Header Ads

LightBlog

CHILIGATI: WAZIRI HATARI, ANATETEA UBABE, ANAPINGA DEMOKRASI, ANACHOCHEA VURUGU



Chiligati, CCM wanaandaa maafa


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kusikia Rais Jakaya Kikwete akifikiria kumteua John Chiligati kuwa mmoja wa mawaziri au washauri wake wa karibu. Amwache.

Kauli ya Chiligati kuhusiana na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukataa kumsikiliza rais akihutubia Bunge la 10, zinaonyesha ni mtu wa shari asiyemwelewa hata rais ambaye anadai kumtetea.

Mfano Na. 1: Chiligati anasema bunge linaweza kuandaa azimio la kuwaondoa wabunge wa Chadema waliotoka nje ya bunge wakati Rais Kikwete ameanza kuhutubia.

Yaani katibu mwenezi taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – bila woga wala aibu – anajenga hoja ya kula njama ya kufukuza wawakilishi wa wananchi wa chama kingine – Chadema, kutoka bungeni.

Kwamba wabunge wengi wa CCM, ambao hujigamba kuwa wanajua demokrasia; watumike kufukuza wawakilishi wenzao wa chama kingine kwa madai ya kutomsikiliza rais akiongea bungeni.

Chiligati ni hatari. Ana lake jambo. Anajenga woga miongoni mwa wabunge. Anajenga wasiwasi, chuki na uhasama miongoni mwa wananchi. Anafanya uchokozi na kutukana wapigakura.

Katibu mwenezi wa CCM anataka kuzua mtafaruku mchafu, wa aina yake, ambao hauwezi kuishia kwenye kauli tupu na ambao Chiligati na waliomtuma hawawezi kuuzima.

Mfano Na. 2: Chiligati anataka watu wakae kimya. Wasitoe neno. Wasilalamike. Wasikemee. Wasisute. Wasilie. Wasilaani. Wasinune. Wasipinge.

Ukiona kiongozi ana akili ya aina hiyo, ujue ni mbegu ya udikiteta, ukatili, lakini pia ni mtu asiye na chembe ya fikra juu ya matokeo ya kauli na matendo yake.

Asiyetoa kauli ya wazi kutokana na vitisho vya watawala, anajenga hazina ya hasira na chuki. Kauli, hasira na chuki ambavyo havikutoka leo kutokana na ubabe wa watawala, vitatoka kesho lakini kama bomu la maangamizi.

Chiligati hajui hayo au anayajua lakini anayapuuza. Anaongea kwa jazba. Anafoka. Aanaunda bomu la maangamizi.

Msemaji huyo wa CCM anajua kuwa Chadema hawajafanya lolote baya kwa kukataa kumsikiliza rais. Hakuna sheria wala kanuni inayoweza kuwabana wabunge kwa kutomsikiliza rais. Haipo.

Hakuna sheria wala kanuni inayozuia wabunge au hata chama kusema. “…wewe umeniibia kura. Sitambui ulivyopata ushindi.” Haipo!

Chiligati ataleta balaa. Chiligati ataleta maafa. Chiligati anatamka hadharani kuwa wabunge wa Chadema, waliochaguliwa na wananchi, wafukuzwe na wabunge wenzao wa CCM wakishirikiana na wale wa vyama vingine vidogo.

Baadhi ya wananchi na hasa wanachama wa CCM wameanza kuamini kuwa hilo linaweza kutendeka. Haliwezekani! Chiligati anachezea akili za wananchi wapigakura. Ataleta balaa.

Huyu bwana anajaribu kudharau, kuchezea na kusimanga kura za wananchi zipatazo milioni mbili na nusu zilizosema kuwa zimeichoka CCM na zinataka mabadiliko.

Mbona Kikwete mwenyewe anajua haya? Chiligati amekwama wapi? Siyo lazima aseme, lakini Kikwete anajua vema kuwa ana katiba yenye makengeza; inayotumika kuminya uhuru na haki za wananchi.

Mbona anajua kuwa ana katiba na sheria vinavyowazuia wananchi anaotawala kudai haki zao? Hatasema lakini anajua vema kuwa chombo kama vile Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni “mali yake” na chama chake.

Anapokuja mtu wa saizi na viwango vya Chiligati na kusema wabunge wa chama kikuu cha upinzani wafukuzwe bungeni, anamtakia mema Kikwete na utawala wake? Bado anataka kazi?

Itakuwa wapi amani anayohubiri? Utakuwa wapi umoja anaopeperusha midomoni kwake? Utakuwa wapi utulivu anaodai anataka iwapo atatukana na kuvunja uhuru na haki za wapigakura?

Chiligati anaonekana kuwa na tatizo la “kulipua kauli” bila kufikiria matokeo yake. Kwamba anaweza kusema sehemu ya “bunge la CCM” ifukuze sehemu kubwa ya “bunge la upinzani,” ni kutokuwa makini; ni kutumia jazba badala ya fikra ang’avu.

Nani anaweza kusema mtu huyu anamwakilisha rais ambaye angetaka kufikia mwisho wa kipindi chake kwa furaha na hata kupata mahali pa kuishi baada ya urais bila kusumbuliwa?

Nasema Kikwete hakubaliani na Chiligati kwa kuwa huyu Kikwete amekuwa katika nchi nyingi duniani akiwa waziri wa mambo ya nje. Ameona na kushuhudia makubwa zaidi ya kumwacha rais akihutubia.

Kikwete ameona marais wanaotupiwa viatu, mayai viza, mawe, mchanga; wanaosusiwa wanapokwenda kwenye majimbo ya baadhi ya wabunge na wanaopingwa moja kwa moja kwa kauli kali na katili. Kitu gani Chadema kumwacha apumue bila presha!

Na Chadema wana haki ya kuchukia. Walisema hawatambui matokeo yaliyotangazwa na Tume. Hawakwenda kwenye sherehe za matokeo. Hawakwenda kwenye kuapishwa kwa rais. Hawakuwa kwenye kuapishwa kwa waziri mkuu. Na juzi walifunga kazi kwa kutomsikiliza Kikwete.

Basi. Inatosha. Wapigakura wao wamesikia; wanasubiri ufafanuzi tu wakati wa mikutano ya kuwashukuru kwa kuwapa kura ambazo hazijawahi kwenda kwa upinzani.

Wale ambao hawakuwapigia kura nao wamesikia. Wanaoitwa washindi wamesikia. Tume imesikia. Mataifa yamesikia. Kila hatua ina fundo lake. Baada ya hapa wanaanza kazi yao ya uwakilishi.

Hatua zote hizi ambazo Chadema wamechukua, zina maana kwao wakiwa chama; zina maana kisiasa na katika kushamirisha hoja nzito za kuwa na Tume huru ya uchaguzi na katiba mpya inayokidhi matakwa ya sasa.

Anatoka wapi Chiligati kudai kuwa hatua hizi za Chadema ni usaliti? Usaliti upi na kwa nani? Yeye aliwatuma wafanye nini na yeye ni nani kwa chama hiki?

Ni Chiligati anayepandikiza chuki. Hataki kuonwa kama anavyoonekana. Anataka kurembwa kwa marashi, poda na hariri. Azivae basi zionekane nje na ndani ya roho yake. Hana.

Chadema wameonyesha jambo moja kubwa na la kuigwa. Wamekomaa katika kufikiria na kutumia mbinu sahihi kufikisha ujumbe.

Enzi za kuviziana kwa mawe, mchanga na mayai viza zimepitwa na wakati; hasa unapokuwa una uhakika kuwa unachosema ndicho kile ambacho wananchi wengi wanapenda na kusimamia.

Labda kwa kumsaidia Rais Kikwete hapa ni kwamba, hakika watatoka na kuingia, lakini siyo kwa kuibembeleza serikali kutekeleza miradi katika majimbo yao. La hasha!

Wananchi ni walipakodi. Kukataa kupeleka miradi ya maendeleo katika majimbo ya upinzani ni aina nyingine ya rushwa miongoni mwa rushwa kubwa. Ni uhalifu.

Kwa hiyo anayetarajia kupigiwa magoti ili apeleke miradi ya maendeleo katika jimbo la upinzani, ajue anamwita budi kulilia mlangoni mwa chama chake.

Katika mazingira ya sasa, hasa kwa mwamko wa wananchi, acha uchaguzi uje, kiongozi wa namna hiyo atatupwa nje, hata kama amekuwa madarakani mwa miaka 50.

Bali kauli za Chiligati hazinabudi kuogopwa na kukataliwa; njama zake kuvunjwa na yeye kuzomewa. Kwani mbegu yake ikiruhusiwa kumea, ndiyo hatari kuliko hatari zote tulizowahi kutamka nchini.

Chiligati anataka kuua uhuru wetu na haki zetu kama zilivyojitokeza kupitia hatua za Chadema katika wiki mbili hizi. Hatukubaliani na mpango wake; heri ufe mapema.

Bila shaka Chiligati siyo mmoja wa wachapakazi ambao Kikwete anahitaji. Kama ni uchapakazi, basi ni ule wa kuleta maangamizi. Tunayachukia. Tunayakataa.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

MREJESHO: Rais Kikwete hakumchagua Chiligati.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Novemba 2010)

No comments

Powered by Blogger.