Saturday, June 30, 2012

 
Kilichoko mahakamani
kinazungumzika, kinaandikika
 
Ndugu zangu, 
 
Nimekuwa nikieleza na hata kuelekeza, tofauti na baadhi ya wenzangu katika uandishi, kwamba jambo lililoko mahakamani linaweza kuandikwa. Kwa nini? 

1. Kwamba jambo liko mahakamani, hakuzuii mambo mengine kutendeka juu ya hilohilo na nje ya mahakama. Dunia haisimami kwa kuwa jambo liko mahakamani. Mwenendo wa kilichosababisha kuwa mahakamani hausiti au kufutika eti kwa kuwa tayari kuna shauri mahakamani. Hamu na haki ya kujua haviondoki eti kwa kuwa jambo liko mahakamani. Hapana!

2. Sheria haikuzuii na hasa haipaswi kukuzuia kuandika mlolongo wa matukio nje ya mahakama unaohusu watu wenye shauri lililoko mahakamani. Matukio nje ya mahakama yaweza kutoa nuru zaidi juu ya wahusika katika shauri na hata juu ya shauri lenyewe. Taarifa juu ya matukio haya zaweza kuwa za msaada kwa wakili wa utetezi na wakili wa upande wa mashitaka. Wakati zinaweza kumpa mmoja nuru zaidi juu ya kilichotendeka, zaweza pia kumpa mwingine nuru juu ya kujenga ngome.

3. Hakimu au Jaji anahitaji hoja mshibano na ushahidi mwanana. Uamuzi wake haupaswi kuongozwa au kutawaliwa au kufungwa na taarifa za magazeti, redio, televisheni au chombo chochote kile cha kutoa taarifa au habari. Umadhubuti wa hakimu au jaji; hekima, uaminifu wake kwake binafsi na kwa kazi yake juu ya kesi iliyoko mbele yake, havipaswi kupanguliwa na taarifa za nje ya hoja zilizoko mahakamani kwa madai kuwa "zimeathiri maamuzi." 

4. Tuna ushahidi ambako baadhi ya mahakimu na majaji madhubuti wamepuuza na kutupilia mbali madai ya kuathiriwa na vyombo vya habari wakiuliza, "Una uhakika na unaamini kuwa mimi siwezi kufanya kazi hii; siwezi kuwa na maoni na siwezi kuona haki mpaka niambiwe na vyombo vya habari?"

5. Hili lina maana kwamba kupogoka; kuangalia sheria kwa makengengeza na hata kutoa upendeleo wa waziwazi na uliofichika, ni shabaha, tena ya makusudi, ya hakimu au jaji na siyo kuathiriwa na taarifa za chombo cha habari.

6. Twende kwa serikali. Taarifa ya serikali ambayo iliahidiwa; kama ingekuwepo, isingeingilia shauri lililoko mahakamani. Haikuwepo au kuna kilichoingia katikati na kusababisha wasiitoe, ambacho ni wao pekee wanaokijua. Kwamba serikali haitatoa taarifa kwa kuwa imegundua shauri lake na madaktari liko mahakamani, ni sababu ya kizembe mno kutolewa na mamlaka. Na kama serikali inaweza kusahau ilichofanya juzi tu, basi hii ni barua kwa umma ya kuomba kuaga ikulu.

7. Sheria haizuii wala kufunga, kwa mfano serikali, kutoka na taarifa inayosema: "Tumepata fedha za kutosha. Sasa madaktari watalipwa nusu ya wanachodai. Hapa tutapata pa kupumulia na kuendelea na majadiliano." Sheria ipi itazuia hili. Sheria yaweza kununa iwapo serikali itatoka na kusema, "Mtakoma. Msimamo wetu ni uleule, liwalo na aliwe!"

8. Hili halikubaliki mbele ya hekima, achilia mbali mahakama. Huwezi kwenda mahakamani kuomba nafuu; ukarudi kesho yake kukaza nguvu ya amri ya kukupa nafuu; na kesho yake ukatoka kifua mbele, kwa kutumia nafuu ileile, kuwakomalia wale uliozuia, na isivyo haki, lakini ilivyo halali kisheria. Utakuwa umetumia nguvu ya mahakama kujinufaisha binafsi na utakuwa unajigamba kana kwamba umeweka "mahakama mfukoni."

9. Inawezekana serikali "imegundua kweli" kuwa inakwenda kufanya madudu. Ikaacha kutoa taarifa. Imejichanganya kwa kuwa imechanganyikiwa.

(Andishi hili lilitawanywa kwa wana-mabadiliko katika google proup, Alhamisi 28 Juni 2012. Ni sehemu ya mjadala uliohusu kushindwa kwa serikali kutoa taarifa iliyoahidi kutoa bungeni juu ya mgomo wa madaktari. Spika wa bunge Anne Makinda alisema serikali haitatoa tamko kwa kuwa kuna shauri mahakamani).

Wednesday, June 20, 2012


 
Nani dhaifu: Rais au Mnyika?

On Tue, 6/19/12, Mohamedi Mtoi <mouddymtoi@gmail.com> wrote:
From: Mohamedi Mtoi <mouddymtoi@gmail.com
Subject: Re: [Mabadiliko ] Mnyika katolewa Bungeni?
To: mabadilikotanzania@googlegroups.com
Date: Tuesday, June 19, 2012, 12:12 PM

Mnyika amekisema kile kinachosemwa na baadhi ya wananchi wenye ujasiri. Tofauti yake na yetu ni kwamba yeye kasemea bungeni, sisi tunasemea vijiweni tukinywa kahawa. Kama hivi sivyo basi Mnyika ndio mdhaifu kwa kutoa kauli kame bila kuichuja.

1. Kama udhaifu ni kutokujua kwa nini wananchi wako ni maskini wakati wako nchi tajiri, Mnyika yuko sahihi.

2. Kama huwezi kumuwajibisha au  kuona madudu ya katibu mkuu au katibu kiongozi mpaka bunge lishikilie bango na kushinikiza wang'oke ndio uzinduke kufanya maamuzi, basi Mnyika yuko sahihi.

3. Kama kweli watu wameliibia taifa kupitia dili za magumashi halafu una watangazia warejeshe fedha ili wasichukuliwe hatua; na wakati huohuo vibaka wanauawa au kuchomwa moto kwa kuiba kuku na simu, basi ni dhahiri kuna udhaifu wa kiuongozi, Mnyika yuko sahihi.

4. Kama ndege inaingia kwenye anga ya nchi yako na kubeba wanyama kupeleka Arabuni bila hatua zozote kuchukuliwa, ni dhahiri kuna udhaifu wa kimfumo uliokubuhu serikalini; Mnyika yuko sahihi.

5. Kama rais anafunga safari kwenda kuomba misaada na wakati huohuo misaada anayopewa hailingani thamani na raslimali zinazovunwa kwenye nchi yake; basi Mnyika yuko sahihi.

6. Kama rais anadiriki kutoa ahadi 99 ambazo thamani yake ni zaidi ya trilioni 9 huku akijua kuwa hazitekelezeki, ni hadaa kwa wananchi, chama na serikali. Hapa Mnyika yuko sahihi.

7. Kama taasisi ya ikulu na mfumo wake wa utawala umehusika kuingilia maamuzi ya mhimili wa haki kwa kutoa hukumu ya upendeleo ili kumkomoa au kumnyang'anya mbunge wadhifa, kama ilivyolalamikiwa; Mnyika yuko sahihi.

8. Kama serikali inatenga 70% kwa matumizi kwenye bajeti yake na 30% kwenye maendeleo; ni dhahiri kuwa ni aina ya serikali dhaifu yenye viongozi wavivu wa kufikiri.

Kama hivyo ndivyo, nasimama na kijana mwenzangu kwa ukakamavu na kupaza sauti yenye mwale mkali. Namuunga mkono Mnyika.

(Nimevutiwa na blogging ya aina hii. Nimeichomoa kwenye mtandao na kuipa hadhi yake kwwa kuiweka hapa. Kazi hii siyo ya kijana kwa umri, bali kijana wa akili, fikra...) ndimara.

NB: Sikuomba idhini kwa Mtoi.

Tuesday, June 19, 2012


Kila mwaka? Kama ndivyo, basi!
             
Na Ndimara Tegambwage

SASA bia wanywe wao. Soda wanywe wao. Sigara wavute wao. Sisi basi. Ebo!

Hivi hapa ndipo mahali pekee ambako serikali inaweza kupata fedha za bajeti?

Twende kwenye bia. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei ya bia. Ili watu wengi waweze kunywa au watu walewale waweze kunywa bia nyingi.

Ili kampuni ziweze kutengeneza bia nyingi. Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?

Twende kwenye soda. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei ya soda. Ili watu wengi waweze kunywa au watu walewale waweze kunywa soda nyingi.

Ili kampuni ziweze kutengeneza soda nyingi. Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?

Twende kwenye sigara. Kama serikali inajali, kwanini isiteremshe bei ya sigara. Ili watu wengi waweze kuvuta au watu walewale waweze kuvuta sigara nyingi.

Ili kampuni ziweze kutengeneza sigara nyingi. Ili kampuni zipate mapato makubwa. Ili kampuni ziweze kulipa kodi kubwa. Ili serikali iweze kunufaika kwa kodi kubwa. Kwanini?

Sasa wanywaji hawana hamu tena! Ama serikali inywewe bia; inywe soda na ivute sigara. Au wavitumie wanaovitengeneza.

Huo hapo juu waweza kuonekana kama muweweseko wa wanywaji soda, bia na wavuta sigara; bila kujua uchumi wa uzalishaji na masoko. Lakini kwa viwango vyovyote vile, kuna mantiki.

Ukitokea mgomo wa “kunywa” na “kuvuta,” mwezi wa sita wa mwaka wowote ule, nchi ikiwa chini ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), bajeti haitasomwa kamwe. Haitakamilika.

Kila mwaka ni bia, soda na sigara; hadi wenye viwanda wakaonya kwamba mwaka huu wakipandishiwa kodi zaidi ya asilimia 10, hawataielewa serikali.

Kujaribu kuonyesha “ubunifu,” serikali imekuja na pendekezo la wanaotaka usajili wa magari kwa utambulisho wa taarifa za mtu binafsi – majina, labda na picha na chochote kile – kulipa Sh. 5 milioni kwa miaka mitatu.

Ni yaleyale ya bia, soda na sigara. Serikali inasema itakusanya Sh. 50 milioni katika miaka mitato; kwa kutoza Sh. 5 milioni kwa atakayetaka urembo.

Hii ina maana serikali imelenga watu 10 tu. Wakilipa milioni 50 kila mmoja, serikali itakuwa imeridhika. Masikini!

Kama serikali inahitaji fedha kwa njia hii, kwanini isitoze Sh. 200,000 kwa mwaka kwa gari kwa maelfu ya magari ya vijana wanaotaka mbwembwe? Itapata zaidi.

Ukiangalia orodha ya magari binafsi yaliyosajiliwa hadi sasa katika mfumo mpya, utaona yametoka AAA hadi CAG. Haya ni maelfu ya magari. Serikali haitaki wanaoyamiliki washiriki.

Kinachoonekana hapa ni kwamba, watunga bajeti wanataka watu wachache (10), na huenda mafisadi wachafu zaidi, wapate nafasi ya kujitambulisha kwa mbwembwe.

Kwamba wezi wakubwa, wenye mabilioni ya shilingi ya kusambaza; mabilioni waliyopora umma wa nchi hii; wapate nafasi ya kuwakoga wananchi na kuonyesha kwamba wao ni tofauti.

Kwamba mafisadi walioshindikana, sasa wapate nafasi ya kurudi upya katika umma, kwa kuutisha, kuushangaza, kuukoga na kuudhalilisha kwa fedha walizowaibia.

Lakini, hata kama kiwango kisingekuwa Sh. 5 milioni, au laki mbili; wazo lenyewe la mikogo, katikati ya umasikini unaoandama wananchi, hakika ni la kibwege sana.

Aliyetoa wazo hilo barazani na “wataalam” walioliunga mkono ili kupata Sh. 50 milioni, wamedhihirisha uchovu mchafu.

Hiki ni kiasi ambacho serikali inaweza kupata katika siku nne tu kutokana na faini kwa makosa ya barabarani katika jiji la Dar es Salaam peke yake!

Serikali yaweza kupata kiasi hiki katika wiki moja au siku saba, kwa kusimamia kwa makini, ukusanyaji kodi kwenye masoko.

Fedha zinazohitajika ili kukidhi mbwembwe za kifisadi, zinaweza kupatikana – tena mara kumi au ishirini au zaidi – kwa siku moja tu, kwa kufuta wilaya moja iliyoundwa kisiasa na isiyo na manufaa kiuchumi kwa wananchi.

Watunga bajeti hawaoni wezi wanaokwapua madini kweupe. Hawaoni mafisadi wenye kodi za wananchi kwenye akaunti zao Ulaya. Hawaoni mabomba yanayovujisha mabilioni ya shilingi kwa njia ya mishahara hewa.

Hawaoni! Hawaoni safari za ndani na nje za watawala zinazokausha hazina na madarasa ya Ngurdoto yanayokamua walipakodi. Hawaoni dege la serikali lilalo mafuta kama ibilisi. Hawaoni!

Hoja ni hii. Kuna muda mwingi na mrefu wa kuandaa bajeti. Kitendo cha kuonekana serikali inakwanyiakwanyia – shika hili shika lile – dakika za mwisho, ni ushahidi watawala wanaishi kama wapitanjia.

Na mpitanjia hajengi.
0713 614872






Thursday, June 14, 2012


Walimu wabomoa chungu cha ujinga


Na Ndimara Tegambwage

SASA unaweza kusoma Sayansi kwa Kiswahili. Kikwazo cha lugha ya kigeni kimeanza kuondolewa. Chungu cha ujinga kimebomoka.

Walimu na wadau wengine, wamefanikisha uchapishaji wa kitabu cha somo la Kemia kwa Kidato cha I.

Kitabu kinaitwa: Furahia Kemia/Enjoy Chemistry Kwa wanaoanza kujifunza/A textbook for beginners. Kimechapwa mwaka 2011.

Fungua kitabu. Kushoto ni Kiswahili, kulia ni Kiingereza. Kimesheheni maarifa, maelekezo na michoro ya vifaa vya kufanyia mazoezi. Ni sayansi.

Waandishi wanaelekeza: “Soma sentensi, kifungu cha maneno au mada nzima kwa Kiingereza. Pale tu unapoona kwamba huelewi kila kitu ndiyo usome sentensi, kifungu cha maneno au mada hiyo kwa Kiswahili.”

Hapa waandishi wamejikita katika maana na uelewa. Kama hukuelewa, au hukuelewa vizuri kile ulichosoma, basi unageukia lugha nyingine.

Inaelekezwa mwanafunzi asome kwanza Kiingereza. Akielewa, basi aendelee. Asipoelewa, apate msaada wa Kiswahili. Kwa msingi huo, kitabu kinafundisha Kiingereza kwa msaada wa Kiswahili.

Furahia Kemia hakiondoi umuhimu wa kuwa na vitabu vya kiada vya sayansi vilivyoandikwa kwa Kiswahili moja kwa moja – lugha ya mwalimu na mwanafunzi nchini – bali ni moja ya njia za kufikia huko.

Angalia mbele – miaka minne ya kuchapisha vitabu vingine kwa ajili ya vidato vingine na kwa masomo mengine ya sayansi. Kutakuwa na tofauti.

Iko wapi basi, sababu ya kutokuwa na msimamo katika matumizi ya lugha ambayo wote – walimu na wanafunzi – watakuwa wanaelewa vizuri; huku wakijifunza lugha nyingine zozote watakazo?

Ibrahim Kipepe wa MwanaHALISI amehoji wanafunzi jijini Dar es Salaam juu ya kitabu hiki. Rosemary Kelvin wa sekondari ya Zanaki anasema, “Kitatusaidia sana sisi ambao hatukutokea shule za Kiingereza.”

Janeth Julius (Zanaki) anasema, “Wanafunzi watapata msamiati muhimu unaotokea kwenye mitihani.”

Ramadhani Mohamed wa sekondari ya Makoza, Tabata anasema, “Tunaosoma shule za Kata, tutanufaika zaidi kutokana na mafundisho ya sasa kutokidhi uelewa wa masomo.”

Eric Bayona wa sekondari ya Migombani, Segerea, “Kitabu kinaweza kuchanganya wanafunzi ambao wataegemea kwenye Kiswahili na hatimaye mitihani ikaja kwa Kiingereza.”

Bakari Salum wa sekondari ya Tambaza anasema, kitabu hiki kilicho madukani sasa, “Kitaleta ongezeko la wanaofaulu kwa vile wengi watakuwa na uelewa mpana.”

Hussein Juma wa sekondari ya Ananasif anasema, “Unajua tumefundishwa kwa Kiswahili hadi darasa la saba. Hatujui kusoma wala kuandika Kiingereza. Hiki kitakuwa mkombozi.”

Naye Justina Kakuru aliyemaliza Kidato cha IV miaka mitatu iliyopita anasema, “Ningepata msingi kama huu, ningesoma sayansi.”

Furahia Kemia kimechapishwa na kampuni ya Mkuki na Nyota Publishers ya Dar es Salaam kwa udhamini wa HakiElimu – asasi ya kijamii nchini inayopigania uwazi, haki ya kupata elimu bora na demokrasi; na asasi nyingine ya Faire Welt Rastatt e. V.

Hata katika mazingira ya uchumi huria, kitabu hiki ni mkuki kwa mikonga ya kibeberu ya uchapishaji, ambamo kwa miaka mingi, watawala wamenaswa na kukataa kuamua juu la lugha ipi itumike kuvuna elimu na maarifa.

0713 614872


MCT works with gov’t, Mukajanga tells US diplomat

Wednesday, 30 May 2012 15:09
The Media Council of Tanzania (MCT) is pursuing a non confrontational approach and works closely with the government, the Executive Secretary of the Council, Kajubi Mukajanga, said on May 30, 2012.
Briefing the Public Affairs Officer of the Embassy of the United States of America in Tanzania, Dana Banks, on the Council’s activities, Mukajanga said MCT is taking this approach as it is pointless to be confrontational as long as it does not yield positive results.
Mukajanga narrated to the US embassy official on May 30, 2012 the historical background of the Council which began to operate in earnest in 1997.
The Council was established by media stakeholders in 1995 as pre-emptive measure to stem the government’s initiative to set a statutory body to rein in errant by media outlets which mushroomed after policy liberalization in early 90’s and committed many transgressions; Mukajanga told the US official who paid a courtesy call on MCT offices.
During the encounter, Mukajanga also clarified on the Council’s position as regards to the new concept of citizen journalism or social media.
Responding to a question by Ms Banks on how the Council’s relates to the emerging development of social media, Mukajanga said the Council is trying to see how it connects with the new development.
“It is scary as most of players in social media are young  people who are always in hurry “, he said adding the best way is to try to connect with them and enlighten them on  best practices in news dissemination.
Ms Banks on her part said that the new development is unavoidable,  citing the changes they ushered in elsewhere.
The Council’s Regulation and Standards Manager,  Pili  Mtambalike, elaborated the Council’s role pointing out that it has  an ethics and arbitration committee which handles  complaints against the media through mediation.
She also said the Council conducts research, has produced professional code of conduct, publishes training manuals on a various media topics and several publications on media issues including two newsletters Media Watch and Barazani as well as  a professional journal  Scribes.
She also spoke of the Council’s campaign to have new legislations on Right to Information and media services
Banks pledged the US embassy’s readiness to support the Council’s activities and offered to provide publications for its Information Resource Centre.
Ends

How does a media Council work with Government? This is a million dollar question. The reader may wish to comment, taking into account circumstances in which MCT wa fought for and won; and principles of an independent, voluntary and non-statutory institutions.
ndi.



Dawasco, Dawasa na Darasa la waziri
·      Ahoji kutoitwa waandishi wa habari?

Na Mwandishi Maalum

JUMAMOSI iliyopita, waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe na naibu wake, Injinia Dk. Binilith Mahenge, waliandaa darasa “gizani.”

Kwenye kikao chao na wafanyakazi na watawala wa DAWASCO na DAWASA, jijini Dar es Salaam, mawaziri hao waligawa maswali kwa wenyeji wao.

Ni kama kusema, “…jibu maswali hayo, turudishie, halafu sisi tutatafuta jinsi ya kufanyia kazi majibu yenu.” Mmoja wa wafanyakazi aliyehudhuria kikao hicho, amekiri kuwepo mazingira hayo.

Dawasco ni Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam na Pwani; na Dawasa ni Mamlaka ya Majisafi na Majitaka.

Kampuni na Mamlaka, vyote vya umma. Vina wafanyakazi “wengi tu.” Vina mfumo wa utawala unaofanana. Vina matumizi kama kampuni nyingine nchini. Vina makazi katika jiji moja – Dar es Salaam. Vinafanya kazi moja – kazi ya maji. Rejea virefu vyake hapo juu.

Waziri na naibu wake walikuwa katika makao makuu ya Dawasco, Gerezani, Dar es Salaam. Walikwenda kukutana na wafanyakazi wa Dawasco, Dawasa na utawala.

Prof. Maghembe aliondoka mapema ili ahudhurie mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwenye viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam. Alimwacha naibu wake amalizie kazi.

Lakini kabla ya kuondoka aligawa, maswali yaliyokuwa yamechapishwa, kwa watawala na wafanyakazi. Wajaze. Wakusanye. Wampe naibu wake.

Lilikuwa darasa la aina yake. Kuombana kalamu. Kuchungulia majibu ya mwenzake. Kumaliza mapema na kumaliza wa mwisho. Kwa neno moja: Mshikemshike.

Mtihani wa waziri ulikwenda kwa njia hii, bila kujali mtiririko wala idadi ya maswali na maneno sisisi yaliyotumika:

1.           Katika miji yote shughuli za maji zinaendeshwa na chombo kimoja. Je, kuna haja ya kuwa na mashirika mawili (Dawasa na Dawasco) Dar es Salaam? Ukisema ndio au hapana, lazima utoe sababu.
2.           Je, kuna matatizo katika menejimenti ya Dawasco? Kama jibu ni ndiyo toa sababu na eleza nani ana matatizo gani na ameshindwa kutatua au kushughulikia matatizo gani?
3.           Je, kuna vitendo vya wizi ndani ya Dawasco? Kama jibu ni ndiyo, taja majina ya wahusika na maeneo yanayohusika.
4.           Makusanyo katika mwaka wa fedha 2010/2011 yalipungua ikilinganishwa na mwaka 2009/2010. Je, ni kwa nini?

Mtihani wa waziri ulikuwa “mtihani wa umma” lakini ulitolewa na kufanyiwa gizani. Hakukuwa na waandishi wa habari.

Ilikuwa baada ya Prof. Maghembe kuondoka, naibu wake Dk. Mahenge alihoji sababu za kutokuwepo waandishi wa habari katika “mkutano mkubwa kama huu.”

Alihoji, kama hakuna matatizo kwa nini hawataki wawepo waandishi wa habari ili waeleze umma?

Kwenye matengenezo ya bomba la maji Wazo na Salasala jijini Dar es Salaam, ambako naibu waziri alihudhuria na watu walikuwa wachache, waandishi wa habari walialikwa.

Waziri alipokwenda kutembelea mitambo ya maji, waandishi wa habari walialikwa. Mtoa taarifa anasema, akimnukuu naibu waziri, “…iweje leo katika mkutano mkubwa hivi wasiitwe ili waeleze umma?”

Bahati nzuri waziri hakuwa anatafuta jibu. Alikuwa akiwasukumia changamoto. Walitazamana tu.

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Arcard Mutalemwa alisoma risala ya mamlaka yake iliyoonyesha kutetea kuwepo kwa “mashirika” mawili (Dawasa na Dawasco) yote yakishughulikia jambo moja katika eneo moja.

Dawasa wanachimba visima. Wana mpango wa kuchimba visima 40. Hadi sasa visima sita (6) vimekamilika na waziri ameombwa kuvifungua.

Taarifa zinasema waziri “amesita kufanya hivyo,” akielekeza kuwa atafungua vikifika visima 20 na iwe kabla ya bunge la bajeti mwaka huu (kesho); jambo ambalo haliwezekani.

Risala ya Dawasco kwa waziri ilisomwa na makamu mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Salim Yusuf wa Mamlaka ya Mapato (TRA). Hii ilisema, pamoja na mambo mengine, kuwa Dawasco “hakuna matatizo.”

Risala ilisema kuna mambo yaliyoandikwa magazetini kuhusu Dawasco. Ilisema yalikuwa ya “kikundi cha watu wachache wenye maslahi binafsi;” na kwamba hilo “tunalifanyia kazi.”

Katika risala yao, Dawasco walilamikia fedha zinazokatwa kwenye mapato yao kwenda Dawasa, kuwa zimekuwa nyingi (zaidi ya asilimia 40); hasa baada ya ongezeko la bei kwa wateja. Wakaomba kiasi hicho kipunguzwe.

Waziri anasema atafanyia kazi majibu ya wafanyakazi. Yaweza kuwa wiki hii au ijayo au wakati wowote “atakapojisikia.”

Lakini ameacha kiwewe Dawasco na Dawasa. Je, nani ana kazi na nani yupoyupo? Nani anaweza kuondolewa na yupi anaweza kubaki? Kwa ufupi, nani atalia na nani atacheka.

Mmoja wa viongozi wa mamlaka hizo za maji, labda katika kuweweseka, alisikika kwenye kikao akisema, yeye ndiye (akitaja cheo chake) na kwamba bado hajasikia vyombo vya habari “vikitangaza mwingine.”

Mfanyakazi wa Dawasa amemwambia mwandishi wa habari hizi kuwa Jumamosi ilikuwa siku ya “kuanza kufikiria mahali pa kukimbilia endapo moja ya taasisi hizo itauawa.”

Mwandishi: Una maoni gani juu ya kuwepo kampuni moja…?

Mfanyakazi: Ukweli ni kwamba kazi za taasisi hizi zinaweza kufanywa na moja tu na kupunguza matumizi.

Mwandishi: Uliandika hivyo katika mtihani wenu?

Mfanyakazi: Hiyo ni siri yangu. Subiri waziri atangaze matokeo (kicheko).

Mwisho