Tuesday, December 25, 2012

UMASIKINI TISHIO LA AMANI


                       

Padri aonya juu ya umasikini uliokithiri

Na Lilian Tegambwage

PADRI Dennis Massawe wa Parokia ya Tegeta nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam amesema, “…wanyonge wa nchi hii wakichoka unyonge wao, yatatokea machafuko makubwa.”

“Tuombe kwa ajili ya wanyonge. Hawa ni wale wanaolala njaa; wanaokwenda hospitali na kuambiwa hakuna dawa; watoto wao wanashindwa kwenda shule kwa kuwa hawana daftari…” amesema Padri Massawe.

Alikuwa akihubiri leo Jumanne, kwenye Misa ya Krismasi katika Kigango cha Mtakatifu Petro cha Parokia ya Tegeta kilichoko Tegeta Masaiti.

Amesema wanyonge wakichoka Tanzania kutatokea “machafuko makubwa sana;” akiongeza, “Tuombe sana kwa ajili yao. Tuombe wasichoke.”

Mahubiri ya Padri Massawe yamechukuliwa kama njia mojawapo ya kukumbusha na kuonya watawala kuhusu “bomu la umasikini” ambalo linaweza kulipuka wakati wowote pale waliotupwa nje ya mzunguko wa kunufaika na raslimali za taifa watakapoamka na kudai haki zao.

Kwa upande mwingine, padri alikuwa akiwatekenya wanyonge wenyewe kuvua unyonge wao na kuelekeza madai ya haki na matakwa yao kwa waliopewa mamlaka ya utawala wa nchi.

Kauli ya padri ilifananishwa na mahubiri ya mapadri wa nchi za Amerika Kusini ambao miongo minne iliyopita walianza kuhubiri kwamba sharti wananchi wao waanze kuishi hapahapa duniani maisha bora ambayo wanahubiriwa.

Ni kauli hizi ambazo ziliunganisha waumini Wakristo na watu wa madhehebu mengine, kwa upande mmoja, na wanaharakati na wapigania mabadiliko, kwa upande mwingine, katika kupigania haki na usawa katika nchi zao.

Akigeukia waumini, Padri Massawe amesema, “…wengine tumekuwa tunakuja hapa kwa mazoea tu. Tunakuja kanisani kujifurahisha. Tukitoka kanisani, sisi ndio tunakuwa vinara wa maovu kama ufisadi, ngono, wizi na chuki.”

Padri alitoa mfano wa waziri mmoja wa India ambaye alimnukuu akisema anampenda sana Yesu Kristo kwa kuwa amefanya kazi kubwa katika dunia; lakini hapendi wakristo kwa sababu hawaishi kama Yesu na kama biblia inavyosema.

Biblia, kiongozi cha madhehebu ya Kikristo, ni moja ya vitabu vilivyosomwa na kuchambuliwa sana duniani; kikiwa kimesomwa na wanaoamini na wasioamini katika madhehebu hayo.

Leo ni siku ya Krismasi inayoadhimishwa rasmi na wakristo kote diniani kwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo zaidi ya miaka 2,000 iliyopita.

Kigango cha Mtakatifu Petro kilifurika waumini waliotumbuizwa na kwaya ya Mtakatifu Andrea ya kigangoni hapo.

Padri aliwaombea waumini wote akisema washerehekee Krismasi kwa amani.

Katika hatua nyingine, washiriki walisimama kwa dakika moja kukumbuka muumini maarufu Erasmus Lunaga, mwenyekiti wa Jumuiya ya Timotheo, Machakani-Sinza, aliyefariki siku ya Krismas mwaka jana.
(Lilian anasomea diploma ya IT (University of Dar es Salaam Computing Centre). Alikwenda kanisani leo asubuhi. Aliporudi nikamwomba anieleze kwa maandishi, kile ambacho kimehubiriwa. Akakaa chini na kuandika taarifa hiyo hapo juu. Nimeongeza aya moja tu. Naona anaweza huko aendako).
  •  Picha juu: Polycap Kardinali Pengo
 
 
 

Saturday, December 15, 2012

Porojo za Msajili John Tendwa

JOHN Tendwa, Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ni mwajiriwa wa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hupenda kutishia kufuta vyama vya siasa.

Mwandishi wa habari, Mwangosi alipouawa akiwa mikononi mwa polisi, Tendwa alitishia kufuta vyama "vinavyosababisha mauaji." Polisi wanaotuhumiwa kuua mwandishi ni wa serikali ya CCM. John tendwa hajafanya lolote. Yeye hutumika kuhalalisha au kutetea waliompa ofisi. Amekaa kimya mpaka Saidi Michael akamwona.

Mkuki kwa nguruwe, kwa binadamu mchungu! 

Nape, CCM na Kadi ya Dk. Slaa



Dk. Willibrod Slaa

Mjadala Kadi ya Dk. Slaa 'kiinimacho'

Sina kadi ya Tanganyika African National Union (TANU) - chama kilichoongoza wananchi kupigania uhuru. Sikuwahi kukata kadi ya chama hicho. Lakini nina kadi ya Umoja wa Vijana wa TANU (Tanu Youth League - TYL). Nilikuwa mwanachama na mwenyekiti wake nikiwa sekondari, Kahororo. Niliishia hapo. Sikuwahi kuwa na kadi ya TANU. Sikuwahi kuwa na kadi ya litoto lake CCM. Sikuwahi kuwa na kadi ya Umoja wa Vijana wa CCM.

Lakini bado nina kadi yangu ya TYL. Kadi hii bado imewekwa mahali salama. Imefanyiwa uzuderi (lamination) isije kupauka. Itakaa sana. Siichani. Siitupi. Simpi mtu. Ni mali yangu. Acha historia inukuu ushiriki wangu hata katika kuchanga senti 50 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Vijana, Lumumba, Dar es Salaam ambalo sasa "vijana" wa chama kinachoheshimu na kulinda mafisadi (CCM) wameuza kwa pesa mbili.

Pointi: Kadi ni mali yangu. Rudi Darasa la Kwanza miaka yetu. Mwalimu anaanza kutufundisha Kiingereza: This is my book. It is my book. It is mine. 

Sasa rudi kwenye kadi: This is my TYL card . It is my card. It is mine. Nikitaka kugawa, naigawa. Nikitaka kutupa, naitupa. Nikitaka kuchoma moto, naichoma. Nikitaka kuuza kwenye mnada, naiuza. Sasa kwanini Dk. Slaa asibaki na kadi yake na hata nyingine zozote atakazoweza kuwa nazo (sasa na baadaye) hadi pale atakapotaka kuachana nazo?

Bali mjadala wa "Kadi ya Dk. Slaa" una maana pana. Unaonyesha jinsi viongozi wa chama kilichopanga ikulu kwa miaka 51 wanavyoweza kuacha hoja kuu za kufikirisha mtu binafsi na jamii; na badala yake kujiviringisha na kuviringisha wananchi katika malumbano dhaifu (triviality) ili kupoteza muda na kuondoa akili zao kwenye hoja kuu za wakati tuliomo. Ndiyo, ni ndoana. Lakini nani ataimeza wakati anajua ni ndoana?

ndimara