Kufungia magazeti ni uhalifu dhidi ya wananchi na haki yao
SERIKALI inaendelea kufungia vyombo vya habari. Orodha inaongezeka. Mara hii ni zamu ya Mwananchi na Mtanzania.
MwanaHALISI lilifungiwa miezi 15 iliyopita (mwaka mmoja na robo). Hakuna dalili za kulifungulia. "Redio mbao" zinasema hata wamiliki wake wasiruhusiwe kuanzisha gazeti jingine. Limekuwa suala la binafsi.
Hatua
ya serikali ya kufungia gazeti hilo imeathiri na inaendelea kuathiri
waandishi, wake/waume zao na watoto wao; wazazi wao, ndugu
waliowategemea, wauza magazeti, wenye maduka karibu na ofisi za gazeti
hili, wauza matunda, mihogo, karanga, kahawa na kashata waliokuwa
wakitua MwanaHALISI.
Wengi wameathirika hivyo kiuchumi. Sasa
waandishi wamekuwa wabangaizaji kwa kuomba vibarua katika magazeti ya
wengine. Wananchi wengi wameathirika kwa njia ya kukosa taarifa.
Mtu
mmoja serikalini au kundi la watu; wanatumia nafasi zao kutaka kuua kwa
njaa waandishi na familia zao; na kunyima wananchi taarifa muhimu
zinazowawezesha kupata uelewa juu ya wanavyotawaliwa na jinsi ya
kujinasua kutoka mkenge wa ghiliba, wizi na ufisadi.
Jana
serikali iliongeza machungu kwa waandishi na wananchi na orodha yote
niliyotaja hapo juu kwa amri ya kufungia magazeti ya Mwananchi na
Mtanzania. Na serikali inajua. Hiyo siyo njia sahihi ya kutenda kazi.
Serikali inaingilia kazi na majukumu ya mahakama.
Kwa ufupi,
serikali inapuuza na kudharau mahakama. Kuna sheria ya Magazeti ya mwaka
1976, katili kama ilivyo lakini bado inatumika na watawala ndio
wameiweka mbelekoni. Kwanini serikali haiitumii kwa njia ya kwenda
mahakamani? Inaogopa nini? Woga wake ni upi?
Kuna Baraza la
Habari Tanzania (MCT). Limejaa na linashirikisha wataalamu wa nyanja
muhimu katika tasnia hii - waandishi wa habari na wanasheria. Lina uwezo
mkubwa wa kusikiliza na kutolea uamuzi malalamiko ya mtu au taasisi
yoyote. Serikali hailitumiii.
Wahusika ndani ya serikali wanatumia ubabe wa amri kwa nia ya "kuua sisimizi kwa kutumia nyundo," lakini nje ya mkondo wa sheria au ushauri wa kitaaluma ambao unaheshimika zaidi kuliko amri au mitulinga.
Kesho
serikali itazima gazeti au chombo kingine cha habari. Itaondosha ajira
za waandishi. Itafinyaza fursa za kujiendeleza katika taaluma hii.
Itanyakua haki ya uhuru wa kupata taarifa na habari. Itafanya kazi zake
gizani na kwa hiyo bila mrejesho kutoka kwa jamii pana iliyokuwa inapata
taarifa kupitia vyombo vya habari vinavyofungiwa.
Kufungia au
hata kufuta chombo cha habari, licha ya kwamba ni kuvunja haki za
binadamu; vilevile ni kuziba mifereji ya fikra ya jamii; kuongeza
umasikini, kuasisi woga miongoni mwa watu, kujenga visima vya chuki na
hasira dhidi ya serikali; kutaka watu waishi kwa umbeya na kurudisha
jamii katika ujima.
Hatupendi kuamini kuwa haya yanatendwa na
serikali inayojiita ya "kidemokrasia" na inayojigamba kuwa na uwazi na
utawala bora. Hapana! Kuna serikali ngapi - moja itende demokrasia na
nyingine itende uhalifu dhidi ya haki ya uhuru wa habari? Ghiliba!
Tumependekeza
tangu 1985. Kwamba serikali iache wananchi na waandishi wa habari
waiseme wanavyoiona. Kama sivyo ilivyo, basi ipuuze. Kama ndivyo ilivyo,
basi ijisahihishe. Serikali ina maguvu mengi ya kutumia kuleta
mabadiliko kwa maslahi ya watu; na siyo kwa kuangamiza uhuru wa kufikiri
na kutoa mawazo.
Inakokwenda serikali, siko!
ndimara.