watawala;
-          Watumiaji wa mitandao ya kijamii hasa vijana;
-          Vyombo vya habari yakiwemo magazeti, vituo vya radio na TV;
-          Taasisi za fani na stadi zinazohoji kama ilivyotokea kwa TLS; na
-          Wana-CCM wenye mawazo yanayokinzana na yale ya Watawala.

(e)  Baraza Kuu linasikitishwa na mtindo unaoonekana kutaka kujengwa wa kutojali Katiba na Sheria katika kuongoza na kuendesha nchi na badala yake kutegemea matamko ya Rais. Mengi ya matamko hayo na matendo yanayofuatana nayo hayaendani na Katiba na Sheria za nchi ambazo aliapa kuzilinda wakati anashika madaraka ya nchi.

(f)   Baraza Kuu linaona mwenendo huu unaoelekea kukandamiza demokrasia na hatimaye kuiua kabisa hauleti taswira njema kwa mustakbali wa Taifa letu. Taifa ambalo halitoi nafasi kwa watu wake kutoa mawazo yao hadharani huwa linakaribisha manung’uniko ya chini kwa chini ambayo ni hatari kwani yanapelekea watawala kutojua hisia halisi za wananchi. Baraza Kuu linaitaka Serikali na vyombo na taasisi zake kujitathmini upya juu ya wapi wanalipeleka Taifa.

Mwisho