Header Ads

LightBlog

KUMEKUCHA: WANANCHI WATAKA KATIBA MPYA


Waziri Kombani ametukana wananchi





Na Ndimara Tegambwage

CELINA Kombani – Waziri wa Sheria na Katiba, ametukana Watanzania. Hata akiomba radhi hatakubaliwa.

Watanzania wenye nia nzuri wanasema tuwe na Katiba mpya inayoondoa uwezekano wa wananchi kuchinjana pale watakapokuwa wameshindwa kuelewana.

Lakini Kombani anawajibu kuwa Katiba mpya haina maslahi kwa serikali wala taifa. Kwamba serikali haina fedha za kuanzisha mchakato wa kuandika katiba. Kwamba wanaodai katiba hawajampelekea madai yao.

Wenye nia njema kwa taifa lao wanasema kuwepo mkataba mpya (katiba), kati ya watawala na wataliwa; ule unaolingana na matakwa ya sasa; wenye kwenda na wakati tuliomo na siyo wakati wa ukoloni na utawala wa kikiritimba wa chama kimoja.

Lakini waziri Kombani anawajibu kuwa wale wanaodai kuwepo katiba mpya ni watu wa barabarani na wasiokuwa na uelewa juu ya masuala ya katiba na utawala.

Wenye uchungu na nchi hii wanasema kuwepo katiba inayoruhusu kila mmoja kushiriki siasa za nchi yake – kuchagua na kuchaguliwa – na siyo ubaguzi uliowekwa ndani ya andiko kuwa ili uchaguliwe sharti uwe mwanachama wa chama chochote.

Lakini Kombani anasema serikali yake inaridhika na katiba iliyopo na kwamba itaendeleza utaratibu wake kuiwekea viraka kila itakapoona inafaa.

Watanzania wenye shauku ya kuona ustawi wa nchi yao wanasema kuwepo katiba mpya, itakayokuwa mwongozo katika kila kitu ili kuepusha migogoro kwa kujenga misingi ya haki.

Wanasema ukasuku wa “umoja, amani na utulivu” si lolote si chochote, mahali ambapo hakuna katiba inayounganisha fikra za watu wote na kusimamia haki ya kila mmoja.

Lakini Kombani anasema serikali anayotumikia hailazimiki kuwa na katiba mpya kwa vile kuwa na katiba mpya siyo sera ya Chama Cha Mapinduzi.

Ni bahati mbaya kwamba tunatukanwa na mtu mdogo sana aliyeibuliwa mvunguni na kuitwa waziri. Lakini ni bahati mbaya zaidi, kwamba Kombani amemtukana na kumtukanisha Rais Jakaya Kikwete ambaye amempa kazi.

Celina Kombani, kwa kauli zake, andhalilisha umma wa Tanzania; anajenga ghadhabu mioyoni mwa wengi; anaelekeza watu watupe chini matumaini yao; wakate tamaa na kuamua kuishi utumwani milele.

Wenye nia nje na nchi hii wanasema kuwepo tume huru ya uchaguzi. Tume isiyo ya rais. Tume isiyo na madaraka ya kuteua rais, bali yenye majukumu ya kusimamia uchaguzi ili wananchi wapate matokeo ya uchaguzi wao.

Celina anasema, tena kwa jeuri, kuwa hayo hayamo katika ilani ya uchaguzi wa chama chake.

Kipofu huyu; kipofu na siyo asiyeona; hawezi kutambua haki ya wananchi kumrudi mbunge au rais wao. Hawezi kuheshimu uhuru wa wananchi kuchagua watu safi na siyo wezi wakuu na majambazi yaliyokubuhu kwa kuliibia taifa.

Celina Kombani hawezi kuona umuhimu wa fursa kadha wa kadhaa za wananchi kukataa kutawaliwa na wezi ambao wamethibitika kwa ushahidi wa mahakama.

Huyu ni waziri wa sheria anayekataa kuwa na katiba mpya inayotoa fursa zote hizo ambazo zinakuza uhuru wa mtu binafsi; kunawirisha fikra za jamii na kuwapa wananchi madaraka ya kujitawala kwa kusimamia uongozi safi uliochaguliwa.

Kwa jeuri au kutojua, Celina Kombani anasema wanaodai katiba hawajampelekea madai yao.

Kwa akili yake, anaona kuwa ana uwezo wa kushika utumwani taifa hili kama anavyopenda; na hadi atakapoamua kulifungulia.

Waziri huyu anafikiri kuwa mabadiliko ya katiba huanza kama madai ya wastaafu wa iliyokuwa jumuia ya Afrika Mashariki. Anataka orodha. Anadhani ni jambo la binafsi.

Hii ina maana yake. Kwamba akiwa mtawala, Celina hawezi kuona mambo yanayoweza kuleta hatari ya baadaye hadi atakapoandikiwa kwenye karatasi na kukabidhiwa mkononi. Kipofu.

Celina Kombani ametukosea, lakini kuna aliyetukosea zaidi kama taifa. Ni Rais Kikwete. Amemtoa wapi mtu wa aina hii ambaye anajenga mazingira ya mifarakano katika jamii?

Orodha ya watakaoitwa mbele ya mahakama ya kimataifa kueleza kushiriki kwao katika kuleta machafuko nchini Tanzania, sasa inaendelea kukua.

Tulianza na John Chiligati. Wasomaji wa makala zangu wakaleta majina mengine: Yusuf Makamba na John Tendwa.

Mmoja wa wasomaji aliandika kwa ukali. Soma aliyoandika: “Kwa nini humtaji rais? Unamwogopa?”

Sasa Kombani amejiunga na orodha ya wasiopenda nchi yao. Watu wenye shari. Wasiopenda amani. Waliotayari kuona taifa linaagamia alimradi wao wako madarakani.

Hakuna Mkenya awezaye kujivuna sana kwamba ana katiba. Ipi? Iliyokuja baada ya kukatana mapanga; kuuana na kuwa wakimbizi?

Katiba iliyochelewa, inayokuja kuzika, kukausha majeraha na kuandika kumbukumbu za maafa?

Tanzania inahitaji katiba mpya leo. Benjamin Mkapa, rais mstaafu amesikika, ingawa kwa kupitia sauti ya mwingine na katika nchi ya jirani ya Burundi. Amefumbuka.

Ni maneno yake kuwa Katiba ndiyo “moyo wa nchi; moyo wa binadamu unaofanya mwili mzima ufanye kazi.”

Rais Kikwete, Celina Kombani atafanya nini pale kama siyo kukuumbua na kukuletea uadui zaidi na Watanzania wenye nia njema kwa taifa lao?

Tisifike anakotaka Kombani. Waziri binafsi aweza kukimbia; lakini kuna sisi ambao tuliapa hatutatoka hapa, ije mvua lije jua. Kuna umma usiong’oka kwao.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 8 - 14 Desemba 2010)

No comments

Powered by Blogger.