Thursday, January 31, 2013

Big lie or slip of the tongue?



MwanaHALISI back to centre stage

Statement by Managing Director of Hali Halisi Publishers Limited (HHPL) – publishers of MwanaHALISI, Mr. Saed Kubenea on President Jakaya Kikwete’s remarks that his government will not unban the paper.


To All Lovers Of Press Freedom

MwanaHALISI, our beloved weekly banned by government six months ago (30th June 2012), has refused to die. It has remained in the hearts and therefore on the lips, of its readers – friends and foe. 

In the past two weeks, discussions on radio and TV at a good number of stations in Dar es Salaam, have extolled the paper and further pleaded with government for its immediate and unconditional unban in order to fill what many of them called the void in well dug pieces of news and information.

But, in the midst of such demands and exaltations, President Jakaya Kikwete, speaking from Addis Ababa, the Ethiopian capital where he was attending the APRM forum, sent word that could either sink the weekly further or bring it back on the streets.

The president was quoted by his government’s daily – HABARILEO – saying his government banned one newspaper because it published material that was geared to inciting the army to rebel.

Providing answers and explanations to allegations of suppression of freedom of the press, raised during the APRM session, President Kikwete was quoted as saying, “Yes, there is a newspaper we have banned for inciting the army… There are those calling for its unban but we are not going to do so…this is not journalism.”

On the one part, the president’s stand brought some relief to journalists and management at Hali Halisi Publishers Limited – publishers of MwanaHALISI because the paper is not on record for publishing any material geared to inciting the army; nor had there been any allegations leveled by government against us to that effect.

On the other part, there is on record, one newspaper which stands accused of publishing material the government deems verged on inciting the army. The writer of the disputed article, his editor and printer, have been arraigned in court. None of these has any link with MwanaHALISI.

But MwanaHALISI is the only paper in the country banned by government; therefore the president could have been referring to it even if it had not been accused of inciting the army; and when those accused of incitement have already been arraigned in court. Could it be a riddle?

The government newspaper published the president’s remarks on Monday, 28th January instant. Today is the fourth day and no signs of government rescinding the statement nor any official elaborating on the matter.

However, at MwanaHALISI we have made efforts to reach authority – including the president’s office – to seek government action: To unban the weekly. This is because, accusations and allegations regarding publication of material geared to incite the army, which the president said necessitated the ban of “a newspaper,” do not concern us at all.

We count on every honest soul in this matter.

      sgnd

Saed Kubenea
Managing Director

Picture: President Jakaya Kikwete

Soma: www.facebook.com/ndimara.tegambwage

Monday, January 21, 2013

Nani watalinda bomba la gesi?







Gesi ya Mtwara na 
ubabe wa serikali

Gesi ikipatikana Mtwara, isombwe hadi Dar es Salaam ili izalishwe nishati ya umeme. Ikipatikana Tanga, ipelekwe Dar es Salaam. Ikipatikana Kigoma sharti pia ipelekwe Dar es Salaam. Huu ni ukame wa akili. Lakini ukame huu siyo wa leo. Kuna wakati watawala na watendaji wao nchini waliwahi kuishiwa akili kama ilivyo sasa. Ni nyakati zile nilipoandika kitabu kiitwacho “Duka la Kaya” – unyafuzi wa akili usiomithilika!

Sukari itazalishwa Kagera. Itasombwa na kupelekwa Dar es Salaam. Ile ya Mtibwa, Morogoro itapelekwa Dar es Salaam. Ile ya Moshi itapelekwa Dar es Salaam. Kutoka Dar es Salaam wataandaa kile walichoita “mgao” au “mgawo.” Sukari itasombwa kutoka Dar es Salaam kurudishwa kijiji jirani na kiwanda cha sukari Kagera, Mtibwa na Moshi. Ni ukame wa akili na wizi usiovumilika, vilivyodhihirika miongoni mwa wanasiasa na watendaji.  Yalikuwa matusi ya aina yake kwa wasomi na usomi wao.

Nenda Morogoro. Angalia viwanda vilivyolundikwa mjini Morogoro wakati waziri wa viwanda alikuwa pia mbunge wa Morogoro – Amir Jamal. Pale waliweka hata kiwanda cha ngozi huku wakijua vema kuwa kiwanda kama hicho kingewekwa maeneo ya wafugaji – kwenye ngozi nyingi – Mwanza, Shinyanga na Umasaini; wakaweka kiwanda cha tumbaku huku wakijua kiwanda kingekwenda Tabora ambako wanalima asilimia 60 ya zao hilo. Angalia na vingine. Ni makengeza ya makusudi alimradi muhusika amepindishia kwake au kwao.   

Ujuha huu wa kiuchumi ni ghali sana. Siyo ghali kwa wanaoupanga na kuutekeleza – kwani wao ndio wanufaikaji wakuu wa mipango, mbinu na mikakati – bali kwa wananchi ambao wangenufaika angalao na hicho kidogo kinachosalia. Lakini ni mipango ya “potelea mbali;” mipango ya “watakaokuja baadaye watatafuta vyao;” mipango ya “chukua chako mapema.”

Kwani umeme ukizalishwa Mtwara, penye gesi, hauwezi kusambazwa nchi nzima? Ukizalishwa popote pale nchini hauwezi kufikishwa unapohitajika; ni mpaka gesi italii ndani ya mabomba, ifike Dar es Salaam ndipo umeme upatikane?

Kwa wenye nia safi na waliodhamiria kuleta mabadiliko kila sehemu ya nchi hii, kugundulika kwa utajiri (maliasili/raslimali) pale wanapoishi, sharti kuchochee akili mpya; siyo ya kuhamisha utajiri huo, bali kuutumia hapo ulipo ili kubadili maisha ya wenyeji na kuondoa hadithi za kisiasa za “tutawaletea” wakati hakika “tunawanyang’anya” utajiri, maendeleo, mabadiliko.

Tunaweza kujiuliza: Kuna nini katika usafirishaji gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam badala ya kuzalisha umeme palepale Mtwara na kuusambaza kwingine? Jibu la haraka ni swali hili: Kulikuwa na nini katika kuchukua sukari kutoka viwanda vya sukari (Kagera, Mtibwa na Moshi) hadi Dar es Salaam na baadaye kuirejesha huko ndipo iuzwe kwa wananchi katika vijiji jirani na viwanda; tena mara hii kwa bei ya juu zaidi! Ni njia nyingine ya kuongeza gharama ambayo hailipwi na watunga “dili” bali wananchi; ni njia nyingine ya ukwapuaji. Ni wizi.

Kama nilivyowahi kuandika kwa njia hii, wananchi wa Mtwara hawataki kupewa gesi katika makopo, vikapu, madumu na chupa; bali wanataka angalao, kufanana na wanaoishi karibu au katikati ya utajiri wao na nchi yao. Njia pekee ya kufanana au hata kuwa hivyo; na inayowezekana mara moja, ni kuzalisha umeme kutoka gesi ya Mtwara, hapohapo Mtwara.

Historia imetuonyesha, siyo tu Tanzania na Afrika, bali hata nje ya bara hili, kwamba pale ulipopatikana utajiri wa maliasili, wananchi wakazi wamekumbwa na adha ainaaina. Badala ya neema imekuja balaa. Nchini hapa, kuhamishwa kwa nguvu, kutopewa fidia, kuuawa, kulemazwa kwa risasi za moto, kunywa maji yaliyoingia sumu kutoka migodini na umasikini usiomithilika hatua 10 tu kutoka kwenye uzio wa mgodi, yote haya yamekuwa balaa la aina yake.

Kama kwamba haitoshi, serikali haionekani kufanya lolote kulinda na kuhifadhi watu wake. Inachofanya ni kuendelea kugawa kwa kampuni za nje, maeneo zaidi ya kuchimba madini na hivyo kuhamisha wananchi zaidi na kufukarisha maelfu kwa maelfu. Sasa kampuni za kuchimba madini zimeanza kuingia ubia na polisi mikoani ili ziweze kulindwa “dhidi ya wananchi” ndani ya nchi yao. Hao ndio polisi wanaodaiwa kuwa walinzi wa raia na mali zao! Kama mali ya raia imeishachukuliwa au kuharibiwa na polisi yuko upande wa tajiri kutoka nje ya nchi; uko wapi usalama wa raia na iko wapi mali yake? Tumebakiza nini kama siyo kuuza mioyo yetu!

Mtwara wana ujumbe mfupi na unaoeleweka. Wanasema zalishia umeme hapa. Toa umeme hapa na peleka kwingine. Elekeza wawekezaji kwenda Mtwara au chochea wakazi wake kuzalishia bidhaa Mtwara kwenye gesi na umeme. Hili lina maana pana kwa wakazi wa Mtwara.

Sikilizeni mkazi wa Mtwara. Albert Msosa, fundi bomba anayeishi mjini Mtwara anasema, pamoja na mengine mengi, kuzalishwa kwa umeme kutokana na gesi hapo Mtwara kutachochea fikra juu ya matumizi ya umeme maishani mwao; kutakuwa moja ya vichocheo vya wananchi na hata watu kutoka nje kwenda na kuwekeza kwa njia ya viwanda; kutachochea kuibuka kwa viwanda vidogo na vya kati; kutaondosha uwezekano wa kufanya wakazi wa Mtwara kuwa kolokoloni wa kulinda bomba la gesi; kutazalisha ajira kwa watu wengi zaidi.

Huyo ni fundi bomba. Wengine wa viwango tofauti vya elimu, maarifa na uelewa wanasemaje? Serikali ya Rais Jakaya Kikwete iwasikilize. Aliyeumwa na nyoka hukimbia mjusi au hata kamba gizani. Yaliyowakumba North Mara, Bulyanhulu, Geita, Nzega, Buzwagi na kwingineko ambako utajiri ulitengwa haraka na wamiliki wao wa asili, yanatishia pia uhai wa wakazi wa Mtwara. Hicho ndicho chimbuko la  kilio chao!

Picha: Prof. Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini

Soma: www.facebook.com/ndimara.tegambwage

KATIKA JINA LA HAKI


Miswada ikienda kimyakimya 
watapitisha kanyaboya, tutalia

Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, waandishi wa habari nchini Tanzania wamekuwa wakitaka serikali kuwasilisha bungeni miswada miwili ya habari. Hii ni miswada iliyotokana na juhudi kubwa ya waandishi wa habari, marafiki wa habari, wanaharakati ainaina wanaopigania uhuru wa habari na wananchi – makundi na mmojmmoja – kwa shabaha ya kujenga mazingira bora ya haki na uhuru wa kukusanya, kupewa na kutawanya habari. Ni kazi nzuri ambayo serikali imekalia kwa kipindi chote hicho.

Sasa kuna kinachoonekana kuwa juhudi za kuwataka wabunge kujadili kwa kina “miswada hiyo” ya habari na kuipitisha. Lakini kuna haja ya kujiuliza kwanza: Ni miswada ipi wanataka wabunge wajadili na kupitisha?

Kilichopelekwa serikalini kutoka kwa wadau wa habari, ni mapendekezo. Serikali imeyakalia kwa miaka yote hiyo chini ya mawaziri watatu – anatoka huyu anaingia huyu – bila kuyafanyia kazi. Hatimaye tumeanza kusikia serikali ikisema, kupitia wasemaje wake wanaojikanganya kwa tarehe za kuwasilisha bungeni, kuwa itapeleka miswada hiyo bungeni.

Utaratibu ni kwamba serikali inasoma mapendekezo. Inafanya maamuzi. Inapeleka mapendekezo kwa mwandishi mkuu wa sheria ambaye anaumba maoni na hoja za serikali katika sura ya muswada wenye mwelekeo wa mapendekezo ya wadau wa habari. Tuko pamoja?

Hapa ndipo kuna kazi. Serikali inaweza kuazima na kutumia maneno yaleyale yanayotumiwa katika mapendekezo ya wadau lakini ikaja na “moyo tofauti wa sheria” katika maumbile mapya yanayopelekwa bungeni.

Ninajua kuna wanaoamini serikali kwa asilimia 100/100. Lakini naomba kuwakumbusha mapendekezo ya muswada wa mashirika yasiyo ya serikali. Tuliumba kitu chetu. Tukaipa serikali. Ikachukua. Ikapongeza. Ikampa mwandishi wa sheria. Kilichotoka humo ni kibaya zaidi – katili, nyakuzi, ning’inizi na hatarishi kuliko hali ilivyokuwa kabla ya sheria.

Ikitokea hivyo katika miswada ya sheria, serikali itasema: “Walitaka sheria, tukawapa sheria; sana wanalalamikia kitu gani?” Tutagota upya.

Hoja: Kama serikali inasema ipo tayari kupeleka miswada ya habari bungeni; basi kwa nia njema ifanye hivi: Iweke wazi miswada hiyo kwa waandishi wa habari, wadau wa habari na wananchi; waisome, waijadili, wailinganishe na mapendekezo ya wadau wa habari, waijazie (kama itahitaji kujaziwa), wapendekeze mengine – mapya au ya awali yaliyonyofolewa, kabla ya kuiwasilisha bungeni.

Hili ni muhimu sana. Lisipofanyika, serikali itawaambia wabunge, “Hiki ndicho wadau wamekuwa wakidai. Tunaomba muwapitishie.” Ni wabunge wachache watagundua tofauti au ghiliba; na hao wachache hawatazuia miswada kupitishwa. Tutarudi palepale – kubishana na kuzozana na serikali na wa serikali.

Katika jina la haki, miswada ya serikali iwekwe wazi kwanza; tuione, tuisome, tuijadili na kuijazia. Na kama serikali ingekuwa ya uwazi, kwa kipindi chote tangu ikabidhiwe mapendekezo, ingekuwa imeumba miswada yake, kuiweka mbele ya umma kwa mjadala na kupata miswada muwafaka. Haikufanya hivyo. Sasa yaweza kuleta bomu litakaloua hata chembechembe za kilichokuwepo na kilichotupa fursa ya kudai haki ya habari.

see also ndimara's facebook

Thursday, January 17, 2013

Kufungia gazeti: Ni woga, ubabe au ulimbukeni?

MwanaHALISI: Nusu mwaka kifungoni
 'Kwa kufunga gazeti wamewaweka pia wasomaji gerezani popote walipo'

LEO ni siku 172 tangu serikali ifungie gazeti la MwanaHALISI “kwa muda usiojulikana.” Siku hizo ni sawa na miezi mitano na siku 22 au miezi sita kasoro siku nane. Ni nusu mwaka.

Kwa muda usiojulikana maana yake ni mpaka serikali itakapotaka (yenyewe). Itakapojisikia. Itakapofurahi. Itakapopigiwa magoti na wamiliki wa gazeti. Itakapoombwa na marafiki wa gazeti. Itakaposhinikizwa vya kutosha na wapigania uhuru wa habari.

Kwa muda usiojulikana yaweza kuwa pale viongozi wa serikali waliofungia gazeti watakapotembelewa na akili na uelewa kuwa hawapaswi/hawakupaswa kuingilia uhuru wa kupata, kutafuta na kukusanya habari; au pale serikali itakapoamuliwa na mahakama; au wenye gazeti watakapoamua kulichapisha kwa mapenzi ya wananchi bila kujali serikali inasema nini. Hilo nalo linawezekana.

Nusu mwaka. Serikali inayojidai kutenda na kulinda haki za raia wake imeamua kuwa wafanyakazi wa gazeti la MwanaHALISI wawe ombaomba mitaani; au wasambaratike kwa kuhama kampuni au wafe kwa njaa – potelea mbali! Kama hii ndiyo haki, basi ni haki ya mashetani.

Imekuwa safari ndefu – nusu mwaka – lakini iliyojaa karaha na kinyaa. Hapa kuna serikali inayojigamba kutawala kwa “misingi ya demokrasia;” lakini ni serikali hiyohiyo inayotaka kutawala gizani – kishirikina; na inayonyakua uhuru wa wananchi wake wa kutoa, kupata na kusambaza taarifa na habari.

Hapa kuna watawala wanaojigamba kuwa wakweli na wawazi lakini wanaficha hata kilichowazi kwa kila mmoja. Wanafungia gazeti kwa nia ya kuua jicho la nyongeza la jamii; kuziba sikio la nyongeza la jamii na kusiliba mdomo wa nyongeza ya jamii. Wanataka jamii mfu – isiyoona uoza, isiyosikia mipango ya “uhaini” dhidi ya jamii na isiyotoa kilio cha wengi.

Kufungiwa kwa MwanaHALISI kulisononesha nyoyo; kukazika shauku, kukanyakua maarifa, kukapora uhuru na kukaondoa mategemeo. Watawala wanajua lakini hawajali.

Hili ni gazeti lililofungiwa wakati habari kuu katika vyombo vyote vya habari nchini ilikuwa “Utekaji na utesaji wa Dk. Steven Ulimboka.” Kufungiwa kwa gazeti, katika mazingira haya, tena kwa muda usiojulikana, kulionekana kwa wasomaji wake, wafuatiliaji na wachunguzi kuwa njia ya kuzima mifereji ya ukweli iliyokuwa ikielekea kumwaga ushahidi mwanana katika macho na masikio ya wasomaji wake.

Funga! Ili lisiandike habari nyeti juu ya unyama aliofanyiwa kiongozi wa madaktari katika kudai vitendeakazi na mazingira bora ya kazi. Funga! Lisifumue taarifa za nyongeza na mkondo wa mawasiliano. Funga! Ili lisiendelee kuumbua wahusika – kuanzia waliobuni “mradi” hadi waliotekeleza. Funga! Ili dunia nje ya Tanzania isije kujua unyama unaohusishwa na serikali.

Leo, kama ilivyokuwa siku ya kwanza ya siku 172 za kifungo cha MwanaHALISI, ninaendelea kukubaliana na wasomaji, wafuatiliaji na wachunguzi juu ya sababu za kufungiwa kwa gazeti: Kuingiza taifa gizani ili lisiweze kuona masuala muhimu ambayo gazeti hili limekuwa likiibua.

Kinachosikitisha ni kwamba watawala, kwa upofu wao, katika suala la Ulimboka, hawakuona kuwa gazeti lilikuwa linatoa taarifa za ndani na za kweli ambazo zingesaidia serikali kujiondoa katika tope la “kutaka kumuua Ulimboka.”

Watawala walishindwa, labda kwa kiwewe tu, kueleawa kuwa taarifa za ndani na za kina zingeonyesha muhusika mmoja na siyo serikali yote wala ikulu yote. Hawakuona kwamba taarifa za kina zingesafisha hata Usalama wa Taifa na Polisi – ambao ndio walikuwa wanatungwa kidole.

Kwa vipi? Ikulu siyo pango la wauaji. Ni makao makuu ya mtawala wa nchi. Haitarajiwi kuwa makazi ya watekaji, watesaji au wauaji. Kwahiyo, kama ikulu kuna mtuhumiwa mmoja, watawala wana haki na sababu ya kuachia wanaojua kazi kuwasaidia kufichua nani anachafua heshima na uhalali wa ikulu.

Vivyo hivyo kwa usalama wa taifa. Hawanabudi kukaa kitako na hata kuomba msaada wa nyongeza kutoka kwa wanaojua kazi yao, ili kufichua wanaotaka “kuharibu sifa” zao. Kwani, kazi ya  usalama wa taifa siyo kuteka, kutesa na kuua. Anayefanya hayo sharti awekwe wazi ili chombo hicho kibaki kikiaminiwa. Vivyo hivyo kwa jeshi la polisi.

Mvumo wa taarifa za gazeti ambao ungetunga wahusika mmojammoja kama shanga katika “sakata la Ulimboka,” ungenusuru ikulu, usalama wa taifa na polisi. Hapo ndipo ukweli na uwazi ambavyo vinaimbwa, vingesaidia serikali kuondokana na uchafu unaoweza kuiondolea imani ya wananchi na uhalali wake.

Tumekuwa tukiiambia serikali, tena mara nyingi tangu 1985 – kwamba iwapo chombo cha habari kitakosea, basi kipelekewe mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Watawala hawataki hilo, bali wanataka kuonyesha kuwa wako juu ya sheria za nchi. Wanatumia ubabe.

Amini usiamini. Hata madikiteta wanahitaji taarifa na habari sahihi na za kina; hata zile zinazoonyesha wanavyonyukana ndani kwa ndani. Wameachana na ubazazi wa kufikiri kuwa, kama gazeti halikuandika au limezuiwa kuandika, basi jambo husika  halitafahamika na hivyo watatulia. Hawafanyi hivyo leo. Wanakataa kuishi kwa umbeya au vitaarifa vya kuwapongeza, kuwasifu na kuwapakata, wakati halihalisi ni tofauti.

Serikali ambayo haina taarifa juu yake na haijui wananchi wanasema au wanajua nini juu yake na wao wenyewe; haiwezi kuchukua hatua. Sasa serikali inayoua vyombo vya habari hadi itakapopakatwa, kubembelezwa na kupigwa busu, siyo serikali ya wananchi. Hata kama watawala wake watadai kuwa walichaguliwa na wananchi, sharti tukubaliane kuwa ilikuwa kiinimacho. Huwezi kuchaguliwa kutawala halafu ukapora waliokuchagua uhuru wao wa kufikiri na uhuru wa kauli.

Ni siku 172 leo tangu serikali izuie wasomaji kuona kipenzi chao MwanaHALISI. Kwamba vyombo vingine vya habari havijaguswa, haina maana kwamba serikali ina ushoga wa kudumu na vyombo hivyo. Vikitaka haki vitazimwa. Vikitaka uhuru vitaning’inizwa. Vikitaka ukweli vitafungiwa “kwa muda usiojulikana.”

Kisichoeleweka vema na haraka kwa wengi ni kwamba, kufungia MwanaHALISI au gazeti kama hilo au lolote lile lililokwishajitambulisha kuwa mdomo wa umma, ni kuweka kifungoni mamilioni ya watu na kuwaondolea kichocheo cha kufikiri.

Wangapi watakubali kubaki kifungoni bila kuhukumiwa na mahakama; bali kwa utashi dhaifu na “hukumu” ya waliobeba mamlaka ya kisiasa? Binafsi, sikubali!

fuatia pia: ndimara facebook

Friday, January 11, 2013

MAONI YA MFUNGWA WA MwanaHALISI


Nani anataka nini katika katiba mpya? Haya ni maoni yaliyowasilishwa na Saed Kubenea wa MwanaHALISI; gazeti lililofungiwa na serikali kwa muda usiojulikana tangu 30 Julai 2012.
                                                                         
JANA (10 Januari 2013) wenye vyombo vya habari na asasi nyingine za habari waliwasilisha kwa Tume ya Katiba Mpya, mapendekezo ya asasi zao na hata kuongeza maoni binafsi kama mwenyekiti wa mkutano wa Katiba, Prof. Mwesiga Baregu alivyoruhusu.

Saed Kubenea, Mkurugenzi Mtendaji wa Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), wachapishaji wa magazeti ya MwanaHALISI na MISETO, aliwasilisha maoni yake. Nimeyasoma asubuhi na kuyafanya moja ya mambo muhimu niliyoona leo na yenye thamani. Naomba kuwashirikisha:

Mapendekezo: Katiba Mpya (Na Saed Kubenea)
1. Kuhusu vyombo vya Habari
KATIBA itamke kuwa vyombo vya kutunga sheria (Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Baraza la Wawakilishi, Bunge la Tanganyika au Bunge la Shirikisho; na vyovyote vile vitakavyokuwepo) visitunge:
a) Sheria inayopingana (inayokinzana), inayokwaza au kuingilia uhuru wa kuwa na maoni (kufikiri)
b) Sheria inayopingana, inayokwaza au kuingilia uhuru wa kujieleza (kutoa kauli)
c) Sheria inayopingana, inayokwaza au kuingilia uhuru wa habari (kupata habari zozote zinazohusu jamii zilizoko mikononi mwa serikali)
d) Sheria inayopingana, inayokwaza au kuingilia uhuru wa vyombo vya habari (kazi za utafutaji, ukusanyaji na usambazaji wa habari inayofanywa na waandishi wa habari na watangazaji)
e) Sheria inayopingana, inayokwaza au kuingilia uhuru wa kujumuika kwa amani (mikutano/maandamano ambavyo kihalisi ni njia za wanajamii kuwasiliana au kupeleka ujumbe kwa wahusika)

2. Kuhusu Mamlaka ya DPP
Katiba itamke kuwa:
a) Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ateuliwe na chombo huru cha uteuzi (siyo rais wa nchi) na athibitishwe na Bunge
b) DPP awajibike kwa Bunge (Chombo cha kutunga sheria)

3. Mapendekezo mengine
1. Katiba itamke kuwa ARDHI ni mali ya Watanzania. Isiwekwe chini ya rais bali iwe chini ya wananchi wa Tanzania. Serikali itakuwa tu na mamlaka ya kutwaa ardhi kwa ajili ya manufaa ya umma ambayo yameainishwa kama vile ujenzi wa miundombinu, utunzaji wa mazingira na uboreshaji makazi. Serikali isiwe na uwezo wa kutwaa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa mtu binafsi au kampuni kama inavyoelezwa sasa na Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999.

2. Katiba itamke kuwa kila kijiji kitakuwa na serikali ya kijiji ambayo itaongoza kijiji hicho pamoja na uwezo wa kutunga sheria ndogo na kuzipitisha chini ya usimamizi wa mkutano mkuu wa kijiji. Serikali za vijiji ndizo zitakuwa na mamlaka ya kusimamia na kulinda haki za wananchi juu ya umiliki wao wa ardhi ya kijiji na kupanga mipango ya matumizi ya ardhi. Zitakuwa na uwezo wa kutoza kodi na kuendesha miradi ya maendeleo vijijini.

3. Katiba itamke kuwa rasilimali za madini, mafuta, gesi na maliasili, ni mali ya Watanzania na ni lazima zitumike na kuvunwa kwa manufaa ya Watanzania. Serikali haitasaini mikataba bila kibali cha bunge; bali itakuwa na uwezo wa kutoa leseni za utumiwaji wake. Utoaji huo wa leseni lazima pia uwe wa wazi na ambao utaidhinishwa na Bunge.

4. Katiba itamke kwamba migogoro yote ya uwekezaji sharti isuluhishwe kwa mujibu wa sheria za Tanzania na Mahakama za Tanzania. Hili ni takwa la Kanuni ya makubaliano ya Calvo na vilevile Azimio Na. 1803 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la Mwaka 1962 na Azimio Na. 3281 la 1974 la Baraza hilo juu ya Haki na Wajibu wa Mataifa juu ya Maliasili.

5. Katiba itamke kuwa rais atachaguliwa kwa kupigiwa kura na kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura za watu wanaotakiwa kupiga kura. Yeye na serikali yake ni lazima awajibike kwa bunge na kila uteuzi anaofanya kwa nafasi za juu za uongozi, sharti uidhinishwe na bunge baada ya Bunge kuhojiana nao.
6. Katiba itamke kuwa Bunge lina madaraka na haki ya kumfuta kazi rais kwa kutowajibika au kwa kutumia madaraka yake vibaya.

7. Katiba itamke kuwa rais hatakuwa na haki au uwezo wa kulivunja bunge kwa sababu yoyote ile.

8. Katiba itamke kuwa rais hatakuwa na kinga dhidi ya mashitaka yoyote yale akiwa madarakani na baada ya kutoka madarakani. Mtu yeyote anaweza kufungua kesi dhidi yake binafsi au ofisi yake.

9. Katiba itamke kuwa uteuzi wa majaji wa mahakama kuu na mahakama ya rufaa ufanywe na chombo huru (badala ya rais) na ufuate umahiri na uelewa wa sheria pamoja na uadilifu wa kimaadili na kisheria.

10. Katiba itamke kuwa mhimili wa Mahakama, ukiongozwa na Jaji Mkuu, ndio usimamie na kuwasilisha bajeti yake bungeni (badala ya serikali kama ilivyo sasa).

11. Katiba itamke kuwa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na viongozi wengine wakuu wa tume, wateuliwe na chombo huru cha uteuzi baada ya wanaotaka nafasi hiyo kuomba na kufanyiwa usaili. Aidha, maamuzi ya tume, kwa nafasi yoyote ile ya wagombea, yaweze kupingwa na mtu yeyote mahakamani.

12. Katiba itamke kuwa kukosa uadilifu au kutumia madaraka vibaya, kama itakavyothibitishwa na chombo husika, ni kosa la jinai.

13. Katiba itamke kuwa wote wanaojipatia utajiri kwa kuhujumu uchumi au watu wanaojitajirisha kwa kutumia madaraka yao ya umma, lazima washitakiwe kwa kosa la uhaini na mali zao zote, ikiwa ni pamoja na zile za walionufaika kutokana na kosa hilo, zitaifishwe.

14. Cheo cha Makamu wa Rais kiondolewe. Kibaki cha Waziri Mkuu.

15. Katiba itamke kuwa wakuu wa mikoa, wilaya (kama ni lazima kuendelea kuwa nao) wapatikane kwa kupigiwa akura ili w3aweze kuwajibika vema katika maeneo yao. Mameya wa miji na majiji nao wachaguliwe na wananchi moja kwa moja badala ya kuchaguliwa na madiwani.

16. Katiba itamke haki ya kuishi katika mazingira safi na salama lazima.

17. Katiba itamke kuwapo haki ya kufungua kesi za kutetea katiba, haki za binadamu na utawala wa sheria bila gharama zozote zile.

18. Katiba itamke kuwa elimu na afya ni haki kwa Watanzania wote.

19. Katiba itamke haki ya starehe.


Mwisho.
  •   Picha: Joseph Warioba: Mwenyekiti Tume ya Rais ya Katiba Mpya
Top of Form