Saturday, August 12, 2017

DC amchapa viboko baba kisa gari kupigwa mawe

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga


Na Renatha Msungu, 
Nipashe, Jumamosi, 12 Agosti 2017


MKUU wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amemcharaza viboko mzazi wa mmoja wa watoto walioshambulia gari lake kwa mawe na kuvunja kioo cha nyuma jana.

Gari hilo lenye namba za usajili STL 669, lilishambuliwa na watoto watatu katika barabara kuu ya Kondoa-Dodoma, kwenye kijiji cha Paranga wilayani Chemba.

Kufuatia kupasuliwa kwa kioo hicho, DC alisimamisha gari hilo na kuwakimbiza watoto waliolipiga mawe, hali iliyozua purupushani kwa muda.

DC huyo aliwakimbiza watoto hao kwa lengo la kuwakamata na kuwaadhibu lakini hakuweza kuwakamata baada ya kumzidi mbio.

Hata hivyo, wananchi walioshuhudia tukio hilo walimtajia DC majina na sehemu wanakoishi watoto hao ili awafuate majumbani kwao.

Ndipo mmoja wa wazazi wa watoto waliohusika na shambulio hilo alikutwa nyumbani akiendelea na shughuli zake na alipohojiwa na DC kuhusu malezi ya mtoto wake, aliingia katika majibizano yaliyomkera DC Odunga.

"Malezi? Malezi gani unataka kwangu? Mtoto ametoka shule, mimi nitajuaje anayoyafanya mtaani?" Aliuliza mzazi huyo wa kiume na kufafanua kuwa "mimi najua (mtoto) yuko shule, sijui kama amevunja kioo chako."

Ndipo DC alipoonekana kukerwa na majibu hayo hivyo kuchukua fimbo na kuanza kumcharaza mzazi huyo huku akimshutumu kwa malezi mabaya.

DC alimcharaza viboko mzazi huyo wa kiume kabla ya kumuingiza kwenye gari la polisi akiwa amefungwa pingu, kwa madai ya kuendelea kujibu kwa jeuri wakati akiulizwa maswali kuhusu  malezi ya mtoto wake.

Mzazi huyo aliendelea kujibu kuwa hastahili kupigwa kwa kuwa kosa si lake na kusema kuwa apelekwe popote pale, lakini haki yake itajulikana kwa sababu wakati watoto hao wanapiga mawe kioo cha gari yeye hakuwepo.

Watoto watatu hao waliofanya tukio hilo wanakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka saba hadi 10.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia Odunga na mzazi huyo wakivutana huku mzazi akisikika akisema "aliyevunja kioo ni mtoto... chukueni tu hatua vyovyote haki yangu nitaipata".

Mwenyekiti wa kitongoji anakoishi mzazi huyo aliingilia kati na kudai kuwa matukio hayo ya kurushia mawe magari katika eneo hilo yapo na walishayakemea katika mkutano wa kitongoji yakapungua.

Alisema wahusika huwa ni watoto na vijana wa eneo hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Odunga alisema kijiji hicho kimekuwa na tabia ya kuweka mawe barabarani pamoja na kupiga magari mawe jambo ambalo siyo sahihi.

Alisema wanajipanga kwa ajili ya kuanza operesheni ya kuhakikisha tabia hiyo inakomeshwa kabisa "kwa sababu ni hatari kwa wasafiri na jamii kwa ujumla".

Alisema wataendelea na msako wa polisi ili kubaini familia ambazo zina vijana wenye tabia hiyo kupitia jamii inayowazunguka.

Kufuatia purukushani hiyo gari la polisi wilaya lilitinga katika eneo hilo na kuwachukua watu sita wakiwahusisha na upigaji mawe magari, akiwemo mtoto mmoja aliyetajwa kuhusika jana.

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo huku akisema ameagiza watu hao waliokamatwa watolewe rumande.

Alisema Jeshi la Polisi litaendelea na upelelezi kwa ajili ya kukusanya ushahidi wa tukio hilo na baadaye hatua zaidi zitachukuliwa kwa wahusika

Kamanda Mambosasa alisema amechukizwa na kitendo cha Mkuu huyo wa Wilaya kujichukulia sheria mkononi na kumjeruhi mzazi huyo.

"Amemjeruhi maeneo ya kichwani kwa rungu na mkono wake umevimba kutokana na kipigo alichokipata." alisema Kamanda Mambosasa. "Hii si haki kiongozi kujichukulia sheria mkononi…"


Friday, August 11, 2017

Magufuli avunja Mayai ya Maafa


Siyo kila chenye watatu au vitatu ni cha “Utatu.” Ndiyo maana kuna “matatu” ambayo hayana uhusiano na waumini katika Utatu wa Maandiko.

Jina la Matatu la Kenya linatokana na magari madogo ya abiria yaliyokuwa yakitoza “mapeni matatu” – senti 10 tatu – zilizokuwa nauli katika miaka ya 1950 katika miji mingi ya nchi hiyo.

Matatu au utatu wa sasa umetoswa kabla haujachipuka. Ni Rais John Pombe Magufuli aliyetosa utatu wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Mbunge Juma Mkamia na muumini wa CCM, Lawrence Mabawa.

Mwinyi: Kama siyo kwa Katiba ya nchi, ningependekeza Magufuli awe rais wa kudumu/milele.

Mkamia: Nitawasilisha hoja bungeni ya kuondoa ukomo wa urais wa vipindi viwili.

Mabawa: Nitazunguka nchi nzima nikifanya kampeni kushawishi kuungwa mkono kwamba Rais Magufuli aendelee kuwepo kwa zaidi ya vipindi viwili.

Pote yalipoanza maasi ya aina hii dhidi ya Katiba, yalianza namna hii: Watu wachache. Nje ya Ikulu. Nje ya nyumba ya rais. Mbali na rais. Wakitamani. Wakinong’ona. Wakisema. Wakiimba. Wakifyatuka: Rais aendelee. Na rais alisikia. Alishawishika. Alikubali. Alijiandaa. Alibaki.

Huo ni ushawishi unaotaga mayai ya maafa! Mayai hayo yakiachwa hadi kuanguliwa, huleta vifaranga ambavyo hujenga woga miongoni mwa watawala ambao huanza kushuku kila mmoja kuwa siyo mwenzao, anawapinga; kuwa anawasema vibaya, kuwa anataka kuwang’oa, kuwa ana njama za “kuwamaliza!”

Kadri vifaranga vinavyokua, huchochea uadui usio wa kisiasa dhidi ya wapinzani wa kisiasa; huongeza woga miongoni mwa walio karibu na mtawala wanayetaka aishi madarakani; huanza kutafunana wenyewe kwa wenyewe kama senene – kila mmoja akimshuku mwenzake katika kupigania kupendwa na kuaminiwa; huwaingiza katika ndumba na ushirikina.

Rais Magufuli amenukuliwa wakati wa ziara ya mkoa wa Tanga wiki iliyopita akisema, katika hili atasimamia kulinda Katiba; atatumikia kwa kipindi chake na kipindi hicho kikiisha, atakabidhi “kijiti kwa mwingine.”

Kwa kauli hiyo, amevunja mayai ya husuda kabla hayajaanguliwa na kutawanya sumu ya kutawala milele au kwa muda zaidi ambayo tayari kwingine imeleta kutoaminiana, kusutana, kugombana, kupigana na kuuana.

Lakini nani anasema washawishi wamekoma baada ya kushushuliwa? Wanaweza kuendelea. Wanaweza kuongezeka. Wanaweza kukusanyana na kupeleka ujumbe badala ya kutoa kauli zilizotawanyika. Wanaweza!

Kisingizio chao kitakuwa kwamba wana uhuru wa kufikiri na kutoa maoni. Kweli wanao. Lakini waletacho ni maoni binafsi yenye sumu; yanayolenga kuangamiza misingi mikuu iliyowekwa na Katiba; lakini pia yanayolenga kuua utashi, uhuru na haki za wengi wengine kwa kutumia sheria au marekebisho ya Katiba.

Afrika ina somo moja kuu. Kule wenye fikra hizo walipojaribu na kufanikiwa; hata wanaotawala hawana raha. Hawana furaha ya kuwa madarakani. Hawana amani. Hata kinachoitwa ushindi wa mia kwa mia, hakileti tabasamu kwenye nyuso zilizokunjamana kwa woga; na nyoyo zilizofura kwa mihuri ya suto.


Je, Magufuli anahitaji kukumbushwa mara zote juu ya hili, ili ajenge uthabiti na asitetereke? Au, akumbushwe pia maeneo mengine mengi ambako Katiba imesema na kuzingatia lakini hajapatamka kwa uthabiti huohuo?

Wednesday, August 9, 2017

Barabara ya Dar es Salaam iliyoleta ugomvi



Jana tarehe 8/8/217 niliokoa vijana wawili wasitoane macho na kung’oana meno. Nilikuta wamekabana koo. Nikaamuru dereva wangu asimame.

Wakati ninatoka katika gari, wakawa ndio wanaangushana chini na kuanza kuviringishana kwenye vumbi huku wakipigana ngumi kichwani.

Ilichukua kama dakika tano hivi kuwaachanisha. Nikauliza kilichowasibu.

Mmoja akasema: “…huyu ni mpumbavu. Anasema kuwa barabara hii ilikuwa ya lami lakini sasa ni udongo mtupu. Mimi nikamwambia haiwezekani lami itoke kiasi cha kubaki vumbi namna hii; lakini yeye anabisha. Ndipo tukashikana…”

Mwingine akasema: “…hili jinga tu. Mimi nimekuwa nikipita barabara hii kwa miaka mitano sasa nikienda shule. Ilikuwa ya udongo; baadaye wakaweka lami. Sasa lami imekwisha yote katika kipindi cha miaka mitatu hivi na imerudia hali ileile ya vumbi.

“Huyu (aliyekuwa akipigana naye) hakuwepo hapa lakini anabisha na kuanza kunitukana na kusema kuwa lami haiwezi kuisha katika kipindi hicho. Ndio umekuta tumekamatana lakini ni kutokana na huyu kunitukana.”

“Barabara ya Ugomvi” ni ile inayochomoka kwenye Barabara ya Shekilango, Sinza Afrika Sana kupitia Kituo cha Polisi cha Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Ni kweli, barabara hii ilikuwa vumbi wakati wa jua na matope wakati wa mvua. Wakaweka kifusi (sijui nani!). Baadaye wakaweka lami (sijui nani) ikateleza na karibu dunia yote ikahamia huko. Leo ni vumbi tupu.


Je, unaweza kusaidia kuoroshesha visababishi vya ugomvi huu wa kung’oana meno na macho? Barabara yenyewe ni hii katika picha.