Tuesday, April 28, 2009




Mr.Venance Muliki W'ialango (picture), has been appointed Secretary General of Mouvement National de Congo - Lumumba (MNC-L)with effect from February 2009. Mr. W'ialango has been secretary general of the youth movememnt of the party of Lumumba for over 12 years now and his recent elevetion talks a lot about his industriousness and capability to handle current issues in a party whose most leaders have been living in exile.Mr. W'ialango has told reporters in Dar es Salaam, Tanzania that he will be going to his home constituency - Fizi in South Kivu where he says elders have asked him to become their member parliament.

Dr. Albert Onawelho, the president of MNC-L lives in London and is expected to run for the presidency in the general elections coming April 2010.

Saturday, April 25, 2009

WAZIRI GHASIA ANATETEA SIRI ZIPI?

Waziri Ghasia anayeleta ghasia

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI Hawa Ghasia kwa kuwa analeta ghasia katika mjadala kuhusu siri na hasa kile kinachoitwa “nyaraka za siri za serikali.”

Kauli ya waziri huyu wa Utumishi bungeni wiki hii, inaonyesha kuwa yeye binafsi, na huenda siyo serikali, anataka wananchi watembee wamebana pumzi kwa kuogopa kuwa kila walichonacho mkononi ni siri ya serikali.

Ameonya kwamba yeyote atakayekutwa na nyaraka za siri za serikali, “hata kama ni mbunge,” atachukuliwa hatua za kisheria. Ni onyo kali kutoka kwa Waziri wa Utumishi katika Ofisi ya Rais.

Hoja ya siri imejadiliwa mara nyingi. Nilidhani wahusika serikalini walielewa. Kumbe tulipoifikisha kileleni wengine walikuwa hawajaingia serikalini. Ndio sasa wanajaribu kuitoa kileleni na kuirudisha sakafuni.

Kila serikali duniani ina siri. Siri hizi hupangwa kwa viwango maalum – ndogo, kubwa kidogo, kubwa, kubwa sana, kubwa kabambe, kubwa na nene, kubwa na nzito, kubwa kuliko…

Mtanuo huu wa ukubwa hutegemea mfumo wa utawala na tabia ya wachache walioko madarakani ambao hutunga sheria za kulinda kile wanachoona ni siri za serikali. Wakati mwingine, katika ukorokoroni wa nyaraka, watawala hujikuta wanaona kila kitu ni siri na hakuna viwango tena.

Upele mgongoni mwa serikali huitwa siri. Mba shingoni mwa serikali huitwa siri. Jipu makalioni mwa serikali huitwa siri. Kikohozi cha muda mrefu huitwa siri. Tatizo hapa ni kwamba hufikia wakati hata mkubwa kwenda haja kubwa hadharani huitwa siri!

Ni katika hatua hii, watu huangalia pembeni; hutema kwa kinyaa, huku wakibinua midomo kama waliolamba tone la shubiri na kunong’ona, “Ee, kila kitu siri, siri.”

Siri ya serikali inabidi iwe siri kwa manufaa ya nchi. Haiwezi kuwa kwa manufaa ya watawala au kundi la watawala peke yao. Lakini ainisho hili huleta mgogoro kati ya watawala na watawaliwa.

Ununuzi wa ndege za kijeshi huitwa siri. Ukodishaji ndege za jeshi kwa watu binafsi huitwa siri. Uuzaji ardhi, mikataba ya kuchimbaji madini, mikataba ya uzalishaji na ugavi wa nishati ya umeme, vyote huitwa siri. Vivyo hivyo uuzaji wa raslimali nyingine za taifa nje ya nchi.

Siri hupanuka hadi kuhusisha shughuli za rais nje ya shughuli kuu ya utawala. Mikataba ya ununuzi wa rada na manunuzi mengine panapotumika fedha za umma hufanywa siri pia. Siri za aina hii hufikia wakati zikawakwama kooni wale waliopewa jukumu la kuzilinda, nao wakaamua kuzitoa; siyo kama siri bali kama makabrasha tu.

Hapa ndipo yanapotokea maasi. Ni hapa ambapo serikali inashindwa kuthibitishia hata mlinzi kuwa kile anacholinda ni siri. Ni hapa ambapo mlinzi anaamua kusema, “Potelea mbali. Hata kama nitapoteza kibarua, lakini sharti hili lifahamike kwa wengi.”

Hakuna anayenunua vikaratasi vyenye mikataba na viapo vya wahusika katika mikataba hiyo iliyofanywa siri. Hayupo. Mengi ambayo serikali inaita nyaraka za siri yanatolewa kwa hisani tu na hata bila juhudi za uchunguzi wa kina.

Wanaodaiwa kuwa walinzi wa siri hawajatoa taarifa zozote za kuibiwa kwa nyaraka wala kuvunjwa kwa sefu za nyaraka na kukwapuliwa kwa siri. Taarifa hizo hazipo. Raia wema waliochoka kuona “siri” zisizo siri ndio wanawapelekea “makaratasi” wabunge na waandishi wa habari.

Ukitumia viwango sahihi, na kwa kuzingatia misingi ya uandishi wa habari za uchunguzi, utaona kuwa sehemu kubwa ya kile ambacho wengi wanaita “uchunguzi,” hasa siyo uchunguzi kwa maana halisi.

Taarifa nyingi zinapatikana kwa njia ya nyaraka zilizotolewa kwa hisani – na mara nyingi bila ufundi wala ubunifu – na wakati mwingine bila juhudi za mwandishi au mbunge. Hii waweza kuita “chakupewa.”

Hata hivyo, kwa kutumia ustadi na ufuatiliaji wa kiwango cha “kuku wa kujitafutia,” taarifa hizo zimetoa mwanga wa kile kinachoendelea na wakati mwingine kupanua wigo wa kidogo kilichopatikana kuwa mkubwa zaidi na kuhusisha wengi.

Vyovyote ilivyo, serikali inapaswa kulinda kile ambacho inaita nyaraka zake za siri. Hakuna mwenye uwezo wala mamlaka ya kulinda siri za serikali isipokuwa serikali yenyewe.

Ni serikali itakayobuni na kuweka njia “bora” za kulinda siri zake – ziwe siri kweli au viinimacho. Ni serikali inayostahili kujua nani mwenye uwezo wa kulindia siri na uwezo huo hunawirishwaje, huongezwaje na hulindwaje.

Mpaka hapa ni muhimu basi kukubaliana kuwa kama serikali ina siri, basi ilinde siri zake. Serikali ikishindwa kulinda siri zake; na siri hizo zikatoka, haina sababu ya kulalamikia yeyote – awe mbunge au mwandishi wa habari.

Maswali ambayo huulizwa mara nyingi ni: Kama serikali imeshindwa kulinda siri zake, walioko nje ya serikali watazilinda vipi? Watawajibikaje kuzilinda? Watajuaje kuwa ni siri na kama ni siri za serikali?

Lakini hata wakijua, kwa maelezo rasmi kuwa ni siri, kwanza watajuaje kuwa hazijachoka na ndiyo maana zimeachiwa kuranda mitaani? Pili, watashindwaje kuzitumia katika hoja iwapo wanaona kuwa zina chembechembe za kuinua uelewa wa jamii juu ya mwenendo wa serikali yao?

Tatu, hata wabunge na waandishi wakizisaka kwa mbinu, ufundi na ujanja wao, kwa lengo la kuneemesha jamii na kukuza mwamko na uelewa, bado hilo haliwezi kuwa kosa machoni mwa wananchi ambao walifichwa ukweli husika.

Bali kuna haja ya kuzingatia jambo moja. Mjadala juu ya wizi au matumizi ya nyaraka za siri za serikali unarudi wakati wadau wa utawala bora, wakiwemo waandishi wa habari, wanasheria, wabunge, wanaharakati wengine wanasubiri serikali kuwasilisha bungeni muswada wa Uhuru wa Habari.

Kwa kuzingatia mwelekeo uliotolewa na wadau nje ya serikali, kuhusu umuhimu na njia za “kukomboa habari,” mapendekezo hayo yakizingatiwa katika sheria ya Uhuru wa Habari, yatamaliza malalamiko ya Ghasia.

Kwani hadi sasa, kila kilichosemwa bungeni na kuandikwa na kutangazwa na vyombo vya habari – kile ambacho serikali ilikuwa haijakitoa rasmi – hakina madhara kwa serikali adilifu wala jamii kwa ujumla.

Kama serikali iko makini na inajiandaa kuwatendea haki wananchi wake kwa kutambua uhuru wao wa kupata taarifa na habari, na kusimamia utekelezaji wa uhuru huo, basi Ghasia hana budi kuanza mazoezi ya kuishi nje ya mipaka bandia.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii itachapishwa katika safu ya SITAKI ya gazeti la Tanzania Daima Jumapili la 26 Aprili 2009)

Friday, April 24, 2009

UNYANG'ANYI UNAOSIMAMIWA NA SERIKALI

Wananchi wanapoitwa ‘wavamizi’ Kilosa

Na Ndimara Tegambwage

NI vilio vitupu. Baadhi ya wananchi wenye mifugo – Wamasai, Wairaqw, Wabarbaig na Wasukuma wanawindwa kama swala. Wanaambiwa waondoke wilayani Kilosa. Eti warudi makwao.

Je, kila Mtanzania angeambiwa arudi kwao, nani angebaki alipo? Nani siyo uzao wa mzunguko wa mataifa madogo? Nani mtu wa asili Tanzania?

Lakini makabila haya yanawindwa na kufanyiwa ukatili kwa kuwa yana mifugo. Wilayani Kilosa serikali inaendesha kile wanachoita “operesheni” ya kupunguza mifugo na kufukuza wenye mifugo wasiokuwa “wenyeji” wa wilaya hiyo.

Wamasai wanasema ni “presheni ya kupilisi” – operesheni ya kufilisi.

Viongozi wa Kata, wakiandamana na polisi na mgambo, wanavamia eneo la mwenye mifugo, ndani au nje ya mipaka yake. Wanaswaga mifugo hadi wanakodai ni “zizi la serikali.” Kuwagomboa sharti ulipe Sh. 30,000 kwa kila kichwa.

“Wanatwambia tuuze mifugo yetu palepale; au tuisombe kwa malori hadi kwenye mnada, Pugu, Dar es Salaam, au tuhamie mkoani Lindi ambako wanasema wametenga ardhi kwa ajili ya wafugaji,” anaeleza mfugaji Kalaita Parkuris huku machozi yakimlengalenga machoni.

Kalaita ni mwathirika wa operesheni. Polisi wenye silaha na mgambo waliingia kwake na kukomba mazizi – ng’ombe 340 na mbuzi 120 katikati ya eneo la eka zipatazo 70 ambako ameishi tangu 1963.

“Presheni nini hii? Nini hii kama siyo taka kutupilisi,” alihoji Kalaita alipoongea wiki iliyopita na waandishi wa habari, chini ya mti, nje ya nyumba yake.

Kalaita anasema alikataa kugomboa mifugo yake na kuacha ichukuliwe chini ya ulinzi wa polisi. Anaulizwa kama angekutana na Rais Jakaya Kikwete angemwambia nini.

Anajibu, “Ningesema awachukue watoto awalishe. Watakufa hawa,” huku akionyesha watoto wapatao 30 walioketi nyuma yake.

Ndugu yake anadakia, “Kuwachukua ni kama kuwapoteza. Ni kama wamekufa, maana hawapo.”

Hapo ni kijijini Mkundi, Kata ya Dumila. Lakini ndivyo ilivyo katika maeneo mengi wilayani Kilosa. Haishangazi basi kukuta akina mama wa kitongoji cha Ngaiti wakiimba mbele ya waandishi wa habari:
Maisha bora
kwa mwekezaji
Maisha bora
kwa mafisadi
Maisha duni
Kwa mfugaji

Wanawake hawa ni sehemu ya jamii ambayo shughuli yake kuu, kwa miaka yote, ni ufugaji wa asili. Kuwaondolea njia yao ya maisha, kwa kasi ya kuwafilisi, hakika ni kuvunja haki za binadamu.

Kupora mifugo ambayo ni ajira, uchumi na egemeo la uhai wa wananchi, kuna athari nyingi na kubwa kwa maisha yao.

Watakosa chakula – nyama na maziwa.
Watakufa kiuchumi na kupoteza uhai kabla ya wakati wao. Watoto wao watashindwa kwenda shule au kubaki hai wakichunga mifugo ya kaya zao.

Unyang’anyi huu kwa njia ya “operesheni ya kupunguza mifugo na kuondoa wahamiaji Kilosa,” tayari umezaa mifarakano. Sasa utazaa vita vikubwa.

Bibi Yasoi Kadege, mwenye umri wa miaka 97, wa kitongoji cha Ndagani kijijini Mabwegere, amechoka, amekata tamaa, anatamani ujana wake umrejee mara moja. Hauji.

Hapa unasimuliwa jinsi polisi na mgambo, walivyokomba ng’ombe 385 wa kaya hii wakiacha nyuma ndama wachanga 21. Hadi wiki iliyopita ni ndama watatu waliokuwa wamebakia; wakiwa taabani. Watakufa.

Sikiliza kikongwe Yasoi akijadiliana na mmoja wa waliofika nyumbani kwake:

Yasoi: Huko kwenu peresheni hii imefika?
Mgeni: Ipo. Wamechukua mifugo mingi tu.
Yasoi: Sasa wewe kaa hapa; ungana na mwanangu ili mwende Morogoro; piganeni vita mkomboe mali zenu.
Mgeni: (Kicheko cha kugegema) Sawa bibi, ni kweli.

Yasoi hana nguvu tena. Alibebwa na watu watatu kutoka ndani ya banda lake. Hata pale nje alipokaa, alihitajika mtu wa kuegemea na mwingine kuzuia asiangukie mbele.

Hana amani. Hana chakula. Chakula chake ni maziwa na “maziwa yote” yalichukuliwa na serikali. Maziwa ya kopo ambayo amepelekewa na wajukuu wake yanamletea kiungulia na sasa hataki hata kuyaona. Atakufa.

Mita 200 kutoka kwa Yasoi ni kwa Tisini Madamanya, mwenyekiti wa kitongoji cha Madagani, kijijini Mabwegere ambaye anasema askari walikomba mbuzi wake wapatao 250.

Tisini ana wake tisa na zaidi ya watoto 40 (jirani yake anasema ana watoto zaidi ya 70), watakufa njaa kama hawakupata msaada wa haraka. Mtoto mwenye umri mdogo hapa ana siku 14.

Kijiji cha Mabwegere ni cha wafugaji. Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilosa, Ephrem W. Kalimalwendo anadai kuwa halmashauri haijawahi kufanya operesheni kijijini humo.

Anapoelezwa unyang’anyi katika sehemu mbalimbali ambako waandishi wamefika na kusimuliwa uporaji, anakana kuhusika kwa serikali yake ya wilaya. Sasa nani amefanya uhalifu huo?

Kalimalwendo anakataa pia kuwa watu wanaporwa mifugo; anadai kuwa wanauza wenyewe au wanaondoka nayo kwa kuwa hawana “vibali” vya kuishi Kilosa.

Anapoulizwa iwapo kuna wanaoweza kuwa wanafanya “operesheni” nje ya operesheni maalum ya wilaya, anajibu kuwa hajui; ghafla anasema hawapo; baadaye anasema, ninyi (waandishi) mnaadika kwa kupendelea wafugaji. Kigeugeu.

Bali Mkurugenzi Kalimalwendo anasema wenye mifugo kutoka bonde la Ihefu mkoani Mbeya ambako walifukuzwa na wengine kutoka mikoa kadhaa nchini, “wamevamia Kilosa” na kupunguza uwezo wake wa kuhimili mifugo.

Anasema wilaya ina eneo la hekta 530,000 kwa kilimo na hekta 430,000 kwa kufuga na kwamba kwa eneo hilo la wafugaji, wilaya inahitaji ufugaji wa kisasa wa ng’ombe 150,000 tu (wastani wa ng’ombe watatu kwa kila hekta).

Hadi sasa halmashauri imefanikiwa kuondoa wilayani humo zaidi ya ng’ombe 18,000, anasema mkurugenzi na kusisitiza kuwa wasiokuwa wenyeji wa Kilosa “lazima waondoke.”

Kalimalwendo siyo mwenyeji wa Kilosa lakini tayari anamiliki ardhi ipatayo eka 10 katika kijiji cha Malangali ambamo wenye mifugo wametimuliwa na inadaiwa ardhi itamilikishwa kwa wawekezaji kutoka nje ya nchi.

Kuhusu kwa nini mkurugenzi amiliki ardhi katika wilaya ambayo anadai ina ardhi haba, Kalimalwendo anang’aka, “Hilo haliwahusu. Haliwahusu kabisa. Yaani mtu kununua eka 10 tu…nasema haliwahusu.”

Hivi sasa Kilosa ni kilio na kusaga meno kwa wenye mifugo. Mifugo inakamatwa. Kama mfugaji hana fedha za kuigomboa, inauzwa kwa “bei ya bure.”

Kwa mfano, ng’ombe ameuzwa kwa Sh. 120,000 hata 80,000 badala ya Sh. 450,000 au 500,000 na wanunuzi wanakuwa tayari wameandaliwa na madalali.

“Wanatuvamia. Wanaamuru twende Lindi au tuuze mifugo papo hapo huku tumeshikiwa bunduki. Huu siyo ubinadamu,” anaeleza mkulima na mfugaji wa Mabwegere.

Utaratibu wa serikali wilayani umezaa ubaguzi, unyanyapaa kwa wafugaji na hasa Wamasai ambao wana mifugo mingi na umetoa mwanya kwa uporaji kwa kisingizio cha operesheni.

Kuna tatizo Kilosa. Panahitajika mpango mpana, wa kistaarabu, wa muda mrefu wa kugawa ardhi, kwa kushirikiana na mikoa mbalimbali ili wenye mifugo wapate maeneo ya kufugia na kulishia bila manyanyaso.

0713 614872
ndimara@yahoo.com
(Makala hii ilichapishwa katika gazeti la MwanaHALISI toleo la Jumatano15 Aprili 2009)

UVUNJAJI HAKI ZA BINADAMU + +

Viongozi waoga, katili wa Bukombe

Na Ndimara Tegambwage

SITAKI viongozi wa wilaya ambao uwezo wao wa kufikiri ni mdogo na ambao wana haraka na uchu wa kutenda makosa.

Viongozi wa aina hiyo ni kama aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Bukombe, mkoani Shinyanga, Magesa S. Mulongo na kamati ya ulizi na usalama ya wilaya hiyo ambao wanalalamikiwa kwa kuwafukuza baadhi ya waandishi wa habari kutoka wilayani humo.

Madai ya mkuu wa wilaya na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama yametajwa kuwa “waandishi wa habari kukiuka maadili ya kazi zao.” Hapa ndipo penye mnofu wa mjadala na uchambuzi.

Hivi nani hasa anapaswa kujua maadili ya kazi au taaluma fulani? Naomba kujibu haraka. Ni yule mwenye taaluma au kazi husika. Kwamba muhusika anaweza kutenda kinyume, haina maana kwamba hajui maadili. Anaweza kuwa ananufaika binafsi kwa kutofuata maadili.

Kama kuna mwingine ambaye anaweza kuwa anajua maadili ya kazi au taaluma yoyote, ni yule anayefanya utafiti na anayejali kufuatilia misingi na utekelezaji wa kazi inayohusika.

Najenga mashaka juu ya uwezo wa mkuu wa wilaya ya Bokombe kujua kinachoitwa “maadili ya waandishi wa habari.” Najenga mashaka pia juu ya uwezo wa wajumbe wa kamati ya ulizi na usalama wa wilaya ya Bokombe kujua nini hasa kinaitwa uandishi wa habari, unavyofanywa na maadili yake.

Kwa nini? Kwa sababu viongozi wa ngazi hii wameumbwa kwa woga. Ni katope wa tuhuma, shutuma na hata malalamiko. Wanayeyuka kwa sentensi moja ambayo mwandishi amenukuu kutoka mdomoni mwa mwananchi mmoja mwenye malalamiko halali.

Najenga mashaka, juu ya tabia ya viongozi wa wilaya, ya kuogopa hata kishindo cha paka, inavyoweza kujua kazi na maadili ya waandishi wa habari.

Naharakisha kusema, tena kwa uhakika, kwamba hakuna hata mmoja kati ya walioshiriki uamuzi wa kufukuzwa waandishi wa habari kutoka wilayani Bukombe, ambaye anajua hata msingi mmoja na muhimu – ule wa kuandika au kutangaza ukweli – wa taaluma ya habari.

Wanasiasa hawa wa ngazi ya wilaya, kama baadhi ya wale wa ngazi ya kitaifa, na hasa tunapojadili suala la habari, uhuru wa habari na haki na uhuru wa kupashana habari, siyo watu wa kutumainiwa kutoa maamuzi.

Watu waliotengenezwa ama kwa hariri au mabonge ya barafu, ni watu hatari sana. Watachanika kwa upepo mdogo au watayeyule kwa joto la mpakato tu. Kwa hiyo sharti waishi kwa mashaka na woga, wakidhani kila mmoja anataka kuwachana au kuwayeyusha.

Wanasiasa wa Bukombe wanawatilia mashaka waandishi wa habari. Wanawaona, wanaamini, na ni kweli, kwamba hata waandishi wanawaona viongozi hao. Lakini viongozi wanataka sura zao, matendo yao na hata fikra zao, viishie Bukombe ambako wamewafungia wananchi katika giza la taarifa na kuwaaminisha kuwa wanafikiri kwa niaba yao.

Yeyote anayeweza au anayejaribu kuonyesha sura halisi ya wanasiasa hao; jinsi wanavyotenda na wasivyotenda; jinsi walivyoshindwa au wasivyoweza kutenda, lazima ataonekana mbaya, mchafu, mfitini, mchochezi.

Niliwahi kufukuzwa mkoani Ruvuma. Ilikuwa katika miaka ya 1970. Mkuu wa mkoa Athumani Kabongo, akikaa na kamati yake, alinilazimisha kuhudhuria kikao ndani ya ofisi ya TANU na kudai mbele ya wajumbe kuwa nimeandika uwongo.

Alichukua hatua baada ya siku tatu za kuzungukia kata mbalimbali, ikiwemo kata ya Kilagano kujionea mwenyewe na wajumbe wake kwamba mahindi yalikuwa yanaoza wakati taifa likikabiliwa na njaa kubwa. Nilikuwa nimeandika taarifa hizo.

Amri ya mkuu wa mkoa ilitolewa saa mbili tu baada ya mkoa kuunda kile ulichoita Operesheni Okoa Mazao ikisimamiwa na mkuu wa polisi mkoani. Angalia unafiki huu wa kiwango cha juu!

Lakini niliwaambia viongozi kuwa sifukuziki. Badala ya kuondoka mkoani, nilichukua usafiri wa lori na kujichimbia wilayani Mbinga ambako niliibua makali zaidi.

Nakumbuka mwandishi wa Radio Tanzania wakati huo, Abysai Stephen alinikuta Mbinga na kunieleza kuwa ameagizwa na mkuu wa mkoa anambie kuwa niondoke mkoani vinginevyo wangenikamata na kunifunga.

Kuna somo hapa. Nilikataa kuondoka mkoani. Niliendelea kuandika. Viongozi na polisi waliendelea kunisaka. Mkurugenzi wa wilaya aliona umuhimu wa kazi yangu. Akanipa gari la kwenda hadi Lipalamba na Mitomoni, kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji. Niliibua mengi.

Kwa ukaidi huu na kwa kazi iliyojaa usahihi wa aina ya kipekee, umma ulinufaika na serikali ilijua nani alikuwa anasema uwongo. Kilichofuatia ni viongozi wengi kuhamishwa, akiwemo mkuu wa mkoa, Athumani Kabongo.

Wanasiasa wa ngazi ya kijiji, kata, wilaya, mkoa, taifa, hata kokote walipo, hawana uwezo wala mamlaka ya kuamua juu ya taaluma ya habari isipokuwa kwa sheria kandamizi ambazo wamezitunga.

Hawana uelewa katika taaluma hii. Hawana nia njema kwa uandishi na waandishi. Lakini hakuna anayewazuia kuwa na maoni. Acha wawe hivyo, nasi tuwashangae. Lakini wakitaka kuchukua hatua yoyote ya kuzuia waandishi kufanya kazi yao, sharti wafikirie kwanza uhuru wa wengine.

Mwenye uwezo wa kutoa uamuzi juu ya malalamiko yao ni mahakama. Waende huko. Washindwe. Warudi kwenye vigoda vyao na kupiga miayo; kwani katika mazingira haya, hakuna mahakama yenye uwezo wa kutoa hukumu ya kuzuia, kuzima wala kunyang’anya uhuru wa habari.

Lakini sharti waandishi wa habari nao wakatae kufukuzwa. Ukondoo haulipi. Afadhali mwandishi akakamatwa, kuswekwa lupango na kuondolewa kesho kwa amri ya mahakama, kuliko kubaki huru mitaani lakini kichwa chini kama kondoo.

Hapo ndipo somo litakolea. Tujifunze kusema: Hapana.

0713 614872
ndimara@yahoo.com

(IMECHAPISHWA KATIKA GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI)