Sunday, September 9, 2012

Kiatu cha John Tendwa kinapwaya


Polisi, mauaji, polisi, mauaji

Na Ndimara Tegambwage
SITAKI John Tendwa. Amenukuliwa akisema kuwa polisi kuua raia ni jambo la kawaida. Swali linakuja: Kwa hiyo?

Wengi tunajiuliza: Kwa hiyo nini? Kwa hiyo polisi wa Tanzania waue tu? Kwa hiyo waige au waendelee kuua? Kwa hiyo liwe taifa la polisi kuua raia tu badala ya polisi kulinda raia na mali zao? 

Tendwa alinukuliwa akisema hayo Ijumaa usiku katika kipindi cha “Kiti Moto” kupitia kituo cha televisheni cha ITV. 

Kauli ya Tendwa inatokana na utetezi wake wa kile kinachofanyika nchini: Mauaji ya wananchi yanayofanywa na polisi. Wanamjadala wenzake walimpa mifano mingi ambako polisi wameua raia.

Katika mjadala huo, Tanzania ilitajwa kuwa miongoni mwa nchi nne zenye idadi kubwa ya wananchi waliouawa na polisi.

Ikatajwa kuwa polisi wa Tanzania hawana hata chombo cha kuwaangalia au kuchunga mwenendo wao. 

Ikaelezwa kuwa polisi wa Tanzania wakiua wanaunda tume yao kuchunguza mauaji waliyofanya na kumalizia kwa kunyamaza au kuhalalisha mauaji.

Ni hapo Tendwa alipopakua kilichokuwa rohoni mwake kwa kusema mbona hata katika nchi nyingine polisi wanaua wananchi.

Haihitaji akili ya nyongeza kuona kuwa Tendwa anatetea mauaji. Anatetea udhalimu. Anahalalisha mateso na vifo. Anafurahia tendo la polisi kuua.

Tusema tu hapa kuwa kuna baadhi ya askari polisi wanaochukia mauaji. Wapo! Nimeongea nao. Sasa Tendwa anatetea nani?

Jana niliongea na baadhi ya maofisa wa ngazi ya juu katika jeshi la polisi kuwauliza iwapo Tendwa alikuwa anaongea kwa niaba ya jeshi la polisi au alitumwa kufanya hivyo. Wote wanne wakasema hawezi kutumwa kitu kama hicho.

Siyo kweli basi kwamba msajili wa vyama aliishiwa msamiati ndipo akasema aliyosema. Siyo kweli kwamba alipitiwa. Siyo kweli kwamba alikuwa amechoka. Hapana! 

Kauli ya Tendwa ndiyo “mlo” aliokuwa ameandalia wasikilizaji wake katika kipindi cha Kiti Moto. Ndiyo mvinyo aliyotaka isindikize kauli zake nyingine. Kama sivyo, aliingizaje hili la hata katika nchi nyingine polisi huua wananchi?

Mfano wa mauaji wa hivi karibuni ni ule wa Mufindi, Iringa ambako mwandishi wa televisheni Daudi Mwangosi alilipuliwa kwa bomu akiwa mikononi mwa polisi.

Niliwahi kuandika kuwa sitaki John Tendwa, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kwa sababu nyingi nilizotaja moja wapo ikiwa vitisho kwa vyama vya upinzani na kubeba, katika mbeleko, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Leo simtaki Tendwa kwa kuwa anatetea umwagaji damu. Amevaa kiatu kisicholingana na mguu wake. 

Ni hivi: Tendwa alipewa kiatu. Aliyempa kiatu ni rais. Huyu rais hakumpima. Wala hakumpa kwanza ajaribu. Alimwabia “Vaa hiki hapa!” 

Angalia kiatu chenyewe. Kwa mwonekano ni kizuri. Ni cha gharama kubwa pia. Ni cha heshima. Ni cha kwendea mahali pa wenye hekima. Lakini bahati mbaya saizi ya kiatu hiki ni kubwa mno. 

Tendwa alionekana akivaa kiatu kile, lakini hakika alikuwa anachomeka tu miguu.  Alichomeka. Akavuta. Akavuta, mithili ya mtoto anayeanza kusimama na kutembea huku wazazi wakiimba “…kasimama dede.” Huyooo!

Sasa Tendwa hata kuvuta kiatu kile havuti. Amegundua hakikuwa chake. Matambara na karatasi za kupachika mbele, nyuma na upandeni ili kuimarisha mguu, ama yamekuwa ghali au tendo lenyewe limeleta usumbufu. 

Tendwa sasa anavaa ndala. Hizo ndizo saizi yake. Tatizo ni kwamba pale alipowekwa si mahali pa ndala bali kiatu; tena kiatu kutoka kwa rais.

Sitiari hii inafaa kuelezea jinsi Tendwa alivyoshindwa kufanya kazi yake. Jinsi anavyopwaya katika nafasi hii na jinsi anavyoacha kilichochake na kufanya kisichochake.

Kwa nafasi aliyonayo Tendwa, akionekana anashabikia na hata kufikia hatua ya kutetea walioua; na kuonyesha kuwa hata raia katika nchi nyingine huwa wanauawa na polisi, basi anakuwa ameonyesha mchoko wa aina yake.

Mara chache wateule wa aina yake hujiingiza katika mijadala ya aina hii ambayo inaweza kuchukuliwa kuwa ndio msimamo wa waliowateua. 

Tendwa anafanya yote haya kuhalalisha ubabe wa chama chake. Kila mahali ambapo polisi wanaua, na kama kulikuwa na shughuli ya kisiasa, basi Tendwa atasikika akisema “Nitafuta chama.”

Mara zote ametishia kufuta chama cha siasa. Chama anachotishia kufuta siku zote ni chama cha upinzani. Hawezi kusema lolote kwa CCM. Hawezi kuuma kidole kinachomlisha! Tendwa huyo! 

Haina maana kupendekeza Tendwa afukuzwe kazi. Hatafukuzwa. Haina maana kumwambia ajiuzulu. Hatajiuzulu.

Haina maana kumwambia Tendwa aombe radhi kwa wananchi. Hataomba maana huenda asielewe vilevile kile alichofanya anachostahili kuombea radhi. 

Kitu kimoja ni wazi. Marais wetu watakumbukwa, pamoja na mambo mengine, kwa kuweka watu wasio na uwezo madarakani na wakadumu humo kwa kupakatwa hata walipothibitika kupwaya, kunyauka na kupauka.

Kwani kwa kauli ya Tendwa, na kwa serikali inayojali na kuthamini haki na utu wa watu wake, jamaa huyu angevalia ndala zake nje ya ofisi ya umma.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la TanzaniaDaima Jumapili tarehe 9 Septemba 2012)

Tuesday, September 4, 2012

ITIKA WA DAUDI MWANGOSI


Masalia ya Daudi Mwangosi



ITIKA HAITIKI

Itika haitiki
Hakuna anayemwita.
Naye Itika haitwi
Aliyemwita hayupo.

Jinale watoto hawajui
Wao siku zote waita "mama"  
Mwenye Itika haitiki
Aliyemwita kabaki vipande.

Itika aliitwa na Daudi
Yule Daudi wa Mwangosi
"Mke" au mama fulani
Kinywani hayakutoka
Itika lilinoga mdomoni
Itika lilikuwa jina
Lakini pia lilikuwa wito
Na Itika na Daudi
Waligwaya kwa vicheko.

Mume kabaki masalia
Yule aliyemwita Itika.
Itika hana cha kuzika
Vidole vitatu na kucha
Na vipande vya miguu?
Pande la baba alobusu
Kwa mbwembwe na madaha
Kila litokapo na kuingia;
Limebaki minofu
Mikononi mwa polisi.

Itika anabumbabumba 
Vitoto vyao vinne
Cha mwisho hakielewi 
Umri umekizonga
Miaka miwili ni kinda
Kingali chafyonza Itika;
Na minofu ya baba
Wadai muhali kuona.

Itika katu haitiki!
Amwitike nani?
Aliyemfungia ngama
Amerudishwa vipande.
Anakabidhiwa furushi
Ni minofu ya mumewe.

Mito na maziwa ya machozi
Ndio kitambulisho cha Itika
Anawaka na kuzimika 
Ukiita haitiki Itika.
Hata kwa mtikiso mnono
Abaki kutetemeka
Alotoka akiwa mtu, 
Akiwa mume
Anarudishwaje minofu?

Vipandevipande kwa chungwa
Hilo halina maswali
Vipandevipande kwa embe
Hilo halina ubishi
Vipandevipande kwa muhogo
Nani atakuuliza 
Vipandevipande kwa mtu -
Kwa Daudi Mwangosi
Itika na mimi hatuelewi.

Wei! Wei! Wei!
Waile minofu yao
Wangu hakuwa minofu
Wangu alikuwa mtu
Wangu alikuwa mume;
Niliyejichagulia
Niliyezaa naye wanne hawa.
Warudishe mume wangu...
Wei! Wei! Wei!

Huulizi swali
Husikii Itika akifoka
Unaona uso ukivimba
Unaona uso ukinyauka
Unaona Itika anatweta
Unaona akibubujikwa machozi
Akikamka jasho
Ghafla ananyauka
Ghafla anaibuka
Ni wewe tu unayeyaona
Kwani Itika haitiki

Ni nini hii?
Ni bahati mbaya nyingine?
Ni bahati mbaya ya makusudi?
Sasa waja na jipya:
Wadai wanafanya uchunguzi
Uchunguzi upi kwa minofu?

Wanachunguza nini?
Kilichomuua mume wa Itika?
Kwani hawakijui
Wanachunguza nani?
Aliyemuua Mwangosi wa Itika?
Kwani hawamfahamu
Kwani hawakumuona
Kwani hawakuwepo
Wanamtania nani
Katikati ya majonzi?

Wauawe wangapi…?
Nauliza wangapi ndipo tunune?
Ndipo tuchukie
Ndipo Itika asikike
Yeye na maelfu wengine
Tukilaani bunduki walizobeba
Tukilaani waliowatuma
Tukilaani walioshindwa kazi
Lakini ving’ang’anizi ofisini?

Wauawe wangapi tuape
Tujiapize kuishi
Kuishi…kui...

Woga watakufa kihoro
Jasiri watasonga mbele
Historia inaandikwa
Wa kileleni wasome nyakati.



MWISHO



YA DAUDI MWANGOSI YAENDELEA


 Daudi Mwangosi

Nimeweka makala hii hapa kwa kuwa nimeona mwandishi wa TanzaniaDaima amedonoa vitu vingi kutoka blogu yangu lakini hakukiri kufanya hivyo. Nitaongea na mhariri juu ya hili.



Wanataka tufe kama kuku wa kisasa
TanzaniaDaima, 4 Septemba 2012


Na Mwandishi Wetu

MWANDISHI Daudi Mwangosi ameuawa. Alikuwa kazini katika kijiji cha Nyololo, wilaya ya Mufindi katika mkoa wa Iringa. Ameuawa akiwa mikononi mwa polisi.

Alikuwa akirekodi moja ya matukio muhimu katika maendeleo na mabadiliko ya nchi hii kisiasa na kiuchumi.

Mwangosi amelipuliwa kwa bomu; angalau mpaka sasa ndivyo waandishi walioshuhudia kwa macho na kamera, walivyomudu kutuelezea. Ndivyo pia hali hali ya mwili wake inavyoonyesha.

Amekatikakatika mwili. Amevurugwa mwili mzima. Ni nyama tupu – nyekundu kwa damu – mithili ya mnyama aliyeraruriwa na wenzake katikati ya pori la mawindo.

Kinachoonekana katika picha muhimu ni matumbo nje, vipande vya nyama na vidole vitatu vya mkono wa kushoto alikosukumizwa na kulalia mara ya mwisho.

Picha nyingine inaonyesha akiwa bado anazongwa na askari; akinyang’anywa kamera zake, akisukumwa chini huku mmoja wa askari akilenga kwa makini na karibu sana na mwili wake, “bunduki yenye mdomo mpana.”

Kilichobakia kwa Daudi Mwangosi ni miguu kuanzia chini ya magoti – masalia ya mwandishi wa televisheni na aliyewahi kuwa mwandishi wa muda wa baadhi ya magazeti nchini.

Mwandishi alikuwa akisaka habari. Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilikuwa kinafanya kazi ya kisiasa ya kufungua matawi yake na ofisi yake.

Kuna umuhimu wa waandishi wa habari kuwa katika maeneo haya. Kuona. Kusikia. Kunusa. Kushuhudia kwa makini. Kuandika na kutangaza. Kuweka rekodi ya kilichosemwa na kilichotendeka kwa manufaa ya waliombali na karibu, kwa manufaa ya watafiti, lakini pia kwa kumbukumbu za vizazi vijavyo.

Aliuawa katika mazingira hayo kijijini Nyololo. Maneno yake ya mwisho yaliyonukuliwa na mmoja wa waandishi wa habari ni “…msiniue…msiniue…mimi niko kazini.” Hakika alikuwa kazini. Aliuawa.

Kinachotia moyo ni kwamba baadhi ya waandishi waliokuwa pamoja naye waliendelea kupiga picha. Ndiyo hizi hapa. Waliendelea kuandika. Taarifa ziko magazetini, redioni na katika televisheni.

Mashujaa waandishi walibuni haraka jinsi ya kufanya kazi katika mazingira mapya yaliyoibuliwa na polisi. Mazingira ya vita. Mazingira hatarishi.

Baadhi wamerekodi tukio kwa kutumia kamera zao na wengine kutumia simu za mkononi. Mbona teknolojia itaumbua wengi! (?)

Wamerekodi tukio. Wanatunza tukio. Wanasambaza tukio dunia nzima. Ni kazi takatifu: Tuone. Tuzingatie. Tufikiri. Tutende.

Hivi vita dhidi ya waandishi wa habari vimeanza. Vitaendelea mpaka wapi na mpaka lini? Nani atavikomesha? Nani ana nia ya kuvikomesha kama siyo waandishi wenyewe?

Mazingira yaliyotoa roho ya Mwangosi yamepoteza pia viungo vya miili ya waandishi na wananchi waliokuwa kwenye ofisi za Chadema kushuhudia ufunguzi. Siyo mkutano wa hadhara.

Woga waweza kuua waandishi wote. Ujasiri waweza kusalimisha wengi na kuunda wengi wengine katika taaluma inayokua kwa kasi.

Tuandike. Tuandike. Hata mengine mengi ya Mwangosi ambayo hayajafahamika yatahitajika kuwekwa wazi kwa dunia kuona na kuchukia unyama huu usiomithilika.

Hii ni muhimu hasa tukizingatia ripoti ya mwandishi wetu kutoka Iringa akimnukuu Mkuu wa Polisi Mkoani (RPC), Michael Kamuhanda.

RPC amenukuliwa akisema kuwa …Chadema hawana jeshi wala vifaa vya kupambana na polisi, hivyo wakijaribu kutotii sheria lazima washurutishwe.

Maana ya kauli hiyo ni kwamba mwandishi aliuawa wakati polisi wakipambana na Chadema ambayo wanaelewa fika kuwa haina silaha wala vifaa vyovyote vya kuwawezesha kupambana na jeshi lake.

Mwaka juzi polisi waliua watu watatu Arusha kwenye maandamano ya Chadema. Wote hawakuwa wanachama wa chama hicho.

Juzi mjini Morogoro silaha zao zimerekodiwa kuua mtu mmoja akiwa barazani kwake. Hakuwa mwanachama wa Chadema.

Jumapili hii Daudi Mwangosi ameuawa mikononi mwa polisi wakati akifanya kazi za kampuni yake ya televisheni na wala siyo kutafuta nafasi ya uongozi kisiasa katika Chadema.

Watakufa wangapi ndipo polisi wakemewe? Wafe wangapi ndipo umma ustuke na kusema: Hapana? Nani mwandishi mwingine au wengine wafie mikononi mwa polisi ndipo waandishi wapate maarifa?

Monday, September 3, 2012

POLISI WAUA MWANDISHI WA HABARI


Mwandishi wa habari wa 
Channel Ten TV aliyeuawa mikononi mwa polisi
Jumapili, 2 Septemba 2012. Aliwahi kuandikia 
gazeti la michezo la MSETO, mdogo wake 
MwanaHALISI lililofungiwa na serikali kwa muda 
usiojulikana kuanzia 30 Julai 2012.
1.
 
2.
                                                     David Mwangosi

3.

 Katikati ya watesi wake. Kamera hiyoooo, juu inachukuliwa. Bomba kubwa la bunduki yenye mdomo mpana likielekezwa kwenye tumbo lake.

4.
Masalia ya Daudi Mwangosi 

 5.
 Masalia ya Mwangosi. 
Askari aliyekuwa karibu
 naye alikumbwa na moto wa bomu. 
Amejinyosha pembeni mwa masalia 
yaMwangosi: Atakuwa ana mengiya 
kusimulia; huenda pamoja
na kueleza kuwa alijitahidi kusihi wenzake kuwa
 "...huyo ni mwandishi wa habari ninamfahamu..." 
Nani atamhoji? Waandishi? Serikali? Lini?


Nani anaweza kumtambua Mwangosi hapo juu baada ya kulipuliwa kwa bomu tena mikononi mwa polisi, kijijini Nyololo, Mufindi mkoani Iringa, Jumapili tarehe 2 Septemba 2012?

Waandishi wa habari na wapigapicha waliochukua picha hizi na kuzisambaza, hakika wanastahili heshima inayolingana na kazi waliyofanya. 

Kutoa picha hizi hadharani siyo kuvunja maadili. Hapana! Kutumia neno "maadili" katika hili ni kuotesha kichaka au  kujenga andaki ambamo wahusika wanataka kuficha ukatili, unyama na kila uchafu ili wananchi na dunia nzima wasiweze kujua na kuchukua hatua. 

Naomba vyombo vya habari - hasa magazeti na televisheni - vitoe picha hizi ambazo haziumizi hata wazazi wa Daudi au mke wake na watoto; bali zinaonyesha unyama usiomithilika uliotendwa na wanaodaiwa kuwa "walinzi wa raia na mali zao."
  
Lengo la kuua kwa njia hii ni:

1. Kupandikiza woga miongoni 
mwa waandishi wa habari. 

2. Kutumia woga huo kugawa waandishi 
- huku wakikaa wanaodai wanataka 
"amani" na kule wakikaa wanaosema 
"tutaendelea kurekodi matukio kwa 
usahihi" na kuyapa tafsiri mwafaka.  

 3. Kupanda mbegu ya woga miongoni 
mwa umma kwamba vita vyaja na hivyo
wakae kama kuku wa "kisasa" - mabroila - 
wachinjwao bila kutoa purukushani 
wala mlio wa kujipigania.

Leo, gazeti la TanzaniaDaima lilichapisha makala yangu iliyokuwa itoke jana, Jumapili katika safu ya SITAKI hata kabla ya kujua kuwa Daudi Mwangosi angeuawa. Mhariri anasema hawakuipata mapema na ndiyo maana ameamua kuitoa leo. Isome:

 
Polisi, ukombozi na ‘bahati mbaya’

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI polisi wazuie maandamano na mikutano ya vyama vya upinzani. Sitaki wazuie maandamano ya vyama. Sitaki wapige na kujeruhi waandamanaji. Sitaki waue wanaoandamana.

Jirani yangu hapa ananiambia, “…wanaua kwa bahati mbaya. Siyo kwa kukusudia.” Nakataa. Polisi wenyewe wanakataa.

Huwezi kuzuia maandamano kwa bahati mbaya. Huwezi kuswaga wananchi kwa kiboko kwa bahati mbaya. Hapana! Huwezi kupiga wananchi mabomu ya machozi kwa bahati mbaya.

Huwezi kufyatua risasi ya plastiki katikati ya wananchi waandamanaji wasio na silaha kwa bahati mbaya. Nasema huwezi! Huwezi kutwanga risasi ya moto katikati ya umati kwa bahati mbaya.

Huwezi kuendeleza vitisho kwa wananchi, viongozi wao na vyama vyao kwa bahati mbaya. Huwezi kujiapiza, kwa bahati mbaya, kuvuruga mikutano ya vyama vya siasa.

Huwezi kufinyanga na kuvaa sura ya ukatili wakati wa kubugudhi wananchi halafu ukasema ni bahati mbaya. Hapana.

Huwezi kutumwa, ukatii, ukafinyanga na kuvaa sura ya ukatili; ukashika silaha, ukafyatua risasi katikati ya waandamaji – iwe ya plastiki au ya moto – halafu ukasema ni bahati mbaya.

Nasema yote haya kwa kuwa polisi ni chombo cha serikali. Katika demokrasi, serikali huja na kuondoka. Leo kuna serikali hii. Kesho kuna serikali ile. Keshokutwa kuna serikali nyingine.

Hata katika udikiteta, serikali huja na kuondoka. Ama lidikiteta kuu litapinduliwa kwa mabavu kama linavyotawala, litazeeka, litalewa na kusambaratika akili na wenzake watachukua au litakufa.

Kwa vyovyote itakavyokuwa, jeshi la polisi linabaki la serikali iliyoko madarakani. Hii ndiyo maana askari polisi hupaswa kuwa; na hasa kubaki waandilifu.

Hii ndiyo maana polisi wakaitwa walinzi wa raia na mali zao. Hii ndiyo sababu baadhi ya wananchi hujitolea kufanya kazi ya polisi – ulizi – wakati baadhi ya polisi wamelala na kukoroma.

Mlinzi wa raia hafanyi mambo kwa bahati mbaya. Mlinzi wa mali za raia haongozwi na bahati mbaya. Kukubali upolisi ni kukubali bahati nzuri ya kulinda raia na mali zao. Bahati mbaya inatoka wapi?

Upolisi unaingiliwa na wanaotaka kulindwa kuliko wengine. Wanaotaka kuiba haki za wengine. Wanaotaka kupora mali za wengine. Wanaotaka kuneemeka zaidi kuliko wengine.

Hapa ndipo upolisi unapochafuliwa. Ni hapa panapozaliwa kinachoitwa bahati mbaya. Sasa tukubali kwamba “bahati mbaya” ni moja ya kazi ya polisi.

Tunajadili haya kwa kuwa Tanzania imo katika hatua muhimu ya mabadiliko. Kuna vyama vya siasa vinapambana kuhakikisha utawala uliodumu kwa miaka 50 unapisha akili mpya na mipango mipya.

Akili iliyogota haikukwamisha elimu peke yake; biashara peke yake; usafiri peke yake, tiba peke yake; ilikwamisha pia mafao kwa wananchi wakiwamo polisi.

Mafao ya jamii ni mengi – siyo mishahara peke yake. Ukosefu wa mipango inayohakikisha kwamba mtumishi wa kima cha chini anastahili kuishi hata baada ya kustaafu, ni mipango ya kwenda kuzimu.

Ukosefu wa mipango na taratibu za kukuza kilimo cha mkulima mdogo – kwa ushindani tu wa kununua mazao yake ili achocheke kuongeza eneo, kutumia mbegu bora, mbolea na mbinu za kisasa ili aweze kupata zaidi na kuuza zaidi – ni kuita kifo kije haraka.

Mipango ya kufuga wananchi kama kuku wapumbavu aina ya broila; kwa kuwazuia kusema au kuzima nyenzo zao za mawasiliano na hivyo kunyamazisha umma na kuziba mifereji yake ya fikra, ni kuandaa jahanamu kwa waliohai.

Kushiriki, kuruhusu au kufumbia macho wizi, uporaji, ufisidi fedha na raslimali za umma na halafu kukaa kimya na kupakatana na wezi na mafisadi, huku ukijiita mtawala; siyo tu kudharau akili ya umma uliohai, bali pia ni kuangamiza umma huo.

Wanapotokea wenye hoja mpya, sera mpya, muono mpya – wakitafuta mabadiliko katika utawala wa siasa, uchumi na utamaduni wa wengi waliopoteza matumaini zamani – inatoka wapi “bahati mbaya” ya polisi kuwapiga?

Au ni bahati mbaya kwamba polisi wametumwa au wameamrishwa na wakubwa zao, kwenda kuzima nyota iliyoanza kutoa nuru kwa jamii iliyoishi gizani kwa miaka nendarudi?

Iko wapi bahati mbaya isoyoona umuhimu wa mabadiliko, tena kwa njia bora ya majadiliano na umma?

Nani asiyeona umuhimu wa wananchi kufikia hatua wakasema, tena katika mazingira ya amani: nataka huyu aniongoze na sitaki yule anitawale?

Inatoka wapi bahati mbaya ya kuzima matumaini ya umma? Polisi, acheni wananchi watafute ukombozi wao na wenu pia.

0713 614872