Header Ads

LightBlog

Tunalala na maiti ya Muungano bila kujua?

Na Ndimara Tegambwage

WAJUMBE wa Bunge Maalum la Katiba, juzi Jumamosi jijini Dodoma, walishuhudia Chama Cha Mapinduzi kikishinikiza matakwa yake katika utungaji wa Katiba Mpya.

Walimwona Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa CCM, kwanza akiuma na kupuliza na baadaye akimwaga nyongo na hapa na pale, akitetea na kushinikiza matakwa ya chama chake.

Hakika Rais Kikwete hakwenda Dodoma kufanya ufunguzi wa shughuli za kujadili Rasimu ya Katiba Mpya; bali alikwenda kuweka vijembe, vitisho na msimamo wa chama chake juu ya mambo kadhaa; lakini zaidi juu ya mfumo wa Muungano wa serikali tatu.

Kinachosumbua wengi ni kwamba rais kwanza, ameonyesha kutoona mambo muhimu; na pili, ameonyesha kuwa mwoga.

Rais amekataa kuona kuwa leo hii hakuna Tanzania moja kama ilivyokuwa tangu mwaka 1964. Bali wajumbe wengi na baadhi ya wananchi mitaani wanajiuliza iwapo kweli rais haoni au anafanya ajizi.

Makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 yanaelekeza kuwepo nchi moja inayoitwa Tanzania; na kuwepo serikali mbili – moja ya Zanzibar na nyingine ya Muungano ambayo itakuwa na serikali ya Tanganyika ndani yake.

Utani ambao umekuwa ukisambazwa kimyakimya na kwa miaka mingi shuleni na vyuoni ni kwamba Muungano ulizaliwa “ukiwa na ujauzito.”

Kwahiyo kumekuwa na wanaosema kuna siku Tanganyika itazaliwa na kuwa na serikali yake kama ambavyo Zanzibar ina serikali yake.

Tanganyika haijazaliwa. Lakini Zanzibar ambayo ina serikali yake, imejinyofoa kikatiba kutoka kuwa sehemu ya nchi moja ya Tanzania na kujitam bua, kujitambulisha na kujitangazia mipaka yake na hata kukwangua na kuchukua mamlaka ya Muungano.

Hapa ndipo maelezo ya Tume ya Warioba yanasema, “Katiba imevunjwa.” Imevunjwa mbele ya Rais Jakaya Kikwete. Mbele ya macho yake. Mbele ya kimya chake kana kwamba alikubaliana nao.

Rais Kikwete ama anaogopa kutoa amri kwa Zanzibar kufuta katiba yao; au anaona aibu kushuritisha mabadiliko kwa kuwa yalifanywa – tena kupitia chama chake – na kupitishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walio wanachama wa chama chake; au anaona kama nionavyo, kwamba amri yake haitasikilizwa; haitatekelezwa.

Kwa rais kutoa amri au hata pendekezo analojua kuwa haliwezi kutekelezwa, ni kama jaji kutoa amri ambayo anajua haitekelezeki. Ni kudhoofisha mamlaka, lakini pia ni kukiri kushindwa ambayo ni njia ya kuandika barua ya kuomba kufukuzwa kazi.

Aidha, hatua yoyote ya kulazimisha Zanzibar kubadili walichokwisha kufanya, italeta mgogoro wa kikatiba na kukuza mgogoro wa kisiasa. Nani ana ubavu wa kuhimili migogoro hii? Bali hapa kuna pendekezo:

• kwa kuwa Zanzibar imekwishafanya “utukutu” na siyo rahisi kuikemea;
• na kwa kuwa tayari Zanzibar imekwishapora hata mamlaka ya serikali ya Muungano;
• na kwa kuwa mambo yote yamefanywa mbele ya viongozi wote wa Zanzibar na Muungano bila yeyote kuonyesha kustuka;
• na kwa kuwa hadi sasa hakuna hata onyo au karipio;
• na kwa kuzingatia kuwa mfumo wa Muungano sasa umebadilika kutoka nchi moja na kuwa nchi mbili na serikali mbili;
• na kwa kuwa kumekuwa na madai ya kutaka kutoa serikali ya Tanganyika kwenye “koti” la Muungano;
• na kwa kuwa kuna hoja Zanzibar kuwa nchi hiyo iliungana na Tanganyika na siyo Muungano hivyo kuwepo Tanganyika ndiko kunaipa Zanzibar uhalali;
• na kwa kuelewa kuwa mfumo wa serikali mbili umeshindikana kwa “migogoro isiyoisha;”
• na kwa kuwa imethibitika kuwa watawala wamekuwa wakipanga mambo mengi bila utekelezaji na hivyo kuua Muungano kimyakimya;
• na kwa kuona kuwa watawala wamekuwa wakitoa ahadi za kuondoa kero za Muungano katika miaka 30 bila kuzitekeleza;
• na kwa kuwa imedhihirika kuwa watawala hawako makini na wanachosema na Muungano wenyewe;

Basi, badala ya kuwa na serikali mbili ndani ya nchi mbili, kuwe na serikali nyingine ya tatu itakayokuwa kiungo kikuu cha nchi mbili na serikali mbili za watu walioamua kuwa na Muungano.

Tatizo hapa ni kwamba badala ya kujadili mazingira ya serikali tatu na mustakbali wa Muungano, Rais Kikwete alijikita katika kejeli, kebehi, laana na vitisho. Yote haya yalilenga kusisitiza kile ambacho wamekuwa wakitangaza, “msimamo wa CCM wa serikali mbili.”

Ilifikia mahali rais akafyatua kombora kuwa serikali tatu zitakuwa aghali na kwamba kuna uwezekano wa kukosa hata fedha za kulipa mishahara ya askari. Akatishia kuwa askari wanaweza kuasi na hatimaye wakavua gwanda na kuvaa kiraia na “kuja kugombea.”

Katika mazingira ya Tanzania, mara ngapi askari wamekwenda miezi mingi bila malipo na hakukuwepo dalili wala harufu ya vurugu? Hivi ni vitisho ambavyo havistahili kutoka kwa mkuu wa nchi.

Wananchi wengine ni wazazi, ndugu, watoto na marafiki wa vijana walioko katika majeshi. Wanajua lini wamelipwa na lini hawajalipwa; wanajua nani wanaomba misaada kutoka kwao pale wanapokuwa hawajalipwa. Kampeni hii ya vitisho haiingii akilini.

Bali kuna hoja dhaifu kuwa Muungano utakufa iwapo kutakuwa na serikali tatu. Nionavyo, afadhali ijulikane kuwa Muungano umekufa kuliko kukaa na maiti ya Muungano kwa miaka yote bila wananchi kufahamu; na mpaka Warioba achunguze.

0713 614872
Mwisho
(Imechapishwa katika gazeti la TanzaniaDaima Jumapili, 23 Machi 2014, uk.7) na www.ndimara.tegambwage.facebook.com

No comments

Powered by Blogger.