Atolewa kwenye ndege, akamatwa na polisi Mwanza
Niliongea na Dk. Azaveli Lwaitama akiwa Mwanza baada ya kuandika maelezo
yake kwenye kituo cha polisi cha uwanja wa ndege Mwanza na kuachiwa kwa
kilichoitwa "dhamana ya polisi." Anatakiwa kuripoti polisi uwanjani
hapo kesho asubuhi kuona iwapo polisi wameamua kumfikisha mahakamani.
Nasimulia alivyonisimulia.
Dk. Lwaitama alitoka Dar es Salaam leo asubuhi. Akatua Mwanza. Alikuwa
anakwenda Bukoba. Alipanda ndege ya kampuni ileile iliyomtoa Dar es
Salaam leo hii - PrecisionAir. Hii ya kwenda Bukoba ilikuwa Na. PW 0492.
Alikwenda hadi kwenye kiti chake Na. 2B. Hapa ndipo kuna milango ya
dharura kwa pande zote mbili za ndege - kulia na kushoto.
Ndipo akaja mfanyakazi wa ndege. Akamuuliza iwapo anajua Kiingereza.
Baada ya mzaha wa kawaida katika kuuliza iwapo ni lazima kujua
Kiingereza, ndipo mfanyakazi akamwambia kuwa kama hajui lugha hiyo basi
ahame kiti na kukaa kwingine kwani kuna maelezo rasmi ambayo yanatolewa
kwa "lugha ya anga" - Aviation Language.
Ilikuwa katika kujibizana kwanini lugha ya anga isiwe lugha ambayo
abiria wengi wanaelewa - huku Dk. Lwaitama akisema katika ndege nyingi
alizosafiri kote duniani alikokwenda, lugha za anga huwa zile za
wasafiri wengi wa eneo husika na lugha nyingine za kimataifa; huku
akishauri kuwa maelezo yangekuwa kwa Kiswahili na Kiingereza - ndipo
mhudumu alikimbilia mwenzake ambaye naye hakutaka kumsikiliza Lwaitama
na wote wawili wakakimbilia kwa chumba cha rubani kushitaki kuwa kuna
mtu "anafanya fujo." Tayari Dk. Lwaitama akawa abiria "hatari."
Rubani hakutaka kusikiliza abiria wake anasema nini; hakumuuliza hata
mwenzake waliokaa pamoja juu ya fujo alizoripotiwa; alimwambia hawezi
kusafiri. Akaita polisi ambao pia hawakuuliza lolote juu ya fujo zake
bali walifanya kazi moja ya kumtoa nje mkukuku.
Ni rafiki yake aliyemwita Diallo na mwanaharakati Sungusia ambao anasema
aliwapigia simu wampelekee mawakili ili aweze kuandika maelezo yake
mbele yao. Mawakili walifika na yeye kuadika maelezo. Mizigo yake
imepelekwa Bukoba. Yeye amebaki Mwanza na kompyuta yake ndogo ya
mkononi.
Dk. Lwaitama anasema, "Sina mgogoro na kampuni ya PrescisionAir, bali
wahudumu ambao hawataki hata kupata maoni ya abiria. Kwanza, walipata
bahati ya kuona mtu anahiari maoni moja kwa moja. Pili, kama wanafanya
kazi kwenye ndege watakuwa wamesafiri katika ndege za wengine ambako
niliyokuwa nayasema ni maneno na vitendo vya kawaida. Sasa fujo ni nini
katika hili?
Mwalimu huyo mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, "Hata
polisi ni wa kushangaza. Mtu anakwambia huyu kafanya fujo, wewe huulizi
ni fujo gani. Unambeba tu mzegamzege. Sidhani kama huu nao ni utendaji
bora katika nchi iliyohuru; ambako polisi wanapaswa kuwa na utulivu wa
akili na kufanya kazi kwa kufikiri kuliko kwa kuambiwa tu."
Dk. Lwaitana anaamkia kituo cha polisi uwanja wa ndege kesho asubuhi kuambiwa "uamuzi wa polisi."
Haikufahamika iwapo mhudumu wa ndege mswahili, aliyekuwa anaongea
Kiswahili, hakuwa na tafsiri ya maneno ya Kiingereza ambayo alitaka
kumwambia abiria wake.
ndimara.
Sunday, January 26, 2014
Saturday, January 18, 2014
VURUGU CHADEMA KUUA HARAKA IMANI YA WANANCHI WENGI
Mbowe: Jenga chama ndani ya umma, acha
mahakama
Na
Ndimara Tegambwage
JE, kuna haja ya mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe kumburuza Zitto
Kabwe mahakamani kwa madai ya kumtuhumu kupokea fedha kutoka kokote kule?
Ushauri: Hakuna
haja wala sababu.
Vyombo vya habari vimeripoti
wiki hii kuwa Mbowe “anasadikiwa” kuwa na nia ya kumshitaki Zitto Kabwe
mahakamani.
Kisa? Eti Zitto, ambaye tayari
amenyang’anywa unaibu katibu mkuu wa chama na unaibu msemaji mkuu wa upinzani
bungeni, “amemdhalilisha” Mbowe kwa kumtuhumu kuchukua fedha kutoka kwa Nimrod
Mkono na Rostam Aziz.
Katika mazingira ya kawaida,
kila mwanasiasa anapaswa kujibu tuhuma alizotwishwa. Kujibu na siyo kushitaki.
Kama anayetoa tuhuma amekwenda
mahakamani, ni vema kwenda kujibu mahakamani. Kama ametoa tuhuma kupitia redio,
ni vema kujibu kupitia redio. Kama ni kupitia televisheni au magazeti, ni
muhimu kujibu kupitia hukohuko.
Siku hizi kuna mitandao ya
kijamii. Kama tuhuma zimepitia huko, ni vema mtoa tuhuma akajibiwa hukohuko au
kupitia chombo ambacho kimenukuu tuhuma za mtandao na kuzichapisha au
kuzitangaza. Siyo kushitaki na siyo mahakamani.
Muhimu hapa ni kujibu tuhuma.
Ukiwa mwanasiasa na ukatuhumiwa kuwa gari lako limewahi “kukamatwa na nyara za
serikali;” fanya hima ujibu. Usipojibu, basi tuhuma inaganda na kudumu.
Ukituhumiwa wizi wa kuvunja
benki au kuibia wananchi kupitia miradi yao midogo au mikubwa, jibu haraka na
ikiwezekana papohapo au siku hiyohiyo.
Usipojibu, tuhuma inaganda au
inatapakaa; utaendelea kutoa mwanya kwa muhusika kusambaza tuhuma kwa shabaha
anayojua mwenyewe.
Ukituhumiwa ujangili, hakikisha
unajibu haraka na inakuwa kwenye rekodi kuwa ulitoa majibu na majibu thabiti
yanayoendana na tabia na mwenendo wako kama unavyoonekana katika jamii.
Usipojibu, tuhuma itaenea na
wote waliopata kuisikia watakuwa wakikutazama na kukuona katika sura hiyo
ulimochorwa.
Kama jamii haijaelewa na
kukubali mienendo ya ushoga, na wewe siyo shoga au ni shoga, ni vema kujibu
haraka tuhuma kwamba wewe ni shoga.
Ni vema kuweka msimamo wako
katika hilo na kwa wafuasi wako kujua na labda hata kuheshimu au kudharau.
Usipojibu, siyo tu utaendelea kudhoofisha wafuasi wako, bali utakosa pia fursa
ya kujenga mantiki ya kile ufanyacho au unachosimamia.
Hoja hapa ni kujibu na siyo
kushitaki. Hakika hakuna sheria inayozuia mtu kwenda mahakamani na kujibu kwa
njia ya kushitaki. Hapana! Bali jambo linalohitaji jibu kupitia njia
lilimotokea, halina sababu ya kugeuzwa kuwa shitaka.
Usipojibu uko matatani. Wanaoweka
rekodi zako kisiasa ni wengi. Wanaodondosha unyayo wao kila unapotoa wako ni
wengi. Wanaofuatilia kauli zako tangu
alfajiri hadi uendapo kitandani ni wengi. Wanaotaka kuchukua nafasi yako ya
kisiasa ni wengi pia.
Usipojibu, siku ya siku, ukiwa
unatafuta nafasi ya kisiasa, utatwangwa kombora la kile ambacho hukujibu na
wakati huo hutaweza kupata majibu ya kuwaridhisha waliokulenga tangu zamani.
Ni kwa msingi huu sharti ujibu
tuhuma. Katika hili, Mbowe anaweza kushauriwa na wenzake kuwa hana haja wala
sababu ya kwenda mahakamani kumshitaki Zitto. Iko wapi? Kama anayemtuhumu
hakwenda mahakamani, yeye anakwenda huko kufanya nini?
Chukua mfano wa Nimrod Mkono,
wakili wa mahakama kuu na mbunge wa Musoma Vijijini. Akijibu tuhuma za kutoa
mamilioni ya shilingi kwa Mbowe, alisema hajawahi kufanya hivyo. Basi. Rekodi
inabaki hiyohiyo hadi zitakapopatikana taarifa tofauti.
Naye Rostam Aziz amejibu kwa
kejeli kwamba tangu alipoona kuna “siasa uchwara” katika chama chake (CCM),
amekaa kimya na hataki kurejea katikati ya minyukano kupitia madai ya yeye
kumpa Mbowe mamilioni ya shilingi.
Hilo nalo linabaki hivyo hadi
yatakapopatikana maelezo ambayo yanakinzana na kauli hiyo – na majibu hayo.
Kujibu tuhuma na hata malalamiko, ni muhimu katika siasa.
Bali tuhuma za sasa, kutoka kwa
mmoja wa waliokuwa viongozi wakuu wa Chadema, zinaweza kuzua mtafaruku mkubwa
ndani ya chama tawala: Kwamba viongozi wake wanatoa fedha za kuneemesha chama
cha upinzani ili mgombea urais wake ashinde!
Kwamba akishinda iweje? Kwamba
wanataka kuhamia upinzani? Kwamba wao ni popo – wamesimama kuwili? Kwamba
wanasaliti chama chao, ili iweje? Kwamba wameona mgombea wao anapwaya? Tuhuma
hizi zinaweza kuwa zinalenga nini?
Hii ndio maana hata anayejibu
tuhuma sharti awe makini. Kwa mfano, tuhuma hizi zinalenga nini: Kuchongea
viongozi wa CCM? Ili iweje? Wafukuzwe? Wakifukuzwa itakuwaje nafuu kwa Chadema
au faida kwa CCM? Lakini hata bila kufika huko, na hata kama walitoa, ni kweli
walitoa kama viongozi wa CCM?
Hapa kuna kitu gani cha
kupeleka mahakamani? Hakipo. Ikitokea akawepo wa kusema “twende mahakamani,”
anakwenda kusema nini na kwa manufaa ya nani?
Haiwezi kuwa “potelea mbali,
acha chombo kizame?” Kama ni hivyo, hoja ya kupeleka mahakamani iko wapi? Na
nani hajui mahakama – kwamba hata kama huna hoja na hutaki kushinda; unaweza
kutumia uwanja huo kumwaga mchele kwa ajili ya kuku na njiwa na kunguru na tai?
Nani asiyejua kuwa mahakama
zinachukua muda mrefu kukata mashauri? Nani hajui kuwa katika mambo ya siasa,
na katika chama kilekile; mkondo wa mahakama unaanika uongo ambao wahusika
wameapa kutosema?
Yuko wapi asiyejua kuwa katika
mazingira ya kihasama – ndani ya chama
kimoja – na hasa katika mwonekano wa wazi wa upande mmoja kupoteza, lazima
upande huo uwe na tabia ya “potelea mbali?”
Turejee katika mazingira ya
sasa ya Chadema: Nani anaweza kuthibitisha kuwa hivi sasa na kati ya upande wa
Zitto na upande wa chama kuna ambaye bado anashikilia kupatikana kwa MWAFAKA,
kushikana mikono na kusema “yamekwisha?” Nani?
Tunapofikia hatua ya kutokuwa
na matumaini ya kushikana mikono, kukumbatiana na kusema yamekwisha, basi hapo
ndipo kila tuhuma inahitajika kujibiwa na hatua ya kwenda mahakamani kupuuzwa;
labda kuwe na uhalifu na siyo madai ya jumlajumla tu yanayotokana na minyukano
ya kisiasa.
Kuna ukweli kwamba kuandikwa na
kutangazwa kila siku katika vyombo vya habari; na hasa kutangazwa kwa ugomvi,
malumbano na minyukano mbalimbali kunaweza kuleta kile kinachoitwa “sura mbaya”
kwa chama.
Lakini kuandikwa ni bora kuliko
kutoandikwa; ambako ni kuwa mfu. Minyukano yenye mwelekeo wa kusafisha safu,
yaweza kuanika yaliyofichika ambayo sharti yawe wazi na kuondolewa kwa afya
njema ya chama cha siasa.
Kwa kuzingatia haya, hakuna
sababu ya Mbowe kwenda mahakamani kutokana na tuhuma zilizotajwa. Azijibu.
Zijibike. Wasonge mbele ndani ya CHAMA na ndani ya UMMA; na siyo ndani ya
mahakama.
Mwisho
(imechapishwa katika MAWIO la 16 Januari 2014)