Saturday, September 26, 2009

ADHABU YA KIFO IMEPITWA NA WAKATI



Kunyonga siyo adhabu, ni kuua tu


Na Ndimara Tegambwage


SITAKI kuona wananchi na watawala wakishabikia hukumu ya kunyonga, hata kama kuna sheria ya nchi inayoruhusu mtu “kunyongwa hadi kufa.”

Sheria iliyopo ni katili, chovu, inayopaliliwa na kuendelea kurutubishwa na mfumo unaoendeshwa na watu ambao wamekuwa wagumu kuelewa mantiki ya thamani ya maisha na umuhimu wa adhabu.

Iwapo hawatakata rufaa, au wakikata rufaa na kushindwa, Masumbuko Madata, Emmanuel Masangwa na Charles Kalamuji, waweza kuuawa kutokana na hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibalila.

Jumatano iliyopita, mjini Kahama, Jaji Rwakibalila aliwakuta vijana hao watatu na hatia ya jinai ya kuua Masumbuko Dunia, mtoto wa shule, umri wa miaka 13 na mwenye ulemavu wa ngozi (albino). Sasa kuna wanaoshangilia hukumu ya kifo.

Kifo cha Masumbuko kiliuma na kuumiza wengi, hata kama hawakuwa na uhusiano wowote naye. Umri wake mdogo; nafasi yake katika jamii iliyosababisha kuitwa majina ya kumtelekeza; utu wake ambao ulikuwa na bado ni sehemu ya utu wa kila mtu; ni sehemu tu ya chimbuko la uchungu.

Uchungu unakuwa mkubwa pale jamii inaposhuhudia mauaji yakilenga watu wenye ulemavu wa ngozi; wadogo kwa wakubwa, kwa sababu dhaifu, za kijinga na potofu – eti kupata viungo vya kuwawezesha “kuwa matajiri.”

Uchungu huu usio na udhibiti, unapokutana na sheria ambayo hata Jaji Mkuu Augustino Ramadhani amewahi kusema kuwa hafurahii kuitumia, ndipo unazaliwa ukatili mpya; ule wa kuondoa uhai wa aliyepatikana na hatia ya kuua.

Mahakama Kuu nchini Tanzania iliishawahi kutamka kuwa adhabu ya kifo ni ya kikatili na ya kudhalilisha na kutaka ifutwe. Pamoja na maeneo mengine, maneno “katili” na “kudhalilisha” ni ya msingi sana katika kuchambua hukumu ya kifo.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano inakataza ukatili na udhalilishaji. Kwa hiyo kuwepo sheria inayoruhusu kuua; hivyo kuendesha “ukatili” na “udhalilishaji,” ni kuvunja katiba ya nchi. Lakini Mahakama ya Rufaa haikuafiki.

Hakuna ubishi kwamba vijana watatu wa Kahama, kwa kupatikana na hatia ya kumuua Masumbuko, walivunja haki za binadamu. Bali “haki za binadamu” haziwekwi na watu; zipo na zinahusu kila mmoja.

Watawala, sheria na hata Katiba za nchi, haziweki haki za binadamu. Ngazi zote hizo hazina uwezo wa “kugawia” watu haki za binadamu. Kinachofanyika ni kwa watawala, sheria na Katiba kutambua kuwepo kwa haki hizo na kutafuta jinsi ya kuzilinda na kuziendeleza.

Kwa hiyo, hapa siyo mahali pa hoja za jino kwa jino. Hoja ni kutovunja haki za binadamu. Kutoua. Kutofanya ukatili. Kutodhalilisha.

Hoja hii inaleta maana zaidi pale tunapojadili “thamani” ya adhabu anayopewa mkosaji. Watatu wa Kahama wamepatikana na hatia. Wamevunja haki za binadamu kwa kumuua Masumbuko. Wanastahili adhabu na ikiwezekana iwe adhabu kali.

Tujiulize. Je, hukumu inayoruhusu kifo ni adhabu? Je, kifo kinaweza kuwa adhabu? Je, adhabu hufanywa na aliyekufa? Kama sababu ya kuadhibu ni kutaka mtu ajirudi na kurejea katika utu wa jamii yake je, aliyeuawa anajirudi vipi, lini na wapi?

Hizi zinaonekana hoja ndogo kwa waliovimba vichwa na vifua, kwa hasira na uchungu wa kweli wa kupoteza watoto, ndugu, jamaa, rafiki au wenzao katika tabaka au kundi tambulishi kama walivyo albino.

Bali hasira zilizokaba koo za wafiwa; chuki zilizotunisha misuli ya shingo za ndugu wa aliyeuawa; na woga uliokumba nyoyo za wahusika; vyote vinaziba mifereji ya fikra kuhusu uhai wa mtu mwingine na nafasi ya muuaji mpya.

Vijana watatu wamepatikana na hatia ya kuua. Sheria inaruhusu wauaji kuuawa. Jaji, kwa mujibu wa sheria hajakosea kutamka hukumu hiyo kwa shabaha ya kulinda sheria na kazi yake. Bali Jaji aweza kuwa anaasi “shangazi wa mtima” wake.

Majaji wengi duniani wameeleza jinsi wanavyosutwa na dhamira zao pale wanapotamka hukumu ya kifo. Wameeleza jinsi kunavyokuwa na mapambano makali “rohoni” mwao na hatimaye kuanguka na kuwa mateka wa sheria na mfumo.

Leo kuna vijana watatu wa Kahama. Wanakabiliwa na mauti na siyo adhabu. Atakayeua vijana hao ni nani kama siyo muuaji?

Kuna tofauti gani kati ya aliyeua albino kwa panga na anayeua muuaji wa albino kwa kamba ya shingoni? Haipo. Wote ni wauaji. Mmoja anakanwa na sheria na mwingine anaruhusiwa na sheria. Wote wanatoa uhai wa watu wenye thamani ileile.

Ninaelewa ugumu wa wafiwa kuzingatia hoja hii haraka. Lakini malezi ya jamii hayawezi kwenda kwa misingi ya walioko madarakani kujipa fursa ya kuua na kujikinga na sheria walizotunga wenyewe.

Niliishawahi kuuliza katika safu hii wakati wa kujadili somo hilihili: “Kama serikali inaua, nani ataua serikali – ambayo sasa ni muuaji?” Sikupewa majibu.

Kuna haja ya kufikiri upya kuhusu sheria inayoruhusu kunyonga watu. Kunyonga ni kuangamiza maisha; siyo adhabu ya kurejesha mtu kwenye mstari wa maandili na utu wa wote.

Kunyonga ni kunyima aliyepatikana na hatia fursa ya mabadiliko katika maisha. Ni mabadiliko haya ambayo huweza kuwa mfano mkuu kwa jamii na kufanya watu wengi kukiri udhaifu wao na kuwa wanyoofu maishani.

Kuua hakuleti nafuu kwa mfiwa. Hakuna mafao kwa serikali. Hakuleti faida kwa jamii. Kunaendeleza vilio. Kunasimika hasira na chuki mpya. Kunafanya jamii ishindwe kuelewa nani anaweza kuikinga na ukatili huu.

Sheria zinazoruhusu mauaji kwa njia ya kunyonga ni za kuviziana; za kumalizana na mara nyingi, kama siyo mara zote, zinawaelemea wa tabaka la chini katika jamii. “Wakubwa” wana kila njia ya kuzipinda na hata kuzikatakata.

Sheria za kunyonga zinafanya jamii ianze kuona kuwa maisha hayana thamani. Zinafundisha usugu na kutothamini uhai binafsi na ule wa mtu mwingine. Zinazaa tabia ya “nitakuua hata kama wataniua.”

Sheria zinazoruhusu mauaji zinakomaza chuki na ghadhabu na zinafuta msamaha na tabia ya kujirudi ambayo ni nguzo kuu katika kupata suluhisho na muwafaka. Zinainyang’anya jamii ujasiri wa kufunza waliopogoka na kuikosesha jukumu la kufunza vizazi na vizazi.

Adhabu ilenge kurekebisha muhusika; kumfanya ajutie tendo lake na kutamani kurejea katika utu wake wa asili. Aliyekufa hajutii makosa yake; harekebiki pia.

Natamani kuona hukumu ya kifo ikifutwa na nafasi yake kwa sasa kichukuliwa na adhabu ya kifungo cha maisha. Aliyeua akiuawa, aliyeua muuaji anakuwa amekamilisha ukoo wa wauaji.

Katika ukoo huu, mauaji hayataisha. Hayataogopwa. Hayatapingwa kwa kuwa hayatachukiwa. Natamani yaishe. Jamii ivunje kimya.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 26 Septemba 2009 chini ya safu ya SITAKI)

Saturday, September 19, 2009

NGUVU ZA UNAFIKI NA SIASA ZA NJIAPANDA



Yusuf Makamba: Mara joto, mara baridi…

Na Ndimara Tegambwage
SITAKI tabia ya Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuwa mara baridi, mara joto, mara vuguvugu na mara baridi, tena katika muda mfupi.

Kwa mbunge, mteule wa rais, kiongozi mkuu wa utendaji katika chama kinachopanga ikulu, kuwa na tabia ya kubadilika kila kukicha au pale kipenga kinapopulizwa; siyo ishara ya kuwa makini.

Joto lilipokuja – kwa msukumo wa chama au makundi au mtu binafsi – Makamba alifura kwa hasira na kutangaza ubabe. Alifanya hivyo baada ya vikao vya CCM vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu jijini Dodoma hivi karibuni.

Alimwakia spika Samuel Sitta na wajumbe wa chama chake kumkaripia, kumtishia, kumpa onyo na kutaka kumlegeza. Ni Makamba aliyesimama na kusema, “Kama siyo CCM, Samwel Sitta ahojiwe na nani?”

Ndani ya vikao vya CCM, Samwel Sitta alikuwa anakabiliwa na tuhuma nyingi zilizopelekwa kwa njia ya mjadala juu ya hali ya hewa ndani ya chama na serikali.

Kwamba spika amejitwisha jukumu lisilo lake la “kupambana na mafisadi.” Kwamba ana upendeleo – anatoa nafasi mara nyingi kwa wenye “kupinga serikali” na hata wapinzani, kuhutubia bunge kuliko wale wanaotetea chama na serikali.

Ofisa mdogo katika ofisi ya Makamba, John Chilligati, kwa ushirikiano na Makamba au kwa kutumwa na chama chake, aliwawakia wale ambao wanadaiwa kupewa muda mwingi na spika “kukemea ufisadi,” akihoji nani aliwapa wajibu huo.

Ikaja asubuhi, ikaja jioni, siku zikapita. Makamba yuleyule, wiki iliyopita, akaenda jimbo la Urambo, mkoani Tabora. Huko ndiko nyumbani kwa spika Samwel Sitta. Akachukua sura ileile ya kuumbika na kuumbuka.

Aliwaambia viongozi wa chama chake vikaoni na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, kwamba CCM inatambua kuwa Spika Samwel Sitta anafanya “kazi yake vizuri” na hasa anafanya kazi ya chama.

Makamba wa leo siyo wa jana, wa kesho wala keshokutwa. Anaumbika na kuumbuka au kuumbuliwa. Anafura kwa hasira, lakini dakika chache zifuatazo, anatoa kicheko – cha kweli au cha unafiki.

Vyombo vya habari vimemnukuu Makamba akisema kuwa Sitta ni mbunge wao imara na kazi anayofanya bungeni ni kazi nzuri ya chama chake; na kuwataka wamuunge mkono hata katika uchaguzi ujao. Hata walokole hawafikii hatua hii.

Joto la ndani ya vikao vya CCM ndilo lilifanya Makamba awe mkali, jeuri na aongee kwa kujiamini. Wajumbe walioongea kwa kukandia Sitta, tena mbele ya mwenyekiti wa chama na rais wa Jamhuri, Jakaya Kikwete, huku wakipendekeza afukuzwe uanachama, ndio walikuwa msukumo wa Makamba.

Msukumo mwingine ulikuwa “Kamati ya Mwinyi” iliyoundwa rasmi kuchunguza “msuguano” kati na baina ya spika, bunge na serikali. Kamati iliundwa katika kikao cha Halmashauri Kuu.

Kwa maandalizi ya vikao hivyo vya Dodoma; kwa taarifa kwamba wajumbe kutoka Zanzibar walikuwa wameandaliwa rasmi kumkabili Sitta na hivyo ndivyo ilivyojitokeza; na kwa wingi wa wajumbe walioongea kutaka “Sitta amalizwe,” hakika Makamba asingekuwa na mtu wa kutembelea Urambo anayeitwa Samwel Sitta – spika.

Tabia ya Makamba ya kubadilika haraka – kutoka joto sana hadi baridi na huenda kesho atakuwa vuguvugu – huenda ndiyo inamfaa yeyote anayetaka kuwa katibu mkuu wa CCM ya sasa.

Akiombwa na kundi moja linalopingana na lingine kuwa aandae mazingira ya uhasama na mashambulizi, basi afanye hivyo. Akiambiwa sasa apoe, ananyamaza kama aliyekwenda safari.

Lakini akitekenywa kwamba amwakie fulani, kwa sababu zozote zile, atafanya hivyo. Vilevile akiambiwa kurejesha amani, atawaangukia aliokorofishana nao na kukumbuka walivyopeana pipi wakiwa darasa la pili.

Makamba anakuwa mkuu wa maabara isiyofuzu – CCM. Hawaamini kuwa waliishamaliza utafiti juu ya utengenezaji hewa ya oksijeni. Kwao utafiti ni utafiti tu usioisha hata kama waliishapata matokeo; ili mradi waonekana wako kazini, wanalipwa na wanatumiwa na waajiri wao.

Safari ya Makamba nyumbani kwa Sitta imekuja baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa kubanwa na wananchi na balozi za nchi za kigeni zilizoko Dar es Salaam, kuhusu vitisho alivyofanyiwa spika na nia mbaya ya kumdhoofisha.

Kama kwamba Rais Kikwete alijua kuwa hali hiyo ingedhoofisha uhusiano kati ya serikali yake na wananchi, asasi za kijamii zinazopigania haki za binadamu na hata nchi wahisani, akatafuta jinsi ya kulegeza msimamo kwa kutoa “maelezo ya nyongeza” kwa yale yaliyotolewa na Makamba na Chilligati.

Rais Kikwete alisema wiki iliyopita, katika kujibu “maswali ya wananchi ya papo kwa papo” katika televisheni kwamba, halmashauri kuu iliyokemea wabunge “wenye msimamo mkali,” ililenga tu kuleta nidhamu na siyo kuwatishia.

Alisema wabunge walikuwa wanatakiwa kujadili mambo ya chama chao ndani ya vikao vya chama na siyo hadharani; na kwamba kwa hatua hiyo, chama kamwe hakikulenga kuwanyamazisha.

Kama kauli ya Kikwete ilikuwa ndiyo kauli ya halmashauri kuu ya CCM, basi Makamba na Chilligati hawajui kuripoti na kuwasilisha taarifa za chama chao kwa wananchama, wananchi na dunia.

Lakini kama taarifa zao, na hasa Makamba, ziliwakilisha yaliyojiri ndani ya vikao vya chama chake; na kauli za Kikwete ni tofauti na zilizolenga kupoza wanachama na kurejesha “amani” ndani ya CCM, basi kuna mgogoro ndani ya chama hiki.

Bali kinacholeta nuru juu ya yaliyotendeka ndani ya vikao na iwapo yalilengwa; ni kwamba hakuna hatua yoyote waliyochukuliwa Makamba na Chilligati kwa kutoa taarifa tofauti na zile za chama na tofauti na kauli za mkuu wa kaya.

Dunia ya nje isiyotafiti wala kuchokonoa, yaweza kuamini kuwa aliyosema Kikwete ni sahihi na yale ya Makamba na Chilligati ni kauli binafsi au taarifa za chama zilizotiwa hamila. Kumbe sivyo.

Makamba ni mchekeshaji wa kweli. Aweza kutumika kwenye sherehe na kwenye misiba. Si yumo katika vikao vya kumsulubu Sitta? Leo kapewa ngwe ya kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Hadithi zatufundisha: Lini sungura anakuwa rafiki wa simba? Ni pale tu simba anapokuwa ameshiba au anapokuwa na swala upandeni. Bali ni urafiki wa muda.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii haikuchapishwa katika toleo la Tanzania Daima Jumapili, 20 Septemba 2009 katika safu ya SITAKI kwa sababu ambazo mhariri aliniambia kwa simu kuwa ni "matatizo ya kiufundi.) Badala yake makala ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la Jumatano 23 Septemba 2009).

Sunday, September 13, 2009

DC AKISHINDWA SERIKALI IMESHINDWA

DC Tarime anapokiri kushindwa

Na Ndimara Tegambwage


SITAKI kauli na mipango ya mkuu wa wilaya (DC) ya Tarime, Frank Uhahula aliyoitoa hivi karibuni. Inatishia maisha ya wananchi.

Gazeti hili lilichapisha habari kuwa mkuu huyo ametishia “kufuta shughuli za ufugaji wa ng’ombe mkoani Mara, endapo wenyeji wa mkoa huo wataendelea kuibiana mifugo, hali ambayo inachangia vitendo vya mauaji.”

Kwa kuwa hakuna taarifa zozote za kukanusha taarifa hiyo tangu ichapishwe, 7 Septemba mwaka huu, inaweza kuchukuliwa kuwa ni kweli alitoa kauli hiyo.

Katika hali ya kawaida, kauli hiyo haiwezi kutolewa na mkuu wa wilaya aliyepata mafunzo ya uongozi; aliyekulia katika mfumo wa uongozi au mwenye maarifa juu ya taaluma ya uongozi.

Ni muhimu kurudia, kurudia na kurudia kusema kuwa uongozi ni menejimenti na menejimenti haiji tu kwa kuteuliwa kuwa mkuu wa mahali fulani.

Ama umesomea shuleni, umepata mafunzo kwa njia mbalimbali, umeelekezwa ukiwa kazini na umetenda kwa kutumia misingi husika.

Katika baadhi ya nchi, ukuu wa wilaya na mkoa ni vyeo vinavyojazwa na watumishi ambao wamefikia ngazi fulani katika mpangilio wa madaraka serikalini. Hachomolewi mtu kutoka popote kule na kufanywa DC.

Mahali pengine vyeo hivi hupewa wale waliopata mafunzo na wenye maarifa ya uongozi na wamethibitika kuelewa jinsi ya kutumia taaluma hiyo ya menejimenti ya watu na raslimali zao.

Haikutarajiwa basi, kusikia mkuu wa wilaya ya Tarime akitishia “kufuta ufugaji” ng’ombe mkoani Mara. Amekerwa sana? Hana njia ya kukabili tatizo la wizi? Ameshindwa kazi? Anakiri kwa niaba ya serikali kwamba utawala wa nchi umeshindwa kudhibiti wizi wa mifugo Tarime?

Kama mkuu wa wilaya ameshindwa kazi, si amwambie aliyemteua, tena kimyakimya, “Mzee hapa sipawezi,” ili atafutiwe pengine au aachwe njiapanda? Si kauli ya DC inadhalilisha hata serikali nzima? Na serikali ikishindwa, wananchi wafanyeje?

Hata hiyo kauli ya DC ilitolewa mahali pabaya. Ni pale alipokuwa anazindua kikundi cha ulinzi shirikishi wa wananchi na polisi katika kijiji cha Kitenga. Je, kwa kauli hiyo alitaka kusema kuwa hata uzinduzi wa ulinzi aliokuwa anafanya haukuwa wa maana yoyote?

Kauli ya DC iligongana na kauli ya Polisi Jamii wa Mkoa Maalum wa Tarime-Rorya aliyesema ndani ya polisi kuna askari “wachache” wanaosaidiana na wezi wa mifugo. Alitaka wafichuliwe.

Kumbe tatizo siyo mifugo. Tatizo siyo wafugaji. Tatizo ni wizi. Wizi ni uhalifu endelevu unaoweza kukabiliwa na njia endelevu. Kama hakuna njia hizo endelevu, basi akili za watawala zitakwama; watalia, watalalamika na kujawa ghadhabu; watashindwa kazi.

Kwa kauli ya DC, ambayo ni kauli ya serikali, wizi wa ng’ombe ukiendelea, serikali “itafuta” ufugaji huo. Wizi wa mbuzi ukianza na kupanuka, serikali itafuta ufugaji wa mbuzi. Wizi wa kondoo ukianza na kuenea, serikali itafuta ufugaji wa kondoo; na wizi wa kuku ukishamiri, serikali itafuta ufugaji wa kuku!

Fanya mwendelezo hapa. Kila kinachoshindikana kipigwe marufuku. Watu wakiibiana mno nguo, serikali ifute uvaaji nguo. Wakiibiana mno chakula, serikali ifute kilimo cha mazao ya chakula. Wakiibiana mno fedha, serikali izuie watu kuwa na fedha!

Hii ndiyo dhana ya “Uhahulism” inayotokana na fikra za Uhahula wa Tarime. Huku ndiko kukiri kushindwa.

Uhahula anapendekeza kufuta mifugo. Maana yake ni kwamba hajui uhusiano kati ya wananchi na mifugo yao. Inaonekana hajajitahidi kujifunza mazingira ya watu aliokabidhiwa kuongoza na hana ujuzi na maarifa ya kutawala.

Mifugo ni uhai wa wafugaji. Mifugo ni mali. Mifugo ni fedha. Mifugo ni benki. Mingi au michache kama ilivyo, mifugo ndio utajiri wa pili kwa wafugaji. Kwanza ni watu – ndugu na marafiki ulionao; na pli ni mifugo.

Kwa hiyo kutenganisha wafugaji na mifugo ni kuwaondolea uhai – chakula – lishe ya nyama na maziwa. Ni kuwaondolea usalama wa maisha – watakosa kinga na kimbilio pale watakapokuwa na matatizo ya kiuchumi.

Kufuta mifugo ni kupora mali za wafugaji; ni kuwaibia fedha; ni kubomoa mabenki yao; ni kuua udugu, urafiki na uwezo wa jamii wa kujilisha, kujitunza na kuweka misingi kwa jamii zao za baadaye.

Hili ndilo linadhihirisha hatari iliyopo pale viongozi wanapokuwa hawakutokana na mkondo wa ngazi za utawala; wanapokuwa wa kuotesha tu, na hasa wanapokuwa wanaamini kuwa kila kitu huenda kwa amri na siyo fikra na ushawishi.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba mkutano alikohutubia DC haukuwa wa wezi wa ng’ombe. Ulikuwa wa wafugaji na wananchi wengine, hata kama ndani yake kulikuwa na watuhumiwa wawili au watatu.

Kwa hiyo vitisho vya DC, kama vililenga wezi, basi havikuwafikia au viliwachochea. Kilichofika kwa wengi ni hatua za uonevu ambazo serikali wilayani ilikuwa inaahidi kwa watu na mali zao. Huu siyo uongozi. Siyo utawala.

Kuna haja ya kurudia kuuliza: Serikali ikishindwa kazi ya ulinzi wa watu na mali zao, na ikakiri hivyo, wananchi wafanyeje? Labda wananchi na viongozi wao wa kweli wanajua. Tuwasikilize.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii imechapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo ya 13 Septemba 2009)

Saturday, September 5, 2009

UJANGILI ULIORUHUSIWA NA SERIKALI

Uwindaji wa leseni ni ‘ujangili’ pia
• Maliasili ya Tanzania, dunia itaisha

WAFUGAJI wanaofukuzwa kwenye makazi yao katika mbuga wana mengi ya kusema. Wengi hawana elimu ya darasani lakini ni wajuzi wa mazingira yao na wepesi wa kutambua mabadiliko. Hapa wanasema wanachoona ambacho serikali inaweza kufuatilia ili kuokoa maliasili wanyamapori.


Na Ndimara Tegambwage

WAMECHOMEWA makazi. Wakapigwa na wengine kuswekwa rumande kwa madai kuwa wamekaidi amri ya kuhama mbuga ambamo wameishi kwa miaka nendarudi. Lakini bado wana uchungu na nchi yao.

Wana uchungu na maliasili za Tanzania. Wanapendekeza kuwa uwindaji katika mbuga ungesimamishwa ili kuruhusu wanyamapori kuongezeka na kurejesha utajiri mkubwa wa taifa na dunia.

Wafugaji wa ng’ombe, mbuzi na kondoo ambao wameishi kwa kuingiliana sana na wanyamapori, wanasema serikali ingeweka sheria kali, kama hazipo, au kusimamia zilizopo ili kuokoa maisha ya wanyamapori.

“Sisi ndio walinzi wa wanyama hawa, usione wanatufukuza. Tungewabughudhi wasingekuwa hapa. Wala hatuwali. Sisi tunakula mifugo yetu. Lakini kwa mtindo wa sasa, wanyama watatoweka,” anaeleza mkazi wa kijiji cha Ololosokwan.

Kuna masimulizi mengi na marefu juu ya wanyamapori wanavyouawa kwa wingi. Mwanaume wa umri wa kati kijijini hapa anasema, “Kwa mfano, simba ni simba tu. Hawana mbadala. Kama simba watamalizika, hakuna tunachoweza kuona katika nafasi yake kiitwacho simba.”

“Tumeona mengi humu Loliondo. Hata wenzetu kutoka mbali wamekuja na kusimulia kuwa hali ni hiyohiyo. Wawindaji kutoka nje ya nchi wanaua hata watoto wa simba,” anaeleza.

Kijana wa umri upatao miaka 25 wa kijiji cha Magaiduru-Lorien anadakia na kusema, “Nimewahi kuona watalii wamebeba watoto wa simba na puma ndani ya gari lao.”

Kijana mwingine anaingilia kati, “Unasema simba tu? Mwaka jana wanamgambo wanaohudumia jumba la mfalme wa Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE) pale kilimani, walipita wakitangaza kuwa atakayepata chatu akiwa hai atalipwa shilingi milioni moja (1,000,000/=).”

Swali: Kwa hiyo na wewe uliingia vichakani kuwinda chatu?
Jibu: Hapana. Mimi nina shughuli zangu. Angalia ng’ombe wote hawa (kama 1,200).
Swali: Si ungemwambia mdogo wako akachangamkia hilo?
Jibu: Tuliacha wengine wanaohitaji fedha za haraka watafute.
Swali: Sasa chatu alipatikana?
Jibu: Alipatikana. Tulisikia walipatikana sita, wakubwa kwa wadogo. Waliwachukua wakiwa hai.
Swali: Kwani wewe umewahi kuona wanyama wakisafirishwa wakiwa hai?
Jibu: Si unaona uwanja wa ndege ule pale (ndani ya Loliondo)? Madege makubwa yanatua hapo hata yenye uwezo wa kubeba magari makubwa. Nendeni ukaulize maeneo yale utapewa taarifa. Hata simba na chui wachanga wanasemekana kuchukuliwa…lakini usinifanye shahidi wako.

Ni madai makubwa na mazito. Yanahitaji kuthibitishwa. Wafugaji wanasema walichoona. Huenda wanyama wanaodaiwa kuchukuliwa kutoka mbugani wakiwa hai ndio tunawakuta katika “hifadhi za wanyama” mijini (mazuu) katika baadhi ya nchi za nje.

Maelezo ya aina hii yanafanya wafugaji wakazi wa mbuga za Loliondo wachukiwe na watu kutoka nje ambao walipewa mbuga kufanyia biashara ya utalii na bila shaka baadhi ya maofisa wa maliasili wanaoshirikiana nao.

Mbuga za Loliondo ziko chini ya kampuni ya Ortelo Business Corporation (OBC) ya Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo imekuwa ikiendesha biashara ya utalii wa uwindaji wanyama na upigaji picha kwa karibu miaka 17 sasa.

Wafugaji wanachukiwa kwa kuwa “wanasema uongo.” Kusema uongo, katika hali hii ni kusema ulichoona; kwamba wanaoitwa watalii wanafanya zaidi ya kile walichotarajiwa kufanya.

Kuna masimulizi kuwa “watalii” – ambao wananchi hapa wanapenda kuwaita “majangili wenye leseni” – wanaua hata wanyamapori ambao hawapo kwenye orodha ya kuwindwa na kuchukua hata wanyama hai.

“Uwongo” wa aina hii ni aghali. Vijana wengi wanasema wakijulikana kuwa wametoa taarifa kwa watu wa nje, huenda wakakamatwa na “kuwekwa ndani.”

“Kweli, mfano tukijulikana kuwa tuliongea nanyi kuhusu mambo haya, wanaweza kutupoteza au kututupa rumande kwa muda mrefu mpaka tukakuta mifugo yetu yote (ng’ombe 210, mbuzi 90 na kondoo 45) vimeibwa,” anaeleza kijana akitupa macho huku na kule.

“Sisi tunawajua wanyamapori. Wakiongezeka tunajua; wakipungua tunajua,” anasema Mzee Ngirimba mwenye umri wa miaka 59 kutoka kijiji cha Arash ambaye alikutwa Ololosokwan.

Bali kama ambavyo hakuna mbadala wa simba, vivyo hivyo hakuna mbadala wa swala, tembo wala digidigi.

Kwa mfano, taarifa kuhusu idadi ya wanyamapori zinaeleza kuwa swala-twiga wamepungua sana katika mbuga nyingi nchini. Tandala wadogo na tandala wakubwa – wote wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Wanyama wengine ambao wakazi wa mbugani na baadhi ya maofisa wanyamapori wanakiri wamepungua ni digidigi wadogo ambao hutembea wawili-wawili na palahala.

Lakini wazee sita waliohojiwa juu ya wingi wa simba katika maeneo yao, walisema hata simba, chui, duma na mbwamwitu wamepungua.

“Hatuna elimu juu ya taratibu za wanyamapori na uwindaji, lakini tunajua kuwa siyo wanyama wote wanaowindwa. Lakini huku kwetu huwa tunaona wanapiga tu kila mnyama,” ameeleza mmoja wa wazee wa Olorien.

“Kwa mfano tumeona walioua twiga na siku zote tunaambiwa kuwa twiga siyo mnyama wa kuwinda,” anaeleza.

Anasema amesikia kuwa hata simba, duma na chui hawastahili kuwindwa lakini wameona wawindaji wa kitalii wakiburuta mizoga ya wanyama hao.

Masimulizi juu ya uwindaji shelabela – unaoua wanyama wakubwa na “watoto wao;” ukamataji wanyama hai na usafirishaji wake nchi za nje, ni mambo ambayo wafugaji katika mbuga wanasimulia kwa uwazi.

Wauaji wakuu wa maliasili wanyamapori ni wale wenye leseni za kuwinda. Wanadaiwa kuua wanyama wengi kuliko idadi ya waliopangiwa na wanaua hata wale wasio kwenye orodha ya kuwindwa, wenye mimba na wachanga.

Wawindaji wa aina hii basi, hata kama wana leseni, ni wahujumu ambao tunaweza kukubaliana na wananchi wa eneo hili wanaowaita “majangili wenye leseni.”

Uwindaji wa aina hii unateketeza wanyamapori; unaua vizazi vya maliasili hii adimu duniani. Walinzi wa mbuga na wanyama waliomo wana mapendekezo, kama anavyosema mmojawao katikamahojiano:

Swali: Kwa hiyo unaona afadhali utalii wa kuwinda wanyamapori upigwe marufuku?
Jibu: Wewe! Nani atakubali hilo? Hawa wazungu na waarabu wanaokuja wanataka kujiburudisha na serikali yetu inataka fedha. Unadhani nani atakubali hilo?
Swali: Kwa hiyo waendelee kuwinda?
Jibu: Hapana. Sisi tunaona wakisimamisha uwindaji kwa miaka kumi (10) wanyama watazaana na kuongezeka. Kuanzia hapo uwekwe utaratibu wa kuzuia kuangamiza wanyamapori.
Swali: Unadhani uuaji wanyama bila kujali nani ana mimba, nani ana umri mdogo na nani hastahili kuwindwa unatokana na nini?
Jibu: Sisi hayo hatuyajui. Hatuna majibu. Tunaona ni ukatili tu. Labda pia hawana mtu wa kuwaongoza ili kuwaambia ‘huyu msiue.’ Lakini tunaambiwa kuna masharti wanayopewa kabla ya kuingia kwenye mbuga kuwinda.
Swali: Na hili la kubeba wanyamya hai?
Jibu: Kwanza hilo hatukulikubali haraka. Tulidhani vijana wanasema hovyo. Jinsi siku zinavyokwenda ndipo tukapata ukweli. Inaonekana hakuna usimamizi. Hilo halipo hapa Loliondo peke yake. Tunasikia hata Serengeti katika eneo la Gumeti (Grumet).

Mzee huyu anasema hawajui iwapo wawindaji wa kitalii wanaruhusiwa kubeba nyama na kupeleka kwao

Wafugaji ndio wamekuwa walinzi wa mbuga. Wanyama wote waliomo wamekusanyika, kuzaana na kuishi bila bughudha kwa kuwa wafugaji hawakuwawinda.

Dunia nzima inayokusanyika katika mbuga za Tanzania inakuja kushuhudia, bahati mbaya bila kujua, utashi, ujasiri na mapenzi ya wafugaji kwa wanyamapori. Bali leo hii wafugaji na mifugo yao wanaswagwa nje ya makazi yao na mali zao kuharibiwa.

Laiti wanyama wangekuwa na uwezo wa kutambua kuwa marafiki wao wa karibu, wa miaka mingi, wanatendewa ukatili. Wangepinga kwa maandamano na kauli kali.

Tetesi hizi ni muhimu kwa serikali na dunia nzima. Wanaopenda wanyama na mapato kutokana na wanyamapori, sharti wachukue baadhi ya hatua zifuatazo:

Kwanza, kufanya uchunguzi juu ya madai ya walinzi wa miaka mingi wa wanyamapori. Hawa ni wafugaji ambao wamekuwa karibu na wanyama kiasi cha kujua hata tabia zao.

Pili, uchunguzi uongoze katika kuchukua hatua madhubuti za kusimamisha uwindaji wa kiharamia katika mbuga zote nchini. Hii ni kuzuia uteketezaji maliasili ya dunia.

Hatua hizi zitazuia pia ukamataji na usafirishaji wanyama hai nchi za nje, kama utakuwa umegundulika na kuthibitika; na au kusitisha uwindaji kwa kipindi kirefu ili kuruhusu wanyamapori kuongezeka.

Tatu, kuangalia jinsi ya kusimamisha uwindaji wa aina fulani ya wanyamapori na kuweka usimamizi wa kutosha wa mamlaka ya wanyamapori katika hatua zote za uwindaji.

Nne, kubadili masharti ya miliki au ukodishaji wa mbuga ili kuondoa ukiritimba wa wamilikishwaji au wenye leseni.

Wamiliki au wenye leseni za kukodi wanapokuwa na mamlaka kama yale ya nchi, waweza kufanya wapendalo ikiwa ni pamoja na kuua kishelabela na hata kuhamishia wanyama nchi za nje.

Tano, kuacha kuchoma makazi ya wafugaji na kusitisha hatua za sasa za kuwafukuza, wao na mifugo yao, kutoka kwenye mbuga. Badala yake watengewe maeneo ya kilimo na mifugo pale walipo.

Mashamba madogo ya mahindi ya wafugaji, chini ya kilima ambacho kilele chake ndiko liliko “kasri” la mfalme wa UAE, yanaonyesha mabadiliko muwafaka katika maisha ya wafugaji.

Wafugaji hawa, wanaoanza kuwa wakulima pia, wanaendelea kuwa walinzi wa wanyamapori na chanzo cha taarifa muhimu za kunusuru maliasili ya Tanzania na dunia. Huu nao ni ulinzi wa aina yake. Serikali yaweza kuanzia hapa.

Wako wapi akina Luteni mstaafu, mfugaji na mkulima, Lepillal ole Molloimet, ili wajiunge na jumuia ya kimataifa katika kusemea wasio na sauti na kupigania maliasili za taifa na dunia?

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(MAKALA HII ILICHAPISHWA KATIKA GAZETI LA MwanaHALISI TOLEO LA 19 AGOSTI 2009)

ASKOFU KAKOBE ATAMANI UDIKITETA



KUZIMA MAWAZO KWAWEZA KULETA VURUGU;
KUKUBALI YATOKE KWAWEZA KUZIEPUSHA


Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Askofu Zakaria Kakobe wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) ajiingize katika mjadala ambao hauwezi na hautaleta manufaa kwa kanisa wala waumini wake.

Mapema wiki iliyopita alinukuliwa akiwaambia waandishi wa habari kuwa Rais Jakaya Kikwete amezidi kwa upole kwa vile hajakemea kanisa Katoliki kwa kutoa “Waraka” wa elimu ya uraia kwa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kakobe alisema pia rais amekuwa mpole mno kwa kutokemea Shura ya Maimamu kwa kutoa “Muongozo” wa waislamu ambao maimamu wanasema unalenga kumwelimisha mwislamu juu ya nafasi yake katika siasa za nchi hii.

Askofu wa kanisa la FGBF anasema maandishi haya yanaweza kuleta utata mkubwa na hata mifarakano katika jamii. Alimpongeza Kingunge Ngombale-Mwiru, mbunge mteule wa rais, kwa kukemea Waraka na kufikia hatua ya kusema “wauondoe” na kwamba Ngombale-Mwiru “aliona mbali.”

Lakini ukali wa rais unahitajika kwa lipi hapa? Katoliki wanasihi wananchi kujadili aina ya viongozi wanaowahitaji na ndio hao wawapigie kura. Wametoa andishi la kusaidia kuendesha mijadala miongoni mwa waamini na jamii kwa jumla.

Shura ya Maimamu imetoa andishi la kukumbushia lawama zao kwa utawala; malalamiko kuhusu kubaguliwa; nafasi ya mwislamu katika siasa za awali katika kutafuta uhuru na kuhimiza waislamu kuwachagua waislamu au wale wanaoona wataendeleza maslahi yao.

Kwanza, tujadili ukali wa rais. Huyu ni mtawala mkuu wa nchi. Ametokana na mfumo wa utawala ambao analazimika kuulinda, kuutetea na kuuendeleza. Ni mfumo huo ambao unatoa viongozi wanaolalamikiwa kwa kutokuwa makini.

Rais awe na ukali upi zaidi; wa kiasi gani kuliko huu alionao sasa; anaoutumia na kuusimamia na unaosababisha kupatikana kwa viongozi wanaolalamikiwa?

Askofu Kakobe anasema Rais Kikwete anatembeza tabasamu tu. Lakini tabasamu la rais ni ishara ya utulivu wake moyoni; kwamba hana presha; kila kitu kinakwenda kama anavyotaka na kwa mujibu wa mfumo anaosimamia.

Laiti Kakombe angejua kuwa mfumo wa jana na leo, ambao rais anasimamia, ni wa kibaguzi; unanyima fursa ya kuwa kiongozi wa siasa mpaka uwe mwanachama wa chama cha siasa.

Ni mfumo katili unaokufungia katika “mahabusu” ya chama hichochicho kiasi kwamba ukihama unakuwa umejifukuza kazi uliyopewa na umma kwa njia ya sanduku la kura.

Vilevile ukiwa na maoni tofauti, hata yanayolenga kuimarisha chama chako, kama yanaelemea baadhi ya wazito ndani ya vikao vya juu vya chama hicho kilichoko ikulu, basi utakuwa unajipalia mkaa; tena wa moto. Utawindwa. Unaweza kuuawa kisiasa. Huo ndio mfumo ambao rais anasimamia huku akiwa anatabasamu.

Katika mfumo huu ndimo aliyeiba mabilioni ya shilingi anasamehewa kwa kurejesha kiasi, lakini aliyeiba chungwa anafungwa miaka mitatu. Ubaguzi mzito.

Ni humuhumu ambamo kuna makubwa ya kukamua utajiri wa taifa hili. Mikataba ya kinyonyaji; wizi wa waziwazi kabisa wa fedha za umma; uporaji raslimali hata wanyama, magogo na mchanga.

Yote haya, hata kama hayakuanzishwa na viongozi wa utawala wa sasa, yako chini ya utawala wa rais anayeambiwa na Kakobe kuwa anunie barua ya kanisa kwa waamini na malalamiko ya waslamu.

Pili, katika mfumo huu ndimo kuna waandishi wa Waraka na Muongozo. Machapisho haya yanaeleza ama jinsi ya kujikwamua kutoka katika mazingira tuliyomo kwa kuwa na viongozi wakweli na thabiti; au yanawasilisha maoni ya makundi na watu binafsi katika mustakabali wa siasa za nchi yao.

Sasa Kakobe anataka rais awe mkali katika kuzuia maoni ya makundi, asasi na taasisi za wananchi? Akifanya hivyo atajuaje maoni yao? Atajuaje kuwa anapingwa katika hatua hii au ile? Atajuaje malalamiko na lawama ambazo serikali yake inabebeshwa?

Askofu Kakobe atakuwa ameona kuwa baadhi ya madhehebu duniani yameingia katika mageuzi ya fikra. Yanakiri kuwa hayawezi kuhudumia “roho za waamini na na waumini bila kufikiria hali zao kidunia.”

Roho za wafuasi wa madhehebu hayo zinakaa katika makasha yaitwayo “miili.” Kama miili itakuwa imedhoofika kwa njaa, maradhi na ujinga, hata kile wanachohubiriwa ili kukidhi matakwa ya roho hakitaingia.

Kunahitajika maandalizi ya roho. Haya yanaanza kwa kutambua kuwa kuna mwili. Kwamba mtu yupo; tunamwona na anashikika; siyo wa kufikirika. Kwamba ana mahitaji ambayo sharti ayapate ili aweze kuwa na uwezo wa kupokea mahubiri.

Maandishi makuu kwamba binadamu haishi kwa mkate (chakula) peke yake yana makali ya pili; kwamba binadamu haishi kwa kuhubiriwa tu, bali kwa chakula pia na mahitaji mengine ya mwili.

Ukamilifu wa mwili unahitajika ili kupata ukamilifu wa roho. Mbingu siyo kwa watu masikini na hohehahe peke yao, bali hata matajiri kwa njia ya halali ambao wamepondeka mitima.

Hii ndiyo maana hata kama rais hataki Waraka au Muongozo, sharti ajitahidi kuvisoma, kupata maoni ya wengine, kuyachambua na hata kuyatumia kutekeleza yale ambayo maandishi yanasema hata kulalamikia.

Bali kuna tabia ya serikali kuhusudu ukimya wa watu, ujinga na umasikini wao. Hii ni mitaji mikubwa ya serikali nyingi duniani. Vilevile ni mitaji mikuu ya baadhi ya madhehebu ambayo yanataka “kupakia” wananchi mahubiri kama anayepakia gunia.

Wanaohubiriwa ni watu wenye akili timamu na wana uwezo wa kufikiri. Wakipata fursa ya kujadili na kufanya maamuzi, wanaitumia vilivyo kuliko kutaka rais awanunie, awazibe mdomo na hivyo kuziba akili zao ili wasifikiri. Hapa Kakobe amekwama.

Fikra za Kakobe zinafanana na za serikali ya Zanzibar ambayo juzi ilitangaza kupiga marufuku Waraka na Muongozo. Bali hii siyo mara ya kwanza kwa serikali ya Zanzibar kufanya viroja.

Kuna wakati ilizuia ufundishaji wa historia (na fasihi?) mashuleni kwa madai kuwa historia inaibua chuki na uhasama. Haya ni maamuzi ya woga, ya kidikiteta; yenye shababa ya kudhibiti akili za watu na utashi wao.

Mbona nchi hii inahitaji nyaraka nyingi tu zenye maoni mbalimbali, tena ya mirengo tofauti. Zinaweka wazi maoni ya waandishi na wananchi. Zinasaidia watawala kuona walikofika au walikoshindwa kufika.

Kuziba maoni ni kujifungia katika kiza cha ujinga na ubabe wa kidikiteta. Ni kuhalalisha juhudi za wananchi, kupitia asasi mbalimbali, kuandaa mikakati halali ya kuondoa watawala madarakani.

Hata katika ukimya wa uzao wa udikiteta, mawasiliano hupenya na mikakati huundwa. Kipi bora: Kupata maoni ya wananchi au kusubiri hasira zao zijae vifuani na utokee mlipuko?

0713 614872
ndimara@yahoo.com

(Makala hii itachapishwa katika safu ya SITAKI ya gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 6 Septemba 2009)