Thursday, December 23, 2010

UTETEZI WA LUGHA ZA WATU NA HAKI ZAO



Lugha ya Tume ya Uchaguzi haisikiki










Na Ndimara Tegambwage

SITAKI uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) wa kulazimisha matumizi ya Kiswahili peke yake katika kampeni za uchaguzi mkuu.

Nakumbuka ilikuwa hivyo mwaka 1995 wakati nagombea ubunge jimbo la Muleba Kaskazini. Bado ni hivyo hata leo. Safari hii matumizi ya lugha yamekuwa moja ya masharti ambayo vyama vimelazimishwa kusaini.

Kiswahili ni lugha ya taifa. Ni lugha kuu inayotumiwa na wengi ndani ya soko la ajira – serikali na makampuni yake, shuleni na baadhi ya vyuo; katika biashara za kati, ndogo na katika mawasiliano ya kawaida.

Kiswahili kimeenea mijini – miji mikubwa na midogo na katika baadhi ya vijiji ambako kimetumiwa kwa muda mrefu au wakazi wake wamekuwa na mwingiliano mkubwa na wale wanaozungumza lugha hii.

Kwingineko Kiswahili kimeenezwa na shule za msingi na sekondari ambako walimu na wanafunzi wameathiri matumizi ya lugha za asili, bila kusahau juhudi za makusudi za kupambana na ujinga kwa njia ya Elimu ya Watu Wazima (Kisomo Chenye Manufaa).

Kampeni za kisiasa nazo zimekuwa na mchango mkubwa kwa uenezi wa lugha hii, zikiongezea kwa mipango ya awali, mara baada ya uhuru, ya kusambaza vipeperushi na filamu juu ya matakwa na mbinu za “maendeleo” katika Kiswahili.

Pamoja na yote hayo, bado nchini Tanzania kuna maeneo ambako kuta za lugha za asili zingali imara; na hasa imara sana.

Ni lugha hizi za asili ambazo zimeendelea kuwa chimbuko la misamiati na istilahi mbalimbali kwa matumizi ya sasa ya kukuza Kiswahili na hata kueleza maana halisi ya kile wanachosema wale wanaotumia lugha yao.

Siyo bahati mbaya basi kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuna idara inayoshughulikia lugha za asili. Watafiti katika eneo hili hawafanyi kazi ya “kuzienzi” lugha hizi za asili – iwapo tutaazima vineno vya kisiasa – bali wanavuna maarifa ndani ya lugha hizo na kupitia lugha hizo.

Kuwepo kwa lugha hizo kunakoweza kusaidia kuelewa jamii na utamaduni wake – kwa kudhamiria au kwa utuki tu – kumekuza na kunawirisha Kiswahili na hata lugha nyingine za asili.

Hii ndiyo maana kumekuwa na wanaharakati wa ngeli na ngeli wakitetea kuendelea kuwepo lugha za asili zilizohifadhi hekima na falsafa za jamii ambako zinatumika.

Aidha, ni lugha hizi ambazo watafiti wanaoumba kamusi za Kiswahili na hata lugha nyingine zinazotumika katika maeneo haya, wanakimbilia kupata maneno halisi – hasa istilahi katika ufundi na teknolojia ya kale na sasa.

Hizi basi siyo lugha za kuua hivihivi tu kisiasa. Bado zina nafasi muhimu katika jamii kama vile walivyo watu wanaozitumia; na wanaendelea kuwa Watanzania hata kama hawawezi kuongea Kiswahili.

Sasa Tume ya Uchaguzi inasema wanasiasa wanaotafuta kura katika uchaguzi mkuu wasitumie lugha nyingine yoyote ile isipokuwa Kiswahili.

Maagizo ya tume yanafanana na kanuni za Wizara ya Habari zinazolazimisha kila chombo cha habari kilichosajiliwa nchini, kutumia ama Kiswahili au Kiingereza – lugha mbili peke yake.

Ukichanganya haya ya maeneo mawili, utaona kuwa wasiojua Kiswahili hawapaswi kujua kinachotangazwa redioni au kinachoandikwa kwenye magazeti.

Ni hivi: Kama hawajui lugha hizo – Kiingereza na, au Kiswahili – basi potelea mbali. Ndiyo tafsiri ya kile ambacho Tume inasema na ambacho serikali inasisitiza. Ndivyo wenye vyama walivyoweka saini kutetea.

Anayeomba kura, aingie Usukumani. Maeneo ambako Kiswahili hakitumiki kwa kiwango kikubwa. Pale ambako maneno ya Kiswahili yanatumika kwa ushabiki tu – ama kueleza kuwa anayeyajua ni “mkora” au “mwerevu” kutoka mjini.

Hapa, Tume inataka anayeomba kura atumie Kiswahili. Atatumia. Baada ya hotuba kuna kipindi cha maswali. Hakuna anayeuliza kwa kuwa hakuna aliyeelewa. Kuna haja gani basi ya kufanya kampeni katika “lugha ya kigeni?”

Nendeni Loliondo vijijini, katika mkoa wa Arusha. Kuna shule za msingi. Wanafunzi na walimu wana akili nzuri. Wanajua kuwa Kiswahili na Kiingereza, zote ni lugha za ngeni.

Baadhi ya walimu wanafundisha kwanza kwa Kimasai na baadaye kuweka katika Kiswahili. Njia bora kabisa. Ni kwa misingi sahihi kwamba lugha ya kufundishia iwe ile ambayo mwalimu na mwanafunzi wanaelewa. Mara hii ni Kimasai.

Wazazi katika eneo hili ambao ndio wapigakura, wanajua vema lugha yao moja – Kimasai. Wanaokwenda magulioni mara kwa mara ndio wameokoteza istitahi za kibiashara katika Kiswahili.

Sasa aende mwanasiasa anayetafuta kura. Amwage hapa kampeni yake kwa Kiswahili. Ataondoka kama alivyokwenda. Mtupu. Bila kura hata moja. Kwa nini? Kwa kuwa hawakumwelewa; lakini pia kwa kuwa naye ni mpumbavu – anatumia lugha ambayo anajua vema kuwa anaowaambia hawaijui.

Hili lina tafsiri moja kuu. Kwamba kwa miaka 50 ya utawala wa chama kimoja, watawala wamekuwa wakiimba na kijipiga vifua kuwa wana “lugha ya taifa – Kiswahili.”

Kumbe yamekuwa majigambo yasiyo na mashiko. Wameshindwa kueneza lugha hiyo hapa nchini kama walivyoshindwa kutumia wataalam wake kuigeuza kuwa “bidhaa” ya kuingiza fedha za kigeni.

Wameshindwa kukuza Kiswahili; wameshindwa kukuza lugha za asili; wameshindwa kutoa ajira kwa wanaojua lugha hizo ili wawe wakalimani kwa wasiojua lugha za kigeni; wamebakia na amri – “Tumia Kiswahili!”

Kwa amri na mantiki ya Tume, wasiojua Kiswahili “shauri yao.” Hii siyo haki.

Wananchi wanaojua lugha zao wanastahili kupelekewa kampeni katika lugha zao; na kama njia ya kueneza lugha kuu, wapiga kampeni waombwe kudondosha maneno ya Kiswahili hapa na pale kama kupanda mbegu.

Vinginevyo itafikiriwa kuwa serikali, na vyombo vyake, imeamua kuwatenga, kuwatelekeza, kuwasahau na kuwanyima haki ya kushiriki siasa za nchi yao, wale wote ambao hawajui Kiswahili au Kiingereza.

Sheria, kanuni na taratibu zinazoondoa haki ya mtu; kupoteza utashi wake, tena ndani ya nchi yake, hazistahili kuheshimiwa na haitakuwa mara ya kwanza kukataa kuzishemu.

Njia bora ya kuzipinga ni kuongea na wananchi katika lugha yao. Wananchi ndio watakuwa watetezi.

0713 614872
ndimara@yahoo.com

(Makala hii ilichapishwa Tanzania Daima mwanzoni mwa kampeni za uchaguzi, Agosti 2010)

BAADA YA KUONA WAMEZIDIWA KETE NA UMAARUFU WA DK. WILLIBROD SLAA

Wachovu wa CCM na umbeya wao: MWANZO WA UCHAKACHUAJI

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI wananchi waingizwe kwenye ubishi wa kipuuzi unaopaliliwa na kunawirishwa na wachovu wa siasa.

Wiki hii tumesikia baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakidai kuwa watashitaki Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wamesema watapeleka malalamiko kwa Tume na Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba Chadema imefanya kampeni kabla ya Tume kuruhusu.

Kinachotia kichefuchefu ni baadhi ya wanasiasa upande wa upinzani kuitikia kibwagizo cha CCM na wao kuimba kuwa Chadema na CCM wanaweza “kuchukuliwa hatua.”

Hali iko hivi: Dk. Willibrod Slaa anateuliwa na chama chake kugombea urais. Chama kinaanua kufanya mikutano katika miji mikuu ya mikoa kadhaa. Kinambeba mteule wake. Hii ni kwa sababu kuu mbili:

Kwanza, kumtambulisha kwa wanachama wake na wananchi. Pili, kuendeleza kazi yake ya kisiasa kama chama chochote kile kilichohai.

Chama kilichohai, kikipata fursa, sharti kiitumie kuwafikia majaji wakuu katika taratibu za kidemokrasia; ambao ni wananchi wapigakura.

Chadema haikufanya hivyo juzi tu. Imekuwa ikifanya hivyo kila inapotaka kuwa karibu na wananchi; na wapigakura.

Hivyo ndivyo CCM imefanya. Imetangaza wagombea wake, halafu ikawapeleka kwenye mikutano ya hadhara – kwa wapigakura – ili wanachama wenzao na wananchi wawafahamu.

Chama kingine chenye ushindani ni Chama cha Wananchi CUF. Hiki hakikuwa na kiongozi wa kutambulisha kwani mgombea urais wake mwaka huu, ni Profesa Ibrahim Lipumba ambaye tayari amepigiwa kura za urais mara tatu.

Hata hivyo, CUF muda mfupi baada ya kutangaza mgombea wake, iliweka wazi kwa mgombea, ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho kitaifa, atatembelea mkoa wa Dar es Salaam kwa madhumuni ya “kuangalia uhai wa chama.”

Hiyo nayo ni fursa nyingine kwa chama makini kuwa karibu na wananchi na wanachama wake wakati muhimu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Ukiangalia kwa makini, utaona kuwa kila chama kina njia zake za kufanya kazi za kisiasa – iwe asubuhi, adhuhuri, alasiri, mangharibi au usiku.

Muda huu wa maandalizi ya kuingia kipindi maalum cha kampeni na uchaguzi mkuu, hautawaliwi na pingu za NEC. Ni muda na eneo huru la kuzidisha kazi za kisiasa.

Hasa ni kipindi maalum kwa vyama upande wa upinzani, kutekenya jamii, kuizindua, kuielimisha, kuishawishi na kuiandaa kuachana na ukale ulioizonga na kuipa kilema – kudumaa.

Kwa mfano, kwa upande wa Chadema, ni wakati wa kuendeleza na kuhitimisha kwa nguvu, kazi ya kisiasa inayoitwa “Operesheni Sangara” – iliyovuma na kuvuna nyoyo za wengi – kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu.

Kwa upande wa CUF, ni wakati mzuri wa kuendeleza na kuhitimisha kazi ya kisiasa iliyoitwa “Zinduka” – iliyozindua wengi – kabla ya kuingia katika uchaguzi mkuu.

Kwa hiyo, kinachoipa kiwewe CCM, siyo Chadema “kufanya kampeni” kabla ya muda uliopangwa na Tume, bali umaarufu wa mgombea wa Chadema anapolinganishwa na yule wa chama chao.

Kiwewe kinatokana na mgombea mpya anayefahamu vema serikali na nyendo zake. Anayejua serikali ilivyokwama kwenye tope la ufisadi, ukosefu wa ubunifu; ukame wa mbinu mpya na ahadi tuputupu.

Kelele za CCM zinalenga kufanya mwendelezo wa ghiliba kwa wananchi. Chama hiki, kama ilivyo serikali yake, kina midomo mingi na uwezo wa kupakazia.

Kina vyombo vya habari vya serikali (wanadai ni vya umma), ambavyo vinatawaliwa na makada wake. Humu hupitishwa kampeni na propaganda angamizi.

CCM ina “marafiki” wenye vyombo vya habari ambao huipendelea kwa kila hali kuliko hata gazeti lake la UHURU.

Kwa kutumia midomo yake mingi; laghai wake wengi; ujuzi na uzoefu wa kutunga ghiliba na kupakazia, chama hiki kinaweza kuanzisha mjadala finyu, kikaupa mvumo, ukapandikiza mitafaruku na kupotosha wananchi wengi.

Chama hikihiki kinaweza kutumia kauli za nguvu kuyumbisha watendaji serikalini; kutishia walioko madarakani katika sehemu muhimu kama Tume ya uchaguzi na kuogofya wananchi.

Haitakuwa mara kwanza kwangu kujenga hoja kwamba watawala wetu wamekuwa wakitegemea sana ujinga, woga na umasikini wa wananchi (vilivyosimikwa na chama kinachopanga ikulu), kama mitaji yake mikuu katika juhudi za kubaki madarakani kwa nusu karne sasa.

Chama hiki kina watu wenye ujasiri wa kukataa ukweli; wakaidi wa kutaka kila mmoja aone, kwa mfano, kuwa hili ni chungwa wakati ni kiazi kikuu.

CCM isingekuwa hivyo, kama ilivyofafanuliwa hapo juu, viongozi wake wasingejitokeza kupandikiza uzushi kwamba Chadema imefanya kampeni kabla ya NEC kutangaza.

Kwani kampeni za kuwaelimisha wananchi kujua kuwa diwani, mbunge au rais huyu hafai; anayefaa ni fulani kutoka chama kingine, hazisubiri uchaguzi mkuu.

Hii ni kazi ya Oktoba hadi Oktoba, kwa kipindi chote cha miaka mitano ya wanaokuwa madarakani na wanaokuwa wakisubiri kuingia.

Katika kipindi chote hiki NEC inajiandaa kusimamia uchaguzi lakini wanasiasa wanakata mbuga kuandaa wananchi kwa “mavuno.”

Hapa hakuna udhibiti hadi unapoingia rasmi kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu. Kazi za kisiasa za chama chochote, haziruhusiwi wala hazipaswi kuzuiwa na Tume. Na pasito zuio kuna uhuru kamili.

Chukua mfano huu: Katika mazingira ambako hakuna sheria inayolazimisha kila mmoja kuvaa tai shingoni, hakuna anayeweza kukamatwa na kushitakiwa kwa kutovaa tai. Hakuna sheria inayombana.

Hiyo ndiyo hali iliyopo katika kipindi ambapo wachezaji watarajiwa wa mchezo wa siasa hawajajifunga kushiriki; na mchezo wenyewe haujaanza.

Huwezi kuwabana. Huwezi kusema aliye nje ya uwanja ameharibu kanuni na taratibu za mchezo. Kudai hivyo ni kupanda mbegu ya uhasama ambao CCM na serikali yake, havina uwezo wa kuzima ndimi zake pale zitakapokuwa zimechomoza.

Hivi sasa, CCM ni chama kinachokwenda kwa mazoea tu. Hakina jipya ingawa kinataka kubaki ikulu, kwa “gharama yoyote ile.”

Na hili la kubaki madarakani kwa gharama yoyote ile, ndilo liwezalo kuleta maafa kwa nchi na watu wake.

Kwani wanajua kuwa kuondoka kwao kutaweka wazi mengi machafu ambayo yamekuwa yakitendeka. Hili, viongozi wake hawataki kuliona wala kulisikia.

Wako tayari kuua mbegu mpya na bora kwa kupitia madai yasiyo kichwa wala miguu, alimradi wamebaki ikulu.

Lakini katika hili la kupakazia kufanya kampeni mapema, tundu limezibwa. Hata kwa mgongo wa “tu-vyama twingine” kwenye upande wa upinzani, kama vile Tanzania Labour Party (TLP) ka Augustine Mrema, CCM itaendelea kukaliwa kooni.

Tayari kuibuka kwa Dk. Slaa kumebadili mwelekeo wa siasa nchini na kuleta uwezekano wa kuifinyaza CCM na mikonga yake.

Bali wananchi wanataka umoja wa vyama; kwa maana ya ushirikiano katika uchaguzi huu ili mradi wa kuadabisha CCM uweze kufanikiwa.

Umbeya na ghiliba ya CCM vyaweza kuzimwa. Je, hili la ushirikiano laweza kufikiwa? Tusubiri.

0713 614872
ndimara@yahoo.com

(Makala hii ilichapishwa katika Tanzania Daima, Novemba 2010 katikati ya vuguvugu la uchaguzi na CCM ilipoanza kuhaha)

USHINDI 'CHAKUPEWA' WA CHAMA CHA MAPINDUZI



MADAI YA WIZI WA KURA YATAWALA MIJADALA
MAJUMBANI, SHULENI, VYUONI, SOKONI, MAOFISINI


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kuwaudhi wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwaambia kuwa aliyeshinda katika uchaguzi mkuu siyo Jakaya Kikwete bali Dk. Willibrod Slaa na kambi ya upinzani.

Pamoja na kutotaka kuwaudhi, sitaki pia kuandika kwa urefu kwa kuwa matukio ya hivi karibuni, yanayohusu uchaguzi, yangali mabichi na wananchi wanahitaji kuyajadili, kuyatafakari na kuyafanyia kazi.

Niseme tu kwamba waliokuwa bado na shaka juu ya uwezekano wa CCM kuwekwa kando, kufungiwa virago na kuondoshwa ikulu, sasa waanze kufikiri upya. Inawezekana!

Kile ambacho kinatangazwa kuwa ushindi wa CCM wa asilimia 61 katika uchaguzi mkuu ndicho hasa kinaonyesha mporomoko wa chama hicho na uwezekano wa kuenguka.

Lini Tanu na CCM viliwahi kufikia asilimia 60 za kinachoitwa “ushindi” hata katika mazingira ya “ushindani wa mwendawazimu” anayekimbia peke yake na hatimaye kudai ameshinda?

Lini, tangu kurejeshwa kwa maneno ndani ya katiba “mfumo wa vyama vingi vya siasa,” lakini kubakia chama kimoja kifikra na kiutendaji, CCM imewahi kupewa asilimia 60?

Nani, miongoni mwa viongzi wa CCM, akiwemo mwenyekiti Jakaya Kikwete, aliwahi kuota Tume inawapa asilimia 60 au kupata kiwango hicho kwa njia zao za abrakadabra?

Hata Kikwete alipokuwa anaanza na kufunga kampeni, alitangaza kuwa atashinda kwa “kishindo kuliko hata ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita” – 2005. Yako wapi?

Je, ni mtindo wa watawala wa Uingereza wakati wa Vita Vikuu vya Pili? Walikuwa wakitangaza kuwa tayari vita vimeisha; Wajerumani wamesambaratika na wengine wamejisalimisha.

Nia ilikuwa kuamsha na kujenga morali ya wapiganaji wao na kuzamisha na kufisha morali ya Wajerumani na waliowaunga mkono.

Yawezekana CCM imefikia viwango hivyo? Propaganda za “kyakutinisa kitakulye” – kinachoogopesha lakini kina madhara kidogo au hakina madhara kabisa?

Chukua mfano mmoja. Kwa maamuzi ya haraka na ya dakika ya mwisho, kwamba Dk. Slaa ndiye awe mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama cha zamani CCM kimetikisika hadi mizizi.

Kwa miezi mitatu tu ya kuwafikia wananchi, hata mahali ambapo chama cha Dk. Slaa hakikuwahi kusikika, elimu ya uraia kwa njia ya mikutano ya hadhara imepenya kwa kasi.

Kwa miezi mitatu tu ya kuwafumbua macho wananchi na kuwasaidia kuchambua matatizo yao, wameelewa kuwa kumbe watawala wao wamekuwa sehemu ya matatizo yao. Hivyo hawana msaada kwao.

Yote hii ni kwa vile kwa miaka mingi wameishi kama wafungwa; wana utulivu ya magereza lakini bila amani. Sasa wameona anayewasaidia kutafakari maisha yao na kwa kiasi fulani kukata baadhi ya minyororo kwa kauli chambuzi.

Kwa mzunguko wa miezi mitatu, ulioongozwa na Dk. Slaa, kwa hoja nzito na kauli za matumaini mapya, CCM imeporomoka kutoka “ushindi wa kishindo” hadi asilimia 61 ilizopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Katika baadhi ya maeneo, na hasa kule ambako CCM iliishakuwa serikali, polisi, mahakama na bwana jela, ujumbe wa Chadema na Dk. Slaa umefanya baadhi ya wananchi waone kuwa “kumbe CCM ni chui wa karatasi.”

Miezi mitatu ya kutafuta kuwaamsha wananchi kuchukua serikali yao kutoka kwa waliochoka na walioshindwa kuleta, siyo tu mabadiliko bali hata matumaini, imezaa uelewa mpana.

Ukichukua asilimia 61 za wanaotamba kubakia ikulu na kulinganisha na maarifa – uelewa, ung’amuzi, mwamko, matumaini mapya na utayari wa wananchi kushiriki katika kuleta mabadiliko katika maisha yao, ndipo utagundua kuwa CCM “wameliwa” au “wamejila wenye.”

Chukua mfano mwingine. Profesa Kulikoyela Kahigi alishinda katika kura za maoni ndani ya CCM; jimbo la Bukombe. Akafanyiziwa. Rufaa yake ikazimwa. Vijana na wazee wakasema, “…nenda kule tutakupigia kura hukohuko.” Leo ni Mbunge.

Juhudi za Yusuf Makamba, katibu mkuu wa CCM, kujaribu kugeuza mkondo, zilikwama. Alifikia hatua ya kutukana wanachama na viongozi wake kuwa wamrejeshee mashati yake ya kijani, kama wanakuwa wanachama mchana tu na usiku wanakwenda upinzani. Kyakutinisa kitakulye!

Mfano huohuo unahusika Maswa Magharibi ambako ghiliba na husuda vilikuwa sehemu ya sala ya viongozi wa CCM kwa shabaha ya kumzima John Shibuda.

Shibuda alihama CCM baada ya kuenguliwa. Naye akasema hakuna chama pale na kwamba kilikuwa kinaishi kwa pumzi ya rushwa. Wananchi wamemlinda. Wamemchagua.

Miezi mitatu ya kazi ya Dk. Slaa na chama chake; juu ya kazi ya awali ya sauti ya mageuzi; vimejenga ujasiri usiomithilika nyoyoni mwa umma.

Kila mahali ambako uelewa na maarifa vimesambazwa na kuzama vichwani na nyoyoni mwa wananchi, CCM imedaiwa kuvuna sifuri au kujichukulia “kwa mbinu.”

Wala Dk. Slaa hana sababu ya kusononeka na kulia. Hapana! Ameshinda. Mara hii ushindi wa kishindo; tena ulio halali na tofauti na vungavunga ya CCM.

Kiwewe kilichotembelea CCM kutokana na wimbi kubwa la upinzani na nguvu ya mgombea wa Chadema, vimefanya chama hicho kilichopanga ikulu kiweweseke, kiishiwe nguvu na hata kuwa butu.

Ni kiwewe kilichofanya viongozi wa CCM wajiingize katika kujadili uchumba, ushenga na ndoa ya Dk. Slaa. Ni hichohicho kilichofanya waanzishe mtandao wa vineno vya kashfa na kuvisambaza nchi nzima.

Kiwewe hichohicho ndicho kilifanya CCM wabuni uwongo juu ya Dk. Slaa kuwa ni mbishi, kaidi na anayegombana na vyombo vya ulinzi na usalama na anayetaka kuleta vita.

Walilenga kuwa wananchi wakisikia Dk. Slaa “anagombana na askari,” basi watamkimbia na CCM itakuwa imepona upele ulioletwa na upupu wa ufisadi.

Eti wananchi waogope vita vya kujikomboa lakini wasijali mafisadi wanaowaibia na kufanya maisha yao yatoweke haraka kuliko kama kungekuwa na vita! Kyakutinisa kitakulye.

Ni CCM waliopenyeza katika hotuba zao, madai ya vita na kumbukumbu za vita vya Burundi na Rwanda ili wananchi wakatae mpiganaji wa Chadema.

Ni chama hicho chenye kupanga ikulu, ambacho kilianzisha na kuvumisha kuwa kuna “udini” kikilenga kuzamisha sauti za wapenda mabadiliko.

Wakati askofu wa katoliki anasema, mwaka 2005 kuwa Kikwete, ambaye ni mwislam, ni “Changuo la Mungu,” CCM walikaa kimya. Leo, Kikwete anachuana na mkristo mwenye rekodi nzuri na ambaye hashikiki kwa hoja, CCM inaibua madai ya udini.

Chadema imetumia uchaguzi mkuu huu kuandaa mtaji kwa ajili ya uchaguzi ujao. Kile ilichobakiziwa kwa njia ya idadi ya kura na asilimia, ni ushahidi tu.

Wekezo kuu la Chadema katika uchaguzi ni elimu iliyowaacha wananchi na maarifa mapana; ujasiri wa kusema “hapana” na utashi wa kuchagua chenye thamani na endelevu.

Kwa kutumia mizani hiyo, mbegu ya mabadiliko imepandwa nyoyoni mwa wananchi wengi; haiharibiki kwa ukame wala mafuriko ya kisiasa.

Ndiyo maana ni halali kusema Chadema imevuna; ukitaka – imeshinda. Si kwa asilimia peke yake ambazo zaweza kutiliwa shaka, bali hasa kwa wekezo la maarifa na ujasiri ambavyo ni muhimu kesho, kuanzia ngazi ya kaya.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima mara baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu, Novemba 2010)

MUNGU, WACHAWI NA UCHAGUZI TANZANIA

Baadhi ya imani zinazoathiri fikra za
wengi katika siasa na maisha ya kawaida


NI mahojiano ya chapuchapu, kwenye kaunta ya M.S. Hotel jijini Mwanza, Jumatano 27 Oktoba 2010. Ndimara Tegambwage aliyeko hapa kwa ushauriano na waandishi wa habari wa kanda ya Ziwa Viktoria, anakutana na Fikiri Mabula na kwa muda mfupi anapata “fikra” za binti mdogo juu ya Mungu, uchawi na uchaguzi mkuu wa 31 Oktoba. Fuatilia.

Swali: Wewe unaonekana mdogo. Unafanya kazi hapa?

Jibu: Hapana. Nimemfuata dada yangu. Kwa nini unauliza hivyo?

Swali: Niliona kama mwenyeji vile; halafu nikaona kwa umri huo usingekuwa mfanyakazi.

Jibu: Siyo mfanyakazi hapa lakini natafuta kazi.

Swali: Una umri gani?

Jibu: Mimi? Miaka mingi.

Swali: Miaka mingi mingapi? Kama yangu?

Jibu: Ehee! Miaka 22.

Swali: Una watoto wangapi?

Jibu: Mimi? Mmoja tu.

Swali: Ungetaka kuwa na wangapi?

Jibu: Wengi.

Swali: Wengi ni wangapi?

Jibu: Watano.

Swali: Wote hao utaweza kuwatunza na kuwasomesha shule?

Jibu: Eee, wewe vipi? Hivyohivyo tu. Sasa nikizaa…kwani wewe ungetaka nizae wawili au watatu?

Swali: Unaniuliza mimi tena? Naona ungekuwa na watatu tu.

Jibu: Watatu? Watatu tu?

Swali: Si ndiyo? Halafu urudishe mwili; utulie na kutafuta njia za kuwalea na kuwasomesha.

Jibu: Mimi naona nizae watoto watano.

Swali: Wote hao wa nini?

Jibu: Sikiliza. Nikizaa watano, Mungu atachukua mmoja; dunia itachukua mmoja na wachawi watachukua mmoja. Nitakuwa nimebakia na hutu tuwili (akionyesha kwenye vidole).

Swali: Kwani Mungu anahitaji mtoto wako?

Jibu: Eee! Imeandikwa. Yeye akitaka anachukua wakati wowote.

Swali: Aache kuchukua mtu mzima kama mimi hapa achukue kifaranga chako?

Jibu: Eee! Hata akichukua mtu mzima; atakuwa amechukua mtoto wangu. Yeye anaamua lini anataka kumchukua; uwe mdogo au mkubwa.

Swali: Na wachawi je? Wana sababu gani ya kuchukua mtoto wako?

Jibu: Wewe! Wenye roho mbaya; hawapendi kuona mtu akipata kitoto chake kizuri.

Swali: Mbona watoto wazuri wako pote duniani. Hivi wachawi hawajawaona au wameelemewa kwa kuwa dunia ni kubwa?

Jibu: Labda huko kwingine hakuna wachawi; lakini katika maeneo yetu haya, wapo na wana roho mbaya kweli.

Swali: Au dini ndiyo imepunguza wachawi?

Jibu: Inaonekana wewe hujui mambo mengi. Hao wanaoonekana waumini wakuu ndio wanakamatwa kila siku wakifanya uchawi makaburini; lakini Jumapili au Ijumaa ndio wako mbele karibu na mchungaji au sheikh.

Swali: Wewe ni mwislamu au mkristo?

Jibu: Mimi mwislamu.

Swali: Lakini kwa ulivyoelezea waumini wachawi, ina maana kuwa huendi msikitini kusali.

Jibu: Naenda. Mimi ni mwislamu lakini dada zangu wawili na baba, ni wakristo. Kila mmoja na madhehebu yake. Mimi nimekaa upande wa mama.

Swali: Hapo nyumbani hamgombani kwa kuwa na imani tofauti?

Jibu: Tugombanie nini? Kila mtu anaamini vyake. Kuna mambo yanayofahamika kuwa ni mabaya, kama wizi, uchawi, hayo mmoja wetu akiyafanya lazima tutagombana.

Swali: Je, kama mnatofautiana kisiasa?

Jibu: Kisiasa? Hayo si mambo ya wanasiasa? Sisi kazi yetu kupiga kura tu.

Swali: Si mnaweza kugombania nani awe diwani, mbunge au rais?

Jibu: Wewe unachekesha. Tugombanie chakula cha wengine? Kwa nini? Mimi kwa mfano, nitapiga kura kwa mara ya kwanza. Nitampigia Kikwete. Wengine wote pale nyumbani wanasema watampigia Dk. Slaa. Sasa ugomvi utatoka wapi? Kila mtu na chaguo lake.

Swali: Kwa nini unataka kumpigia Kikwete?

Jibu: Wewe unataka niseme mengi. Kwanza nimeishatoa siri yangu ya nani nitampigia; na sasa unataka sababu za kumpigia kura ninayependa. Au wewe mwandishi wa habari?

Swali: Nadhani sababu za kupenda mgombea siyo siri. Kila mmoja anasema… na hakuna siri, au vipi?

Jibu: Mimi sina sababu kubwa. Ni kama wasemavyo “zimwi likujualo...” Kwa kuwa amekuwepo, basi naona aendelee huyohuyo. Halafu kuna maneno yanapita…mh, hayo tuyaache. Nitachagua huyo. Kwani wewe utachagua nani?

Swali: Unataka nami nitoe siri? Nitachagua mmoja wa wagombea (kicheko).

Jibu: Sawa, lakini nimekuuliza, wewe ni mwandishi wa habari?

Swali: Napenda kuwa mwandishi wa habari. Kwani wewe unaona nafanana mwandishi wa habari?

Jibu: Huwa wanasema waandishi wa habari huuliza maswali mengi.

Swali: Kwani polisi hawaulizi maswali mengi?

Jibu: Sijawahi kuhojiwa na polisi. Sijui (kicheko).

(Makala hii ilichapishwa katika toleo maalum la gazeti la MwanaHALISI,20 Oktoba 2010 kwa lengo la kuhamasisha wapigakura)

CHILIGATI: WAZIRI HATARI, ANATETEA UBABE, ANAPINGA DEMOKRASI, ANACHOCHEA VURUGU



Chiligati, CCM wanaandaa maafa


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kusikia Rais Jakaya Kikwete akifikiria kumteua John Chiligati kuwa mmoja wa mawaziri au washauri wake wa karibu. Amwache.

Kauli ya Chiligati kuhusiana na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukataa kumsikiliza rais akihutubia Bunge la 10, zinaonyesha ni mtu wa shari asiyemwelewa hata rais ambaye anadai kumtetea.

Mfano Na. 1: Chiligati anasema bunge linaweza kuandaa azimio la kuwaondoa wabunge wa Chadema waliotoka nje ya bunge wakati Rais Kikwete ameanza kuhutubia.

Yaani katibu mwenezi taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) – bila woga wala aibu – anajenga hoja ya kula njama ya kufukuza wawakilishi wa wananchi wa chama kingine – Chadema, kutoka bungeni.

Kwamba wabunge wengi wa CCM, ambao hujigamba kuwa wanajua demokrasia; watumike kufukuza wawakilishi wenzao wa chama kingine kwa madai ya kutomsikiliza rais akiongea bungeni.

Chiligati ni hatari. Ana lake jambo. Anajenga woga miongoni mwa wabunge. Anajenga wasiwasi, chuki na uhasama miongoni mwa wananchi. Anafanya uchokozi na kutukana wapigakura.

Katibu mwenezi wa CCM anataka kuzua mtafaruku mchafu, wa aina yake, ambao hauwezi kuishia kwenye kauli tupu na ambao Chiligati na waliomtuma hawawezi kuuzima.

Mfano Na. 2: Chiligati anataka watu wakae kimya. Wasitoe neno. Wasilalamike. Wasikemee. Wasisute. Wasilie. Wasilaani. Wasinune. Wasipinge.

Ukiona kiongozi ana akili ya aina hiyo, ujue ni mbegu ya udikiteta, ukatili, lakini pia ni mtu asiye na chembe ya fikra juu ya matokeo ya kauli na matendo yake.

Asiyetoa kauli ya wazi kutokana na vitisho vya watawala, anajenga hazina ya hasira na chuki. Kauli, hasira na chuki ambavyo havikutoka leo kutokana na ubabe wa watawala, vitatoka kesho lakini kama bomu la maangamizi.

Chiligati hajui hayo au anayajua lakini anayapuuza. Anaongea kwa jazba. Anafoka. Aanaunda bomu la maangamizi.

Msemaji huyo wa CCM anajua kuwa Chadema hawajafanya lolote baya kwa kukataa kumsikiliza rais. Hakuna sheria wala kanuni inayoweza kuwabana wabunge kwa kutomsikiliza rais. Haipo.

Hakuna sheria wala kanuni inayozuia wabunge au hata chama kusema. “…wewe umeniibia kura. Sitambui ulivyopata ushindi.” Haipo!

Chiligati ataleta balaa. Chiligati ataleta maafa. Chiligati anatamka hadharani kuwa wabunge wa Chadema, waliochaguliwa na wananchi, wafukuzwe na wabunge wenzao wa CCM wakishirikiana na wale wa vyama vingine vidogo.

Baadhi ya wananchi na hasa wanachama wa CCM wameanza kuamini kuwa hilo linaweza kutendeka. Haliwezekani! Chiligati anachezea akili za wananchi wapigakura. Ataleta balaa.

Huyu bwana anajaribu kudharau, kuchezea na kusimanga kura za wananchi zipatazo milioni mbili na nusu zilizosema kuwa zimeichoka CCM na zinataka mabadiliko.

Mbona Kikwete mwenyewe anajua haya? Chiligati amekwama wapi? Siyo lazima aseme, lakini Kikwete anajua vema kuwa ana katiba yenye makengeza; inayotumika kuminya uhuru na haki za wananchi.

Mbona anajua kuwa ana katiba na sheria vinavyowazuia wananchi anaotawala kudai haki zao? Hatasema lakini anajua vema kuwa chombo kama vile Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni “mali yake” na chama chake.

Anapokuja mtu wa saizi na viwango vya Chiligati na kusema wabunge wa chama kikuu cha upinzani wafukuzwe bungeni, anamtakia mema Kikwete na utawala wake? Bado anataka kazi?

Itakuwa wapi amani anayohubiri? Utakuwa wapi umoja anaopeperusha midomoni kwake? Utakuwa wapi utulivu anaodai anataka iwapo atatukana na kuvunja uhuru na haki za wapigakura?

Chiligati anaonekana kuwa na tatizo la “kulipua kauli” bila kufikiria matokeo yake. Kwamba anaweza kusema sehemu ya “bunge la CCM” ifukuze sehemu kubwa ya “bunge la upinzani,” ni kutokuwa makini; ni kutumia jazba badala ya fikra ang’avu.

Nani anaweza kusema mtu huyu anamwakilisha rais ambaye angetaka kufikia mwisho wa kipindi chake kwa furaha na hata kupata mahali pa kuishi baada ya urais bila kusumbuliwa?

Nasema Kikwete hakubaliani na Chiligati kwa kuwa huyu Kikwete amekuwa katika nchi nyingi duniani akiwa waziri wa mambo ya nje. Ameona na kushuhudia makubwa zaidi ya kumwacha rais akihutubia.

Kikwete ameona marais wanaotupiwa viatu, mayai viza, mawe, mchanga; wanaosusiwa wanapokwenda kwenye majimbo ya baadhi ya wabunge na wanaopingwa moja kwa moja kwa kauli kali na katili. Kitu gani Chadema kumwacha apumue bila presha!

Na Chadema wana haki ya kuchukia. Walisema hawatambui matokeo yaliyotangazwa na Tume. Hawakwenda kwenye sherehe za matokeo. Hawakwenda kwenye kuapishwa kwa rais. Hawakuwa kwenye kuapishwa kwa waziri mkuu. Na juzi walifunga kazi kwa kutomsikiliza Kikwete.

Basi. Inatosha. Wapigakura wao wamesikia; wanasubiri ufafanuzi tu wakati wa mikutano ya kuwashukuru kwa kuwapa kura ambazo hazijawahi kwenda kwa upinzani.

Wale ambao hawakuwapigia kura nao wamesikia. Wanaoitwa washindi wamesikia. Tume imesikia. Mataifa yamesikia. Kila hatua ina fundo lake. Baada ya hapa wanaanza kazi yao ya uwakilishi.

Hatua zote hizi ambazo Chadema wamechukua, zina maana kwao wakiwa chama; zina maana kisiasa na katika kushamirisha hoja nzito za kuwa na Tume huru ya uchaguzi na katiba mpya inayokidhi matakwa ya sasa.

Anatoka wapi Chiligati kudai kuwa hatua hizi za Chadema ni usaliti? Usaliti upi na kwa nani? Yeye aliwatuma wafanye nini na yeye ni nani kwa chama hiki?

Ni Chiligati anayepandikiza chuki. Hataki kuonwa kama anavyoonekana. Anataka kurembwa kwa marashi, poda na hariri. Azivae basi zionekane nje na ndani ya roho yake. Hana.

Chadema wameonyesha jambo moja kubwa na la kuigwa. Wamekomaa katika kufikiria na kutumia mbinu sahihi kufikisha ujumbe.

Enzi za kuviziana kwa mawe, mchanga na mayai viza zimepitwa na wakati; hasa unapokuwa una uhakika kuwa unachosema ndicho kile ambacho wananchi wengi wanapenda na kusimamia.

Labda kwa kumsaidia Rais Kikwete hapa ni kwamba, hakika watatoka na kuingia, lakini siyo kwa kuibembeleza serikali kutekeleza miradi katika majimbo yao. La hasha!

Wananchi ni walipakodi. Kukataa kupeleka miradi ya maendeleo katika majimbo ya upinzani ni aina nyingine ya rushwa miongoni mwa rushwa kubwa. Ni uhalifu.

Kwa hiyo anayetarajia kupigiwa magoti ili apeleke miradi ya maendeleo katika jimbo la upinzani, ajue anamwita budi kulilia mlangoni mwa chama chake.

Katika mazingira ya sasa, hasa kwa mwamko wa wananchi, acha uchaguzi uje, kiongozi wa namna hiyo atatupwa nje, hata kama amekuwa madarakani mwa miaka 50.

Bali kauli za Chiligati hazinabudi kuogopwa na kukataliwa; njama zake kuvunjwa na yeye kuzomewa. Kwani mbegu yake ikiruhusiwa kumea, ndiyo hatari kuliko hatari zote tulizowahi kutamka nchini.

Chiligati anataka kuua uhuru wetu na haki zetu kama zilivyojitokeza kupitia hatua za Chadema katika wiki mbili hizi. Hatukubaliani na mpango wake; heri ufe mapema.

Bila shaka Chiligati siyo mmoja wa wachapakazi ambao Kikwete anahitaji. Kama ni uchapakazi, basi ni ule wa kuleta maangamizi. Tunayachukia. Tunayakataa.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

MREJESHO: Rais Kikwete hakumchagua Chiligati.

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Novemba 2010)

KATIBA MPYA! KATIBA MPYA TANZANIA



WANANCHI WAANZA KUDAI KATIBA MPYA
SERIKALI YA KIKWETE YAWEWESEKA


Katiba mpya ndilo jibu pekee

Na Ndimara Tegambwage

BAADA ya wabunge wa Chadema kumwacha Rais Jakaya Kikwete bungeni, kwa shabaha ya kusisitiza umuhimu wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, watawala wameweweseka.

Huyu anadai Chadema wanataka kuvunja umoja, amani na utulivu wa Tanzania. Yule anafura mithili ya kufutu akidai Chadema “wahaini.” Mwingine analoloma kuwa Chadema ni wasanii; na mwingine anasema wafukuzwe bungeni.

Kila watawala wanapobanwa hukimbilia kauli zenye utata au uwongo wa moja kwa moja: kuwa wanaodai haki yao au ya jamii au taifa zima, wanataka kuleta vita na kuondosha amani na utulivu.

Hivyo ndivyo wananchi wamezoeshwa. Watawala hawataki wananchi wafikiri zaidi ya hapo. Kauli za “wanaotaka kuleta vita na kuondoa amani,” ni silaha kuu za watawala katika kunyamazisha umma na hata kuufanya usifikiri tofauti.

Kwa miaka 18 sasa kumekuwa na madai ya wazi kwenye majukwaa ya siasa kuwa nchi inahitaji katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

Watawala ama wametoa majibu ya kejeli au wamekaa kimya. Walichoona kwenye marekebisho ya katiba ni kutamka tu kwamba nchi ni ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kamba, minyororo, pingu na magereza, vilivyomo ndani ya Katiba ya nchi na sheria za uchaguzi, vimebaki vilevile. Siyo kwamba watawala havioni. Wanaviona kuwa ni vya ubabe na katili, lakini wanaviacha viendelee kuwemo kwa kuwa vinawasaidia kubaki madarakani.

Tuchukue mfano halisi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Jielekeze kwenye Ibara 41 (7). Inasema hivi:

“Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Chini ya utawala wa mfumo wa chama kimoja, lilikuwa kosa kumpinga rais. Kwanza, rais alikimbia peke yake kama mwendawazimu na hatimaye kijitangaza kuwa ameshinda. Alikuwa anashindana na nani?

Hapa kuna “Ndiyo” na hapa kuna “Hapana.” Ukiandika ndiyo ina maana kuwa ni yuleyule. Ukiandika hapana, ina maana kuwa hapana mwingine isipokuwa huyohuyo.

Yule ambaye chama tawala kimetaka awe rais, hata akipata “Hapana” nyingi, lazima ziwe au zionekane, au zisomeke au zionyeshwe kuwa ni “Ndiyo.”

Kwa kuelewa kuwa hatimaye taarifa zitavuja, kwamba “hapana” zimefanywa “ndiyo,” ibara ikasukwa ndani ya katiba, kwamba pale mtu atakapokuwa ametangazwa kuwa rais, isiwepo mahakama yoyote ile “itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Mtu aweza kujiuliza: Kwa nini kuwe na katiba inayoruhusu mwanya wa kutenda uhalifu? Kwa nini kuwe na katiba inayotilia mashaka nguzo muhimu ya dola – mahakama – katika usimamizi wa haki?

Inawezekana watawala wanajua kuwa siyo wasafi? Kwamba hawana sifa isipokuwa ghiliba? Kwamba hawakubaliki isipokuwa kwa shinikizo? Kwamba hawawezi kumudu kushindanishwa na wengine mpaka kuwepo mwanya wa kukiuka taratibu, kanuni na sheria?

Kama kwamba hilo halitoshi, maandalizi ya uchaguzi yanakabidhiwa kwa tume iliyiochaguliwa kwa utashi binafsi wa rais. Ni tume hii inayopewa mamlaka kisheria ya kuandaa, kusimamia uchaguzi na kutangaza mshindi.

Hili tuliangalie hivi: Msimamizi wa uchaguzi ni mteule wa rais. Yule ambaye mteule wa rais atatamka kuwa ndiye mshindi, basi ndiye huyo. Huyo aliyetangazwa hapaswi kupingwa mahakamani.

Hii maana yake ni nini? Ni kwamba tume ya uchaguzi imepewa madaraka makubwa sana kiasi kwamba inaweza “kuchagua” nani awe rais; na ikiishatamka, basi aliyetangazwa hawezi kulalamikiwa mahakamani.

Kuna mwanya mdogo. Mlalamikaji aweza kulalamikia tume kwa kutofuata kanuni, taratibu na sheria; au kwa watendaji wake kukiuka sheria. Mahakama yaweza kutolea maamuzi malalamiko hayo.

Lakini hakuna uwezekano wowote kwa maamuzi hayo kumwondoa madarakani rais aliyepatikana kwa rushwa, wizi wa moja kwa moja; kwa fedha za mafisadi au kwa udanganyifu.

Faida pekee ya njia hiyo ni kuweka wazi kilichotendeka; nani walitenda nini na uhusiano kati ya yaliyotendekake na aliyetangazwa kuwa rais.

Kila baada ya uchaguzi mkuu, waliochaguliwa wamekuwa wakiapa kulinda katiba hiihii yenye upogo; ambayo ina uwezekano wa kuleta viongozi waliopatikana kwa njia chafu lakini hawawezi kuhojiwa mbele ya mahakama.

Si hayo tu, katiba ya Tanzania imejaa vipengele ambavyo havilingani na mazingira ya sasa ya mfumo wa vyama vingi.

Moja ya mifano inayotajwa mara kwa mara ni pamoja na ule wa katiba kutaja kuwa hii ni nchi ya “kidemokrasi na ya kijamaa.”

Hoja zinajengwa: Iko wapi demokrasi katika mazingira ya kukatalia mahakama kusikiliza malalamiko kuhusu aliyetangazwa kuwa mkuu wa nchi?

Ujamaa ni itikadi. Uko wapi utekelezaji wa itikati ya ujamaa chini ya utawala wa CCM?

Tunachoona ni uwezeshaji, kwa kauli, taratibu, kanuni na sheria wa makampuni na mataifa ya nje, kuingia nchini na kuvuna kana kwamba ni “shamba la bibi.” Hakuna ujamaa hapa.

Kwa msingi huo, Chadema wanapojaribu kuweka wazi, kilio chao na cha wananchi kuhusu umuhimu wa katiba mpya na tume huru ya uchaguzi, hakika wanastahili kusikilizwa.

Wasiposikilizwa wanatafuta njia mwafaka, kama ile ya juzi bungeni, ambako rais, watawala wenzake, wageni rasmi walipata ujumbe wa moja kwa moja; bila kuchujwa.

Bali bahati mbaya, wenye fikra za John Chiligati, Katibu mwenezi wa CCM, wanajitokeza na kudai kuwa Chadema wanataka kuleta “uvunjifu wa amani.” Kwa kudai katiba mpya na tume huru?

Nani hapa anatishia uhuru, umoja, amani na utulivu wa nchi, kama siyo yule anayelinda katiba iliyopitwa na wakati na ambayo wananchi wana kiu ya kuibadilisha lakini bila mafanikio.

Ni halali kusema hapa, kwamba kuendelea kuwa na katiba kama hiyo na sheria kandamizi, ndiyo kuvunja umoja, kuangamiza amani na kupoteza utulivu.

Ni sahihi kabisa kuanza sasa kuandika majina ya wote wanaong’anga’ania hali hii ya hatari – ya kuendelea kuwa na katiba iliyopitwa na wakati na isiyokidhi matakwa ya wengi – na kuyawasilisha mahakama za kimataifa.

Hii ni kwa kuwa ikitokea amani ikavunjika, wawe wa kwanza kuhojiwa kwa kusababisha hali hiyo. Kwa leo, tuanze kwa kufikiria kupeleka jina la John Chiligati.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la tarehe 8 - 14 Desemba 2010)

TCRA YAAMKA NA KUTUNISHA MSULI

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


KUTOA TAARIFA ZA SIRI KATIKA MAWASILIANO YA ELEKTRONIKI NI KOSA LA JINAI
Hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imegundua kuzuka kwa tabia ya uvunjaji wa kanuni ya utunzaji wa siri za mawasiliano binafsi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi. Mawasiliano hayo yamefikia hatua ya kuchapishwa katika vyombo vya habari.

Mamlaka ya Mawasiliano inapenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wenye makampuni ya Simu na wananchi kwa ujumla kuwa, kutoa taarifa za mawasiliano binafsi ya simu bainA ya watumiaji wa huduma hiyo, ni uvunjaji wa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Na. 3 ya mwaka 2010 na Kanuni za Mawasiliano (Kulinda Wateja) za mwaka 2005.

Kifungu cha 98 ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kinasema;

(1) “Mtu yeyote ambaye ni mfanyakazi wa kampuni yenye leseni ya kutoa huduma za mawasiliano, au mwakilishi wake, ana wajibu wa kutunza siri za mawasiliano binafsi na taarifa zozote za siri za wateja kwa mujibu wa sheria hii”

(2) “Mtu yeyote haruhusiwi kutoa taarifa binafsi za mteja yeyote alizopokea au kusikia kwa mujibu wa sheria hii isipokuwa tu mtu huyo ameruhusiwa kwa mujibu wa sheria”

Kifungu cha 123 (1) kinasema:-

Mtu yeyote ambae bila sababu za msingi atasababisha kuingilia au kuzuia kupokewa kwa mawasiliano yeyote ya kielektroniki anafanya kosa and akipatikana na makosa atatakiwa kulipa faini ya shilingi za kitanzania zisizopungua milioni tano au kwenda jela kwa muda wa usiopungua miaka miwili au adhabu zote kwa pamoja”

Kanuni ya 12 ya Kanuni za Mawasiliano za mwaka 2005 za Tanzania (Kulinda Wateja) inasema:-

“Mtoa huduma za Mawasiliano haruhusiwa kuingilia kati, kusikiliza au kutoa taarifa zozote za mazungumzo ya mteja yeyote yaliyopitia kwenye mtandao wa mtoa huduma, isipokuwa kwa ruhusa kulingana na mahitaji maalumu kwa mujibu wa sheria zilizopo”

Kutolewa kwa taarifa za mawasiliano binafsi ya watumiaji wa simu za mkononi ni lazima kunafanywa na mtu mwenye ujuzi na uelewa wa jinsi ya kupata taarifa hizo na wenye ruhusa ya kufanya hivyo katika mtandao wa Kampuni husika ya kutoa huduma ya mawasiliano; ama peke yake au kwa kushirikiana na wenzake kwa kuingia kwenye mtandao kwa makusudi kwa lengo la kuingilia mawasiliano binafsi ya watu, ambayo ni uvunjaji na kinyume na matakwa ya kifungu cha 123 cha Sheria Na. 3 ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Mamlaka ya Mawasiliano inayakumbusha Makampuni ya simu kuweka uzuizi na kuhakikisha siri za mazungumzo binafsi ya wateja zinahifadhiwa na hazitolewi kwa yeyote isipokuwa kwa mujibu wa sheria na; kuhakikisha yanafanya uchunguzi kugundua walioiningilia mazungumzo binafsi ya wateja.

Wananchi wanapewa tahadhari kuhusu kutafuta au kutaka kupata taarifa za mawasiliano ya siri kutoka kwa watoa huduma na kuzitumia taarifa hizo binafsi za mawasiliano pasipo kufuata utaratibu ulioruhusiwa kisheria.

Kwa taarifa ambazo zimechapishwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari hivi karibuni, Mamlaka ya Mawasiliano inafanya uchunguzi wa uvunjwaji huo wa sheria kwa kutoa taarifa binafsi za wateja kinyume na sheria. Baada ya kuwabaini wahusika, Mamlaka itachukua hatua za sheria kwa yeyote atakayebainika kuvunja sheria hiyo.



Imetolewa na

Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
22 Desemba 2010

MSUKUMO WA KATIBA MPYA WAONGEZEKA





















Katiba mpya siyo kwa hisani

Na Ndimara Tegambwage

KATIBA mpya ya nchi ambayo wananchi wanataka, si mali ya rais. Si mali ya waziri mkuu. Wala katiba hii haipatikani kwa hisani ya mtawala yeyote. Hapana.

Wananchi wanataka kuandaa makubaliano juu ya mamlaka ya usimamizi na utawala; na misingi inayoweka udhibiti wa mamlaka katika mahusiano ya watawala na watawaliwa na miongoni mwa vyombo vingine vya dola.

Kwa ufupi, wananchi wanataka kushiriki kuandaa taratibu, kanuni na misingi itakayokuwa mwongozo mwafaka wa jinsi wanavyotaka kujitawala; na siyo katiba ya kuviziana ya mfumo wa chama kimoja.

Hapa unaweza kusema wananchi wanataka kuandika mkataba kati yao na watawala, wa sasa na wa baadaye, jinsi nchi yao inavyopaswa kuendeshwa katika nyanja zote za maisha.

Itakuwa historia. Sharti iwe. Wananchi wote – kwa kuulizwa au kwa utaratibu wowote ule wa kushirikisha maoni yao, akiwemo mtawala mkuu – watakuwa wamepata fursa ya aina yake ya kukubaliana jinsi wanavyotaka kujitawala.

Wiki iliyopita, kwenye ukurasa huu, tulieleza jinsi watawala wanavyojua vema jinsi katiba iliyopo ilivyo na kasoro nyingi.

Kwa ufupi tulisema wanajua kuwa rais anaweza kupata kura zisizo halali; lakini hawezi kulalamikiwa mahakamani. Katiba inaziba fursa hiyo.

Tulionyesha pia kuwa katiba ya sasa inazuia mtu kugombea nafasi yoyote ya kisiasa iwapo si mwanachama wa chama cha siasa. Ni ubaguzi mchafu.

Rafiki yangu anasema huo ni “ukabila wa kichama;” wa kuziba haki ya mtu kwa sababu dhalili lakini za uchu wa kunyanganya haki ya mwingine.

Watawala wanaelewa vema kuwa kuna raia wenye akili nzuri, elimu ya kutosha na uwezo wa kufikiri na kutenda kuliko baadhi ya wanachama wa chama chao waliopachikwa madaraka; lakini kwa “ubaguzi wa kichama,” wanaziba fursa zao za kutumikia taifa.

Haya yote Rais Kikwete anayajua. Pinda anayajua. Wanajua kuwa siyo sahihi. Siyo haki. Lakini wanayaendeleza. Wanayapakata kwa kuwa yanawawezesha, wao na chama chao, kukaa kileleni. Yanawachafua.

Chukua mfano mwingine. Watawala wanajua kuwa kazi kama zile za mkuu wa wilaya (DC) na mkuu wa mkoa (RC), zingekuwa zinachukuliwa na watu waliopatikana kwa kupanda ngazi kikazi katika maeneo ya utawala.

Sasa wafanyakazi wenye elimu na uzoefu wanaachwa; badala yake wanachukuliwa “wowote wale,” wakiwemo maaskari wastaafu ambao hawana ujuzi wala uzoefu katika kazi hizo.

Inagharimu serikali muda na mabilioni ya shilingi ya kodi za wananchi, kufundisha, bila mafanikio, watu wazima ambao hata siku moja maishani mwao hawakuota kuwa kwenye utawala.

Mkono wa kuteua unafika hata kwa wakurugenzi wa halmashauri na manispaa kwa sababu moja kuu: Kuongeza idadi ya wafuasi na watendaji kisiasa kwa niaba ya chama kilichoko ikulu.

Mteule wa rais anakuwaje kiranja katika utawala wa wananchi katika halmashauri, badala ya madiwani kutafuta na kuajiri mtendaji ambaye wanaona ana sifa za kuwatumikia?

Ni baadhi ya wateule hawa ngazi ya wilaya (wanaokuwa wasimamizi wa uchaguzi), ambao wamekuwa chanzo cha migogoro wakati wa uchaguzi kwa vile wamekuwa wakitishiwa kuwa, kama chama tawala hakikushinda watapoteza kazi.

Haya yanaweza kupatikana katika mazingira ya katiba ya sasa na safu hii itaendelea kufafanua.

Sasa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anasema serikali iko tayari “kufanya marekebisho” ya katiba ya nchi.

Alikuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Ijumaa iliyopita na kunukuliwa akisema atamshauri rais ili marekebisho hayo yafanyike katika kipindi cha “miaka mitatu.”

Hauhitajiki uchunguzi wowote kujua kuwa Pinda tayari aliishakutana na Kikwete na kujadili hoja hii kabla hajatangaza kuwa atakwenda kumwona.

Waziri mkuu hatangazi kila anapotaka kumshauri rais. Aidha, siyo lazima rais akubaliane na uamuzi wa waziri mkuu. Kwa hiyo, hatua ya kutangaza kuwa anakwenda kumshauri rais inaweza kutafsiriwa kuwa ameagizwa na rais kutoa kauli hiyo.

Hata hivyo, hiyo siyo hatua mbaya wala ndogo. Ni hatua inayoonyesha kuwa, angalau mara hii, masikio ya watawala yamefunguka.

Tatizo lipo kwenye hatua ya Pinda kumshauri Kikwete. Kama ilivyoelezwa hapo awali, katiba haiji kwa hisani ya rais. Rais anahitaji katiba mpya. Itakuwa yake kama ilivyo kwa raia yeyote wa nchi hii.

Rais anahitaji katiba itakayomwondolea uwezekano wa kushutumiwa na kutuhumiwa kutenda visivyo; kuwa anaminya, ananyang’anya au anavunja haki za raia na haki za binadamu.

Rais anataka katiba nzuri, kuliko hii iliyopo, ili huko tuendako, watawala wapya wasije kumgeuzia kibao na kuitumia kumminya kama Frederick Chiluba alivyomtendea rais mstaafu Kenneth Kaunda huko Zambia.

Rais aliyeko madarakani anahitaji katiba inayotabasamu kwa wote; isiyojenga kinyongo wala kuminya haki ya mwingine. Hii italeta mazingira bora ya utawala ambapo kila aliyeko madarakani atajisikia kuwa huru hata pale anapokuwa amestaafu.

Katiba mpya itamfanya rais na watawala wenzake, kutembea bila kujishuku; na wasipotenda haki, ama watasahihishwa waziwazi, bila woga wala aibu; au watatemwa kabla muda wao wa utawala kumalizika kwani kutakuwepo utaratibu mwafaka na mwepesi wa kufanya hivyo.

Katiba isiyo na nia mbaya, inamhakikishia rais anayemaliza muda wake, utulivu kwa maisha yake yote, akila chake, akifurahia shahada zake za heshima alizopewa na vyuo vikuu ambazo zitakuwa zikipamba kuta za nyumba zake maridadi.

Rais Kikwete hana cha kupoteza kwa kuanzisha sasa mchakato wa katiba mpya. Kama kipo cha kupoteza ni woga usio na msingi. Bali kwa hili, aweza kunyakua sifa ambazo zimewashinda marais wote waliomtangulia.

Hata hivyo, nimekuwa nikipata ujumbe wa simu (sms) kutoka kwa baadhi ya wasomaji kuwa wananchi wengi hawajui katiba ya sasa inasema nini na kwamba wanahitaji kuelimishwa kwa “muda mrefu” kabla katiba mpya haijapatikana.

Nimewajibu kuwa wananchi wanajua kuwa utawala bora ni ule unaotambua, kuheshimu na kulinda haki zao binafsi za kuzaliwa.

Ni utawala unaopaswa kusimamia na kuhakikisha kuwa haki zao za kiuchumi, kisiasa, kiimani na nyingine zote zinafurahiwa na wote.

Lakini wanapoona kuwa haki zao hizo zinakanyangwa, unakuwa ujumbe wa kutosha kuwa hakuna katiba; kama ipo basi si “katiba nzuri” au hakika sio yao. Wanataka katiba tofauti; mpya.

Wanajua hakuna makubaliano kati ya watawala na watawaliwa; kama yalikuwepo basi yamefutwa au watawala wameasi; na hivyo kuna umuhimu wa kuwa na “kitu kipya.”

Ni muhimu kweli kusoma katiba, lakini haina maana kuwa ambao hawajaisoma hawajui kuwa, ama katiba haipo au iliyopo ni katili. Wanataka katiba mpya.

(Wiki ijayo: Mifano ya uhusiano kati ya katiba na maisha ya kawaida ya wananchi)

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 22-29 Desemba 2010)

KUMEKUCHA: WANANCHI WATAKA KATIBA MPYA


Waziri Kombani ametukana wananchi





Na Ndimara Tegambwage

CELINA Kombani – Waziri wa Sheria na Katiba, ametukana Watanzania. Hata akiomba radhi hatakubaliwa.

Watanzania wenye nia nzuri wanasema tuwe na Katiba mpya inayoondoa uwezekano wa wananchi kuchinjana pale watakapokuwa wameshindwa kuelewana.

Lakini Kombani anawajibu kuwa Katiba mpya haina maslahi kwa serikali wala taifa. Kwamba serikali haina fedha za kuanzisha mchakato wa kuandika katiba. Kwamba wanaodai katiba hawajampelekea madai yao.

Wenye nia njema kwa taifa lao wanasema kuwepo mkataba mpya (katiba), kati ya watawala na wataliwa; ule unaolingana na matakwa ya sasa; wenye kwenda na wakati tuliomo na siyo wakati wa ukoloni na utawala wa kikiritimba wa chama kimoja.

Lakini waziri Kombani anawajibu kuwa wale wanaodai kuwepo katiba mpya ni watu wa barabarani na wasiokuwa na uelewa juu ya masuala ya katiba na utawala.

Wenye uchungu na nchi hii wanasema kuwepo katiba inayoruhusu kila mmoja kushiriki siasa za nchi yake – kuchagua na kuchaguliwa – na siyo ubaguzi uliowekwa ndani ya andiko kuwa ili uchaguliwe sharti uwe mwanachama wa chama chochote.

Lakini Kombani anasema serikali yake inaridhika na katiba iliyopo na kwamba itaendeleza utaratibu wake kuiwekea viraka kila itakapoona inafaa.

Watanzania wenye shauku ya kuona ustawi wa nchi yao wanasema kuwepo katiba mpya, itakayokuwa mwongozo katika kila kitu ili kuepusha migogoro kwa kujenga misingi ya haki.

Wanasema ukasuku wa “umoja, amani na utulivu” si lolote si chochote, mahali ambapo hakuna katiba inayounganisha fikra za watu wote na kusimamia haki ya kila mmoja.

Lakini Kombani anasema serikali anayotumikia hailazimiki kuwa na katiba mpya kwa vile kuwa na katiba mpya siyo sera ya Chama Cha Mapinduzi.

Ni bahati mbaya kwamba tunatukanwa na mtu mdogo sana aliyeibuliwa mvunguni na kuitwa waziri. Lakini ni bahati mbaya zaidi, kwamba Kombani amemtukana na kumtukanisha Rais Jakaya Kikwete ambaye amempa kazi.

Celina Kombani, kwa kauli zake, andhalilisha umma wa Tanzania; anajenga ghadhabu mioyoni mwa wengi; anaelekeza watu watupe chini matumaini yao; wakate tamaa na kuamua kuishi utumwani milele.

Wenye nia nje na nchi hii wanasema kuwepo tume huru ya uchaguzi. Tume isiyo ya rais. Tume isiyo na madaraka ya kuteua rais, bali yenye majukumu ya kusimamia uchaguzi ili wananchi wapate matokeo ya uchaguzi wao.

Celina anasema, tena kwa jeuri, kuwa hayo hayamo katika ilani ya uchaguzi wa chama chake.

Kipofu huyu; kipofu na siyo asiyeona; hawezi kutambua haki ya wananchi kumrudi mbunge au rais wao. Hawezi kuheshimu uhuru wa wananchi kuchagua watu safi na siyo wezi wakuu na majambazi yaliyokubuhu kwa kuliibia taifa.

Celina Kombani hawezi kuona umuhimu wa fursa kadha wa kadhaa za wananchi kukataa kutawaliwa na wezi ambao wamethibitika kwa ushahidi wa mahakama.

Huyu ni waziri wa sheria anayekataa kuwa na katiba mpya inayotoa fursa zote hizo ambazo zinakuza uhuru wa mtu binafsi; kunawirisha fikra za jamii na kuwapa wananchi madaraka ya kujitawala kwa kusimamia uongozi safi uliochaguliwa.

Kwa jeuri au kutojua, Celina Kombani anasema wanaodai katiba hawajampelekea madai yao.

Kwa akili yake, anaona kuwa ana uwezo wa kushika utumwani taifa hili kama anavyopenda; na hadi atakapoamua kulifungulia.

Waziri huyu anafikiri kuwa mabadiliko ya katiba huanza kama madai ya wastaafu wa iliyokuwa jumuia ya Afrika Mashariki. Anataka orodha. Anadhani ni jambo la binafsi.

Hii ina maana yake. Kwamba akiwa mtawala, Celina hawezi kuona mambo yanayoweza kuleta hatari ya baadaye hadi atakapoandikiwa kwenye karatasi na kukabidhiwa mkononi. Kipofu.

Celina Kombani ametukosea, lakini kuna aliyetukosea zaidi kama taifa. Ni Rais Kikwete. Amemtoa wapi mtu wa aina hii ambaye anajenga mazingira ya mifarakano katika jamii?

Orodha ya watakaoitwa mbele ya mahakama ya kimataifa kueleza kushiriki kwao katika kuleta machafuko nchini Tanzania, sasa inaendelea kukua.

Tulianza na John Chiligati. Wasomaji wa makala zangu wakaleta majina mengine: Yusuf Makamba na John Tendwa.

Mmoja wa wasomaji aliandika kwa ukali. Soma aliyoandika: “Kwa nini humtaji rais? Unamwogopa?”

Sasa Kombani amejiunga na orodha ya wasiopenda nchi yao. Watu wenye shari. Wasiopenda amani. Waliotayari kuona taifa linaagamia alimradi wao wako madarakani.

Hakuna Mkenya awezaye kujivuna sana kwamba ana katiba. Ipi? Iliyokuja baada ya kukatana mapanga; kuuana na kuwa wakimbizi?

Katiba iliyochelewa, inayokuja kuzika, kukausha majeraha na kuandika kumbukumbu za maafa?

Tanzania inahitaji katiba mpya leo. Benjamin Mkapa, rais mstaafu amesikika, ingawa kwa kupitia sauti ya mwingine na katika nchi ya jirani ya Burundi. Amefumbuka.

Ni maneno yake kuwa Katiba ndiyo “moyo wa nchi; moyo wa binadamu unaofanya mwili mzima ufanye kazi.”

Rais Kikwete, Celina Kombani atafanya nini pale kama siyo kukuumbua na kukuletea uadui zaidi na Watanzania wenye nia njema kwa taifa lao?

Tisifike anakotaka Kombani. Waziri binafsi aweza kukimbia; lakini kuna sisi ambao tuliapa hatutatoka hapa, ije mvua lije jua. Kuna umma usiong’oka kwao.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 8 - 14 Desemba 2010)