Saturday, October 17, 2009

KUENZI NYERERE KWA ULEVI, USINGIZI



WANANCHI WANAAMBIWA WALALE NA HUKO WATAMSAHAU

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kumkumbuka Mwalimu Julius Nyerere kwa njia ambayo haifanani kabisa na matendo na fikra zake pale alipokuwa kiongozi wa nchi hii.

Sitaki kushiriki uchovu wa watawala unaoelekeza taifa kuwa kumkumbuka Mwalimu ni kuwa na siku ya mapumziko; siku ya kulala na kukoroma. Wengine wanaongeza hapo: kula na kuvimbiwa na kunywa na kulewa.

Nyerere aliyemaliza zaidi ya wiki mbili akichimba mtaro wa mabomba ya maji wa Ntomoko, mkoani Dodoma, hawezi kukumbukwa kwa usingizi wa pono unaotokana na ulevi wa siku nzima isiyo na shughuli ya maana.

Hapa kuna Nyerere aliyemaliza wiki nzima katika kijiji cha Muyama, wilayani Kasulu, mkoa wa Kigoma akijenga nyumba za wanakijiji. Tulikamilisha nyumba 15. Huwezi kukumbuka kiongozi wa aina hii kwa kile watawala wa sasa wanaita “mapumziko.”

Mwenyekiti wa kijiji atakwenda kwa Nyerere na kumwambia, “Mwalimu, unaona jua limekwenda; afadhali upumzike.” Nyerere atamwangalia kwa sekunde kadhaa, kumtolea macho na hatimaye kumwambia huku akicheka; kile kicheko chake cha mpasuko:

“Hah, ha, ha! Mwenyekiti, hayo si maneno yako. Umetumwa na wale paleee. Watu wa mjini wale. Naona vitambi vyao vinaanza kuporomoka. Hapana. Siyo maneno yako. Mwenyekiti, siyo maneno yako. Njoo tufanye kazi.” Ataendelea kufanya kazi.

Nyerere mchapakazi; aliye karibu na wananchi, hastahili kukumbukwa kwa kulala, kuamka, kula, kunywa, kulewa na kulala. Hapana. Nyerere asiyepumzika anaenziwa kwa mapumziko; tena ya nchi nzima? Kama siyo kejeli ni kashfa.

Kuanzia saa 12 au saa moja asubuhi, Nyerere anakata mbuga na viongozi akikagua “miradi ya maendeleo,” ya kweli na uwongo. Hapa anakuta usiku wa kuamkia siku anayofika, ndipo wamesimika miche ya kabichi udongoni. Wanamwambia, “Mzee tunajitahidi kutekeleza siasa ya kujitegemea.”

Tunazunguka bustani. Anaona. Hatimaye anachukua kifimbo chake na kusukuma mche mmoja, unaanguka. Anasukuma wa pili, unaanguka. Anasukuma wa tatu, unaanguka. Anasonya na kuondoka. Ataongea na viongozi wa wilaya au mkoa baadaye.

Ni mwenye kutambua haraka. Ni mwenye kutonywa haraka na wale wanaomwamini. Ni mwepesi wa kusikia kilichonong’onwa na kuuliza, “Kuna nini? Maana yake nini?” Huyo ndiye taifa linaongozwa kukumbuka kwa usingizi?

Twende kwenye chumba cha mkutano. Harufu. Ni harufu ya rangi iliyopakwa jana. Mwalimu anashika pua. Anaifinyanga. Anatoa kitambaa mfukoni; anaipangusapangusa kama anayetaka kupiga chafya. Anarudisha kitambaa mfukoni na kusema, “Hata kupiga rangi ni mpaka niwe ninakuja hapa?” Meseji delivadi.

Anafundisha kila aendapo. Anasema mkoa wa Shinyanga umezidi kwa ukame; sasa unageuka jangwa. Anaagiza wapande miti. Mkuu wa mkoa katika mkutano wa viongozi anasimama na kusema, “Mheshimiwa rais, tunaomba mradi wa kupanda miti uwe wa kitaifa.”

Nyerere anag’aka, “Nasema Shinyanga inageuka jangwa. Panda miti.” Lakini angalia Nyerere katika kijiji cha Mwamihanza ambako anaambiwa kuwa mzeee mmoja analima bangi. “Mimi, mimi sina tatizo kana hafanyi biashara. Wengine wanatumia majani hayo kwa dawa.”

Anawafikia wananchi wengi. Anatumia muda mwingi ndani ya nchi yake. Anasikiliza na kusikia matatizo mengi. Mwaka 2005, baadhi ya wafugaji waliokutwa Msata, mkoani Pwani, walipoulizwa wanataka kumpigia nani kura, kila mmoja alisema, “Nyerere.”

Nyerere huyo bado amegota vichwani mwao. Hakuwaibia wala kuwaswaga kama mifugo kutoka kwenye makazi yao. Leo wanahitaji njia bora ya kumuenzi mchapakazi. Siyo kupumzika. Siyo kulala.

Nyerere mwenye ujasiri wa kutunga maadili ya uongozi kwa viongozi – watu wazima na siyo watoto wa shule, akilenga uadilifu katika utawala; kiongozi wa kutangaza Azimio la Arusha na kutaifisha mashamba, majumba na mabenki, kwa nia njema kwa kadri ya uelewa wake na nia yake; leo anakumbukwa kwa kupiga usingizi? Ama ni mzaha au kashfa.

Rais aliyepeleka nchi vitani na ikarudi na ushindi – kwa sababu zozote zile za kuwepo kwa vita dhidi ya dikiteta Idi Amin Dada wa Uganda; aliyekuwa jemedari wa vita vya ukombozi Kusini mwa Afrika akifundisha wananchi kujitolea damu na uhai wao; akumbukwe kwa kula, kunywa na kulala?

Kiongozi wa nchi ambaye wakati wake elimu ya watu wazima ilifikia kiwango cha asilimia 90; aliyethamini elimu na aliyesoma wakati wote hata baada ya siku nzima ya kuongea na wakulima, kufokoeana na wataalamu wa kilimo, wakuu wa wilaya na mikoa, aenziwe kwa “mapumziko,” tena ya nchi nzima?

Mwalimu Nyerere – kile “kitabu” cha rejea juu ya fikra na maoni mbalimbali duniani; mpambanishaji hoja hadi kuitwa kaidi; aliyeandika vitabu vingi akiwa madarakani na aliyethamini elimu; sasa anakumbukwa kwa mapumziko. Ili iweje?

Kiongozi wa nchi ambaye hakupora fedha wala mali ya taifa; hakujilimbikizia mali wala kutumia vibaya kile alichopangiwa; yule ambaye alilinda utajiri wa ardhini, misitu na wanyama hadi anatoka madarakani; anakumbukwa kwa kulala usingizi wa pono.

Nyerere alikuwa binadamu. Alitokeza kwa wakati wake na kufanya mengi ya wakati wake, hasa taifa lilipokuwa linamea na kukua kuelekea tulipo sasa. Alisisitiza uzalendo – mapenzi kwa nchi, watu wake na raslimali zake.

Hili lina maana kubwa katika maisha ya taifa. Lina maana ya kutaka matumizi ya raslimali za nchi kwa manufaa ya wengi, kama siyo wote; lina maana ya kutumia raslimali za nchi kwa kiwango kikubwa ili kuepuka kuwa tegemezi. Kiini cha kujitegemea.

Taarifa zitaandikwa. Makala zitaandikwa. Vitabu vitaandikwa juu ya Nyerere na mijadala juu yake haitaisha leo wala kesho. Kiongozi aliyetetea na kuishi maisha ya aina anayofundisha – ya uadilifu; hakustahili kuenziwa kwa mapumziko, bali kazi.

Kama hili halieleweki kwa watawala ambao aliwaacha madarakani, wanataka nani aje kuwafundisha kuwa hata kama alikuwa TANU na CCM, Nyerere alikuwa mtu kabla ya kuwa mwansiasa na mtawala.

Siku ya kumkumbuka Nyerere watawala wanatutangazia mapumziko ili tule na kuvimbiwa, tunywe na kulewa na kulala usingizi wa pono ili kujisahaulisha aliyotenda au kumzika na mema aliyoyatenda? Naomba kutoa hoja: Mapumziko haya yafutwe.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii itachapishwa katika Tanzania Daima Jumapili, toleo la 18 Oktoba 2009 katika safu ya SITAKI)

Sunday, October 11, 2009

WATU NA MIFUGO YAO WATAKUFA




SERIKALI IMEKWENDA WAPI LOLIONDO?

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kuambiwa kuwa kuna serikali. Haipo. Kama ipo imelala, tena usingizi wa pono? Imezimia? Waliolala hawaamki? Waliozimia hawazinduki? Haipo!

Wafugaji wilayani Ngorongoro wanasema, tena kwa sauti kubwa kuwa kuna ukame. Kuwa mifugo yao – ng’ombe, mbuzi na kondoo haina chakula. Hakuna malisho. Hakuna maji. Mifugo inakufa. Serikali haipo.

Mwandishi kutoka Loliondo anapaza sauti, kwa simulizi na takwimu: Hakuna maji. Hakuna nyasi. Mifugo inakufa. Ng’ombe sasa anauzwa kwa Sh. 2,000 hadi 20,000. Serikali kimya.

Mfugaji anapaza sauti. Anadhani serikali haijasikia. Anasema maji yapo; wamekuwa wakiyatumia. Lakini maeneo yenye maji yamefungiwa kwenye mipaka ya vitalu vya uwindaji ambavyo serikali imegawa kwa watu wa nje – “wawekezwaji” – wale waliowekezwa badala ya kuwekeza. Serikali tebilimu!

Kuna vilio, kwamba ng’ombe wawili wameuzwa kwa debe moja la mahindi. Kwamba bei ya debe la mahindi ni kati ya Sh. 8,000 na 10,000/=. Kwamba lazima ng’ombe auzwe haraka, hata kama ni kwa hasara, kabla hajafa. Serikali haipo.

Sikilizeni sauti zao, hao wafugaji. Kwangu ng’ombe wamekufa watano. Kwangu wamekufa 20. Kwangu wamekufa 50. Elias Kagili wa kitongoji cha Kirtalo anasema: Kwangu wamekufa 100. Ni hatari tupu. Vifo. Vifo. Mwandishi kaona. Kasikiliza waathirika. Kaona na kupiga picha za mizoga. Serikali haipo.

Sikilizeni kilio cha Ole Taki Saile wa kitongoji cha Ilichooroi. Ng’ombe wake 60 wamekufa. Wengine walio karibu kuwa taabani kawauza kwa bei ya kati ya Sh. 2,000 na 5,000. Naye Lekaneti Shekuti wa kitongoji cha Sekunya anasema karibu kila siku wanakufa ng’ombe wake 10. Serikali kimya.

Kauli ya Shekuti hii hapa. “Maji yapo pale. Nyasi zipo pale, lakini ng’ombe wetu wanakufa. Kampuni ya Thomson Safari inatuzuia kunywesha mifugo yetu pale,” anaonyesha sehemu husika kwa fimbo.

Maji yako Ngorika – mwekezwaji hataki. Maji yako Polelete; mwekezwaji hataki. Maji yako Sukenya, mwekezwaji hataki. Maji yako Olkimbai, mwekezwaji hataki. Maji yako Walaasaye, nako mwekezwaji hataki yanywewe. Kote huko ni visima na vijito vilivyoko katika ardhi waliyopewa wawekezwaji ili wafanyie “utalii wa uwindaji,” au ujangili ulioruhusiwa kisheria, ndani ya nchi ya wafugaji wanaotaabika.

Teremka kijitoni au kisimani wakukute; utakiona cha moto. Sukuma mifugo yako kijitoni na wakukute; ndipo utajuta kwa nini ulizaliwa. Huu ndio ukatili unaosababisha vifo vya mifugo. Serikali haipo.

Katika mazingira ya Ngorongoro na Loliondo, vifo vya ng’ombe, mbuzi na kondoo maana yake ni vifo vya watu. Wanaohangaika kutafuta chakula na maji kwa ajili ya mifugo, wao hawana chakula. Ni mizoga inayotembea; inahangaikia mifugo yake. Siku moja itadondoka njiani. Serikali tebilimu!

Serikali imetoa ardhi ya wananchi kwa makampuni kutoka nchi za nje, iwe sehemu ya kuwindia kwa ajili ya kujifurahisha. Katika mazingira ya sasa, nyasi na maji vinapatikana katika maeneo ambako wawekezwaji hawaruhusu mifugo kuingia.

Hata hivyo, kuanzia Aprili mwaka huu, nyumba na maboma ya wafugaji yamekuwa yakichomwa moto kwa nia ya kuwafukuza wafugaji kutoka makazi yao ili wawindaji wa wanyamapori wapate kustarehe. Ni starehe ya wawekezwaji na adha kwa wananchi.

Ni ukatili. Ni unyama usiomithilika. Haustahili kusimamiwa au kuvumiliwa na wanaojigamba asubuhi, mchana na jioni kuwa wao ni walinda haki na watetezi wa demokrasi na haki za binadamu. Haiwezekani. Ni kwa kuwa serikali haipo. Serikali tebilimu!

Kama serikali ipo inasubiri nini? Inasubiri mifugo ife na kumalizika? Ili iweje? Ili wafugaji wawe masikini? Ili wawe ombaomba? Au ili wafe kama mifugo yao, huku wawekezwaji kutoka nje wakimeremeta; wakitweta kwa shibe na kunenepeana kwa faida na ziada ya uwindaji Loliondo?

Wawekezaji hutegemewa kuleta fedha. Wawekezaji hutegemewa kuongeza ajira. Je, wawekezwaji wanaleta nini kama siyo adha; wanaongeza shida na dhiki. Wanasababisha roho mbaya. Wanafungia maji na nyasi “kabatini;” ili mifugo ife; ili wenye mifugo wafe au wahame.

Sitaki kuamini kuwa kuna serikali. Ipo? Inamlinda nani? Inalinda wawekezwaji ili watanue, huku ng’ombe wa wafugaji wakifa? Huku mbuzi na kondoo wanakufa? Huku wafugaji wakisubiri kufa pia?

Kungekuwa na serikali ingeona mahangaiko ya wafugaji wa Kimaasai. Tuseme ipo lakini haioni? Ingekuwepo ingesikia kilio cha wafugaji, waandishi wa habari, wanaharakati na wafanyabiashara wanaonunua ng’ombe mmoja kwa Sh. 2,000. Tuseme haina masikio au yameziba?

Kungekuwa na serikali, kwa maana ya watawala, ingekumbuka kuwa iliapa kutumikia watu, kuwalinda na kuwatendea haki; na iliapa kwa Mungu kuwa aisaidie kuyatenda kwa ukamilifu. Tuseme imesahau kiapo? Au wafugaji na maeneo yao siyo sehemu ya Tanzania? Au kiapo kimelainika? Nani amelainisha kiapo cha serikali?

Hata kama mambo haya yangekuwa yanatendeka Nigeria au Kongo; huwezi kukaa kimya juu ya unyama wanaotendewa binadamu wa Ngorongoro. Risasi za moto zinatafuta nini katika makazi ya Wamaasai na mifugo yao?

Alikuwa Desmond Tutu aliyesema, “Ukiona mguu mnene wa tembo umekanyaga mkia wa panya, na ukaangalia pembeni na kusema hayakuhusu na wewe huna upande; panya hataelewa msimamo wako wa kutokuwa na upande katika ukatili huu.”

Kuna kila sababu ya kuwa na upande katika kutetea haki. Na haki ya wananchi kuishi kwao na kufurahia matunda ya ardhi yao, haiwezi kupitwa na ujanjaujanja wa wawekezwaji hata kama wanamwaga mabilioni ya shilingi kwa yeyote yule.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la tarehe 11 Oktoba 2009 chini ya safu ya SITAKI)