Friday, May 22, 2009

JINSI SERIKALI INAVYOTAKA KUUA UHURU WA MAONI

Serikali inavyotaka kuua uhuru wetu

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI serikali iwe kipofu au ifanywe kipofu. Kuwa kipofu ni tofauti na kutoona. Wakati kutoona ni kuondokewa na uwezo wa kuona, kuwa kipofu ni kupoteza fahamu na akili, na mara nyingi kwa kudanganywa au kwa utashi binafsi unaotokana na tamaa na, au ujinga.

Kwa mapendekezo mapya katika Sera ya Habari na Utangazaji, kwamba mtu mmoja ataruhusiwa “kumiliki aina moja tu ya chombo cha habari, kama ni magazeti, au redio au televisheni, na siyo vyote kwa wakati mmoja,” basi serikali imejitia upofu.

Kujitia upofu ni kukataa kufikiri. Ni kukata tamaa. Ni kujisalimisha kwa vihoja na viroja. Ni kushindwa kujitazama na kujitathmini. Ni kutafuta visingizio vya kuziba penye udhaifu. Ni kukoleza kulala na kusinzia kwa mishipa ya fahamu.

Kinachokoleza upofu katika mapendekezo ya marekebisho ya Sera ya Habari na Utangazaji ni maelezo ya nyongeza. Inatajwa kuwa mmiliki aliye na vyombo vyote hivyo, “apewe muda wa miaka mitano kuuza hisa za vyombo vyake vingine.”

Kwa mujibu wa muundo, kanuni na taratibu nchini, vinavyoitwa vyombo vya umma, hakika ni vyombo vya serikali. Uanzishwaji, uendeshaji, uwajibikaji na hata ugharimiaji wake, vyote ni kwa mfumo wa kumilikiwa na serikali na siyo “umma.”

Mateka wa kwanza basi sharti awe serikali ambayo kwa jina la “umma” inamiliki redio, televisheni na magazeti. Huu ndio mgongano wa kwanza wa maslahi katika utekelezaji kwa upande wa serikali.

Kwa takribani miaka 24 sasa, baadhi yetu tumetaka serikali iachie vyombo vya habari inavyomiliki ili iandikwe na kutangazwa kama inavyoonekana na siyo kwa kurembwa, kuonewa haya au inavyotaka. Serikali imekataa.

Tumependekeza serikali ijiondoe katika umiliki wa vyombo vya habari ndipo itapata hadhi na uhalali wa kuvisema na kuvikosoa, badala ya mtindo wa sasa ambapo serikali ni mshindani kama wengine lakini inatumia nafasi yake kukandamiza mshindani mwenzake.

Serikali imekataa yote hayo. Imebaki mmiliki wa vyombo vya habari; msajili wa vyombo vingine vya habari, mtunga sera, msimamizi wa sera, mdhibiti wa vyombo vya habari na bado mshindani miongoni mwa wenye vyombo vya habari. Mgongano wa maslahi.

Bali kwa uzoefu wa ukaidi wa serikali, hatutaona ikiuza redio, televisheni au magazeti yake. Tutashuhudia shinikizo kwa wenye vyombo kuuza vyombo vyao.

Mapendekezo ya sera ndiyo huzaa sera na hatimaye kuelekeza mfumo wa sheria. Marekebisho yanayopendekezwa kwenye sera ya mwaka 2003 yanaonekana yamelenga mtu mmoja au wawili wenye kumiliki aina nne za vyombo vya habari – redio, televisheni, magazeti na shirika la habari.

Hata hivyo, katika haraka ya serikali ya kudhibiti iliowalenga, haitaji Shirika la Habari kuwa aina nyingine ya chombo cha habari katika kifungu 2.3.2 kinachosomeka, “Maelekezo ya Sera.”

Wenye aina tatu za vyombo vya habari ambao serikali inaweza kuwa imelenga, ni Reginald Mengi, Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP na Media Solutions anayemiliki redio, televisheni na msululu wa magazeti, baadhi yakiwa na msimamo mkali wa kukosoa na kuibua taarifa za rushwa na ufisadi.

Mwingine mwenye aina tatu za vyombo vya habari ni Anthony Diallo, mmiliki na Mtendaji Mkuu wa Sahara Communications yenye redio, televisheni na gazeti moja.

Katika siku za hivi karibuni ni Reginald Mengi ambaye amelalamikiwa na serikali kwa kuipa nguvu hoja ya ufisadi nchini. Ameibuka na majina ya watu watano aliowaita “mafisadi papa.”

Hoja ya Mengi ilipojibiwa na mmoja wa waliotuhumiwa, Rostam Aziz, naye Waziri wa Habari George Mkuchika akaibuka na kudai kufunga mjadala huo kwa madai kuwa unataka “kuligawa taifa.”

Vyombo vya habari vya IPP na Media Solutions, hasa magazeti – This Day, KuliKoni na Nipashe – vimejizolea tuzo katika ushindani wa kuandika habari za uchunguzi katika rushwa na utawala bora.

Aidha, ni vyombo vya IPP, hasa televisheni, ambayo imemulika hata kelele za chinichini na mikwaruzo kati na baina ya wabunge na kutoa mwanya kwa wengi kujieleza, ambao bila chombo hicho, wangepotea kimyakimya kutoka jukwaa la siasa.

Mapendekezo ya serikali basi, yanalenga kuzima nguvu ya vyombo hivyo; mvumo na mfumo wake ratibishi na hatimaye kurejesha taifa katika usiku wa giza nene la upungufu na hata ukosefu wa taarifa ambazo, bila vyombo hivyo zisingepatikana.

Serikali inalenga kuua stadi na uwezo wa viwango ainaaina wa watumishi katika vyombo hivi; kwani pamoja na kupendekeza kuwa wenye aina zote tatu wauze hisa za aina nyingine mbili za vyombo vya habari, hakuna mwenye hakika ya vyombo vilivyouzwa kuendelea kukua, kushamiri na kutumika kwa malengo na manufaa yaliyotarajiwa.

Hapa kuna mkakati wa kuua ajira ya mamia, kama siyo maelfu ya wafanyakazi wanaotegemea vyombo hivi na wengi wanaotegemea mafao yatokanayo na mishahara ya watumishi katika vyombo hivi.

Mapendekezo ya serikali katika sera yanalenga kuzima ujasiri katika uandishi wa habari za uchunguzi; ujasiri uliopatikana baada ya muda mrefu wa mafunzo darasani na kwa njia ya vitendo.

Haya ni mapendekezo maalum ya kuzima ushindani wa kibiashara kati ya vyombo vya habari vya serikali na vyombo binafsi na kurejesha wananchi katika mazingira ya kutokuwa na utashi juu ya chombo gani wanataka kiwape habari na taarifa.

Mapendekezo yanalenga kukatisha tamaa na kuogofya wale ambao tayari walikuwa wamehamasika na wanataka kuanzisha vyombo vingine vya habari.

Hatua ya serikali kupitia mapendekezo, inalenga kupunguza kiwango cha taarifa zilizokuwa zinawafikia wananchi. Hii ina maana ya kujenga mazingira ya uficho zaidi kwa serikali na watendaji wake. Uko wapi uwazi bila vyombo vingi vya kuuweka wazi?

Hatari kubwa ipo kwenye uhuru wa maoni. Hapo ndipo kuna janga. Kuwepo kwa vyombo vingi vya habari kunaweka mazingira ya wananchi wengi kutoa na kupata habari na taarifa; kubadilishana mawazo, kuelimishwa na kuelimishana na kuwa na maoni yao juu ya mambo mbalimbali.

Sauti nyingi za wananchi juu ya wanavyoona utawala na wanavyotaka uwe; juu ya furaha, huzuni, pongezi, malalamiko, vilio, shangwe na maafa, huweza kufika kwa wenzao na watawala kama kuna vyombo vingi vya habari.

Kupunguza idadi ya vyombo vya habari katika mazingira ya sasa, ni kutaka kuziba mifereji ya fikra na elimu; ni kutoa mwanya kwa uvumi na ujinga; ni kutaka wananchi wasikilize sauti moja kutoka kileleni; ni kuzika wananchi wakiwa hai katika mazingira ambamo hawatasikika wakipambana au wakilia na kuomba msaada.

Turudi darasani kidogo na kwenye uzoefu. Uhuru wa maoni kwa maana ya uhuru wa kujieleza, haukamiliki mpaka mtu aseme maoni yake – kwa kauli au vitendo.

Ni mpaka maoni yake yasikike kwa mwenzake, kundi au halaiki; au yachapishwe kwenye gazeti, au yatangazwe kwenye redio au televisheni. Vyombo vya habari ndivyo husaidia kukamilika kwa takwa la uhuru wa maoni na ndio maana vyombo hivyo ni sehemu ya uhuru wa kujieleza.

Sasa serikali inapendekeza wenye vyombo waviuze. Labda wanao wanunuzi. Wamuuzie nani ambaye ataviendesha kama vilivyokuwa vinaendeshwa. Mapendekezo haya ndiyo yanatarajiwa kuwa katika sheria mpya ya uhuru wa habari na uhuru wa kupata habari. Hii ni hatari.

Kama pendekezo la serikali litapitishwa na wadau, au litashinikizwa, sheria itakayotokana na sera hii itakuwa moja ya sheria za kishetani ambazo wadau wa habari wamepinga tangu 1985.

Bali kuna masomo mawili yanayopatikana hapa. Kwanza, pendekezo la serikali, ikiwa mdau katika huduma na biashara ya habari, linadhihirisha kuwa imeshindwa mbinu za ushindani na sasa imeamua kutumia mabavu kwa njia ya sera na sheria.

Pili, serikali imejipanga kuingilia uhuru wa wananchi wa kupata habari na kuwa na maoni. Itafanya hivyo kwa kuviondoa vyombo vya habari ambavyo tayari vilikuwa vimepenya jamii na vinakimbiliwa na wengi ili kutoa taarifa.

Mapendekezo ya serikali hayakubaliki na kila mwenye nia njema kwa taifa hili anaitaka serikali iyatupilie mbali. Inabidi hata walioyaleta wajue kuwa wao siyo wapangaji wa kudumu serikalini. Zimwi wanalojaribu kuumba watalikuta nje ya lango pindi wakiachishwa, wakifukuzwa kazi au wakistaafu.

Serikali ingejizolea heshima kwa kuhimiza watu binafsi na asasi mbambali kuanzisha magazeti mengi na vituo vingi vya redio na televisheni, bila kujali nani ana vyombo vya aina zipi. Kinachohitajika ni taifa linaloongea; na siyo la watu walionyang’anywa uwezo wa kuwa na maoni na vyombo vya kutolea maoni hayo.

Hivi kwa nini mtu akatae kujiandalia mazingira mazuri ya uhuru uliotamalaki na badala yake ajiandalie mahabusi akingali madarakani? Tusikubali vipofu wajinyonge. Tuwanyang’anye kitanzi.



0713 614872
ndimara@yahoo.com

(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili, toleo la 24 Mei 2009)

Saturday, May 16, 2009

SERIKALI IKITENDA JINAI, WANANCHI WAFANYEJE?


WAZIRI MKUCHIKA (pichani juu) ATAKA KUNYAMAZISHA WANANCHI

Na Ndimara Tegambwage

SERIKALI imeficha ukweli. Katika hatua hii, serikali inaweza kutuhumiwa kusema uwongo; na kusema uwongo ni kutenda jinai. Je, serikali ikitenda jinai itakuwaje?

Katika taarifa yake, serikali imepiga marufuku kile ilichoita “malumbano” kati ya Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz kwa maelezo kuwa “yanaweza kutumbukiza taifa katika uvunjaji amani.”

Taarifa ya Waziri wa Habari, George Mkuchika kwa vyombo vya habari juzi Jumatatu imesema serikali “haitakubali kusikia malumbano” hayo na “haitavumilia kuona vyombo vya habari vikichangia kuligawa taifa katika makundi na kudumaza maendeleo.”

Hapa ndipo penye mgogoro. Wasomaji wa magazeti, wasikilizaji redio na watazamaji wa televisheni hawajawahi kuona kile serikali inachokiita “malumbano.”

Mengi ametuhumu watu kuwa “mafisadi.” Mmoja wao ni Rostam. Naye Rostam amejibu, tena kwa kutumia chombo cha umma – Televisheni ya Taifa (TBC1).

Kwa akili ya kawaida, kilichotendeka ni kuibua hoja zilizokuwa zikienda chinichini. Kilichoanikwa ni matendo ya watu binafsi yanayohusu uchumi na maisha ya wananchi.

Kile ambacho serikali inaita “malumbano” ni eneo la “soko huria” la mawazo ambamo, kwa miaka miwili sasa, wananchi wamekuwa wakichangia kwa njia ya kulalama kwamba keki ya taifa inaliwa na wachache.

Sasa serikali inasema “haitakubali kusikia” na wala “haitavumilia” kuona vyombo vya habari na waandishi wakichangia kugawa taifa.

Huu ndio udikiteta mchafu. Kwanza, serikali inatafuta nini katika “malumbano?” Kama ni malumbano kweli, si iwaache walumbanao wafanye wafanyavyo? Malumbano si huisha hoja zikiisha?

Pili, serikali inajikoroga. Upande mmoja inasema kuna malumbano kati ya watu wawili; na upande mwingine inasema wananchi wameanza kugawanyika; hawa wakiunga mkono Mengi na wale wakiunga mkono Rostam.

Basi haya siyo malumbano. Huu ni mjadala wa hoja za kina. Ni mdahalo wa gonga nikugonge wa kuibua mazito na machungu yanayohusu jamii. Ni uwanja wa kumwaga taarifa kwa wenye macho kuona na wenye masikio kusikia. Ni kitanzi pia cha wasema uwongo.

Lakini serikali inasema sasa basi! Nyamaza! Huu ni ukatili. Ni udikiteta. Kuna hasara gani kwa wananchi kuwa upande wanaotaka, wanaoelewa, wanaothamini na waliotayari kutetea?

Tatu, serikali haisemi ukweli pale inapodai kuwa nchi itaingia katika “uvunjaji” amani. Watu huru wanapojadili yanayowahusu wao na jamii yao, haitazamiwi serikali ijenge visingizio vya kupotea kwa amani.

Watu wakiona mabaya yanatendeka; wakakaa kimya au wakanyamazishwa, wakajenga chuki kimyakimya, wakafura kwa hasira; basi linalofuata ni mlipuko mkubwa kuliko mabomu ya Mbagala.

Mlipuko huu ni hatari zaidi, hata na hasa kwa watawala, kuliko mdahalo juu ya nani “anakula nini.” Bali sasa ni wazi kwamba kwa hatua ya serikali ya kuzima mjadala, lazima “kuna jambo.”

Nne, serikali makini ingefurahia mdahalo. Ingepata vyanzo vizuri na sahihi vya taarifa mwanana za kufanyia kazi iwapo ina nia kweli ya kufanya kazi. Lakini inaonekana imechoka haraka na mapema.

Sasa siyo tu serikali haitaki kusikia, bali pia haitaki wananchi wasikie na washiriki mjadala. Huu ni udikteta mchafu.

Mtu angetarajia “mapapa” watajwe na “fisadi nyangumi” watajwe ili wananchi waone tofauti kati ya papa na nyangumi. Waone nani anaamsha hisia zao ili waone na kupigania haki na maisha yao.

Hakika, mmoja wa samaki hawa wakubwa aweza kuwa mwandani wa wananchi. Panahitajika uibuaji taarifa. Upembuzi. Uchokonozi wa kina na ushiriki wa wananchi katika mjadala. Kuzima hili ni ukatili wa kidikteta.

Tano, serikali inatumia vitisho kuzima mjadala. Inanukuu na kujivunia sheria katili zenye harufu ya kifashisti kama hii Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 na nyingine yenye chembechembe za kibedui – Sheria ya Utangazaji ya mwaka 2003.

Katikati ya majigambo ya utawala bora, ukiona bado kuna watawala wanaojivunia sheria zinazopingana hata na katiba zao, na uhuru na haki za wananchi, basi ujue udikteta umeota mvi. Wanaua uhuru na haki ili watawale misukule na siyo watu wanaofikiri na wenye utashi.

Sita, kwa serikali “kutahadharisha” wahariri na waandishi, ina maana ya kuwafunga midomo na mikono. Wasifikiri. Wasitende. Wasubiri serikali iamue andika hili, andika lile.

Saba, kuna upandikizaji woga. Waziri anasema sheria “zinakataza mtu, watu kuzungumzia au kujadili suala ambalo tayari liko mahakamani.” Hakuna sheria ya aina hiyo.

Chukua maneno ya waziri kama yalivyonukuliwa hapo juu. Ama waziri hakuelewa sheria inasemaje au ameinukuu nje kabisa ya muktadha. Sheria aina hiyo itakuwa za kishetani.

Magwiji wa sheria waliishafundisha kuwa waamuzi wa kesi mahakamani siyo hakimu au jaji peke yake. Kuna wakili wa pande mbili na kuna wananchi wanaofuatilia kesi.

Kila fungu litatoa hukumu yake; na hilo ndilo hufanya hakimu au jaji awe makini akijua siyo mwamuzi pekee, hata kama waamuzi wengine hawakuketi mbele ya mahakama.

Kwa hiyo suala la kutojadili kilichoko mahakamani ni uzushi unaolenga kutisha na kunyamazisha wananchi. Hata kuibuliwa kwa madai ya nyongeza, nje ya yale ambayo mtuhumiwa tayari amesomewa mahakamani, siyo kosa.

Ni kweli kabisa maoni nje ya mahakama yaweza kusaidia kuweka wazi zaidi kinachoendelea mahakamani. Hiyo ni kama mawakili watakuwa wamepata taarifa zaidi za kunoa stadi kuchokonolea kile ambacho walikuwa hawakukiona na kukiwasilisha kwa ustadi zaidi.

Lakini mjadala nje ya mahakama hauwezi, hata kidogo, kuharibu kinachoendelea mahakamani. Vitisho kama vile vya Mkuchika ndivyo vinaweza kuharibu mbongo za watu na kuwapokonya uhuru wa maoni. Naomba kuwasilisha.

Kwa hiyo, serikali imetumia mabavu kujaribu kuzima mjadala ambao ungeisadia. Sasa kuna madai kuwa imefanya hivyo kwa kuogopa itaguswa pale – kati ya papa na nyangumi.

Kuna kila sababu ya kupinga udhalimu huu katika nyakati tulizomo. Tukinyamaza watawala watashindilia watu kwenye magunia kama dagaa na kututupa mwaloni.

Kuvunjika kwa amani ni visingizio. Kutumia visingizio kukwepa ukweli ni kuficha ukweli hadi kufikia viwango vya kusema uwongo.

Kusema uwongo kuwa mjadala utaleta maangamizi kitaifa ni kutenda jinai.
Serikali ikitenda jinai wananchi wafanyeje?

0713 614871
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com

(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la 13 Mei 2009)

WANAGAPI WATAPIMWA AKILI TANZANIA?

Vimbwanga vya Ikulu, BoT na walinzi

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI kupuuza vimbwaga. Vina maana yake katika mazingira maalum ya utawala uliopo. Ilitokea katika historia ya nchi hii, moto ukaunguza Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Wengi walistuka. Wengine walishangaa. Wengi walihisi kulikuwa na njama za kuficha wizi au kuharibu ushahidi kwa kuchoma nyaraka. Ndani ya benki maofisa walikanuliana macho na kauli za “sihusiki” zikawa salaam za kila siku.

Kilichostua wengi wakati huo na hadi sasa ni aliyeshitakiwa. Alikuwa mlinzi – korokoroni. Kesi ilinguruma. Ulijengwa ushahidi wa kushindilia na kuokoa. Hukumu hii hapa. Ni mbele ya jaji.

Jaji anachukua hukumu iliyoandikwa. Anageuzageuza kurasa. Anateremsha miwani yake ambayo inagota kwenye pua. Anawaangalia waliofurika mahakama kwa kupitia juu ya miwani yake. Anawaangalia washitakiwa. Anaanza kusoma hukumu.

Ni maneno mengi. Ni sentensi nyingi. Ni aya nyingi kwenye karatasi nyingi. Mahakama imetulia, tuli! Anasoma. Anahoji na kujijibu. Anatulia kwa sekunde kadhaa na kuvuta pumzi huku waliojaa mahakama wakisubiri “hukumu.”

Kwa kauli zisizo na usumbufu wa maneno marefu, magumu na ya mchanganyiko wa Kiingereza na Kilatini, ambayo hutumiwa na wanasheria wengi, jaji anasema kuwa, kila anapoangalia pale mahakamani, haoni waliotenda jinai ya kuchoma benki.

Alikuwa na maana kwamba wahusika hawakuwa mahakamani. Hawakushitakiwa. Aliyekuwa kizimbani, kwa maoni yake, uelewa na kwa mujibu wa sheria, hakuwa na hatia. Alimwachia. Mlinzi hakuelewa. Wasikilizaji walipigwa na mshangao.

Waliochoma benki hawajawahi kufikishwa mahakamani hadi leo. Hata hivyo, mabenki hayaungui kwa moto wa sigara za wapita njia na hakuna joto la kukamata watuhumiwa wengine. Labda moto huo ulikuwa mwanzo wa kindumbwendumbwe kilichoko BoT leo.

Sikiliza ya Ikulu, Dar es Salaam. Ni alfajiri au asubuhi. Ikulu kunawaka moto. Nani kaunguza makao ya rais (mara hii yumo Benjamin Mkapa)? Wengi wanastuka. Wengine wanashangaa. Wengi wanahisi kuna kilichounguzwa ili kuharibu ushahidi.

Magari ya kuzima moto ikulu hayapo. Wanaowahi kufika ikulu ni kampuni binafsi ya ulinzi na zimamoto. Lazima walinzi wa langoni wajiulize iwapo zimamoto ya “moto wa binafsi” inaweza kuzima moto wa “ofisi ya umma.”

Subiri kidogo. Wakawasubirisha. Moto haukusubiri. Hadi uamuzi unafanywa, kwamba kampuni binafsi yaweza kuzima “moto wa umma,” moto uliishatafuna vipande vya ikulu.

Hapa hakuna kesi. Wataalam wanaeleza chanzo na hakuna wa kukamata. Lakini ikulu imeungua na ikulu haziungui kwa moto wa sigara za mpitanjia. Ni vimbwanga vya Tanzania.

Wiki iliyopita mwanaume mmoja aliingia ikulu bila kubisha hodi. Akaenda hadi maeneo ya ofisi. Bila shaka akakagua au akashangaa mandhari ya ofisi kuu ya taifa. Kwani wale ndege kishingo – tausi, wanaoranda bustanini humo kila siku hulipa kiingilio?



Baada ya utalii huu wa muda mfupi, mwanaume huyo alichuma ua bustanini ikulu; labda kwa shabaha ya kutaka kuwaonyesha wenzake kuwa alikuwa ndani ya ikulu bila kukaribishwa na rais wala ofisa yeyote. Akaanza kutoka kupitia lango kuu.

Tofauti na vimbwanga vya BoT na moto wa ikulu, hiki kina manjonjo ya aina yake: Kabwela asiye na kitanda kaingia ikulu bila kikwazo. Walinzi walikuwa wapi? Mtoto wa watu kajiingilia ikulu na analo la kusimulia, nyumbani au kijiweni.

Bahati – yoyote ile – mbaya au nzuri, mwanaume huyo akadakwa langoni akiwa anatoka. “Unatoka wapi wewe? Kwanza uliingiaje mpaka kule?” Ni maswali lakini hayana uzito bali mwanaume huyo hafanyi mikwara. Anajieleza. Huko ndiko wanaita kumatwa. Sasa kuna taarifa kuwa mtu huyo apelekwe hospitali kupimwa akili.

Katika hali yakawaida, nani anastahili kupimwa? Hapa kuna kijana aliyeingia ikulu bila kelele wala mikwaruzo na alikuwa anatoka bila kubughudhi yeyote isipokuwa akiwa amebeba ua alilochuma. Huyu apimwe nini?

Pale ikulu anakaa rais wake. Wanakaa watumishi wa umma. Wapo askari wa kulinda amani na amani ni amani yake na wakaao ikulu na wengine wanaoingia. Apimwe nini?

Si angepimwa asiyejua kuwa ikulu inapaswa kuwa eneo la utalii wa watu wa nje na ndani ya nchi na kwamba ni moja ya vivutio na sehemu ya elimu kwa jamii?

Kati ya walinzi na mwanaume aliyeingia ikulu bila hodi, nani apimwe akili? Wale ambao hawakuona mtu anaingia na aliyeingia na kutoka bila kufanya baya lolote, nani hasa apimwe akili?

Kwanza ikulu imekuwa moja ya “vijiwe” maarufu. Imezungukwa na watafuta kivuli wakati wa jua kali; wauza maji, karanga na kahawa. Hivi karibuni, baada ya wakazi wakuu wa ikulu kufoka ndipo askari wakazizunguka na kufanya kamatakamata ya zimamoto.

Lakini Makamu wa Rais Mohammed Shein amestuka zaidi hivi karibuni. Anasema ofisi zimegeuzwa soko. Ni biashara “mtindo mmoja.” Wauzaji wanaingia na kutoka, utadhani kazi za serikali zimehamishiwa kwingine; kilichochukua nafasi hiyo ni uuzaji na ununuzi wa sidiria, suruali, chupi, t-sheti, blausi, mashati, vipodozi na nywele za watu wa kale!

Wangapi watapimwa akili? Yule tu aliyeingia ikulu au na walinzi wa ikulu, watumishi wote wa ikulu, wakuu wa ikulu, wafanyabiashara – wa kuuza na kununua – wa ikulu? Nani atasalia katika kupimwa akili? Wauza karanga getini?

Ukimaliza vituko vya ikulu na BoT, njoo kwenye vituko vya kupotea kwa vilaputopu. Kwa maana ya sasa, “laptop” ni kompyuta ndogo ya mkononi au mezani. Inatumika kama kompyuta yoyote ile bali ni rahisi kubeba.

Sasa sikiliza vimbwanga vya laputopu. Leo laputopu ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) imepotea. Wanasema imeibwa “kiaina.” Huyu ndiye amekabidhiwa mamlaka ya kuamua nani ashitakiwe nani asishitakiwe. Kalaputopu kage kanaweza kuwa na nini?

Leo hiihii laputopu ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeibwa. Wanasema imeibwa “kiaina.” Huyu ndiye mkuu wa idara ya vipimo nyeti anayekimbiliwa wa mwisho kutoa uthibitisho wa lolote linalohitajika kupimwa kikemia. Kalaputopu kake kanaweza kuwa na nini?

Kaa chini utunge matukio haya kama shanga: Moto wa BoT, moto wa ikulu, mwanaume anayetokea lango kuu la ikulu akiwa na ua mkononi na kupotea kwa laputopu za watumishi wa ngazi ya juu serikalini. Kizaazaa! Nani apimwe akili? Watapimwa wangapi?

0713 614872
ndimara@yahoo.com
www.ndimara.blogspot.com
(Makala hii itachapishwa katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili toleo la 17 Mei 2009)